slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Monday, June 27, 2016

TAARIFA KWA UMMA


Wizara ya Maliasili na Utalii itashiriki katika Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 8 Julai, 2016 katika viwanja vya Mwalimu Julius. K. Nyerere, Dar es Salaam.

Wizara itakuwa na washiriki kumi na sita (16) ambao ni Idara pamoja na Taasisi zake mbalimbali. Idara zitakazoshiriki ni Utalii, Wanyamapori, Mambo ya Kale na Misitu na Nyuki.

Kwa upande wa Taasisi ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chuo cha Taifa cha Utalii, Makumbusho ya Taifa, Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) na Vyuo vya Wanyamapori (Mweka, Pasiansi na Likuyu Semaganga).

Taasisi nyingine ni Vyuo vya Misitu na Nyuki (Olmotonyi, FITI Moshi na Chuo cha Nyuki Tabora), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Wakala wa Mbegu za Miti, Taasisi ya Utafiti wa Misitu na Wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Washiriki wote hao watakuwa kwenye banda moja la MALIASILI, Wizara inawakaribisha wananchi wote kwenye banda hilo waweze kujionea na kuelimika na mambo mbalimbali yanayohusu Utalii, Ufugaji wa Nyuki, Uhifadhi wa Misitu, Malikale na Wanyamapori.

Aidha, Wizara itatoa punguzo kwa watanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa gharama nafuu. Safari ya kwenda na kurudi kwa watoto itakua Tsh. 10,000 na watu wazima Tsh. 20,000. Safari ya kulala itakuwa Tsh. 50,000.

Pia katika maonesho hayo itakuwepo fursa ya kuwaona wanyamapori hai mbalimbali kama vile Chui, Nyoka, Ndege wa aina mbalimbali pamoja na SIMBA.

Kaulimbiu ya Maonesho hayo mwaka huu inasema “Tunaunganisha Uzalishaji wa Masoko”

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Maliasili na Utalii
27 Juni, 2016.

Thursday, June 16, 2016

MKURUGENZI WA IDARA YA UTAWALA NA RASILIMALI WATU (DARHM) WIZARA YA MALIASILI, SAID A.S MSAMBACHI ASTAAFU RASMI UTUMISHI WA UMMA, AACHA WOSIA KWA WATUMISHI WA WIZARA HIYO

Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Maliasili na Utalii, Said Msambachi akizungumza na watumishi wa Idara ya Utawala (hawako pichani) katika ukumbi wa Ngorongoro alipowaaga rasmi jana tarehe 16 Juni, 2016 kwa kukamilisha safari yake ya utumishi wa umma. Amewaasa watumishi wote wa wizara kuimarisha ushirikiano kazini, kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu,  kupendana, kusalimiana,  kudumisha uaminifu, utii wa amri halali za viongozi, uadilifu, usawa, usiri wa taarifa za serikali, kuwahi kazini na kujiendeleza kielimu. Amewaasa pia kujiepusha na vitendo vya rushwa, majungu, uchochezi, chuki, ubaguzi na upendeleo wa aina yeyote.
Mkurugenzi Msaidizi Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Aurelia Matagi akizungumza na watumishi wa Idara hiyo wakati akimkaribisha Bw. Msambachi kuzungumza nao.
 Kikao kikiendelea katika ukumbi wa Ngorongoro.
Picha ya pamoja.

Friday, June 10, 2016

SERIKALI YA TANZANIA NA ZAMBIA ZASAINI MAKUBALIANO YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA KUDHIBITI USAFIRISHAJI WA MAZAO YA MISITU NA MAGOGO KUPITIA MIPAKA YA NCHI HIZO

