slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Tuesday, January 30, 2018

SERIKALI YAINGIZA MIL 30.9 KUPITIA MAUZO YA MENO YA VIBOKO

No automatic alt text available.
Serikali imepata mapato ya Shilingi Milioni 30.9 kupitia mauzo meno ya viboko vipande 12,467 vyenye uzito wa kilo 3,580.29 ambayo yameuzwa kupitia mnada wa hadhara uliofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Maliasili na Utalii katika Jengo la Mpingo Jijini Dar es Salaam.

Mnada huo ulioratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango ulijumuisha makampuni 19 yenye Leseni za Nyara Daraja la Kwanza ambapo kampuni ya On Tours Tanzania Limited iliibuka mshindi kwa kutoa dau la Shilingi milioni 30.9.

Mwakilishi wa kampuni hiyo, Grey Kilas alilipa asilimia 25 papo hapo kwa mujibu wa masharti ya mnada huo na kuahidi kulipa asilimia 75 ya kiasi kilichobakia ndani ya siku 14 zijazo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA, Mabula Misungwi alisema biashara hiyo haiwezi kuchochea ujangili kwa vile meno hayo yanauzwa kwa wafanyabiashara maalum wenye leseni za nyara daraja la kwanza.

Mabula alisema meno hayo yalianza kukusanywa tangu mwaka 2004 ambapo kipindi cha huko nyuma yalikuwa yakiuzwa kwa makampuni yenye leseni za nyara kwa utarartibu tofauti na ulioanza kutumika mwaka huu ambao ni kupitia mnada wa hadhara.

Naye Mwakilishi wa Kampuni iliyonunua meno hayo, Grey Kilas aliwashukuru wasimamizi wa mnada huo kwa kuuendesha kwa uwazi wa hali ya juu ambapo ulitoa fursa kwa kila mfanyanyabiashara hatimaye ukamuwezesha kuibuka mshindi.

Akizungumzia kuhusu soko, Kilas alisema meno hayo huuzwa nchini Japan, Marekani na Hongkong ambapo hutumika kutengeneza mapambo, sanamu pamoja na vishikizo vya nguo.

Kwa mara mwisho biashara hiyo ya kuuza meno ya viboko ilifanyika mwaka 2004.
Image may contain: food


Monday, January 29, 2018

DK. KIGWANGALLA AWATAKA WALIOVAMIA KIWANJA CHA MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO KILICHOPO NJIRO, JIJINI ARUSHA KUJIANDAA KISAIKOLOJIA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akipata maelezo ya eneo la kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha ambacho kimevamiwa na watu mbalimbali na kuanzishwa makazi yenye kaya 82 ndani ya eneo hilo kutoka Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Dk. Fredy Manongi (katikati). Eneo hilo ni mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na hati halisi ya eneo hilo ipo kwa jinala Bodi ya Utalii Tanzania. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua eneo la kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha ambacho kimevamiwa na watu mbalimbali na kuanzishwa makazi yenye kaya 82. Eneo hilo ni mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na hati halisi ya eneo hilo ipo kwa jinala Bodi ya Utalii Tanzania.
  Meneja wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Egidius Mweyunge (kulia) akimuongoza Waziri Kigwangalla kukagua eneo hilo.
Dk. Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua eneo hilo.

Sunday, January 28, 2018

DK. KIGWANGALLA AKAGUA KIWANJA CHA MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO KILICHOVAMIWA JIJINI ARUSHA, AWATAKA WAVAMIZI KUDAI HAKI YAO KWA ALIYEWAPA ENEO HILO

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akipata maelezo ya eneo la kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha ambacho kimevamiwa na watu mbalimbali na kuanzishwa makazi yenye kaya 82 ndani ya eneo hilo kutoka Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Dk. Fredy Manongi (katikati). Eneo hilo ni mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na hati halisi ya eneo hilo ipo kwa jinala Bodi ya Utalii Tanzania. 

Na Mwandishi Wetu
........................................................
Waziri wa Malisili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla leo Januari 28, 2018 amekagua eneo la kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha ambacho ni mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kinachodaiwa kumegwa na kuuzwa kinyume cha sheria kwa watu mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu ambaye hata hivyo hakumtaja jina lake.

