slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Saturday, March 26, 2016

WAZIRI MAGHEMBE AWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI TFS NA KAIMU MKURUGENZI IDARA YA WANYAMAPORI

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Machi, 2016. Kulia ni Naibu Waziri Eng. Ramo Makani.
Sehemu ya waandishi wa habari na wajumbe mbalimbali walioshiriki Mkutano huo.
........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini, (TFS) Bw. Juma Mgoo pamoja na Wakurugenzi wawili wa Taasisi hiyo ili kupisha uchunguzi kutokana na mwenendo usioridhisha wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi mbovu wa rasilimali za misitu nchini.

Prof. Maghembe ametaja majina ya Wakurugenzi hao aliowasimamisha kazi kuwa ni Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Bw. Zawadi Mbwambo pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi endelevu ya Misitu, Bw. Nurdin Chamuya

Baada ya kuwasimamisha hao amewateua watu wengine kushika nafasi zao wakati mchakato wa kuwapata watendaji wapya ukifanyika na walioteuliwa kukaimu nafasi hizo ni Kaimu Mtendaji Mkuu TFS, Gerald Kamwendo, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Mwanaidi Kijazi, na Kaimu Mkurugenzi wa Matumizi Rasilimali Misitu, Haji Mpya.

Wengine waliosimamishwa kazi na kanda zao katika mabano ni Hubert Haule (Kusini), Bakari Rashid (Mashariki), Cuthbert Mafipa (Kaskazini), Emmanuel Minja (Magharibi), Haji Khatibu (Ziwa) na Bruno Mallya (Nyanda za Juu Kusini).

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini mapungufu mbalimbali katika ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi usioridhisha wa rasilimali za misitu.

Alisema kuwa hivi karibuni walibaini shehena kubwa za magogo aina ya mninga katika Mkoa wa Rukwa wilayani Kalambo yakiwa yamekatwa na kuwekwa ndani ya makontena ndani ya msitu pamoja na kutengenezewa nyaraka feki zinazoonesha magogo hayo yanatoka nchini Zambia tayari kwa kusafirishwa kupelekwa nchini China.

Amesema kuwa baada ya kubaini tukio hilo na kulitolea maamuzi alipata taarifa kuwa shehena ya Magogo hayo yenye thamani ya shilingi milioni 500 za Kitanzania yaliyotakiwa kupelekwa Makao makuu ya Wilaya ya Kalambo yamemwagiwa petroli na kuchomwa moto wakati wiki mbili kabla alishatoa agizo la magogo hayo kusafirishwa kupelekwa Matai ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo.

Aliongeza kuwa kumekuwa na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.

“Pesa zitokanazo na makusanyo hayo zimekuwa hazipelekwi benki kwa wakati na hata zikipelekwa benki zimekuwa zikipelekwa pungufu na muda mwingine pesa hizo zimekuwa hazipelekwi kabisa”. Alisema Prof. Maghembe.

Katika tukio lingine, Waziri Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dkt. Charles Mulokozi kwa kosa la kukaidi agizo la kusaini vibali vya kusafirisha Wanyamapori nje ya nchi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kukamatwa watu katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro wakitaka kusafirisha nyani 61 “velvety monkeys” na kubaini kuwa Idara ya Wanyamapori ndio iliyotoa vibali vya kusafirisha nyani hao na vibali hivyo kusainiwa na Mkurugenzi huyo.

Alisema watu hao kutoka Ulaya Mashariki na washirika wao wa hapa nchini, walikodisha ndege ili kuwaondoa tumbili hao kwenda Ulaya Mashariki. Alisema harakati za kukamata tumbili hao porini zilianza wiki iliyopita na jumla ya idadi yao ni 450 ilhali kuna taasisi zinazolinda hayo mapori bila walinzi wa mapori hayo kujua

Prof. Maghembe alisema nyani hao walikamatwa maeneo ya Upareni, Hanang Manyara na Kiliamanjaro ambapo aliwaita wasimamizi na kuwapa taarifa juu ya watu hao na kuwakataza kutotoa kibali chochote cha kusafirisha wanyama hao.

“Nikiwa Moshi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa nilimuita Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi na kumuarifu juu ya kamata kamata hiyo na kumuagiza kutotoa kibali cha kusafirisha wanyama ili tuwakamate watu hao, lakini baadaye tukagundua yeye ndio amesaini kibali hicho kutoka Dar es Salaam,” alisema Maghembe.


Ameongeza kuwa ndege iliyokamatwa ilikuwa imekodiwa kutoka Afrika ya Kusini kwa ajili ya kusafirisha nyani hao kwenda Ulaya ya Mashariki, Ndege hiyo imeshikiliwa pamoja na rubani wake kwa mahojiano zaidi.

Prof. Maghembe ametoa onyo kali kwa wale wote wanaohujumu rasilimali za nchi na kusema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali.

“Hatutasita kumfukuza kazi mtu yeyote ambaye atashiriki katika suala hili la kuiibia nchi mali zake au anakaa anaangalia kando wakati fedha za nchi, mali za nchi zinaporwa” Alisema Prof. Maghembe kwa ukali.

No comments:

Post a Comment