slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Wednesday, February 28, 2018

SERIKALI YAAGIZA OPERESHENI YA KUONDOA WAVAMIZI WA KIGENI KATIKA KISIWA CHA IZINGA MKOANI KAGERA


.........................................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa siku 7 kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA  kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Karagwe kufanya Operesheni ya kuwaondoa wavamizi wa nchi jirani wanaodaiwa kulima na kufiga ndani kisiwa cha Izinga kilichopo ndani ya Pori la Akiba la Kimisi mkoani Kagera.

Ametoa agizo hilo jana wakati wa ziara yake wilayani Karagwe mkoa wa Kagera muda mfupi baada ya kupokea taarifa na malalamiko ya kukamatwa kwa mifugo ya Watanzania ndani ya kisiwa cha Mubali huku kukiwepo mazao yanayodaiwa kulimwa na wananchi wa Rwanda katika kisiwa kingine cha Izinga.

“Ndani ya siku saba hicho kisiwa cha Zinga msafishe kila kitu, Mkuu wa Wilaya msaidie mtengeneze kikosi kiende kule kitoe takataka zote zilizoko kule, inakua ngumu kuadministrate (kutawala) wengine wa kwetu tunawatoa alafu wa nchi nyingine wamekaa, unatawalaje?”. Aliuliza kwa mshangao Dk. Kigwangalla.

Alisema watanzania wakienda upande wa Rwanda kuvua samaki ziwa Ihema wanauawa mara moja bila mjadala, wakati kwa upande wa Tanzani raia wa nchi hiyo wapo wengi na wengine wamepewa Uraia wa Kuasili (Citizenship by Naturalisation, CN) na huwa hawafanyiwi vitendo vya unyanyasaji wala mauaji  jambo ambalo alisema  ipo haja kama nchi kuchukua hatua ili kukomesha vitendo hivyo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, David Kenyata alisema atatekeleza agizo hilo la Waziri Kigwangalla kwa haraka ndani ya muda uliotolewa ili kumaliza mgogoro huo.

Katika hatua nyingine Waziri Kigwangalla alikataa ombi la Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashugwa la kuiomba Serikali iwamegee wananchi wa vijiji jirani sehemu ya eneo katika Pori la Akiba Kimisi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.

“Ardhi mimi sitatoa, sjui mlima sjui nini, siwezi kwenda kupeleka hilo ombi kwa Mhe. Rais, kabisa, hicho ni kitu ambacho hatuwezi kufanya kwa sasa’,” Alisisitiza Dk. Kigwangalla.

Mbunge huyo pia aliiomba Serikali kuweka uzio wa waya kwa ajili ya kutenganisha mpaka wa hifadhi hiyo na vijiji kwa madai ya kuepuka ukamataji wa mifugo ya wananchi unaofanywa na askari wa wanyamapori kwenye ardhi za vijiji na kuingizwa hifadhini na kutozwa faini, hoja iliyopigwa vikali na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka.

Hata hivyo, Dk. Kigwangalla alikataa ombi hilo na kusema kuwa mipaka ya hifadhi hiyo ni mikubwa kuwezesha utekelezaji wa ombi hilo. Alisema Serikali itatengeneza mtandao wa barabara zinazounganisha hifadhi hiyo na vijiji kwa ajili ya kuimarisha doria na shughuli za utalii pamoja na kujenga ofisi ndogo za pori hilo katika kila wilaya inayohusika na pori hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka aliwataka wananchi wanaofanya vitendo vya kuingiza mifugo kwenye pori hilo wakati wa usiku kuacha mara moja kwa kuwa wakimatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema malalamiko ya wananchi hao kuwa askari wa wanyamapori wanakamata mifugo yao kwenye maeneo ya vijiji na kuiingiza hifadhini kwa lengo la kuwatoza faini kuwa sio ya kweli na kwamba malalamiko yanakuja kwakuwa hukamatwa asubuhi wakiwa wameshatoka kulisha mifugo hifadhini.