Akiwa katika eneo hilo, Waziri Kigwangalla amepokea taarifa kutoka kwa Meneja wa Huduma za Sheria wa mamlaka hiyo, Egidius Mweyunge ambaye alieleza kuwa, jumla ya hekta 20 (ekari 40) za eneo zilinunuliwa na mamlaka hiyo na kulipiwa Shilingi bilioni 1.8 kwa kamishna wa ardhi Mwaka, 2006 baada ya kuona tangazo la kuuzwa kwa eneo hilo kupitia gazeti la Serikali.

Alisema hata hivyo baada ya manunuzi hayo, Halmashauri ya Manispaa ya Arusha iliingilia na kumega hekta 10 (ekari 20) ambazo waliuziwa watu mbalimbali ambapo hadi hivi sasa eneo hilo lina kaya 83 zinazoishi watu.

"Mwaka 2016, tulipokagua eneo hili, tulibaini ni hekta 10 tu zilizobaki kutoka zile 20, na tulipouliza Halmashauri ya Manispaa ya Arusha walisema eneo ili liligawanywa toka 1996 na kupewa Kaya hizo 83. Lakini kwa upande wa Kamishna wa Ardhi, kule Moshi Title iliyopo ni moja tu, tukajikuta kumbe kitu tulichokinunua hakikuwa ekari 40, ni ekari 20 tu na hapo ndipo tuliporejea kwenye mgogoro", alisema Mweyunge.

Hata hivyo, Waziri Kigwangalla alieleza kuwa hapo hakuna mgogoro na zaidi ni kutaka kujua hao waliochukua hizo hekta 10, ni akina nani na walizipata kwa nani kupitia utaratibu gani.

"Hapa hakuna kumukunya maneno. hao wote hati zao ni feki na hazina msingi wowote kama Kamishna anatambua hati yenu, hao wengine wapishe na waende wakamdai huyo aliyewauzia hayo maeneo.

“Eneo hili lirudi kwa Mamlaka ya Ngorongoro na Bodi ya Utalii wao watatafutiwa eneo jingine. Watu hao kwenye hizo kaya 83 waliochukua hizo hekta 10, waende wakamdai aliyewapa hizo Hati kwa hiyo sisi hatuna mgogoro wowote kwakuwa hakuna mamlaka nyingine inayoweza kutoa hati zaidi ya Kamishna wa Ardhi. Hao Halmashauri hawana mamlaka ya kutoa hati kwa mtu kama si Kamishina wa Kanda kule Moshi" alieleza Dk. Kigwangalla.

Aidha, Dk.Kigwangalla  aliwataka wote waliojenga eneo hilo wakadai fidia kwa halmashauri husika kwani mwenye mamlaka ya kutoa hati ni Kamishna wa Ardhi na si halmashauri. Alisemwa kwa taarifa ambazo hazijathibitishwa eneo hilo waligawana Mawaziri wastaafu ambao walitumia mamlaka zao vibaya wakiwa madarakani na maafisa wa mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na halmashauri kufoji hati.

Akijibu maswali ya waandishi wa Habari waliokuwa wakitaka kujua ni Mawaziri gani hao, Waziri Dk. Kigwangalla amesema kuwa, ametoa wito kwa wote waliuziwa maeneo hayo kupeleka hati zao kwa Kamishina wa Ardhi na hapo watabainika majina yao na watachukuliwa hatua kama watenda makosa wengine.

Kabla ya kununuliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na taasisi ya Serikali ambayo ni kampuni tanzu ya Bodi ya Utalii Tanzania iliyokuwa inajulikana kama Serengeti Safari Lodges.

Hivi karibuni, Waziri huyo akiwa Mjini Dodoma, alitoa ilani ya siku 30 kwa mtu yeyote ambaye anamiliki kiwanja ndani ya eneo hilo kufika kwa Kamishina Mkuu wa Ardhi waweze kuhakikiwa na kuthibitisha umiliki wao halali ama sivyo wavirejeshe Serikalini viweze kumilikishwa kwa mmiliki wake halali. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua eneo la kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha ambacho kimevamiwa na watu mbalimbali na kuanzishwa makazi yenye kaya 82. Eneo hilo ni mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na hati halisi ya eneo hilo ipo kwa jinala Bodi ya Utalii Tanzania.
  Meneja wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Egidius Mweyunge (kulia) akimuongoza Waziri Kigwangalla kukagua eneo hilo.
Dk. Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua eneo hilo.

