slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Saturday, March 26, 2016

WAZIRI MAGHEMBE AWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI TFS NA KAIMU MKURUGENZI IDARA YA WANYAMAPORI

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Machi, 2016. Kulia ni Naibu Waziri Eng. Ramo Makani.
Sehemu ya waandishi wa habari na wajumbe mbalimbali walioshiriki Mkutano huo.
........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini, (TFS) Bw. Juma Mgoo pamoja na Wakurugenzi wawili wa Taasisi hiyo ili kupisha uchunguzi kutokana na mwenendo usioridhisha wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi mbovu wa rasilimali za misitu nchini.

Prof. Maghembe ametaja majina ya Wakurugenzi hao aliowasimamisha kazi kuwa ni Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Bw. Zawadi Mbwambo pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi endelevu ya Misitu, Bw. Nurdin Chamuya

Baada ya kuwasimamisha hao amewateua watu wengine kushika nafasi zao wakati mchakato wa kuwapata watendaji wapya ukifanyika na walioteuliwa kukaimu nafasi hizo ni Kaimu Mtendaji Mkuu TFS, Gerald Kamwendo, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Mwanaidi Kijazi, na Kaimu Mkurugenzi wa Matumizi Rasilimali Misitu, Haji Mpya.

Wengine waliosimamishwa kazi na kanda zao katika mabano ni Hubert Haule (Kusini), Bakari Rashid (Mashariki), Cuthbert Mafipa (Kaskazini), Emmanuel Minja (Magharibi), Haji Khatibu (Ziwa) na Bruno Mallya (Nyanda za Juu Kusini).

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini mapungufu mbalimbali katika ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi usioridhisha wa rasilimali za misitu.

Alisema kuwa hivi karibuni walibaini shehena kubwa za magogo aina ya mninga katika Mkoa wa Rukwa wilayani Kalambo yakiwa yamekatwa na kuwekwa ndani ya makontena ndani ya msitu pamoja na kutengenezewa nyaraka feki zinazoonesha magogo hayo yanatoka nchini Zambia tayari kwa kusafirishwa kupelekwa nchini China.

Amesema kuwa baada ya kubaini tukio hilo na kulitolea maamuzi alipata taarifa kuwa shehena ya Magogo hayo yenye thamani ya shilingi milioni 500 za Kitanzania yaliyotakiwa kupelekwa Makao makuu ya Wilaya ya Kalambo yamemwagiwa petroli na kuchomwa moto wakati wiki mbili kabla alishatoa agizo la magogo hayo kusafirishwa kupelekwa Matai ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo.

Aliongeza kuwa kumekuwa na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.

“Pesa zitokanazo na makusanyo hayo zimekuwa hazipelekwi benki kwa wakati na hata zikipelekwa benki zimekuwa zikipelekwa pungufu na muda mwingine pesa hizo zimekuwa hazipelekwi kabisa”. Alisema Prof. Maghembe.

Katika tukio lingine, Waziri Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dkt. Charles Mulokozi kwa kosa la kukaidi agizo la kusaini vibali vya kusafirisha Wanyamapori nje ya nchi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kukamatwa watu katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro wakitaka kusafirisha nyani 61 “velvety monkeys” na kubaini kuwa Idara ya Wanyamapori ndio iliyotoa vibali vya kusafirisha nyani hao na vibali hivyo kusainiwa na Mkurugenzi huyo.

Alisema watu hao kutoka Ulaya Mashariki na washirika wao wa hapa nchini, walikodisha ndege ili kuwaondoa tumbili hao kwenda Ulaya Mashariki. Alisema harakati za kukamata tumbili hao porini zilianza wiki iliyopita na jumla ya idadi yao ni 450 ilhali kuna taasisi zinazolinda hayo mapori bila walinzi wa mapori hayo kujua

Prof. Maghembe alisema nyani hao walikamatwa maeneo ya Upareni, Hanang Manyara na Kiliamanjaro ambapo aliwaita wasimamizi na kuwapa taarifa juu ya watu hao na kuwakataza kutotoa kibali chochote cha kusafirisha wanyama hao.

“Nikiwa Moshi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa nilimuita Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi na kumuarifu juu ya kamata kamata hiyo na kumuagiza kutotoa kibali cha kusafirisha wanyama ili tuwakamate watu hao, lakini baadaye tukagundua yeye ndio amesaini kibali hicho kutoka Dar es Salaam,” alisema Maghembe.


Ameongeza kuwa ndege iliyokamatwa ilikuwa imekodiwa kutoka Afrika ya Kusini kwa ajili ya kusafirisha nyani hao kwenda Ulaya ya Mashariki, Ndege hiyo imeshikiliwa pamoja na rubani wake kwa mahojiano zaidi.

Prof. Maghembe ametoa onyo kali kwa wale wote wanaohujumu rasilimali za nchi na kusema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali.

“Hatutasita kumfukuza kazi mtu yeyote ambaye atashiriki katika suala hili la kuiibia nchi mali zake au anakaa anaangalia kando wakati fedha za nchi, mali za nchi zinaporwa” Alisema Prof. Maghembe kwa ukali.

SERIKALI YA TANZANIA HAINA MPANGO KWA KUTEKETEZA MENO YA TEMBO YALIYOHIFADHIWA

Serikali ya Tanzania imetoa tamko kuwa kwa sasa haina mpango wowote wa kuteketeza meno ya tembo yaliyohifadhiwa ambayo yametokana na vitendo vya ujangili na vifo asilia vya tembo.

