slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Monday, August 29, 2016

MAJANGILI TAFUTENI KAZI NYENGINE - MAJ. GEN. GAUDENCE MILANZI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi akifunga mafunzo maalum ya kijeshi kwa ajili ya kupambana na ujangili kwa Askari wanyamapori katika Pori la Akiba la Rungwa mkoani Singida hivi karibuni. 
Askari wanyamapori wakionesha kwa vitendo namna ya kupambana na majangili wakati wakiwakamata majangili wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childress akizungumza wakati wa kufunga mafunzo maalumu ya ya kupambana na ujangili kwa Askari wanyamapori katika Pori la Akiba la Rungwa mkoani Singida hivi karibuni. Mafunzo hayo yatawasaidia Askari wanyamapori kupata taarifa za kitenteligensia kwa ustadi wa hali ya juu katika kupambana na kukabiliana na majangili.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Tanzania ( TAWA) Bw. Martin Loibook akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo katika Pori la Akiba la Rungwa mkoani Singida hivi karibuni. 
Askari wanyamapori wakionesha kwa vitendo wakati wa kuhitimu mafunzo maalumu yaliyofanyika katika Pori la Akiba la Rungwa Mkoani Singida yaliyohitimishwa hivi karibuni wakionesha namna ya kupambana na majangili wakati wakiwakamata majangili.

---------------------------------------------------------------

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi ametoa wito kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili waache kazi hiyo mara moja na badala yake watafute kazi nyingine zitakazoweza kuwapatia kipato halali kwa kufanya hivyo wataweza kujiepusha kutiwa nguvuni na askari wanyamapori waliobobea kwa kazi hiyo. 


Maj. Gen Milanzi alitoa wito huo hivi karibuni wakati wa akifunga mafunzo maalumu ya kupambana na Ujangili kwa askari wanyamapori katika pori la akiba la Rungwa mkoani Singida yaliyofadhiliwa na Marekani na yaliyotolewa na Kikosi maalum cha wanajeshi kutoka Marekani. 

 Amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa askari wanyamapori ili kuendelea na kukabiliana na wimbi kubwa la ujangili kwa kuwa majangili wasasa wanatumia silaha za kisasa tofauti na majangili wa zamani ambao walikuwa wakitumia upinde na mishale. 

 Aliongeza kuwa majangili wa sasa ambao askari wanyamapori wamekuwa wakikabiliana nao maporini ni wale ambao wanatumia silaha za kivita hiyo ni lazima askari wetu wapewe mafunzo ya hali ya juu ili waweze kukabiliana nao. 

Aidha Katibu Mkuu, Milanzi alisema Wizara imejipanga kuhakikisha suala la ujangili linakwisha ambapo kituo kingine cha mafunzo ya kijeshi kwa askari wanyamapori cha Mlele kilichopo Mkoani Katavi kimeanzishwa mbali na vyuo vya Pasiansi na Mweka, Likuyu Sekamaganga ambavyo pekee ndivyo vilivyokuwa vikitoa mafunzo kwa askari wanyamapori. 

 Aliongeza kuwa, kwa sasa Serikali imejipanga kwa kushirikiana na Interpol kuhakikisha kuwa hatakamatwa jangili tu aliyehusika kuua mnyama porini bali mtandao wote utakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria mahali popote. 

 Akizungumza na wahitimu wa mafunzo hayo, Milanzi alisema mafunzo hayo yamejikita kuwasaidia kupambana na majangili, magaidi pamoja na majambazi ambapo wao ndo watu wa kwanza kukumbana nao wakiwa porini kwani ndiko wanakotumia kujificha kwahiyo ujuzi walioupata umewaongezea ufanisi katika kulinda maliasili zilizopo kwenye maeneo yao. 

 Aliwataka pia wahitimu hao kufanya kazi kwa kujituma wasiishie tu kusherekea kumaliza mafunzo bali waonyeshe kwa vitendo hii itasaidia na kuipa ari Marekani pamoja na Asasi za kimataifa zenye lengo la kusaidia nchi katika vita dhidi ya Ujangili. 

Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childress amewataka wahitimu wazingatie mafunzo waliyopata kwa kuyafanyia kazi ili Pori la Akiba la Rungwa liwe sehemu salama kwa wanyamapori wanaopatikana katika pori hilo.

 Ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania kwa kuwa suala la ujangili bado ni kubwa linalohitaji ushirikiano wa pande zote ili liweze kutokomezwa.

Tuesday, August 16, 2016

SERIKALI KUPITIA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUBORESHA NA KUIMARISHA VIVUTIO VYA UTALII WA NDANI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Ngorongoro jana. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Eng. Angelina Madete.
-----------------------------------------------------------------
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kuboresha na kuimarisha vivutio vya utalii wa ndani ikiwemo  fukwe na bahari na huduma za hoteli za kitalii nchini  ilikuhakikisha kuwa Wizara hiyo inavuka lengo la ukusanyaji  wa mapato.
  Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa   Maliasili na Utalii, Mhandisi RamoMakani wakati wa mkutano  na waandishi wa habari akizungumzia fursa na mchango wa sekta ya utalii katika kukuza uchumi wa taifa.
  Alisema lengo la uboreshaji wa huduma hizo ni kufikia   utekelezaji na wa Mipango ya Sekta ya Maliasili na Utalii katika kuchangia kuongezeka kwa pato la taifa  hatimaye kukuza uchumi wa nchi.
  “kuna haja ya kuboresha, kuongeza  nguvu na kuimarisha kila  hitaji ili kuwezesha sekta ya Maliasili na Utalii kuzalisha zaidi ili kuchangia pato la taifa na hatimaye kukuza uchumi   wa Taifa “ alifafanua Mhandisi Makani.
  Pia alisema kuwa Wizara inalenga kuboresha utangazaji wa vivutio, bidhaa, na huduma, kuboresha miundombinu ndani ya  hifadhi, kuhifadhi vivutio na mazingira yake, kuboresha utoaji wahuduma pamoja na kuendeleza vivutio vilivyopo na  kuanzisha vivutio vipya.
Akizungumza kuhusu uboreshwaji wa utalii wa ndani Mhandisi Makani alisema utalii huo ukiimarishwa mapato yake yatalingana na mapato yanayokusanywa kutoka kwa watalii wa nje kwani kwa sasa wananchi wana mwamko mkubwa wa  kutembelea vivutio vilivyopo hapa nchini.
“Tukiimarisha utalii wandani mapato yake yatalingana na mapato yanayokusanywa kutoka kwa watalii wa nje, kwa mfano  idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi ya kisiwa cha Saa  imeongezeka hadi kufika asilimia 94.5 kwa mwaka 2015/2016″  aliongeza Mhandisi Makani.
  Kwa mujibu wa Mhandisi Makani alisema katika kuboresha hudumu  za utalii, sekta hiyo bado haijaimarika kutokana na ukosefu wa ujuzi wa baadhi ya watoa huduma na hivyo  kupelekea upungufu wa kiwango cha watalii.


Mhandisi Makani alisema Wizara imeandaa Semina itakayofanyika   kikanda nchini kote kwa ajili yakuwawezesha vijana kupata   elimu juu ya utoaji wa huduma stahiki zinazohusu sekta ya
  utalii.

  Waziri huyo alisema kuwa Wizara itasimamia kwa ukaribu  taratibu nzima za uanzishwaji wa hoteli pamoja na utoaji wa  huduma zitakazokidhi viwango kwa kutoa Elimu, kusajili  nakufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika hoteli hizo.

KATIBU MKUU MALIASILI, MAJ. GEN. GAUDENCE MILANZI ATOA WITO KWA WADAU WA UHIFADHI NCHINI KUKEMEA VITENDO VYA UINGIZWAJI WA MIFUGO KWENYE MAENEO YA HIFADHI NCHINI

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi ametoa wito kwa wadau wa uhifadhi nchini kukemea kwa nguvu zote tabia ya uingizaji wa mifugo ndani ya hifadhi za Misitu na Wanyamapori nchini kwakuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi na kunahatarisha ustawi wa hifadhi hizo ambazo ni muhimu kiikolojia na uchumi na wa taifa.