Saturday, January 27, 2018

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUBORESHA MAKUMBUSHO YA KUMBUKIZI YA NYUMBA YA MWL. NYERERE - DK. KIGWANGALLA


.............................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk.Hamisi Kigwangalla ametembelea Makumbusho ya Kumbukizi ya Nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo Magomeni, Mtaa wa Ifunda Namba 62, Jijini Dar es Salaam na kuagiza kuanzishwa kwa mradi mahsusi wa kuboresha makumbusho hiyo.

Alisema mradi huo utahusisha kununua nyumba za jirani na pia kufanya mazungumzo na ofisi ya Kata ya Mzimuni, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ili kupata eneo la maegesho ya magari la kisasa, eneo la kujenga kituo cha taarifa na Maktaba, lengo ikiwa ni kuboresha mandhari ya kituo hicho iendane na uzito wa jina na heshma ya baba wa Taifa. 

"Hii ni nyumba aliyoishi baba wa Taifa letu, Mwl. Julius Nyerere mwaka 1959 alipoacha kazi ya ualimu Pugu ili kupata muda zaidi wa kuendeleza harakati za kusaka uhuru wa Tanganyika. Tumedhamiria kuiboresha na kuitangaza zaidi kama kivutio muhimu cha utalii.

"Nimefika hapa leo kujionea Kituo hichi ambacho ni kielelezo kikubwa cha Mwasisi wa Taifa letu. Hapa pana hazina kubwa na kituo hiki kina mambo mengi sana ya kumuenzi Baba wa Taifa. Kwa hali tuliyoikuta kwa kweli tutakaa na timu yangu kuona tunafanya maboresho makubwa kabisa ili kiwe kama maeneo mengine ya waasisi wa Mataifa yao, kama eneo alilozaliwa Mzee Mandela kule Afrika Kusini, nyumba yake imehifadhiwa vizuri na imekuwa ikitembelewa na wageni wengi.

"Kwa hapa kwetu na sisi tutakaa na wenzetu kutatua changamoto hizi. Hapa tutajenga Maktaba ambapo watu watakuja kusoma vitabu vya Mwasisi wetu na kuona mambo aliyokuwa akifanya. Lakini pia tutaonana na Viongozi wa Halmashauri ya Kinondoni kuona namna ya kupaboresha mahala hapa ikiwemo miundombinu ya Barabara ya kuingia na kutoka eneo hili" alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema maboresho mengine makubwa yatakayofanywa katika nyumba hiyo ni pamoja na kutengeneza choo, kupaka rangi na kufanya maboresho ya vionyeshwa vya kumbukumbu nzima ya Baba wa Taifa vilivyopo ndani ya nyumba hiyo ikiwemo kukuza picha na kuzijengea fremu za kisasa.

"Kiuhalisia hapa ni hazina kubwa sana ya kumbukumbu ya Taifa letu hasa katika harakati za kupigania Uhuru ambazo zilianzia hapa katika nyumba hii. Tutaiboresha zaidi kwa kuweka studio maalumu, tutaboresha CD zote za Baba wa Taifa na zitakuwa zikioneshwa humo ikiwemo zile za Hotuba zake," alisema Dk. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Makumbusho hiyo, Neema Mbwana alisema changamoto zilizopo ni uchakavu wa nyumba hiyo na vioneshwa vilivyopo ambapo ameiomba Serikali kuboresha madhari ya nyumba hiyo na vioneshwa vyake ikiwemo kuzalisha nakala za kutosha za vitabu ambavyo ni mali ya baba wa taifa kutokana na kukabiliwa na uchakavu mkubwa.

Mbali na kutembelea Makumbusho hiyo, Dk. Kigwangalla pia alitembelea eneo la Mwenge wanapochonga na kuuza vinyago vya Makonde, na eneo la Oysterbay Morogoro Store wanapochora na kuuza picha za Sanaa ya Tingatinga.