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (katikati) akisaini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Zambia,  jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususan magogo katika mipaka ya nchi hizo mbili. Wanaoshuhudia kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili, Gladynes Mkamba na Kaimu Mtendaji Mkuu TFS, Richard Kamwenda (kushoto). Waliosimama kulia ni Mwanasheria wa TFS, David Mung’ong’o na Mwanasheria wa Wizara ya Maliasili, Stephen Mwamasenjele. 
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda akisaini  makubaliano hayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda wakibadilishana hati ya makubaliano waliyosaini kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo katika mipaka ya nchi hizo. 
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi akizungumza katika hafla fupi ya kuweka makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Zambia jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo katika mipaka ya nchi hizo. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda. Maj. Gen. Milanzi alisema kuwa ushirikiano huo utaleta tija katika udhibiti wa biashara haramu ya uvunaji na usafirishaji wa magogo kutoka katika nchi hizo kwenda nchi nyingine kupitia mipaka ya nchi hizo na bandari ya Dar es Salaam. Aliwataka watanzania wanaojihusisha na biashara haramu ya uvunaji na usafirishaji wa magogo nje ya nchi waache mara moja kwani Serikali imejipanga kuhakikisha wanakamatwa na sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda wakiteta jambo wakati wakikagua Makontena 103 ya magogo (nyuma pichani) yaliyokamatwa hivi karibuni katika bandari ya Dar es Salaam kutoka nchini Zambia na DRC. Makatibu Wakuu hao wamesaini makubaliano ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo kwenye mipaka wa nchi hizo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda wakiangalia sehemu ya magogo yaliyokamatwa hivi karibuni katika bandari ya Dar es Salaam kutoka nchini Zambia na DRC. Makatibu Wakuu hao wamesaini makubaliano ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo kwenye mipaka wa nchi hizo.

........................................................................................... 

Serikali ya Tanzania na Zambia zimesaini makubaliano ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo katika maeneo ya mpakani kwa lengo la kulinda misitu na kuimarisha uhifadhi katika nchi hizo.

Makubaliano hayo yalitiwa saini jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili  na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya  Maliasili, Ardhi na Hifadhi ya Mazingira ya nchini  Zambia, Bw. Trevol Kaunda na kushuhudiwa na Wajumbe kutoka Zambia na Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mara  baada ya kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii  Maj. Gen. Gaudence Milanzi alisema hatua hiyo imefikiwa ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zilizopo za uharibifu wa misitu na usafirishaji wa mazao ya misitu na magogo kupitia mipaka ya nchi hizo.

Makubaliano hayo yalifikiwa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha siku tatu cha wajumbe kutoka nchi hizo mbili cha kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta misitu maeneo ya mpakani.

katika kikao hicho Tanzania iliwakilishwa na wajumbe kutoka taasisi za Serikali ambazo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  Mamlaka ya Bandari (TPA),  Ofisi ya Mwendesha Mashitaka  Mkuu wa Serikali na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Katika hatua nyingine mara baada ya kusaini makubaliano hayo, msafara wa Makatibu Wakuu hao ulitembelea Bandari ya Dar es Salaam kukagua shehena ya magogo yaliyokamatwa katika bandari hiyo kuanzia mwezi Novemba mwaka jana kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.

Maj. Gen. Milanzi alisema kuwa jumla ya makontena ya magogo hayo ni 103 ambapo makotena 56 yalikamatwa kuanzia mwezi Novemba mwaka jana yakidaiwa kutoka nchini Zambia na makontena mengine 47 yaliyodaiwa kutoka DRC ambayo yamekamwatwa kuanzia mwezi Januari mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada kukagua makontena hayo, Maj. Gen. Milanzi alisema "Napenda kuwaasa wananchi wanaojihusisha na biashara hii haramu ya kusafirisha magogo waache mara moja kwani inasababisha uharibifu mkubwa wa misitu na endapo tutawakamata tutawachukulia hatua kali za kisheria”.

Kwa upande wake  Katibu Mkuu wa  Wizara ya  Maliasili, Ardhi na Mazingira wa Zambia, Bw. Trevol Kaunda alisema kuwa “Ushirikiano baina ya pande hizi mbili utaleta ufanisi katika suala la uhifadhi wa misitu yetu kwa kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakisafirisha magogo na mazao ya misitu kwa kutumia njia danganyifu, umoja huu utatusaidia kuwabaini ni kuwachukulia hatua stahiki”.

Aliongeza kuwa makubaliano hayo ni mwanzo mzuri wa kuweza kufanya kazi kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika mpaka wa Tunduma ambako mazao ya misitu na magogo toka nchini Zambia yamekuwa yakipitishwa kwenda bandari ya Dar es Salaam na baadae nje ya nchi.

Akizungumzia hatima ya magogo hayo Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohammed Kilongo alisema kuwa “Wafanyabishara wote waliokamatwa na magogo haya wametakiwa kuleta vielelezo halali vya uvunaji na usafirishaji wake jambo ambalo wameshindwa kutekeleza mpaka sasa, muda tuliowapa ukiisha utaratibu wa kuwafungulia mashitaka utafuata ili sheria ichukue mkondo wake”.


