Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Ngorongoro jana. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Eng. Angelina Madete.
-----------------------------------------------------------------
SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imepanga kuboresha na kuimarisha vivutio vya utalii wa ndani ikiwemo fukwe na bahari na huduma za hoteli za kitalii nchini ilikuhakikisha kuwa Wizara hiyo inavuka lengo la ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi RamoMakani wakati wa mkutano na waandishi wa habari akizungumzia fursa na mchango wa sekta ya utalii katika kukuza uchumi wa taifa.
Alisema lengo la uboreshaji wa huduma hizo ni kufikia utekelezaji na wa Mipango ya Sekta ya Maliasili na Utalii katika kuchangia kuongezeka kwa pato la taifa hatimaye kukuza uchumi wa nchi.
“kuna haja ya kuboresha, kuongeza nguvu na kuimarisha kila hitaji ili kuwezesha sekta ya Maliasili na Utalii kuzalisha zaidi ili kuchangia pato la taifa na hatimaye kukuza uchumi wa Taifa “ alifafanua Mhandisi Makani.
Pia alisema kuwa Wizara inalenga kuboresha utangazaji wa vivutio, bidhaa, na huduma, kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi, kuhifadhi vivutio na mazingira yake, kuboresha utoaji wahuduma pamoja na kuendeleza vivutio vilivyopo na kuanzisha vivutio vipya.
Akizungumza kuhusu uboreshwaji wa utalii wa ndani Mhandisi Makani alisema utalii huo ukiimarishwa mapato yake yatalingana na mapato yanayokusanywa kutoka kwa watalii wa nje kwani kwa sasa wananchi wana mwamko mkubwa wa kutembelea vivutio vilivyopo hapa nchini.
“Tukiimarisha utalii wandani mapato yake yatalingana na mapato yanayokusanywa kutoka kwa watalii wa nje, kwa mfano idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi ya kisiwa cha Saa imeongezeka hadi kufika asilimia 94.5 kwa mwaka 2015/2016″ aliongeza Mhandisi Makani.
Kwa mujibu wa Mhandisi Makani alisema katika kuboresha hudumu za utalii, sekta hiyo bado haijaimarika kutokana na ukosefu wa ujuzi wa baadhi ya watoa huduma na hivyo kupelekea upungufu wa kiwango cha watalii.
Mhandisi Makani alisema Wizara imeandaa Semina itakayofanyika kikanda nchini kote kwa ajili yakuwawezesha vijana kupata elimu juu ya utoaji wa huduma stahiki zinazohusu sekta ya
utalii.
Waziri huyo alisema kuwa Wizara itasimamia kwa ukaribu taratibu nzima za uanzishwaji wa hoteli pamoja na utoaji wa huduma zitakazokidhi viwango kwa kutoa Elimu, kusajili nakufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika hoteli hizo.
No comments:
Post a Comment