 "Tingatinga ni michoro ya miigizo isiyo halisi ya vitu mbali mbali inayochorwa kwa rangi 6 (mara nyingi). Mtu wa kwanza kuchora picha hizi ni marehemu Edward Saidi Tingatinga aliyevumbua uchoraji huu mwaka 1968 na kufanya kazi hiyo mpaka 1972 alipofariki. 

"Sanamu za Makonde na picha za Tingatinga ni utambulisho mkubwa wa Sanaa ya Mwafrika nje ya bara letu na huvutia watalii wengi. Katika mikakati tuliyonayo ya kuongeza faida zinazotokana na utalii kwa wananchi tunakusudia kuboresha biashara kama hizi," alisema Dk. Kigwangalla. 
Muhifadhi Mkuu wa Makumbusho nyumba ya Nyerere iliyopo Magomeni Jijini Dar es Salaam, Bi. Neema Mbwana akisoma taarifa za kituo hicho kwa Waziri Dk Kigwangalla alipotembelea kituoni hapo mapema leo Januari 26,2018.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisaini kitabu cha Wageni alipowasili kituoni hapo.
Dk. Kigwangalla akitazama baadhi ya picha mbalimbali za Baba wa Taifa ambazo zipo nyumbani hapo.
Sehemu ya nyumba hiyo.
Mhifadhi Neema Mbwana akimuonesha Waziri Dk. Kigwangalla nyuma ya nyumba hiyo na eneo lilivyo.
Dk. Kigwangalla akiangalia kitanda alichokuwa akikitumia Baba wa Taifa wakati akiishi kwenye nyumba hiyo.
Dk. Kigwangalla akiangalia moja ya vitanda vilivyokuwa vikitumiwa na watoto wa Baba wa Taifa wakati akikaa hapo. (Chumba cha watoto wa Baba wa Taifa walitumia).
Dk. Kigwangalla akiangalia moja ya vinyao vyenye umbo tofauti ambavyo vimekuwa vikitumika sana katika maofisi za Serikali na mashirika ikiwemo Balozi.
Dk. Kigwangalla akiangalia moja ya kinyago cha Umoja abacho kinaelezea taswira mbalimbali ikiwemo hali ya uhifadhi wa hifhadhi za Taifa katika nyanja za Ulinzi wa wanyama.
Akiwa katika Eneo la Vinyago Mwenge, Dk. Kigwangalla alipata wasaha wa kushuhudia baadhi ya bidhaa hizo ambazo pia zimekuwa ni kielelezo kikubwa cha watalii.
Dk.Kigwangalla akiangalia moja ya kinyago kikubwa chenye taswira ya Kimbunga.
Mkurugenzi wa Mipango na matumizi endelevu ya misitu na nyuki nchini, Mohamed Kilongo (kulia) akimwelezea jambo Waziri Dk.Kigwangalla namna wanavyoshughulikia suala la Wachongaji vinyago hao haswa katika vibali vya miti.
Dk.Kigwangalla akimsikiliza kwa makini mmoja wa wachonga vinyago ambao walilalamikia hali ya kutozwa kwa gharama kubwa katika viwanja vya ndege hasa kwa wageni ambao asilimia kubwa ni watalii.
Dk.Kigwangalla akitoa maelekezo kwa viongozi wa Wachonga Vinyago Mwenge kukaa pamoja ili kuona watakavyoelewana namna ya kumiliki eneo hilo huku akiahidi kushughulikia suala la bidhaa zao zinazotozwa ushuru mkubwa viwanja vya ndege vya hapa nchini.
Dk. Kigwangalla akiangalia moja ya michoro ya picha katika eneo la Tingatinga lililopo Oyster bay Jijini Dar es Salaam.
Dk. Kigwangalla akiangalia moja wachoraji wakongwe wa Umoja wa michoro ya Tingatinga alipotembelea kujionea michoro hiyo eneo la Oyster bay Jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Andew Chale)

Thursday, January 25, 2018

FULL VIDEO: DK. KIGWANGALLA AKITAJA ORODHA YA WATUHUMIWA WA UJANGILIDK. KIGWANGALLA ATAJA ORODHA YA WATUHUMIWA WA UJANGILI LEO MJINI DODOMA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara hiyo Mjini Dodoma leo. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Aloyce Nzuki.