Tamko hilo limetolewa hivi karibuni na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress alipotembelewa na balozi huyo ofisini kwake kujadili maendeleo ya sekta ya Maliasili mchini.

Prof. Maghembe alisema hayo baada Balozi huyo wa Marekani hapa nchini kutoa pendekezo kwa Serikali ya Tanzania kuchoma sehemu meno ya tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe mzito duniani juu ya dhamira ya Serikali kukomesha biashara hiyo haramu.

"Naomba niweke wazi kuwa kwa sasa hatupo tayari kuteketeza meno haya, tunaweza kuyatumia kwenye tafiti za kisayansi au vielelezo kwa ajili ya kesi za ujangili ambazo zipo mahakamani na nyingine ambazo bado zinafanyiwa uchunguzi" Alisema Prof. Maghembe.

Zipo nchi mbalimbali duniani ambazo zimechukua hatua ya kuteketeza meno yake ya tembo yaliyohifadhiwa ikiwemo nchi jirani ya Kenya na Malawi ambapo inaaminika kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kushawishi Ulimwengu kukomesha biashara hii haramu ya meno ya tembo.

Nchi nyingine ni Chad, Ubelgiji, Ufaransa, China, India, Marekani na Ureno. Kwa upande wa nchi ambazo zina msimamo sawa na Tanzania katika kuendelea kuhifadhi meno yake ya Tembo ni pamoja na Afrika ya Kusini, Botswana na Zimbabwe.

Akizungumzia kuhusu kuendeleza sekta ya Maliasili nchini, Prof.Maghembe amemuomba Balozi wa Marekani Bw. Mark Childress kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta hiyo kwa kuleta wawekezaji mbalimbali kutoka Marekani kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kusaidia kwenye mapambano dhidi ya Ujangili.

Aliongeza kuwa Tanzania ina fursa nyingi ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa ikiwemo hoteli za kitalii, fukwe za kisasa na kuendeleza vivutio mbalimbali vilivyomo hapa nchini.

Prof. Maghembe amemshukuru balozi huyo kwa misaada mbalimbali kutoka Serikali ya Marekani ya kuendeleza sekta ya Maliasili nchini ukiwemo wa hivi karibuni wa mbwa maalum (Snifer Dogs) kwa ajili ya kusaidia utambuzi wa rasilimali za Maliasili zinazoweza kutoroshwa nje ya nchi kupitia bandari na viwanja vya ndege.

Katika taarifa iliyowasilishwa kwenye kikao baina ya Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Balozi wa Marekani hapa nchini Bw. Mark Childress imeonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali ya Marekani imetoa misaada mbalimbali ambayo jumla yake ni dola za kimarekani Milioni 41.35 katika kusaidia eneo la uhifadhi hapa nchini.Akizungumzia mahusiano baina ya Tanzania na Marekani Balozi Mark Childress alimueleza Prof. maghembe kuwa Serikali ya Marekani itaendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili ambapo pia ofisi yake ya ubalozi imeshatafuta wadau mbalimbali ambao wapo tayari kusaidia fedha, vifaa na mafunzo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na mapambano dhidi ya ujangili. 

Wednesday, March 23, 2016

WAZIRI WA MALIASILI PROF. JUMANNE MAGHEMBE AONANA NA BALOZI WA MAREKANI HAPA NCHINI MHE. MARK CHILDRESS KUJADILI MAENDELEO YA SEKTA YA MALIASILI NCHINI

Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza katika kikao na Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (kulia) na Ujumbe wake katika ukumbi wa Selous Makao Makuu ya Wizara hiyo Mpingo House leo tarehe 23 Machi, 2016. Waziri Maghembe amemuomba Balozi huyo wa Marekani kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza sekta ya utalii nchini kwa kuwakaribisha wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza katika sekta hiyo.
Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (kulia) akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kushoto). Balozi huyo wa Marekani ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Marekani katika kuendeleza sekta ya uhifadhi hapa nchini. Ameahidi pia kusaidia katika vita dhidi ya ujangili.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisisitiza jambo kwa  Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Mark Childress (wa pili kushoto). Mhe. Maghembe alimueleza balozi huyo kuwa Tanzania haiko tayari kuteketeza meno ya Tembo yaliyohifadhiwa mpaka hapo itakapoona namna bora zaidi ya kufanya kwani kwa sasa Meno hayo yanaweza kutumika kwa ajili ya tafiti mbalimbali za kisayansi na kusaidia pia katika utambuzi na vielelezo vya mashtaka ya ujangili. Mhe Maghembe alisema hayo baada ya Balozi Childress kutoa pendekezo kwa Serikali kuona uwezekano wa kuteketeza sehemu ya meno ya Tembo yaliyohifadhiwa ili kutoa ujumbe duniani wa namna Serikali ya Tanzania ilivyodhamiria katika vita dhidi ya Ujangili.
Sehemu ya wajumbe kutoka ubalozi wa Marekani walioongozana na Mhe. Balozi Mark Childress wakifuatilia mada katika kikao hicho. Wajumbe hawa kila mmoja aliwasilisha mada ikionyesha ushirikiano wa Serikali ya Marekani na Tanzania katika sekta ya uhifadhi hapa nchini.  
Baadhi ya wajumbe kutoka ubalozi wa Marekani na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kikao hicho.
Wajumbe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii walioshiriki katika kikao hicho. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Bi. Angelina Madete.