Kisiwa hicho cha Izinga ambacho kipo katika wilaya ya Karagwe mkoani Kagera kina ukubwa wa Kilomita za Mraba 12 na kinapakana na nchi Rwanda.
Pori la Akiba Kimisi liliqnzishwa mwaka 2003 kwa Tangazo la Serikali na 116 na lina ukubwa wa kilomita za mraba 1,030. Pori hilo lina wanyamapori mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Simba na Chui. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozana na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashugwa kukagua Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera jana. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na baadhi ya viongozi wa kijiji cha Mwisheni alipofika kukagua Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya hiyo mkoani Kagera jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozana na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashugwa kukagua Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka wakati akikagua Pori la Akiba Kimisi akiwa kwenye ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya hiyo mkoani Kagera jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akionyesha mpaka wa Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya hiyo mkoani Kagera jana. Kulia ni Mkuu wa Karagwe, Godfrey Mheluka na Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa (kulia kwake).
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Lut. Col. Michael Mutenjele (kushoto) wakati wakivuka kivuko cha Ruvuvu wakati wa ziara yake ya kutembelea na kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya hiyo mkoani Kagera jana. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia baadhi ya mifugo iliyokamatwa ndani ya Pori la Akiba Kimisi wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi katika Wilaya Ngara mkoani Kagera jana. (Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii).

Monday, February 26, 2018

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII NA WIZARA YA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI YA ZANZIBAR ZAWEKA MKAKATI WA KUIMARISHA MUUNGANO

Na Hamza Temba - WMU
..................................................
Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania Bara na Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ya Zanzibar zimeweka mkakati wa pamoja wa kuimarisha ushirikiano wa usimamizi wa maliasili, malikale na kuendeleza utalii kwa maslahi ya pande zote za Muungano. 

Hayo yameelezwa  na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi baada ya mkutano wa pamoja wa wizara hizo uliofanyika hivi karibuni katika Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa siku moja uliongozwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Joseph Meza.

Akifungua Mkutano huo wa siku moja,  Maj. Gen. Milanzi alisema pamoja na Wizara hizo kutokuwa za muungano imekuepo haja kubwa ya kukutana kwa ajili kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha sekta ya maliasili na utalii na kukabiliana na changamoto zinazogusa sekta hiyo katika Muungano.

"Tumejadiliana kuona ni namna gani tunaweza kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ya biashara ya mazao ya misitu, biashara ya Wanyamapori inayohusiana na mikataba ya CITES na mikataba mingine ya ndani na ya Kimataifa.

"Tumekubaliana pia kuhuisha sheria zinazokinzana katika usimamizi wa sekta tunazozisimamia ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza katika utekekezaji na hivyo kuathiri Muungano wetu," alisema Maj. Gen. Milanzi. 

Alisema katika mkutano huo wa siku moja wataalamu kutoka pande zote za Muungano waliagizwa kuwasilisha mapendekezo ya namna bora ya kuendesha biashara ya mazao ya misitu na kupendekeza utaratibu wa kufanya biashara kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo.

Alisema kupitia mkutano huo Wizara hizo zimeunda kamati maalum ya kuratibu utekelezaji wa maazimio ya pamoja ya kuimarisha usimamizi bora wa sekta hizo na utatuzi wa changamoto zilizopo kwa kuandaa mapendekezo ya kimkakati ya muda mfupi na mrefu.

"Kamati hiyo itaongozwa na Afisa Mipango Mkuu Msaidizi kutoka Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka (DFNR), Saleh Kombo Khiari na Mchumi kutoka Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Maliasili na Utalii, Mugure Wambura," alisema Milanzi.

Mbali na hayo alisema kutakuwepo na vikao mbalimbali vya kuimarisha Muungano kupitia Wizara hizo katika ngazi ya wataalamu, Makatibu Wakuu na Mawaziri ambapo kikao kingine kinatarajiwa kufanyika kabla ya tarehe 30 Machi, 2018.