Na Hamza Temba - Dodoma
.........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla leo Januari 25, 2018 mjini Dodoma ametaja majina ya watuhumiwa wa ujangili ambao wengi wao ni wamiliki na washirika wa Kampuni za uwindaji wa kitalii na kuwapa siku saba wawe wamefika kwa hiari yao wenyewe katika ofisi za Wizara hiyo Mjini Dodoma, Swagaswaga House kwa ajili kutoa maelezo kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kujibu tuhuma hiyo na nyingine nyingi zinazowakabili mbele ya kamati atakayoiunda.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Dk. Kigwangalla ametaja baadhi ya tuhuma hizo ambazo ziko kinyume cha sheria na taratibu za uwindaji wa kitalii kuwa ni uwindaji haramu, uhawilishaji wa umiliki wa vitalu vya uwindaji pasipo kufuata sheria, udanganyifu kwenye kujaza fomu za uangalizi,  rushwa, uhalifu dhidi ya rasilimali za wanyamapori na uhujumu uchumi.

Alitaja tuhuma zingine kuwa ni ukiukwaji wa kanuni za uwindaji (kupiga wanyama usiku, kuwinda wanyama bila kujali umri, kupiga wanyama nje ya maeneo waliyopewa), kukutolipa tozo mbalimbali za maendeleo za jamii kwenye vijiji jirani na maeneo wanaoendesha biashara ya uwindaji, kushindwa kuendesha ipasavyo shughuli za kuzuia ujangili.

Dk. Kigwangalla aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni ndugu Pasanis na wenzake ambao wanamilikia kampuni ya Berlette Safari Corporation Ltd na Ngugu Shein Ralgi na wakurugenzi wenzake wa kampuni ya Game Frontiers of Tanzania Ltd.

Wengine ni Ndugu Howel na wakurugenzi wenzake wa kampuni ya Mkwawa Hunting Sfaris Tanzania Ltd, Ndugu Thomas Fredikin na wenzake wa Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd, Wengert Windrose Safaris Tanzania  Ltd na Tanzania Game Trackers Safaris Ltd, na Ndugu Awadh na wenzake ambao wanamiliki kampuni ya Uwindaji wa Greenmiles Safaris Ltd.

Aliwataja washirika wengine kuwa ni Ndugu ni Kwizema, Ndugu Robert, Ndugu Solomon Makulu, Ndugu Siasa Shaban, Ndugu Hamis Abdul Ligagabile na mtumishi wa Wizara Wizara ya Maliasili na Utalii, Alex Aguma.

Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla ametoa Ilani ya siku 30 kwa watu mbalimbali ikiwemo Mawaziri Wakuu Wastaafu waliovamia kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha wafike kwa Kamishna Mkuu wa Ardhi waweze kuhakikiwa na kuthibitisha umiliki wao halali ama sivyo wavirejeshe Serikalini viweze kumilikishwa kwa mmiliki wake halali.

“Natoa ilani ya siku 30 kwa mtu yeyote ambaye anajua alivamia kiwanja katika eneo hili ambalo lina hati namba 4091 kilichopo Njiro, Arusha, haraka sana ajipange kupeleka taarifa zake mbele ya Kamishna wa Ardhi kabla hatujachukua hatua nyingine za kisheria, hati iliyoko pale ipo katika jina la Bodi ya Utalii Tanzania japo wao wanadai wana hati nyingine.

“Wengi wao wamejenga nyumba za kudumu katika eneo lile, na wengine ni viongozi waliokuwa mawaziri wakuu wastaafu nao wana viwanja katika eneo hilo na wamejenga nyumba zao katika eneo hilo,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema kiwanja hicho kilichokuwa na ekari zaidi ya 40 kilikuwa kinamilikiwa na taasisi ya Serikali ambayo ni kampuni tanzu ya Bodi ya Utalii Tanzania iliyokuwa inajulikana kama Serengeti Safari Lodges na baadae kikauzwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi nchini kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wanne wanaojihusisha na mtandao wa ujangili pamoja na kupanga njama zilizopelekea mauaji ya Mhifadhi wa Wanyamapori Ndugu Wayne Lotter, raia wa Afrika ya Kusini ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni Pams Foundation, aliyeuawawa eneo la Chole Masaki Jijini Dar es Salaam mwezi Agosti mwaka jana.