Milanzi ametoa wito huo juzi wakati akifunga mafunzo maalum ya kijeshi katika kituo cha Mlele ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi, Mkoani Katavi kwa Mameneja wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Askari wa TANAPA kwa ajili kubadilisha mfumo wa utendaji katika taasisi hizo kutoka wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu (paramilitary) kuboresha utendaji wao wa kazi.

“Mifugo katika hifadhi zetu sio sahihi ni kinyume kabisa cha sheria za nchi, endeleeni kulikemea hili, tusipige siasa kufurahishana kwakua madhara yake ni mengi ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji, muingiliano wa magonjwa baina ya mifugo na wanyamapori na kuharibu ubora wa vivutio vyetu” Alisema Milanzi.

Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 Ibara ya 18 (2) inakataza kabisa kuingiza mifugo ndani ya hifadhi, Sheria hiyo inasema “Si ruhusa mtu yeyote kuingia na kulisha mifugo ndani ya Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Ardhioevu”.

Milanzi alisema kuwa hifadhi za taifa nchini zina umuhifu mkubwa kwa uchumi wa taifa kwakuwa kupitia utalii zinachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za nje (foreign currency). Aidha sekta hiyo inatoa ajira zaidi ya milioni moja na nusu kupitia huduma za kitalii nchini. 

Mbali na faida za kiuchumi hifadhi hizo pia zina faida nyingi za kiikolojia ambazo ni uhifadhi wa vyanzo vya maji, kusaidia upatikanaji wa mvua na hewa safi kwa viumbe hai ikiwemo binaadamu. Alisema kuharibu hifadhi hizo kwa kulisha mifugo ndani yake ni jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa ni kuhatarisha pia maisha ya binaadamu ambayo yanategemea hifadhi hizo.

Alieleza kuwa Serikali inaenda kulifanyia kazi tatizo hilo pamoja na migogoro mingine ya ardhi kwa ajili ya kuyatafutia suluhu kwa kushirikisha Wizara zinazohusika ambazo ni Ardhi, Kilimo na Mifugo, Sheria na Katiba, Tamisemi, Maliasili na Utalii na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.

Akizungumza na wahitimu wa mafunzo hayo, Milanzi alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uadilifu, nidhamu, ujasiri, uaminifu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa muda mfupi na hivyo kuwataka kuyatumia kuongeza ufanisi katika kulinda maliasili zilizopo kwenye maeneo yao.

Aliwataka pia wahitimu hao kutafsiri mafunzo hayo na maendeleo ya sekta ya uhifadhi nchini na kuliongezea taifa mapato kwa kuboresha huduma za utalii, kubuni bidhaa mpya za utalii na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Alan Kijazi aliwataka wahitimu hao kutumia mafunzo waliyoyapata kuziba mianya yote ya ujangili na kwamba jamii inategemea kuona kazi hiyo kwa vitendo.

Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na UNDP kupitia mradi wa “Spanest” yalifanyika kuanzia tarehe 15 Julai hadi tarehe 13 Agosti, 2016 kwa kuwahusisha washiriki 69 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Tanapa. Mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwa awamu yanatemewa kuhusisha taasisi zote za uhifadhi wa wanyamapori nchini kuelekea kwenye mabadiliko ya muundo wa utendaji kazi kutoka mfumo wa Kiraia  kwenda mfumo wa Jeshi Usu (Paramilitary).

KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, MAJ. GEN. GAUDENCE MILANZI AFUNGA MAFUNZO YA JESHI USU KWA WAHIFADHI WA TANAPA NA NGORONGORO WILAYANI MLELE, MKOA WA KATAVI

Gwaride la wahitimu wa mafunzo ya kijeshi kwa askari na maafisa wa Hifadhi za Taifa likiingia katika viwanja vya mazoezi katika kambi ya mafunzo ya Mlele wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akipokea salamu ya utii kutoka kwa askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Maafisa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (hawapo pichani) wakati wa ufungaji mafunzo kwa askari na maafisa hao yaliyofanyika katika kambi ya mafunzo ya Mlele mkoani Katavi 


Askari na Maafisa wa Hifadhi wakipita kwa heshima mbele ya mgeni rasmi kwa mwendo wa pole na haraka wakati wa ufungaji wa mafunzo ya kijeshi waliyopata katika kambi ya mafunzo ya Mlele mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya kubadili utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuendeshwa katika mfumo wa jeshi usu kutoka mfumo wa kiraia.Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi akikagua gwaride wakati wa kufunga mafunzo kwa askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Maafisa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro yaliyofanyika katika kambi ya mafunzo ya Mlele mkoani Katavi 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi(kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi wakipokea salamu za heshima kwa kupiga saluti wakati gwaride likipita mbele kwa heshima wakati wa ufungaji wa mafunzo kwa askari wa shirika la Hifadhi za Taifa,(TANAPA) na Maafisa wa Mamlaka ya Hifadhi ya taifa Ngorongoro.

Bendi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ikipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa ufungaji wa mafunzo ya kijeshi kwa askari na maafisa wa Hifadhi ,Mafunzo yaliyofanyika katika kambi ya Mlele mkoani Katavi.
Askari na Maafisa wa Hifadhi za Taifa wakionesha umahiri katika matumizi ya silaha wakati wakionesha kwa vitendo mafunzo ya kijeshi waliyopata katika kambi ya Mlele mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya kubadili utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuendeshwa katika mfumo wa jeshi usu. 

Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Witness Shoo (kushoto) pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi Mtango Mtahiko wakifuatilia maonesho ya matumizi ya silaha kutoka kwa wahitimu hao.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete akisherehesha wakati wa ufungaji wa mafunzo ya kijeshi kwa askari na Maafisa wa Hifadhi waliyopata katika kambi ya Mlele mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya kubadili utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuendeshwa katika mfumo wa jeshi usu.

Askari na Maafisa wa Hifadhi wakionesha umahiri katika matumizi ya silaha wakati wakionesha kwa vitendo mafunzo ya kijeshi waliyopata katika kambi ya jeshi ya Mlele mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya kubadili utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuendeshwa katika mfumo wa jeshi usu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi pamoja na Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ,Freddy Manongi wakifuatilia maonesho hayo. 

Askari na Maafisa wa Hifadhi wakionesha umahiri katika matumizi ya silaha wakati wakionesha kwa vitendo mafunzo ya kijeshi waliyopata katika kambi ya Mlele mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya kubadili utendaji kazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuendeshwa katika mfumo wa jeshi usu. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi akitizama matundu ya risasi zilizolengwa na mmoja wa askari wa uhifadhi waliohitimu mafunzo ya kijeshi katika kambi ya Mlele mkoani Katavi.Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi. 
Wakufunzi wa Mafunzo ya kijeshi kwa maofisa na askari wa Hifadhi za Taifa wakitambulishwa mbele ya mgeni rasmi,(hayupo pichani). 
Mhifadhi kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Lilian Magoma akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake wa mafunzo ya kijeshi yaliyofanyika katika kambi ya Mlele iliyopo mkoani Katavi.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi akitunuku vyeti kwa askari na maafisa wa uhifadhi waliohitimu mafunzo ya kijeshi katika kambi ya Mlele mkoani Katavi. 
Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Getrude Lyatuu akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo. 

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,Freddy Manongi akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo. 