FULL VIDEO: DK. KIGWANGALLA ATEMA CHECHE KWA WAFUGAJI MANYARA



DK. KIGWANGALLA ATOA MIEZI TISA KWA WANANCHI KULIPWA FIDIA WAPISHE HIFADHI YA TAIFA TARANGIRE NA PORI LA AKIBA MKUNGUNERO


Na Hamza Temba-WMU-Manyara
........................................................................

Serikali italipa fidia na vifuta jasho kwa vitongoji ambavyo vipo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero ili viweze kupisha maeneo hayo yaendelee kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Kimotorok katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ambao ulihudhuriwa pia na Wakuu wa Wilaya za Simanjiro, Kiteto na Kondoa.

Alisema fidia hiyo italipwa kwa vitongoji viwili vya kijiji cha Irkishbo vya Maasasi na Lumbenek  vilivyopo katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara ambavyo vilikutwa ndani ya Pori la Akiba Mkungunero wakati pori hilo linaanzishwa mwaka 1996 kwa Tangazo la Serikali Na. 307.

"Tutafanya tathmini, tutawaomba wananchi mshirikiane na Serikali ili muweze kulipwa fidia mpelekwe maeneo mengine, jukumu letu sisi ni kugharamia zoezi la tathmini na kulipwa fidia ili muweze kuondoka katika maeneo haya ya hifadhi," alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema kwa upande wa baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kimotorok ambao wameanzisha makazi kimakosa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero hawatalipwa fidia na badala yake watafanyiwa tathmini na kulipwa kifuta jasho na kupelekwa maeneo mengine.

"Kimsingi ukimkuta mtu yupo katika eneo lako hupaswi kulipa fidia, hapa tumekuwa waungwana na kutumia roho ya kibinadamu, vinginevyo tungeweza kusema leo hapa tusione mtu na tungevunja kwa sababu ni eneo halali la hifadhi na hairuhusiwi kwa mujibu wa sheria mtu kuishi ndani ya hifadhi.

"Kwa sasa hatutatumia nguvu, lakini tukikamilisha zoezi la tathmini tukalipa watu fidia yao, tutatoa muda maalum wa watu kuondoka na watu watapaswa kuondoka, ilimradi tutajiridhisha kwamba tulimtendea haki kila mwananchi anayeishi katika eneo hili," alisema Dk. Kigwangalla.

Akizungumzia moja ya zahanati iliyojengwa ndani ya kitongoji hicho cha Kimotorok ambayo nayo itabomolewa baada ya zoezi la kulipa vifuta jasho, aliiagiza TANAPA kujenga zahanati nyingine katika eneo jipya litakalopangwa Halmashauri husika kwa ajili ya wananchi hao kuhamia.

Alisema zoezi la tathmini pamoja na wananchi kulipwa fidia na vifuta jasho linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi tisa ijayo kuanzia mwezi Machi, 2018. 

Akizungumzia hatma ya makazi mapya kwa wananchi watakaondolewa kwenye maeneo hayo ya hifadhi, Dk. Kigwangalla ameziagiza Halmashauri husika za Kiteto, Kondoa na Simanjiro kupanga maeneo mengine mbadala ya kuwahamishia wananchi hao punde baada ya kulipwa fidia zao.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa linalosimamia Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori inayosimamia Pori la Akiba Mkungunero kusaidia jamii jirani na maeneo hayo ya hifadhi kwa kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi, kuendeleza eneo la malisho na kuchimba mabwawa ya maji ya kunywesha mifugo ili kujenga misingi ya urafiki na ujirani mwema.

Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla amefuta mipaka ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makame ambayo imeingia kimakosa ndani ya Pori la Akiba Mkungunero na kumuagiza Meneja wa Pori hilo, Emmanuel Bilaso kuweka ulinzi mkali katika eneo hilo.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula alisema watasimamia utekelezaji wa maagizo hayo ya Serikali ili kuhakikisha mgogoro huo wa muda mrefu unapatiwa ufumbuzi. 