“Natoa siku saba kwa wenzetu wa jeshi la Polisi wachukue hatua dhidi ya watu wanne, ambao mimi majina yao ninayafahamu ambao miongoni mwao watatu wanahusika na kuendesha biashara ya ujangili, na ni watu wakubwa, ni matajiri wakubwa na wana mitandao mikubwa ya ujangili.

“Ninafahamu taarifa hizi polisi wanazo lakini hawajachukua hatua za kuwakamata watu hawa na kuwafikisha kwenye macho ya sheria, muda ni mrefu  na sisi wenye taarifa hizi sasa tumeanza kuchoka kusubiri.

“Hawa watu wanne walihusika kupanga njama ambazo zilipelekea kusababisha mauaji ya kikatili ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Palm Foundation, Ndugu Wayle Lotter mwezi Agosti mwaka jana eneo la Chole Masaki mwezi Agosti mwaka jana.

“Nataka ndani ya siku hizi saba wawe wamechukua hatua na kama hawatochukua hatua manaake tutajua wana vested interest (maslahi) kwahivo tutaenda kuripoti kwa Amiri Jeshi mkuu ambaye ni Mhe. Rais aliyetutuma kazi ya kusimamia sekta hii,”. Alisema Dk. Kigwangalla.
 Dk. Kigwangalla akizungumza katika mkutano huo leo mjini Dodoma.

Tuesday, January 23, 2018

SERIKALI KUENDESHA MNADA WA HADHARA WA MENO YA VIBOKO JANUARI 29 JIJINI DAR ES SALAAM

Mnada huo utafanyika katika Jengo hili la Mpingo (Mpingo House) ambalo awali lilikuwa Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuhamia Makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma. 

Na Hamza Temba - WMU- Dodoma
...................................................................

*Wanunuzi wataruhusiwa kuyakagua (Januari 25 na 26) kabla ya mnada

*Watakaovuruga mnada kukiona cha mtemakuni

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) itafanya mnada wa hadhara wa meno ya viboko vipande 12,467 vyenye uzito wa kilo 3,580.29.

Mnada huo utakaosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango umepangwa kufanyika tarehe 29 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi katika Jengo la Mpingo, Barabara ya Nyerere Jijini Dar es Salaam, zilipokuwa  ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (Ivory Room).

Kupitia taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Dk. James Wakibara amesema  mnada huo utawahusisha wafanyabiashara wa Nyara waliopewa leseni ya Nyara Daraja la Kwanza mwaka 2017.

Amesema wafanyabiashara hao wataruhusiwa kukagua meno hayo kati ya tarehe 25 na 26 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tisa na nusu jioni kabla ya siku ya mnada huo.

Aidha, amesema wanunuzi watakaoshinda mnada huo watatakiwa kulipa asilimia 25 ya malipo yote papo hapo na asilimia 75 itakayosalia itatakiwa kulipwa ndani ya siku kumi na nne zijazo baada ya mnada huo.

“Mtu yeyote atakayekuwa ametamka bei ya juu, kisha akashindwa kulipa asilimia 25 ya bei aliyotamka, atachukuliwa kuwa ni mwenye kutaka kuvuruga mnada na hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” ameonya Mkurugenzi huyo.

Amesema meno hayo yatauzwa kwa wastani wa uzito wa nusu kilo bila kugawanywa au kuchambuliwa wakati wa mnada na wanunuzi wataruhusiwa kuondoa bidhaa kwenye eneo la mnada baada ya kulipia ada na kodi husika kikamilifu na kupewa hati ya kumiliki nyara hizo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Dk. James Wakibara (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya 15 ya Jeshi Usu kwa kwa Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro hivi karibuni Mkoani Katavi. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda.

