slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Sunday, January 31, 2016

KUTOKA BUNGENI

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akiteta jambo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa bungeni hivi karibuni.

Saturday, January 30, 2016

SAD NEWS: MAJANGILI WATUNGUA HELIKOPTA NA KUUA RUBANI WAKE PORI LA MASWA MKOANI SIMIYU...

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akikagua helkopta hiyo.


Watu wanaodaiwa kuwa ni majangili na wawindaji haramu wameitungua kwa risasi helkopta ya doria ya wanyamapori katika pori la akiba la maswa lililoko wilaya ya Meatu mkoani Simiyu kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kumuua rubani wa helkopita na kumjeruhi askari mmoja wa wanyamapori.

Kufuatia tukio hilo, waziri wa maliasili na utalii Profesa Jumanne Maghembe amefika katika eneo la tukio na kusisitiza kwamba serikali kwa kushirikiana na vyombo vyote vya dola na vyombo vya ulinzi na usalama inaanzisha mkakati mpya wa kupambana na ujangili na uwindaji haramu wa maliasili ikiwemo Tembo ambao ni rasilimali muhimu kwa taifa.

Waziri Maghembe amefika kwenye eneo husika na kushuhudia tukio hilo la kihalifu lililosababishwa na Majangili ambapo amesema tukio hilo limewakera wadau wote wa uhifadhi na serikali kwa ujumla na kamwe haliwezi kuachwa lipite bila hatua madhubuti kuchukuliwa. 

Nae kamanda wa upelelezi wa mkoa wa Simiyu Jonathan Shana amesema tukio hilo lilitokea jana jioni wakati helkopita hiyo ikiwa katika doria baada ya kusikika milio ya risasi ya majangili katika pori hilo ambapo ulionekana Mzoga waTembo mmoja uliosemakana kuuwawa na Majangili hao.

Hili ni tukio la kwanza  katika historia ya uhifadhi hapa nchini kwa Majangili kushambulia helkopta ya doria na kusababisha mauaji ya Rubani.

 Kapteni Roger Gower raia wa Uingereza alikuwa akienda kuongeza nguvu ya askari wa uhifadhi waliokuwa wakipambana na majangili hatari wilayani Meatu, Simiyu katika ranchi ya wanyamapori ya Mwiba.

Monday, January 25, 2016

KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII MAJ. GEN. GAUDENCE MILANZI AONGOZA KIKAO CHA KAMATI YA UWEZESHAJI UTALII NCHINI TFC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Generali Gaudence Milanzi (kulia) akizungumza kwenye Mkutano wa Kamati ya Uwezeshaji Utalii (Tourism Facilitation Committee- TFC) uliofanyika hivi karibuni Mpingo House Jijini Dar es Salaam. Wapili kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utalii Leseni na ubora wa huduma Bw. Deogratius Mdamu.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi (kulia) akizungumza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya Wajumbe wa kamati ya Uwezeshaji Utalii (Tourism Facilitation Committee- TFC) ambao walikutana kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Utalii nchini kwa kutoa maoni, ushauri na ufumbuzi wa changamoto ikiwa na kuchangia mikakati mbalimbali itakayowezesha kusaidia kuhamasisha Utalii wa ndani.

.....................................................................................................

Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau wa utalii nchini, imejipanga kuhakikisha inaendelea kukuza utalii wa ndani ambao utakua na uhakika zaidi wa kuliingizia taifa mapato tofauti na hivi sasa ambapo utegemezi upo kwa watalii kutoka nje ya nchi ambapo wakati mwingine hupelekea uhaba kutokana na athari za majanga ya kimataifa.

Baadhi ya Majanga hayo yaliyoathiri Sekta ya Utalii katika kipindi cha hivi karibuni ni milipuko ya magonjwa kama Ebola, matukio ya Ugaidi nchini Kenya na kushuka kwa thamani ya Euro ya Ulaya dhidi ya Dola ya Marekani.

Akizungumza kwenye Mkutano wa Kamati ya Uwezeshaji Utalii ijulikanayo kama Tourism Facilitation Committee (TFC) uliofanyika hivi karibuni Mpingo House jijini Dar esSalaam, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja. Generali. Gaudence Milanzi amesema maendeleo ya Utalii yanahitaji sana Utalii wa ndani kuimarika badala ya kudhani kuwa vivutio vya utalii vilivyopo ni kwa ajili ya wageni kutoka nchi za nje.