Katika ziara hiyo ya siku moja Mkoani Manyara, Waziri Kigwangalla alitembelea na kukagua eneo la Ranchi ya Manyara ambayo pia ni sehemu ya mapito ya wanyamapori,  eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge, Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero ambapo alitoa maelekezo mbalimbali ya kuboresha maeneo hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Herman Batiho kukakua maeneo hifadhi hiyo jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara. 

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akionyeshwa mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na viongozi wa hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Herman Batiho kukakua maeneo ya mapito ya wanayamapori na mipaka ya hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Sezaria Makuta wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi katika Kijiji cha Kimotorok mkoani Manyara jana. Wanaoshuhudia kushoto Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magesa.

Friday, February 23, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA ATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA ARUSHA, ATUMA SALAMU KWA MUWEKEZAJI ANAECHOCHEA MGOGORO KATIKA HIFADHI HIYO


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na viongozi wa TANAPA alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ausha jana na kukagua shughuli mbalimbali za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Katikati ni Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA, Martin Loibooki na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga (kulia). 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia moja ya eneo lenye mgogoro ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha alipotembelea hifadhi hiyo jana na kukagua shughuli mbalimbali za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Katikati ni Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA, Martin Loibooki na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga (kulia). 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA, Martin Loibooki  alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha jana na kukagua shughuli mbalimbali  za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Kulia ni Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga.
Picha ya pamoja Waziri Kigwangalla na baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA.
Waziri wa Malisili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Uhifadhi wa TANAPA, Martin Loibooki kuhusu Kreta ya Hifadhi ya Ziwa Manyara muda mfupi kabla ya kuhitimisha ziara yake katika hifadhi hiyo jana jioni. (Picha na Hamza Temba-WMU)

DK. KIGWANGALLA AAGIZA MBINU MPYA KUDHIBITI WANAOCHIMBA MADINI KWENYE CHANZO CHA MAJI YA MTO ZIGI JIJINI TANGA


Na Hamza Temba, WMU, Muheza Tanga
..........................................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS kujenga kituo cha ulinzi cha kudumu katika eneo la chanzo cha maji ya mto zigi kilichopo ndani ya Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani kwa ajili ya kulinda chanzo hicho.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari  baada ya kutembelea eneo la chanzo hicho na kukuta uharibifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya wananchi wanaodaiwa kuchimba madini ya dhahabu katika eneo hilo la hifadhi kinyume cha sheria

"Nimeagiza watu wa TFS wajenge kituo cha ulinzi cha kudumu katika eneo hili, na waweke walinzi wetu wa kudumu hapa badala ya kutegemea kufanya patrol (doria) na kuondoka, kwasababu eneo hili wananchi wanaamini lina madini ya dhahabu kwahivo kila siku wataendelea kuja kujaribu kuvuna dhahabu kutoka hapa.

"Kwasababu sisi kazi yetu ni kuhifadhi Maliasili ambayo tumepata kama urithi wa nchi yetu, niwahakikishie kwamba tutaimarisha ulinzi kwa kuanzisha kituo cha ulinzi hapa ili askari wawe wanabadilishana na kudhibiti kabisa uharibu ambao umekuwa ukifanyika, kwasababu maji yanayotoka katika chanzo hiki yanakwenda kunywesha Muheza yenyewe na wilaya wa Tanga, tukiharibu hapa yatakosekana maji safi na salama"  alisema Dk. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala huyo, Prof. Dos Santos Silayo alisema pamoja na eneo hilo kwa sasa kuwa linalindwa na askari wa Suma JKT watahakikisha ulinzi unakuwepo muda wote kwa kutekeleza agizo hilo la Waziri la kujenga kituo cha ulinzi cha kudumu ili askari wawepo katika eneo hilo muda wote.

"Lengo letu ni kuhakikisha kwamba wananchi hawaingii ili tusiwe tunawashtukiza kuwakamata na kwachukulia hatua, lazima tuwe watu wa kuzuia uhalifu usitokee, nia yetu ni kuwa na kituo mara moja kama alivyoelekeza Mhe. Waziri na hili jambo tumelichukua kama maelekezo na tutalitekeleza kwa nguvu kabisa," alisema Prof. Dos Santos Silayo.

Awali Dk. Kigwangalla alitembelea kikundi cha wafugaji wa vipepeo katika Tarafa ya Amani ambao waliiomba Serikali ifungulie vibali vya kusafirisha bidhaa hiyo nje ya nchi, aliahidi kuyafanyia kazi maombi yao huku akiwataka kutumia fursa ya ufugaji huo kama bidhaa ya utalii kuwavutia watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani.

Akiwa mkoani Tanga alitembelea pia Kituo cha Mambo ya Kale cha Mapango ya Amboni na kusema Wizara yake itaboresha kituo hicho pamoja na vituo vingine vya Mambo ya Kale ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini viweze kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa.

Katika ziara hiyo ya siku moja mkoani Tanga alitembelea pia shamba la miti ya Mitiki Longuza, Makumbusho ya Shaban Robert na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia vipepeo katika moja shamba la wafugaji katika Tarafa ya Amani Jijini Tanga jana. Mbali na biashara ya kuuza vipepeo hao nje ya nchi aliwataka wafugaji hao kutumia fursa ya ufugaji huo kama bidhaa ya utalii kwa kuandaa maonesho maalum ya kuwavutia watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipokea zawadi ya pambo la vipepeo kutoka kwa mmoja wa wafugaji Asina Athumani muda mfupi baada ya kukagua shamba la vipepeo katika Tarafa ya Amani Jijini Tanga jana ambapo aliwataka wafugaji hao kutumia fursa ya ufugaji huo kama bidhaa ya utalii kwa kuandaa maonesho maalum ya kuwavutia watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisaidia baadhi ya watu kupanda mlima baada ya kukagua chanzo cha maji cha Mto Zigi ambacho kipo ndani ya Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani wilayani Muheza mkoa wa Tanga. Ameiagiza TFS kujenga kituo cha ulinzi cha kudumu katika eneo hilo linalovamiwa na wananchi kwa madai ya kuchimba madini ya dhahabu.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua moja ya shamba la vipepeo katika Tarafa ya Amani Jijini Tanga jana ambapo aliwataka wafugaji hao kutumia fursa ya ufugaji huo kama bidhaa ya utalii kwa kuandaa maonesho maalum ya kuwavutia watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani tofauti na hivi sasa wanapotegemea soko la kuuza nje ya nchi. Kulia ni Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajabu. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Kituo cha Mapango ya Amboni, Jumanne Gekora kukagua kituo hicho jana Jijini Tanga ambapo alisema Serikali itaboresha kituo hicho pamoja na vituo vingine vya Mambo ya Kale ili vichangie zaidi kwenye pato la Taifa. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Kituo cha Mapango ya Amboni, Jumanne Gekora kukagua kituo hicho jana Jijini Tanga ambapo alisema Serikali itaboresha kituo hicho pamoja na vituo vingine vya Mambo ya Kale ili vichangie zaidi kwenye pato la Taifa. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Kituo cha Mapango ya Amboni, Jumanne Gekora kukagua kituo hicho jana Jijini Tanga ambapo alisema Serikali itaboresha kituo hicho pamoja na vituo vingine vya Mambo ya Kale ili vichangie zaidi kwenye pato la Taifa. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata maelezo kutoka kwa Mhifadhi Mkuu wa Kituo cha Mapango ya Amboni, Jumanne Gekora kuhusu kivutio cha utalii cha umbo la asili la ramani ya Afrika alipotembelea mapango hayo jana Jijini Tanga. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo kuhusu asali inayozalishwa na Wakala huyo kupitia shamba la Miti Sao Hill muda mfupi kabla ya kuikabidhi kwa Asha Shaban ambaye ni dada yake na aliyekuwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa riwaya Shaban Robert alipotembelea makumbusho ya mwandishi huyo Jijini Tanga jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi Asha Shaban ambaye ni dada yake na Shaban Robert aliyekuwa mshairi na mwandishi mashuhuri wa riwaya zawadi ya asali inayozalishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS kupitia shamba la Miti Sao Hill alipotembelea makumbusho ya mwandishi huyo Jijini Tanga jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozana na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo kukagua Kituo cha Mapango ya Amboni wakati wa ziara yake ya kikazi Jijini Tanga jana ambapo alisema Serikali itaboresha kituo hicho pamoja na vituo vingine vya Mambo ya Kale ili vichangie zaidi kwenye pato la Taifa. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata maelezo ya namna ya kupanda miti ya Mitiki kutoka Meneja wa shamba la Miti Longuza alipotembelea shamba hilo jana wilayani Muheza Mkoani Tanga. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na wafanyakazi wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi alipotembelea hifadhi hiyo jana mkoani Tanga. 

