Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amezionya na kuzitaka Taasisi
za Uhifadhi kuacha tabia ya kuwabughudhi wananchi wanaoishi katika vijiji na
vitongoji 366 vilivyokutwa ndani ya Hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini
mpaka hapo maamuzi ya Kamati ya Mawaziri saba iliyoundwa kushughulikia suala
hilo itakapokamilisha kazi iliyopewa na kuwasilisha ripoti kwa Mhe. Rais.
Hatua hiyo
ni kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya
wananchi wakiwemo wakulima na wafugaji
wanaoishi katika vijiji na vitongoji hivyo kudai kuwa wamekuwa
wakisumbuliwa na mifugo yao kukamatwa
mara mara kwa madai ya kukutwa imeingia ndani ya Hifadhi.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Kisondoko ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyomo ndani ya Pori la Akiba la
Mkungunero katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Mhe. Kanyasu amezitaka
taasisi hizo kufuata na kuzingatia
maelekezo yaliyotolewa na Serikali kuhusu wananchi wanaoishi katika
maeneo hayo.
Aidha, Mhe. Kanyasu ametumia fursa hiyo
kuwaonya wananchi ambao wamekuwa wakivamia
maeneo mapya ya Hifadhi kwa kisingizio
cha kauli aliyoitoa Mhe. Rais kuacha mara moja na kwamba yeyote atakayekamatwa hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yake.
"
Wananchi ninao walenga ni wale tu ambao walikuwa wakiishi Hifadhini kabla ya kauli ya Rais aliyoitoa mwanzoni mwa
mwaka huu" Alisisitiza.
Hata hivyo, Mhe Kanyasu amebainisha kuwa
Kamati ya Mawaziri saba iliyoundwa na kuzunguka nchi nchi nzima imebaini kuwa
kuna zaidi ya vijiji 820 ambavyo vimo ndani ya Hifadhi mbali ya vile 365
vilivyobainishwa awali na kuwasihi wananchi
wasiendelee kuvamia maeneo mengine.
Mhe.Kanyasu
ameowanya baadhi ya askari wa wanyamapori wanaoomba rushwa Kutoka kwa wafugaji pindi
wanapokamata mifugo yao ili waweze
kuiachia waache mara moja tabia hiyo akisisitiza kwamba askari yeyote atakayethibitika atachukuliwa
hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa Sheria za utumishi wa Umma.
Mkuu wa
wilaya ya Kondoa, Mhe. Sezaria Makota
amewataka wananchi hao kuendelea kuwa walinzi wa maeneo hayo huku
wakisubili hatma ya taarifa ya kamati ya Mawaziri saba itakayotolewa hivi
karibuni.
" Baada
ya taarifa hiyo mtajua hatma yenu na
kama hapa mtabaki au mtahamishwa na kama mtahamishwa tutajua tutawapeleka eneo
gani kwa ajili ya malisho na kilimo." Alisema.
Akizungumza
kwa niaba ya Wananchi, Mwenyekiti wa kijiji cha Kisondoko, Ismail Said
amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa baadhi ya askari wa wanyamapori wamekuwa
wakikamata mifugo yao na kuomba rushwa na pale makubaliano yanaposhindikana
huondoka na mifugo yao.
Amesisitiza
kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikichochea chuki baina ya wananchi na askari hao
jambo linalorudisha nyuma jitihada za Uhifadhi nchini.
Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine
Kanyasu wa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisondoko ambacho ni
miongoni mwa vijiji vilivyomo ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero katika
wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma ambapo ameagiza wananchi hao wasibughuziwe hadi
hapo maamuzi yatakapotolewa juu ya hatma yao. Wengine ni kmati ya Ulinzi na
Usalama wa wilaya hiyo pamoja na Maafisa wa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania,
Kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo, Sezaria Makota.
.Baadhi ya
wananchi wa kijiji cha Kisondoko wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii alipokuwa akizungumza nao kuhusu mifugo yao kukamatwa mara kwa mara na
askari wanyamapori wa Pori la Akiba la Mkungunero katika wilaya ya Kondoa
mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment