Saturday, April 22, 2017

VOTE for Mt Kilimanjaro #Tanzania as Africa's Leading Tourist Attraction in World Travel Awards 2017.


DID YOU KNOW? Mount Kilimanjaro is the 2016 Africa's Leading Tourist Attraction.

HOW TO VOTE? Click link below, register&vote

Pigia kura Mt Kilimanjaro katika Tuzo za World Travel Awards 2017 kama Kivutio Bora Afrika.

JE WAJUA? Mlima Kilimanjaro ndio kivutio bora Afrika mwaka 2016.

Jinsi ya kupiga kura: bonyeza link hapa chini, jisajili (register), nenda kwenye majina (Africa nominees) kisha piga kura kwa kubonyeza kiduara pembeni mwa jina.

LINK

Sunday, April 16, 2017

360 YA CLOUDS TV KWENDA MUBASHARA NDANI YA HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI KESHO

TANAPA kwa kushirikiana na Clouds TV 360 kesho Jumatatu ya Pasaka watakuwa Mubashara kutoka Hifadhi ya Serengeti kuanzia saa 12 asubui hadi saa 4 asubui.Fuatana nasi katika kuhamasisha Utalii wa Ndani.

Thursday, April 13, 2017

KIPINDI CHA 360 KURUSHWA MUBASHARA KUTOKA KATIKA HIFADHI ZA SERENGETI NA NGORONGORO

Watangazaji wa kipindi cha 360 kinachorushwa na Clouds Tv wamewasili mkoani Arusha jana kwa ajili ya ziara katika hifadhi za taifa za Serengeti na Ngorongoro kwa lengo la kutangaza utalii wa ndani. 

Kipindi hicho kinachoendelea kujizolea umaarufu cha 360 kinataraji kurushwa moja kwa moja kutoka katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na Serengeti kikiongozwa na watangazaji wake Baby Kabaye, Sam Sasali, Hassan Ngoma na James Tupa tupa. 

Leo Ijumaa na Jumamosi kitarushwa LIVE kutokea hifadhi ya Ngorongoro na Jumatatu kutokea hifadhi ya Serengeti.

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAANZA KUKUSANYA MAONI KUTOKA KWA WADAU WA UTALII YA KUBORESHA SERA YA TAIFA YA UTALII YA MWAKA 1999


Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki akizungumza katika mkutano huo.
 Picha ya pamoja.
Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Zahoro Kimwaga akizumza katika mkutano huo.

Na. Lusungu Helela - WMU
......................................................
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka wadau wa Utalii nchini kutoa maoni yenye tija itakayopelekea upatikanaji wa Sera bora itakayoleta ufanisi katika uendeshaji wa huduma zinazotolewa katika sekta ya Utalii. 

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni miaka 17 sasa tangu Sera ya Taifa ya Utalii iliyopo ifanyiwe mapitio kwa mara ya mwisho mwaka 1999.  

Katika kutambua hilo, Wizara imeanza kupitia upya Sera hiyo ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Utalii inakwenda sambamba na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani yakiwemo ya kiteknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na mazingira

Akizungumza katika mkutano  uliofanyika kwa muda wa siku mbili  Jijini Arusha kwa mikoa ya kanda ya Kaskazini, Naibu Katibu Mkuu  wa Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki alisema Sera hiyo inafanyiwa marekebisho kwa kuwa imepitwa na wakati kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika sekta hiyo kwa sasa. 

Aidha, alisema kwa kutambua mchango wa utalii kiuchumi , ni wazi kuwa sera wezeshi ya utalii yenye kutoa mwongozo wa utaratibu bora na sahihi wa usimamizi, uendelezaji na utendaji katika sekta hiyo  unahitajika.

"Tunataka kuibadilisha sera hiyo ili iweze kujibu changamoto za aina ya utalii wa sasa ambao kipindi cha nyuma haukuwepo", ametea mfano utalii mikutano pamoja na utalii wa kiutamaduni ambao umekuwa ukikua kwa kasi hapa nchini.

Kutokana na hali hiyo,  Dkt. Nzuki amesema marekebisho ya Sera hiyo yanahitaji mchango mkubwa kutoka kwa wadau kwa kuwa  inaendeshwa kwa kiasi kikubwa na Sekta Binafsi katika kutoa huduma na kufanya biashara za utalii hapa nchini.