Wednesday, February 21, 2018

DK. KIGWANGALLA AAGIZA JUMUIYA YA HIFADHI YA WANYAMAPORI WAMIMBIKI IPANDISHWE HADHI KUWA PORI LA AKIBA


Na Hamza Temba - WMU-Bagamoyo, Pwani
....................................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudence Milanzi kuanzisha mchakato wa kisheria wa kupandisha hadhi Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Wamimbiki kuwa Pori la Akiba ili iweze kuhifadhiwa vizuri baada ya kushindwa kujiendesha.

Ametoa agizo hilo leo mkoani Pwani baada ya kutembelea eneo la Jumuiya hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua shughuli za uhifadhi katika eneo hilo ambalo ndani yake pia kuna mapito ya wanyamapori.

Dk. Kigwangalla amechukua uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa jumuiya hiyo ikiwemo tuhuma walinzi wake kutoka katika vijiji vinavyounda jumuiya kujihusisha na vitendo vya ujangili. Hata hivyo alipokea ombi la Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Omari Tofiki ambaye aliiomba Serikali ichukue jukumu la kulinda hifadhi hiyo kwa asilimia 100.

"Sisi kama jamii tumeshindwa, tunaomba msaada wa Serikali, itusaidie kuondoa hawa wavamizi na ikiwezekana ichukue jukumu la kulinda hifadhi hii kwa asilimia 100," alisema Tofiki.

Alisema jumuiya hiyo ambayo ni muunganiko wa vijiji 24 inakabiliwa na changomoto kubwa ya ujangili uliokithiri ambao umepelekea kuuwawa kwa wanyamapori zaidi ya asilimia 90 ya waliokuwepo tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo mwaka 1997.

Alisema changamoto nyingine ni kukosekana kwa muwekezaji na mapato ya kujiendesha, uvamizi wa mifugo ndani ya hifadhi hiyo na majungu yanayosababishwa na baadhi ya wananchi na viongozi wanaonufaika na vitendo vya ujangili na uharibifu wa hifadhi hiyo.

Dk. Kigwangalla alisema jumuiya hiyo imefeli katika kila eneo jambo ambalo linalazimu kuanzishwa kwa mchakato wa kuirudisha Serikalini ili iweze kuhifadhiwa vizuri. Alitoa wito kwa viongozi wa Wilaya na vijiji kuanza kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kupandishwa hadhi jumuiya hiyo kwa faida ya pande zote.

"Nimepokea maombi mengi ya kuongeza idadi ya wanyamapori katika hifadhi ya Saadan, tatizo kubwa hapa ni kwamba wanyamapori wanapotoka nje ya hifadhi hiyo na kupita kwenye eneo la Wamimbiki wanavunwa na majangili ambao wengi wao wanasuply (wanasambaza) nyamapori Jijini Dar es Salaam," alisema Dk. Kigwangalla akielezea umuhimu wa kupandishwa hadhi hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Abraham Julu amesema Serikali imekuwa ikisaidia katika ulinzi wa eneo la jumuiya hiyo kwa kushiriki kwenye doria mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kuondoa makazi ndani ya hifadhi hiyo.