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Alexander Songorwa akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA)Allan Kijazi akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo. 
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi akimkaribisha Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi kuzungumza na wahitimu wa mafunzo ya kijeshi kwa askari na maofisa wa Hifadhi za Taifa . 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza wakati wa ufungaji wa mafunzo kwa askari na maofisa wa Hifadhi za Taifa. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwa katika pichaya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya kijeshi yaliyofanyika katika kambi ya Mlele mkoani Katavi. Na Dixon Busagaga wa Michuzi

Thursday, August 11, 2016

PROF. MAGHEMBE AZINDUA KITABU CHA KUHAMASISHA ULINZI WA TEMBO NA FARU (TEMBO - FARU WANA HAKI YA KUISHI TANZANIA)

Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mhe. Ally Hassan Mwinyi (kulia) akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha kuhamasisha ulinzi wa Tembo na Faru pamoja na kupiga vita ujangili kilichoandikwa na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam jana katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwl. J.K. Nyerere, Dar es Salaam. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akionesha kitabu hicho kwa wajumbe walioshiriki hafla hiyo kama ishara ya kukizindua rasmi kwa niaba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Mhe. Ally Hassan Mwinyi (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akimkabidhi Mwanasiasa Mkongwe nchini ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa chama cha CUF, Prof. Ibrahim Lipumba nakala ya kitabu hicho. Wapili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Salum.
Picha ya pamoja.

------------------------------------------------------------------

Rais Mstaafu wa Awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ally Hassan Mwinyi ametoa wito kwa watanzania kuongeza juhudi katika kusaidiana na Serikali kupiga vita ujangili hapa nchini.


Wito huo umetolewa jana jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kitabu cha “Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania” kilichoandaliwa na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar  es salaam na kuzinduliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe kwa niaba ya Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais mstaafu huyo, amesema kumekuwa na tatizo la mauaji ya wanyamapori hapa nchini ambayo ni dhambi na ni kinyume na kusudio la Mungu kwa kuwa wanyama hao wana haki ya kuishi kama viumbe wengine.

“Kumekuwa na matukio mengi ya uuaji wa wanyamapori ikiwemo tembo na faru na hivyo kupunguza rasilimali ya taifa kwa vizazi vijavyo na pia kitendo hicho ni kinyume na kusudio la Mungu hivyo ni vizuri kuwatunza, kuwapenda, kuwaendeleza na kuwalinda wanyama hao kwani ni moja ya vivutio vinavyochangia pato la Taifa” aliongeza Rais Mstaafu  Mwinyi.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe amesema kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na mbuga nzuri na bora duniani baada ya nchi ya Brazil na kusisitiza ni muhimu kwa watanzania wote kutunza rasilimali za taifa ikiwemo mbuga za wanyama na wanyamapori.


Aliongeza kuwa wanyamapori ni muhimu sana katika maisha ya kila mtanzania kwa kuwa kupitia utalii wanachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za nje (foreign currency) hivyo hakuna budi kwa kila mtanzania kupiga vita ujangili ambao.
Alisema kuwa jumuiya ya ujangili ni kubwa ambayo inahusisha  makundi mbalimbali ikiwemo watengenezaji wa silaha za kuua tembo, waagizaji wa meno ya tembo, wasambazaji na watu mashuhuri ambao wanatumia nyumba zao kuhifadhina kununua meno ya tembo.


Kitabu cha “Tembo-Faru wana haki ya kuishi Tanzania” kimetayarishwa na kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Dar es salaam kikiwa na lengo la kuwaelimisha waanadamu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na viumbe vilivyopo kwa faida yao na vizazi vijavyo.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum alisema jumla ya vitabu 5,000 vimechapishwa kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la WILDAID, Jumla ya nakala milioni 20 zinahitajika kuchapishwa katika lugha tofauti na kusambaza katika nchi mbalimbali duniani na hivyo kuwaomba wadau mbalimbali kuchangia gharama za uchapishaji huo ambao kwa kila kitabu kimoja kinagharimu dola kimarekani 12.


Akizungumzia uchangiaji huo, Waziri Maghembe alisema kuwa Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (TWPF) utachangia milioni 20 kuwezesha uchapishaji wa vitabu hivyo na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono juhudi za vingozi wa dini na Serikali katika kulinda na kuhifadhi Malisili za taifa kwa kuchangia uchapishaji wa kitabu hicho na kulinda Malisili za taifa.