Sunday, June 5, 2016

MINISTER OF NATURAL RESOURCES AND TOURISM PROF. JUMANNE MAGHEMBE MEETS AMERICAN JOURNALIST ROBERT ROSS

American Journalist Robert Ross (RIGHT) handing over his book called "The Selous of Africa: A long Way from Anywhere" to the Minister of Natural Resources and Tourism, Hon. Prof. Jumanne Maghembe when visited his office recently. The book contains more than 100,000 shots of fauna, flora and dramatic landscapes of Selous Game Reserve. The book will be an important agent in promoting Tanzanian Tourism Worldwide. 
Prof. Maghembe (left) perusing the book, Left is Dr. Ross. The book is published by Officina Libraria and distributed in the U.S. by ACC. It is available to buy now on Amazon. The book was launched by the Minister through his representative Deputy Permanent Secretary Eng. Angelina Madete on 3rd June, 2016, Slipway Hotel, Dar es Salaam.

Thursday, June 2, 2016

WAZIRI WA MALIASILI PROF. JUMANNE MAGHEMBE AIOMBA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA SERIKALI KWA VITENDO KATIKA VITA DHIDI YA UJANGILI

Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kulia) akipokea ndege maalum aina ya drones kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) Dkt. Marco Lambertini (wa tatu kushoto) kwa ajili ya kusaidia doria za kiitelijensia za kupambana na ujangili katika pori la akiba la Selous. Wengine katika picha ni kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa WWF - Tanzania, Amani Ngusaru, Meneja wa Pori hilo la Akiba  Selous,  Mabula Misungwi, Mwenyekiti wa bodi ya WWF - Ujerumani, Dkt. Valentin Von Moscow, Mkurugenzi Mtendaji WWF – Ujerumani, Ebenhard Brandes na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Kuzuwia Ujangili, Faustine Ilobi Masalu. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto), Viongozi wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) na Viongozi wengine wa Wizara wakipokea maelekezo kutoka kwa Mtaalam wa uendeshaji wa ndege maalum aina ya drones na jinsi zinavyofanya kazi, Parmena Elisa, ndege hizo zilitolewa na Mfuko wa WWF kusaidia doria za kiitelijensia za kupambana na ujangili katika pori la akiba la Selous jana tarehe 1 Julai, 2016 Matambwe Selous.
Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya ndege maalum aina ya drones zilizotolewa na Mfuko wa WWF kusaidia doria za kiitelijensia za kupambana na ujangili katika pori la akiba la Selous. Wengine katika picha ni Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) Dkt. Marco Lambertini (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji WWF – Ujerumani, Ebenhard Brandes (kushoto). 
Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) Dkt. Marco Lambertini (wa pili kushoto) akimkabidhi, Namsifu Johannes Marwa (Mhifadhi Wanyamapori), Tuzo ya WWF ya Mhifadhi Bora kwa mchango wake alioutoa katika kupambana na ujangili katika pori la akiba la Selous. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto), Mkurugenzi Mtendaji WWF – Ujerumani, Ebenhard Brandes na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Kuzuwia Ujangili Wizara ya Maliasili, Faustine Ilobi Masalu (wa nne kushoto), tuzo hiyo ilitolewa Matambwe Selous tarehe 1 Julai, 2016. 
Picha ya pamoja.

.....................................................................................................

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ameiomba Jumuiya  ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupiga vita ujangili kwa vitendo katika kuimarisha uhifadhi nchini.Prof. Maghembe alisema hayo jana, Matambwe Selous, katika hafla fupi ya makabidhiano ya ndege maalum 8 zilizotolewa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) kwa Wizara ya Maliasili na Utalii.Ndege hizo ndogo aina ya drones ambazo hazitumii rubani na huongozwa na mitambo maalum zitatumika katika pori la akiba la Selous kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa Wanyamapori kwa kukusanya taarifa za kiitelijensia zitakazosaidia kukamatwa majangili. Ndege hizo zina thamani ya dola za kimarekani 80,000 sawa na zaidi ya Tsh  milioni  172.


"Msaada huu umekuja wakati muafaka ambapo Pori la Akiba la Selous linahitaji teknolojia za kisasa katika kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili ndani na kuzunguka hifadhi hii" alisema Prof. Maghembe.