Monday, January 22, 2018

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kufungua Onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika, Jijini Dar es Salaam

 Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani) wakati wa utambulisho wa tukio hilo linalotarajiwa kufanyika kesho Januari 23.2018. 
Balozi wa Spain nchini, Bw. Felix Costales akizungumza katika tukio hilo mapema leo Januari 23,2018. Kulia kwake ni  Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla. 
Vioneshwa kinachoelezea hatua za binadamu wa kale katika makumbusho ya Taifa ikiwa katika maandalizi ya mwisho mwisho kwa ajiri ya kesho
Na Andrew Chale, Dar es Salaam
............................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla (MB) anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kesho Januari 23.2018, kwenye uzinduzi wa Onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika, tukio ambalo litafanyika majira ya saa 11 jioni katika viunga vya Makumbusho ya Taifa, yaliyopo mtaa wa Shabani Robert, mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).
Akizungumza wakati wa utambulisho wa tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla amebainisha kuwa, tayari maandalizi ya onesho hilo yameenda sawa na watu mbalimbali watanatarajiwa kushuhudia tukio ambalo ni la siku moja wakiwemo viongozi wa Serikali na Mabalozi waliopo nchini, na
watalii wanatarajiwa kuhudhuria.

Profesa Mabulla amebainisha kuwa, Vioneshwa vyote katika onesho hilo hapo kesho, vimepatikana hapa Tanzania kutokana na tafiti za kisayansi na vimehifadhiwa Makumbusho ya Taifa.
“Vioneshwa hivi ni pamoja na masalia ya zamadamu, zana za mawe na
masalia ya wanyama walioishi takribani tangu miaka milioni 4 iliyopita. Pia zipo picha za zamadamu na mazingira waliyoishi wakifanya shughuli zao za kila siku.” alieleza Profesa Mabulla.

Kwa upande wake Mratibu kwa upande wa Tanzania Dk. Agness Gidna amesema Onesho limegawanyika katika sehemu kuu nne zikiwemo Makumbusho ya Taifa la Tanzania ikishirikiana na Ubalozi wa Spain Tanzania. Hii ni pamoja na Makumbusho ya Akiolojia ya
Madrid, Taasisi ya Chimbuko la Binadamu (IDEA) Madrid, Chuo Kikuu cha Alcala Madrid na Makumbusho ya CosmoCaixa Barcelona-Spain huku tamasha zima likidhaminiwa na Kampuni ya Simenti ya Twiga.

“Tunawashukuru kampuni ya Twiga Cement kwa kudhamini onesho la Chimbuko
la Binadamu Afrika (The Cradle of Humankind in Africa). Pia kutakuwa na Semina na onesho hili ni matokeo ya tafiti mbali mbali zinazofanyika bonde la Olduvai na Laetoli, Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro.” alieleza Dk Agness.

Aidha Dk.Agness ameongeza kuwa, Onesho hilo litakuwa katika pande nne ikiwemo sehemu ya kwanza inahusu ushahidi wa nyayo za zamadamu zilizongunduliwa huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dkt. Mary D. Leakey. Nyayo hizo ziliachwa na zamadamu anayeiitwa Australopithecus afarensis na ni ushaidi usiopingika wa zamadamu kutembea
wima kwa miguu miwili takribani miaka milioni 3.6 iliyopia.

Sehemu ya pili inahusu hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus Homo) ambapo kuna masalia ya zamadamu Zinjanthropus au Paranthropus boisei na Homo habilis, zana za mawe za mwanzo (Oldowan) zilizotumika katika kujipatia chakula na ushahidi wa kale wa ulaji wa nyama katika historia ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 2 iliyopita.
Sehemu ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus. Jamaii hii inafanana zaidi na binadamu wa sasa kuliko jamii zilizotangulia. Kuna masalia ya zamadamu Homo erectus, zana za mawe (Acheulian) na ushahidi wa ulaji wa wanyama wakubwa kama vile tembo na nyati wa zamani takribani miaka million 1.7 iliyopita.
Sehemu ya nne inaonesha kipindi cha mwanzo cha binadamu wa sasa (Homo sapiens) walioanza kutokea hapa Afrika miaka laki 2 iliyopita. Kuna masalia ya Homo sapiens na zana za mawe za muhula wa kati na muhula wa mwisho.
Mbali na onesho hilo, pia waandaji hao wa Makumbusho ya Taifa inawakaribisha watu wote kuhudhuria semina na ufunguzi wa onesho la Chimbuko la Binadamu Afrika.
Kwa upande wa Semina ambayo inatarajia kuanzia majira ya saa tisa kamili itaendeshwa na watafiti wa Kimataifa, akiwemo Prof. Manuel Dominguez-Rodrigo wa Chuo Kikuu cha Complutense, Spain; Prof. Audax ZP Mabulla na Dk. Agness Gidna.Vionesho ambavyo vinatarajiwa kuwapo kesho katika tukio hiloAfisa kutoka ubalozi wa Spain akipata maelezo kutoka kwa Mratibu upande wa Tanzania Dk. Agness Gidna  wa Makumbusho ya Taifa. Kulia ni Balozi wa Spain Bw. Felix Costales 