Meja Generali Milanzi amesema Utalii ni sekta nyeti sana katika kuliingiza Taifa pesa za kigeni lakini hata hivyo ni sekta ambayo imekuwa inaathirika kwa haraka sana pindi majanga yanapotokea nchi jirani hivyo ni lazima jamii ijengewe utamaduni wa kutembelea vivutio vya Utalii ili kuweza kujihakikishia Watalii wa ndani wanakuwa wengi.

Baadhi ya mikakati iliyopendekezwa na Wajumbe wa kamati ya Uwezeshaji Utalii (TFC) ni kuwawezesha maafisa Utalii wa Halmashauri wanatengewa bajeti ya kutosha, wanajengewa uwezo kuhusu ya vivutio vya utalii vilivyopo kwenye maeneo yao pamoja na Idara ya Utalii kufungua ofisi kila kanda ili kuweza kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Mkakati mwingine uliopendekezwa ni kwa viwanja vya ndege vilivyopo nchini kuimarishwa ikiwa ni pamoja na nchi kuwa na ndege zake kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya na Rwanda.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi alisema Mkutano wa TFC hutoa fursa ya kuibua na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Utalii hivyo Sekta Binafsi zinawajibu mkubwa wa kuhakikisha changamoto zinazoikabili sekta zinatafutiwa ufumbuzi

Aliongeza kuwa Idara ya Utalii imekuwa ikishiriki katika maonesho mbalimbali ya kitaifa lengo likiwa ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutembelea vivutio vya Utalii nchini.

Mdau wa Utalii, Prof Wineastor Anderson amesema sekta ya Utalii imekuwa ikikua lakini si kwa kiwango cha kuridhisha hivyo jitihada za kutangaza utalii ndani na nje nchi upewe uzito unaostahili kwa kuiwezesha Bodi ya Taifa ya Utalii kuwa na bajeti ya kutosha kujitangaza ndani na nje ya nchi.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya Utalii Tanzania (TCT) Bw. Richard Rugimbana, amesema Utalii wa ndani ili uweze kukua suala la elimu linahitajika kutolewa ili kuweza kuibadilisha jamii ipende kutembelea vivutio vya Utalii vya ndani ya nchi.


Kwa upande wake Kamanda wa Polisi (ACP) Ndaki anayeshughulikia dawati la Utalii (Tourism Police Unit) amewahakikishia usalama watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea vivutio vya Utalii bila kuwa na hofu yoyote kwa kuwa Jeshi la Polisi nchini lipo macho muda wote.

Tuesday, January 19, 2016

KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII MAJ. GEN. GAUDENCE MILANZI AONANA NA KUNDI LA WASHIRIKA WA MAENDELEO KATIKA SEKTA YA MAZINGIRA, MALIASILI NA MABADILIKO YA TABIA NCHI (DPG-E) JIJINI DAR ES SALAAM LEO

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Generali Gaudence Milanzi (kulia) akizungumza na viongozi wa Kundi la Washirika wa Maendeleo katika sekta ya Mazingira, Maliasili na Mabadiliko ya Tabia Nchi (Development Partners Group on Environment, Natural Resources and Climate Change (DPG-E) walipoonana leo tarehe 19 Januari, 2016 katika ukumbi wa Selous uliopo makao makuu ya Wizara hiyo Mpingo House. Kundi hilo liliomba kuonana na Katibu Mkuu huyo kwa ajili ya utambulisho na kujadili mambo muhimu ya maendeleo katika sekta hiyo.
 