Alieleza kuwa changamoto kubwa inayoikabidili hifadhi ya Selous ni ujangili ambao kwa kiasi kikubwa umesababisha idadi ya Wanyamapori hususani tembo kupungua kwa kasi kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa mwaka 1986 idadi ya tembo katika pori hilo ilikuwa  50,000, idadi ambayo iliongezeka mwaka 2003 na kufikia 70,000 baada ya Serikali ya Ujerumani kusaidia kuanzishwa kwa Mpango wa Kuendeleza Selous (Selous Conservation Program) na Serikali ya Tanzania kukubali aslimia 50 ya makusanyo yanayotokana na utalii yabaki kuendeleza uhifadhi katika pori hilo.

Alisema kuwa baada ya mradi huo kuisha na mfumo wa “retention” kuondolewa na Serikali hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi ambapo kati ya mwaka 2008 na 2011 vitendo vya ujangili viliongezeka maradufu, sensa ya mwaka 2013 ilionesha idadi ya tembo hao kupungua hadi kufikia 13,000.

Prof. Maghembe aliongeza kuwa pamoja na hayo Serikali imejipanga kuhakikisha Wanyamapori wanalindwa usiku na mchana na kwamba wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ujangili watakamatwa na kufikishwa mahamani ili sheria ichukue mkondo wake.


"Hatutawavumilia hawa watu wamalize wanyamapori wetu wote tulionao, tunawafuatilia usiku na mchana na lazima tutawakamata" alisisitiza Prof. Maghembe.Aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na washirika wa uhifadhi imechukua hatua za makusudi za kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuanzishwa kwa mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori, mpango ambao umekuwa na matokeo mazuri baada ya kuungwa mkono na washirika hao kwa kusaidia fedha, vifaa na misaada mbalimbali ya kiufundi.


Aliongeza kuwa sehemu ya mpango wa Serikali wa kukabiliana tatizo hilo ni kuanzishwa kwa Jeshi Usu (Paramilitary) ambapo maeneo yote ya hifadhi nchini yatalindwa kijeshi. 

Prof. Maghembe ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine ili kukomesha ujangili ni lazima mataifa yaliyoendelea ambayo ndiko yaliko masoko makubwa ya meno ya tembo na bidhaa zake kusitisha kabisa uingizwaji wa meno hayo katika nchi zao ili kukomesha biashara hii haramu.

“Kuna nchi ambazo tayari zimechukua hatua ya kukataza kabisa uingizwaji wa meno ya tembo nchini mwao, mfano Marekani, tunaiomba sana jumuiya ya kimataifa wakiwemo marafiki zetu China na nchi nyingine wakatae kabisa uingizwaji wa meno haya nchini mwao, hii itasaidia sana kukomesha biashara hii haramu” Alisema.

Katika hatua nyingine Prof. Maghembe aliwataka wafugaji walioingiza mifugo katika maeneo yote ya hifadhi nchini waondoe mifugo yao kwa hiari kabla ya kushinikizwa kufanya hivyo na Serikali kwa mujibu wa sheria.

Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 Ibara ya 18 (2) inasema “Si ruhusa mtu yeyote kuingia na kulisha mifugo ndani ya Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Ardhioevu”

Prof. Maghembe alisema kuwa “mtandao wa ujangili unaanzia na watu wanaoingiza mifugo ndani ya hifadhi, hivyo ni lazima sheria zifuatwe  na waondoke mara moja, watakaokaidi sheria itafuata mkondo wake na mifugo itakayokamatwa itataifishwa na Serikali kwa mujibu wa sheria za nchi, sheria hizi hazina tofauti na sheria zinazokataza watu wasijenge mabondeni au kwenye hifadhi za barabara”  

Awali akitoa taarifa, Meneja wa Pori hilo la Akiba la Selous  Mabula Misungwi alieleza baadhi ya changamoto kuu zinazoikabili hifadhi hiyo kuwa ni pamoja na ujangili, miundombinu mibovu ya barabara kwa ajili ya doria na vifaa ikiwemo magari ya doria na nyumba za watumishi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) Dkt. Marco Lambertini alisema kuwa ili kuimarisha Uhifadhi nchini ni lazima wananchi waishi karibu na maeneo hayo na pia washirikishwe juu ya umuhimu wake ili wasaidie kuyalinda kwa faida yao na taifa kwa ujumla.