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Zahoro Kimwaga alisema uhuishwaji wa Sera hiyo utazingatia namna ambavyo wazawa wataweza kuwa wanufaika namba moja kwa kuwaandalia mazingira rafiki ya kuendesha biashara ya utalii tofauti na sasa ambapo makampuni mengi ya utalii ni ya watu kutoka nje. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TATO, Wilbert Chambulo alisema suala la kuifanyia marekebisho ya sera hiyo ni jambo jema ila sasa serikali iangalie namna ya kuboresha mashirikiano katika utoaji wa maamuzi kwa wafanyabiashara wa utalii nchini badala  ya kuamua peke yake.

Mkutano huo wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau umeanza kufanyika mkoani Arusha kwa kuwashirikisha wadau kutoka mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini na badaaye utafanyika katika kanda zingine kwa muda wa siku mbili kila kanda kwa ushirikiano kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,   Shirikisho la Vyama Vya Utalii Tanzania  (TCT) pamoja na Benki ya Dunia chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu

Wednesday, April 12, 2017

WAZIRI MKUU MSTAAFU WA ISRAEL, EHUD BARAK AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII, APOKELEWA KIA NA WAZIRI WA MALIASILI, PROF. JUMANNE MAGHEMBE

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisalimiana na familia ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Israel, Ehud Barak (kulia) alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) jana kwa ajili ya ziara ya kutembelea vivutio vya utalii nchini. Waziri Mkuu huyo wa 10 wa Israel aliliongoza taifa hilo mwaka 1999 - 2001.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Israel, Ehud Barak (wa pili kushoto) akimueleza jambo Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe muda mfupi baada ya kuwasili na ndege ya shirika na ndege la Israel (Israel Air) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro jana kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii hapa nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akimuongoza mgeni wake, Waziri Mkuu Mstaafu wa Israel, Ehud Barak (kushoto kwake) kuelekea kwenye maandalizi ya ziara yake ya kitalii nchini baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro jana. (Picha na Wizara ya Maliasili na Utalii)

MAAZIMIO YA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA UMMA

Wizara ya Maliasili na Utalii imesitisha utoaji wa vibali vya kusafirisha mkaa kutoka Wilaya moja hadi nyingine kuanzia terehe 01 Julai mwaka huu.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na kuungwa mkono na Baraza la wafanyakazi la Wizara wa Maliasili na Utalii kwa lengo kupunguza uharibifu mkubwa wa mazingira hususan ukataji wa miti hovyo.

Baraza hilo lililofanyika mjini Dodoma tarehe 10 Aprili, 2017 pia lilijadili umuhimu wa kutumia mkaa mbadala kwa miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ambapo mpango mahususi wa kutumia mkaa mbadala utakaozalishwa na kiwanda cha Mufindi – Iringa utawasilishwa ifikapo mwezi Julai mwaka huu.

Baraza la Wafanyakazi wa Maliasili na Utalii pia limepitisha kwa kauli moja kuongeza jitihada katika kukabiliana na ujangili hasa katika Pori la Akiba la Selous, Pori Tengefu la Loliondo, Rungwa na Yaeda Chini. Nguvu zaidi ya kukabiliana na changamoto ya uingizaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi ambao unachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la ujangili pia ilijadiliwa.

Aidha, Baraza liliazimia mali za majangili pamoja na mifugo itakayokamatwa katika maeneo ya hifadhi yataifishwe kwa mujibu wa sheria.

Katika kukabiliana na changamoto ya usafirishaji wa magogo nje ya nchi, Baraza liliazimia kuwa usafirishaji wa magogo ufanyike kwa kutumia nyaraka halisi (Original Documents) badala ya vivuli vya nyaraka (Photocopy).

Baraza hilo la Wafanyakazi pia liliazimia kuwa watumishi wote wa wizara wazingatie sheria na kanuni za utumishi wa umma katika maeneo yao ya kazi pamoja na utoaji wa huduma kwa Umma.

Mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita na kutoa maoni yao kwa bajeti ya Wizara inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni pamoja na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuweka mkakati wa kukabiliana nazo. Wajumbe wa Baraza hilo ni wawakilishi wa watumishi kutoka katika Idara, Vitengo, Taasisi na Vituo vya Wizara.

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Maliasili na Utalii,
11 Aprili, 2017
Dodoma.