Tuesday, January 16, 2018

DK. KIGWANGALLA APONGEZA USHIRIKIANO WA FINLAND KATIKA UHIFADHI WA MISITU NCHINI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini. 

Na Hamza Temba - Dodoma
.............................................................. 

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla ameipongeza Serikali ya Finland kwa ushirikiano na misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikiitoa kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi wa maliasili na uendelezaji wa misitu nchini.

Dk. Kigwangalla ametoa pongezi hizo leo Januari 16, 2018 kwa Balozi wa nchi hiyo hapa nchini, Mhe. Peka Huka ambaye amemtembelea ofisini kwake mjini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na maendeleo ya misitu nchini.

“Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Serikali ya Finland,  mmekuwa washirika wetu wakubwa wa maendeleo kwa muda mrefu ambao mmetusaidia mambo mbalimbali ikiwemo kuendeleza misitu nchini, kuendeleza Chuo cha Mafunzo ya Misitu Olmotonyi na hata mapitio ya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998, ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kudumisha ushirikiano huu”, alisema Dk. Kigwangalla.

Alimueleza balozi huyo kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika uhifadhi wa misitu nchini ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha na teknolojia kwa ajili ya kuwezesha uhifadhi endelevu. Alisema changamoto nyingine ni uvunaji haramu wa mazao ya misitu ambayo husababisha eneo la hekta 372,000 za misitu kupotea kila mwaka.

Alisema mbali na nguvu kubwa inayotumiwa na Serikali katika udhibiti wa uvunaji holela wa mazao ya misitu Wizara yake kwa kushirikiana na taasisi zilizoko chini yake inaendelea kuweka mikakati thabiti kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kiserikali kwa ajili ya kutafuta nishati mbadala pamoja na kuanzisha mashamba kwa ajili ya uzalishaji wa miti ya mkaa kwa njia endelevu.

Akizungumzia umuhimu wa misitu nchini, Dk. Kigwangalla alisema takribani kila kitu hapa nchini kinategemea uwepo wa misitu. Alisema zaidi ya asilimia 80 ya chanzo cha nishati ya umeme nchini ni maji ambayo hutegemea uwepo wa misitu, alitaja pia kilimo na ufugaji ambao pia hutegemea mvua na maji ambayo hutegemea pia uwepo wa misitu.

Kutokana na umuhimu huo, Dk. Kigwangalla amemuomba Balozi huyo kuhamasisha wawekezaji wa Finland  kuja kuwekeza Tanzania katika uzalishaji na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu nchini na kuahidi kuwapa ushirikiano.

Kwa upande wake Balozi Huka, alimueleza Dk. Kigwangalla kuwa nchi yake imekua ikifadhili miradi mbali mbali ya uendelezaji wa misitu katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo mikoa ya nyanda za juu kusini na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.

Alimueleza Waziri Kigwangalla kuwa changamoto iliyopo ya uharibifu wa misitu nchini inahitaji uwepo wa nishati mbadala ambayo mchakato wa upatikanaji wake unatakiwa kushirikisha wadau na Mamlaka nyingine za Kiserikali ikiwemo Wizara ya Nishati.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akimsikiliza Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo.
 Balozi Peka Huka akimsikiliza Waziri Kigwangalla katika kikao hicho.
 Waziri Kigwangalla akifafanua jambo kwa Balozi Peka Huka (hayuko pichani) katika kikao hicho mapema leo mjini Dodoma.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akimuaga Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka baada ya mazungumzo ofisini kwake leo mjini Dodoma .