Alisema eneo hilo ni muhimu sana kwa uhifadhi wa wanyamapori kwa kuwa ni moja ya eneo la mazalia ya wanyamapori na shoroba nne (mapito ya wanyamapori) zinazounganisha hifadhi ya Taifa ya Saadan, Mikumi na Pori la Akiba la Selous.

Katika hatua nyingine baada ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Saadan, Dk. Kigwangalla ameuagiza uongozi wa TANAPA kupitia hifadhi hiyo kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Bagamoyo na vijiji kuweka utaratibu maalum utakaowawezesha wananchi kupita katika barabara zilizopo ndani ya hifadhi hiyo kwa ajili ya shughuli za kijamii ikiwemo kuwatengenezea vitambulisho maalum.

Ametoa agizo hilo kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa kwake na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete kuwa wananchi wake wanazuiliwa kutumia barabara hizo kwa madai ya kushiriki kwenye vitendo vya uharibifu wa hifadhi hiyo.


Amewataka pia viongozi wa hifadhi hiyo ya pekee barani Afrika ambayo ipo katika fukwe za bahari ya Hindi kuwa wabunifu zaidi kwa kuanzisha bidhaa mpya za utalii ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa zilizopo. Alisema hifadhi hiyo ambayo ipo karibu na Jiji la Dar es Salaam na Tanga ni fursa nzuri kwa watalii kutumia ukaribu huo kuweza kuwaona wanyamapori mbalimbali wakiwemo Simba, Twiga na Tembo pamoja na utalii wa fukwe.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na uongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Wamimbiki wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga.

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Wamimbiki wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na wafanyakazi wa Hifadhi ya Taifa ya Saadan wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uhifadhi wa TANAPA, Martin Loibooki. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akioneshwa mazingira ya Hifadhi ya Taifa ya Saadan na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Stephano Msumi wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya hifadhi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadan katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana. Katikati ni Mkurugenzi wa Uhifadhi wa TANAPA, Martin Loibooki. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akioneshwa mazingira ya fukwe ya Hifadhi ya Taifa ya Saadan na Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya hifadhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Jana.
Picha ya pamoja

Tuesday, February 20, 2018

DKT. KIGWANGALLA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA BODI YA UTALII (TTB)

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na uongozi wa bodi hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
...........................................................................

Waziri wa Maliasili na Utaliii, Dkt. Hamisi Kigwangalla leo Februari 20, 2018, amefanya ziara ya kushtukiza katika ofisi za Makao makuu ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Jijini Dar es Salaam na kuitaka kufanya kazi kwa kasi na ubunifu zaidi.

Akizungumza na viongozi wa Bodi hiyo, Dkt. kigwangalla amewataka kuongeza kasi zaidi katika kutangaza Utalii wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuanzisha studio ya kimataifa ya kutangaza vivutio vya Tanzania ndani na nje ya nchi kwa kutumia lugha mbalimbali za Kimataifa.

Aidha,amewataka kuharakisha zoezi la uwekaji wa mabango yanayotangaza Utalii wa Tanzania katika viwanja vya ndege hususani uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam (JNIA).

Hata hivyo amewataka pia kujikita zaidi katika matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kuhakikisha inahuishwa mara kwa mara.

Pamoja na hayo, ameiagiza bodi hiyo, kushirikisha wadau mbalimbali wanaotoa huduma za Utalii ikiwemo madereva taxi na Marubani kwa kuwapa elimu ya kutangaza utambulisho wa Tanzania kupitia Utalii na vivutio vilivyopo.

Akiwa katika ofisi hizo ndani ya jengo la Utalii House, alikagua ofisi mbalimbali za bodi hiyo pamoja na zile za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na kupata maelezo machache kutoka wa maafisa wa Shirika hilo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na uongozi wa bodi hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Devetha Mdachi kukagua mazingira ya ofisi hiyo mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Devetha Mdachi kukagua mazingira ya ofisi hiyo mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na uongozi wa bodi hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza mapema leo tarehe 20 Februari, 2018.