Bi. Lena Thiede (kushoto) kutoka ubalozi wa Ujerumani ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Shirikisho la Kikanda Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kutoka Kundi la Washirika wa Maendeleo katika sekta ya Mazingira, Maliasili na Mabadiliko ya Tabia Nchi (DPG-E) akizungumza katika kikao hicho ambapo alielezea kazi ya Kundi hilo kuwa ni kuandaa mijadala maalum ya kisera na Serikali pamoja na wadau wengine wa maeneo husika, kuratibu miradi na mipango ya kundi hilo na kuhamasisha mawasiliano na utetezi wa pamoja baina yake na Serikali na wadau wengine katika sekta hizo. Katikati ni Bi. Clara Makenya kutoka UNEP ambaye ni Mratibu wa Kitaifa wa Kundi hilo na Bw. Steven Nyagondi Sekretarieti ya Kundi hilo. 
 Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Generali Gaudence Milanzi (wa pili kushoto) akiongoza mazungumzo katika kikao hicho. Katika mazungumzo hayo Meja Generali Milanzi amewaomba wadau hao na wadau wengine wa Maliasili kuungana pamoja katika kuhifadhi Maliasili za Tanzania ikiwemo vita dhidi ya biashara haramu ya Maliasili za Taifa, Ujangili na uharibifu wa misitu. Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Anjelina Madete.
Kutoka kulia ni Mkurugenzi Idara ya Utalii Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Zahoro Kimwaga, Bw. Herman Keraryo (katikati) Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori na Bw. Donatius Kamamba Mkurugenzi Idara ya Mambo Kale ambao wameshiriki katika kikao hicho.
 
Bwana Bernad Lubogo (kulia) Kaimu Mkurugenzi (Mipango na Bajeti) Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Maliasili na Utalii akichangia jambo katika kikao hicho, Wengine ni Bi. Bertha Nyange (Katikati) Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sera na Mipango na Bw. Joseph Sendwa Katibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Dorina Makaya.

Wednesday, January 6, 2016

KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII MEJA JENERALI GAUDENCE MILANZI AKABIDHIWA OFISI RASMI NA ALIYEKUWA KATIBU DKT. ADELHELM MERU

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi (kulia) akikabidhiwa taarifa ya makabidhiano ya ofisi tarehe 04 Januari 2016 na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru (kushoto) ambaye kwa sasa amehamishiwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Picha ya pamoja kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi (wa pili kulia), Katibu Mkuu aliyepita kabla yake, Dkt. Adelhelm Meru (wa pili kushoto) ambae kahamishiwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Naibu Katibu Mkuu, Bi. Anjelina Madete (wa kwanza kulia) muda muda mfupi baada ya makabidhiano hayo. Wengine ni Bi Mariam Malunga (katikati) Katibu Muhtasi na Bi. Judith (wa kwanza kushoto) Msaidizi wa Ofisi.

Tuesday, January 5, 2016

WAZIRI WA MALIASILI PROF. JUMANNE MAGHEMBE AMSIMAMISHA KAZI MKURUGENZI WA MIPANGO WA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS) NA MAOFISA MISITU WA MIKOA YOTE NCHINI LEO

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza katika kikao na Idara ya Misitu na Nyuki pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika ukumbi wa Ngorongoro Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam leo tarehe 05 Januari, 2015. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza katika kikao na Idara ya Misitu na Nyuki pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika ukumbi wa Ngorongoro Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam leo tarehe 05 Januari, 2015.
 Kamu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Nyuki Bi. Gladnes Mkamba (wa pili kulia) akiwasilisha taarifa ya Idara yake kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe wa (pili kushoto) katika kikao hicho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Juma Mgoo (kulia) akiwasilisha taarifa ya ofisi yake kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kulia).  
 Sehemu ya wajumbe wa kikao hicho wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe.
 Sehemu ya wajumbe katika kikao hicho. 
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi (wa pili kulia) akizungumza katika kikao hicho.

......................................................................................................


Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Mohammed Kilongo na Maofisa wa Misitu wa Mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.


Akizungumza leo na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema agizo hilo limekuja kutokana na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.


