slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Tuesday, July 12, 2016

WAZIRI WA MALIASILI PROF. JUMANNE MAGHEMBE AONANA NA BALOZI WA UJERUMANI HAPA NCHINI MHE. EGON KONCHANKE

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akimkaribisha Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Mhe. Egon Konchanke alipomtembelea jana tarehe 11 Julai, 2016 ofisini kwake, Mpingo House, Jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya Maliasili nchini.
Waziri Maghembe (kulia) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi Konchanke (kushoto).
Balozi Konchanke (kushoto) akimueleza jambo Prof. Maghembe (kulia) katika mazungumzo hayo.
Balozi Konchanke (kushoto) akimuonesha Waziri Maghembe (kulia) ramani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambayo Balozi huyo ameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza utalii wake kwa pamoja na ule wa Mkoa wa Kigoma (Hifadhi ya Mahale)
Waziri Maghembe (kulia) akizungumza katika kikao hicho.

______________________________________


Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeweka wazi msimamo wake kuwa haitauza meno yake ya Tembo yaliyohifadhiwa kwa kuwa kufanya hivyo ni kuongeza upatikani wa meno hayo kwenye soko hivyo kuchochea biashara haramu ya ujangili.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alipokuwa kwenye mazungumzo ya na Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke ofisini kwake Mpingo House, Jijini Dar es Salaam.

Balozi Konchanke alimueleza Prof. Maghembe kuwa, mwezi Septemba mwaka huu (2016), Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa unaosimamia biashara ya Viumbe vilivyo hatarini kutoweka vya wanyama na mimea (CITES) watakutana nchini Afrika ya Kusini kujadili mambo mbali mbali ikiwemo baadhi ya nchi wanachama ikiwemo Namibia kutaka kuuza Meno yake ya Tembo yaliyohifadhiwa ili kujipatia kipato.

Katika maelezo yake Balozi Konchanke alimuomba Prof. Maghembe kutoa msimamo wa Serikali ya Tanzania kuhusu hoja hiyo ya kuuza meno ya tembo yaliyohifadhiwa kutokana na matukio ya Ujangili na vifo asilia vya wanyama. “Ni upi msimamo wa Tanzania katika kuelekea mkutano huo kuhusiana na uamuzi wa nchi kama Namibia wa kuuza meno yake ya tembo yaliyohifdhiwa?” aliuliza Balozi Konchanke.

Katika majibu yake Prof. Maghembe alisema “Tanzania tunaungana na mataifa mengine ambayo yanapinga uuzwaji wa meno ya tembo, Kama tukiuza meno haya tutaongeza upatikanaje wake kwenye masoko, hivyo kuchochea zaidi biashara hii haramu, hatuna sababu ya kuyauza wala kuyachoma moto, ukiyachoma moto unakuwa umechoma kila kitu ikiwemo sampuli ambazo zingeweza kutumika kwenye tafiti mbalimbali zikiwemo za kutengeneza madawa ya kutibu maradhi ya wanyama hao”. Aliongeza kuwa nchi zitakazofanya hivyo zitakuwa hazijafanya jambo la busara zaidi ya kuleta maafa kwa nchi jirani ya kuongezeka kwa vitendo vya ujangili.

Wakati huo huo, Waziri Maghembe alimuomba Balozi Konchanke kuleta wawekezaji kutoka Ujerumani kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya Utalii na Uhifadhi hapa nchini. Balozi huyo aliahidi ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania ambapo alisema mwishoni mwa mwezi huu wa Julai Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya Ujerumani Dkt. Gerd Muller atakuja nchini na wafanyabiashara kutoka nchini humo wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya Uhifadhi na Kilimo.

Balozi Konchanke ameahidi pia kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza Utalii kwenye Mikoa ya Kigoma na Katavi kwa kuunganisha utalii wa Hifadhi ya Mahale na Hifadhi ya Katavi. Amesema kuwa eneo hilo linahitajika kuwekewa miundombinu mizuri ya barabara ili liweze kufikika kirahisi.

Kwa upande wake Waziri Maghembe amesema kuwa utalii katika Mikoa hiyo unapewa nafasi kubwa ili uweze kukua na kuliingizia zaidi taifa mapato. Ameeleza kuwa katika kukabiliana na changamoto ya usafiri zitaansishwa safari za ndege za bei nafuu mara tatu kwa wiki kutoka Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Kigoma na Katavi kwa bei ya dola za kimarekani 150.

Akizungumzia kuhusu kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye huduma za Utalii wakati akijibu hoja ya Balozi Konchanke juu ya malalamiko ya watoa huduma hizo kuwa sheria hiyo imekuja ghafla na inapunguza ujio wa watalii nchini, Waziri Maghembe alisema sheria hiyo imepitishwa na bunge na watoa huduma hao walishataarifiwa toka mwaka jana (2015) juu ya mabadiliko ya sheria hiyo kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mabadiliko yake. Aliongeza kuwa ili Serikali ijiendeshe inahitaji mapato na kwamba watalii wanalipa kodi hivyo na watoa huduma nao wanahitajika kulipa kodi.

Katika hatua nyingine Balozi Konchanke aliomba ufafanuzi kwa Waziri Maghembe juu utaratibu mpya wa mashirika ya umma kupeleka fedha zote za makusanyo hazina na kwamba kama wahisani wakichangia kuendeleza mashirika hayo ikiwepo TANAPA na TAWA, pengine lengo lao litakuwa halijafikiwa na hivyo kuwa vigumu kujiendesha. Akijibu hoja hiyo Waziri Maghembe alisema kumekuepo na uelewa hafifu juu ya utaratibu huo ambao kimsingi Mamlaka hizo ikiwemo TANAPA na TAWA zitapelekea fedha zao hazina na kuzitumia pale itakapohitajikwa kwa mujibu wa mpango kazi wao.

No comments:

Post a Comment