NAIBU WAZIRI MHE,KANYASU AWAFUNDA WATUMISHI WA TFS PAMOJA NA WANANCHI
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amewaonya
wananchi wanaofanya shughuli za
kibinadamu ndani ya Hifadhi za Misitu nchini kuacha tabia ya kuwashambulia
Watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanapokuwa wanatekeleza
majukumu yao.
Onyo hili linakuja ikiwa zaidi ya watumishi watano wa TFS katika mikoa ya Pwani, Tabora ,Kigoma pamoja
Kilimanjaro wakiwa wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na wananchi wakati
wakiwa wanatekeleza majukumu yao.
Aidha, Mhe.Kanyasu amewapiga marufuku watumishi wa TFS kujichukulia
sheria mkononi kwa kuwapiga wananchi wanapobainika kutenda makosa.
"Watumishi wa TFS hamruhusiwi
kumpiga Mwananchi mnapomkamata ndani ya Hifadhi au akiwa anasafirisha
mazao ya Misitu kinyume na sheria, atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.
Ametoa onyo hilo wakati
akizungumza na wananchi kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika katika kata ya
Mgusu wilayani Geita mkoani Geita ikiwa ni ziara yake ya
kutatua migogoro ya mipaka kwenye msitu wa Hifadhi Geita iliyopo baina ya
Vijiji ambapo jumla ya hekta 4,462.95 zimefutwa kwa tangazo la Serikali.
Amesema shughuli za uhifadhi ni lazima zifanyike kwa ushirikishwaji kati
ya wananchi na watumishi wa TFS.
" Uhasama unaozidi kujengeka kati yenu hauna tija katika uhifadhi shirikianeni"
amesisitiza Mhe.Kanyasu.
Aidha, Mhe . Kanyasu amewataka
wananchi kuheshimu na kuzifuata sheria za uhifadhi ya Misitu nchini huku
akiwataka watumishi kujiepusha na
migongano kati yao na wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka wananchi wafuate sheria kwa
kulipia vibali kwa TFS pale wanapokuwa na mahitaji ya mazao ya Misitu badala ya
kusubilia mpaka wakamatwe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe.Josephat Maganga amemueleza
Naibu Waziri huyo kuwa hali ya Misitu katika wilaya hiyo ni mbaya kufuatia
shughuli za kibinadamu zinazoendelea kufanyika Misitu hiyo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya
hiyo Mhe.Maganga alisema kufuatia hali hiyo tayari Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana
TFS wameshaanza kufanya doria ya
kuwaondoa wafugaji na wakulima waliovamia
Hifadhi.
Katika hatua nyingine, Diwani ya Kata ya Mgusu, Pastory Lugusa
amemuomba Naibu Waziri huyo kumegewa
eneo la Hifadhi kwa vile idadi ya wakazi
wa kata hiyo imeongezeka hali inayopelea kukosa maeneo kwa ajili ya malisho na Kilimo.
Kwa upande wake Meneja wa Misitu wa
wilaya wa TFS, Fedy Ndandika amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa watashirikiana na wananchi hata hivyo tayari
wameanza kutoa elimu ya umuhimu wa uhifadhi kwa jamii zinazozunguka Hifadhi
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Mgusu, Halmashauri ya wilaya ya Geita mkoani Geita akiwasisitiza wananchi umuhimu wakufuata sheria na kuacha tabia ya kuvamia Hifadhi za Misitu
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati wa mkutano huo wa hadhara.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akiteta jamabo na baadhi
ya wanachama wa CCM wakati alipomaliza
mkutano wa hadhara katika kata ya Mgusu
mkoani Geita.