Ameagiza pia maofisa hao wote wanaokusanya maduhuri ya Serikali katika Wilaya watumie muda wa siku kumi kuanzia leo kuhakikisha maduhuri yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Wale district forestry officers wote wapeleke vitabu vyao wanavyokusanyia maduhuri ya Serikali kwenye ofisi za Kanda, Naibu Katibu Mkuu tusaidie kuwasiliana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali ifanye ukaguzi wa vitabu hivyo ndani ya siku kumi tuhakikishe fedha zinazotakiwa zinaingia kwenye mfuko wa Serikali, Mtu anakusanya fedha  ya Serikali toka mwaka 2004 mpaka leo hajapeleka benki ananeemesha hali yake ya nyumbani, hili hapana”. Alisisitiza Prof. Maghembe.
Kwa mujibu wa Waziri Maghembe Bw. Mohammed Kilongo ambaye Idara yake ndiyo inatoa vitabu kwa ajili ya kukusanya maduhuri ya Serikali katika Mikoa yote na Wilaya zote nchini analazimika kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi ambapo ukikamilika sheria itachukua mkondo wake bila uonevu wowote.  
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amewaagiza pia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kutumia muda wa siku saba kurudi katika jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii maarufu kama Mpingo House ambalo walihama mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka jana na kwenda kupanga katika jengo la NSSF Mafao House lililopo Ilala.
“Wakati tunajenga nyumba hii hapa, tumejenga jengo hili ni kama jengo la misitu ndio maana linaitwa Mpingo House kwa maana ni jengo la Misitu, ninyi wenyewe mmejenga jengo kubwa hili mmemaliza mmehama, Naagiza jumatatu Januari 11 muwe mmesharudi katika jengo hili, ghorofa ya tatu nikija kukagua niwakute, haiwezekani mueleze matatizo yote mliyonayo muhame nyumba ya Serikali mkapange jengo hapo jirani” Alisema Prof. Maghembe.
Katika hatua nyingine ya kuboresha uhifadhi wa Misitu nchini Waziri Maghembe ameiagiza Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili kuhakikisha inajiimarisha katika lengo lake kuu la uhifadhi kwa kushirikiana na wadau wanaohusika kuhakikisha Mamlaka iliyolengwa ya Uhifadhi Misitu inakamilika.
“Tunataka tutoke kwenye Wakala wa Huduma za Misitu (Tanzania Forestry Services Agency) twende kwenye Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu (Tanzania Forestry Services Authority) ili tuweze kufanya vizuri zaidi kwenye eneo la uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini, Katibu Mkuu tunaomba pia usaidie kufanikisha hili” Alisema Prof Maghembe.
Aliongeza kuwa wakati wa kuundwa Mamlaka hiyo ni vizuri pia Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili ikatenganishwa na kila moja kuwa Idara kamili kutokana na umuhimu wa kila sekta katika kujenga uchumi wa nchi kwa kutoa fursa ya kuboresha maeneo hayo na kuongeza pato la taifa.
Ameitaka pia Idara ya Misitu na nyuki kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhakikisha kuwa inaongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuziba mianya yote ya ubadhilifu pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vilivyopo.
Akizungumzia mchango wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwenye pato la taifa Mtendaji Mkuu, Bw. Juma Mgoo amesema katika mwaka huu wa fedha TFS imeweka makisio ya kukusanya Tsh. Bilioni 88 ambapo mpaka hivi sasa wameshakusanya zaidi ya asilimia 52 ya makisio hayo.
Waziri Maghembe akizungumzia kuhusu uvamizi kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba amewataka wananchi wote waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa kwa ajili ya kuchunga mifugo waondoke ndani ya siku saba zijazo, na wale walivamia mapori ya akiba kwa shughuli za kilimo na ufugaji waondoke ndani ya miezi mitatu ijayo.
 "Serikali itawaondoa kwa nguvu wasipotekeleza agizo hili la kuondoka katika maeneo ya hifadhi za taifa na kwenye mapori ya akiba yaliyohifadhiwa” Alisisitiza Prof. Maghembe.
Akizungumzia kuhusu biashara ya Mkaa, Prof. Maghembe amewaagiza wataalamu wa Idara ya Misitu kusimamia biashara ya mkaa kwa kuzingatia taratibu na sheria ikiwa ni pamoja na kuzuia usafirishaji wa Mkaa nje ya nchi.
Ameongeza kuwa nishati ya Mkaa ni muhimu lakini Tanzania ina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe ambapo ameitaka Idara ya Misitu kwa kushirikiana na wadau wengine kuona ni namna gani ya kuweza kutumia mbadala huo kwa kuzalisha makaa hayo ya mawe kwa matumizi ya kawaida ili kuokoa misitu nchini.  
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Waziri yatafanyiwa kazi kwakuwa lengo lake ni kuona dhamira ya msingi ya Serikali ya awamu ya tano inafikiwa ya kubana matumizi, kuongeza mapato ya Serikali na kuhifadhi maliasili za taifa ikiwemo misitu.