slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Tuesday, October 31, 2017

JANGILI AKAMATWA KABLA YA KUFANYA UHALIFU...

 "‪Jana tumefanikiwa kumkamata Ndg. Masalu Wella Nangale wa kijiji cha Mwasengela, Meatu, akijipanga kuelekea Moru, ndani ya hifadhi ya Serengeti kwa malengo ya kuua Faru. Amekutwa na risasi 356, magazines 2, msumeno mdogo na mafuta ya kusafishia silaha! ‬

Tutaendelea kutumia mbinu za kisasa zaidi za intelijensia kudhibiti ujangili. 
Tumekusudia kukamata majangili kabla hawajafanya ujangili kuliko kukamata nyara. 

Tutaisambaratisha na kuifumua kabisa mitandao ya biashara haramu ya ujangili nchini". Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla.

ZIARA YA NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, MHE. JAPHET HASUNGA KATIKA SHAMBA LA MITI SAO HILL NA KITUO CHA MALIKALE ISMILA NA KALENGA MKOANI IRINGA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipotembelea shamba la miti Sao Hill kukakua shughuli mbalimbali zinazofanywa na shamba hilo mkoani Iringa hivi karibuni. Aliagiza uongozi wa shamba hilo kuongeza juhudi za upandaji miti ili kukidhi mahitaji makubwa yaliyopo nchini na hivyo kusisimua ukuaji wa uchumi wa viwanda.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kulia) akikagua baadhi ya vifungashio vya asali alipotembelea shamba la miti Sao Hill kwa ajili ya kukakua shughuli mbalimbali zinazofanywa na shamba hilo mkoani Iringa hivi karibuni. Asali inayozalishwa na shamba hilo imefanyiwa vipimo nchini Ujerumani na kugundulika kuwa ni bidhaa bora isiyo na viambata vya kemikali ya aina yeyote. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza na Afisa Ufugaji Nyuki wa shamba hilo, Said Abubakar. 
Meneja wa shamba la miti Sao Hill, Salehe Beleko (kushoto) akimueleza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) kuhusu moto uliovamia hekta 77 za shamba hilo na hatua zilizochukuliwa kuudhibiti alipotembelea  kukakua shughuli mbalimbali zinazofanywa na shamba hilo mkoani Iringa hivi karibuni, alisema moto huo uliozuka hivi karibuni ulianzia kwenye mashamba ya wananchi haukuwa na madhara makubwa. 
Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill, Salehe Beleko (kulia) akimuelezea Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga kuhusu utafiti unaofanywa na shamba hilo kwa kushirikiana na Kampuni ya Art International kuhusu uvunaji wa utomvu kwa ajili ya kutengeneza madawa mbalimbali, bazooka (chewing gums) na ‘gel’ kwa ajili ya kujiongezea kipato alipotembelea shamba hilo kukagua shughuli mbalimbali hivi karibuni. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri David. 
Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill, Salehe Beleko (kulia) akimuelezea Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (hayupo pichani) kuhusu njia mpya ya kuzalisha mbegu za miti kwa njia ya vikonyo ili kuongeza zaidi uzalishaji alipotembelea shamba hilo kukagua shughuli mbalimbali hivi karibuni. Aliagiza uongozi wa shamba hilo kuongeza juhudi za upandaji miti ili kukidhi mahitaji makubwa yaliyopo nchini na hivyo kusisimua ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza (wa pili kulia) alipotembelea Kituo cha Mambo ya Kale cha Ismila kukakua shughuli mbalimbali zinazofanywa na kituo hicho mkoani Iringa hivi karibuni. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (wa pili kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza (kushoto) wakipata maelezo kutoka kwa Mhifadhi wa Mambo ya Kale, Laurent Nampunju (kulia) kuhusu fuvu la Chifu Mkwawa alipotembelea Makumbusho ya chifu huyo kukakua shughuli mbalimbali zinazofanywa na kituo cha Mambo ya Kale cha Kalenga mkoani Iringa hivi karibuni. 
Jengo la Makumbusho ya Mkwawa ambalo lipo ndani ya Kituo cha Mambo ya Kale cha Kalenga Mkoani Iringa.
 Picha ya Chifu Mkwawa ambayo inapatikana katika makumbusho hayo.
Muonekano wa fuvu la Chifu Mkwawa ambalo pia linapatikana katika makumbusho hayo. (Picha na Hamza Temba - WMU)

Sunday, October 29, 2017

SERIKALI YADHAMIRIA KUFUNGUA UTALII WA KANDA YA KUSINI, YAPO MAPOROMOKO YA PILI KWA KUWA NA KINA KIREFU ZAIDI BARANI AFRIKA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya Greens Construction Limited, Hamimu Bakari wakati akishuka kwenye ngazi maalum zinazojengwa na mkandarasi huyo kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 

Na Hamza Temba - WMU
...............................................................
SERIKALI imesema imedhamiria kufungua utalii wa Kanda ya Kusini ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini na hatimaye kuongeza idadi ya watalii na kipato kwa Serikali na jamii kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga katika kijiji cha Kapozwa Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea Maporomoko ya Mto Kalambo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya Maporomoko ya Tugela yaiyopo nchini Afrika ya Kusini.

Alisema kwa sasa vivutio vingi vinavyotumika kwa utalii nchini ni vile vya ukanda wa Kaskazini hususan vya wanyamapori ambavyo vimeanza kuelemewa kutokana na watalii wengi kutembelea ukanda huo zaidi kuliko Kanda ya Kusini ambayo pia ina vivutio mbalimbali vya asili.

Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo benki ya Dunia kupitia mradi wa REGROW imepanga kuboresha miundombinu ya vivutio vya utalii vya Kanda ya Kusini na kuvitangaza ili kuimarisha sekta hiyo muhimu ambayo inachangia asilimia 25 ya mapato yote ya kigeni na asilimia 17.5 ya pato la taifa.

Katika ziara yake hiyo Mkoani Rukwa, alitembelea eneo la Hifadhi ya Msitu ya Mto Kalambo na kukagua ujenzi unaoendelea wa ngazi maalum zitakazowawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo ambacho ni mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 

Alisema Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania inajenga ngazi hizo ili kuongeza thamani ya maporomoko hayo huku akiagiza Wakala hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine kuongeza juhudi za uwekezaji ili kuimarisha utalii wa kivutio hicho na kupanua kanda yote ya kusini.

"Tumekusudia kupanua wigo wa vivutio vyetu vya utalii kwa kufungua Kanda hii ya Kusini ambayo ina vivutio vingi ambavyo havijachangia ipasavyo kwenye uchumi wetu, maporomoko haya ni moja ya kivutio adimu katika ukanda huu. 

"Ni wakati muafaka sasa tushirikiane kuhamasisha wawekezaji kujenga mahoteli ya kisasa katika eneo hili, tuone uwezekano wa kuanzisha utalii wa 'cable cars' kuwezesha watalii kuona maporomoko kiurahisi, tujenge maeneo ya kupumzikia ili kuweka mazingira rafiki ya kupata watalii wengi na mapato yaongezeke" alisema Hasunga.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Kapozwa ambao wanaishi jirani na hifadhi hiyo kushirikiana na Serikali katika uhifadhi wa uoto wa asili wa hifadhi hiyo pamoja na kudumisha tamaduni zao kwa kusajili vikundi vya ngoma na kutunga nyimbo za kabila lao kwa ajili ya kutumbuiza watalii watakaofika kuona maporomoko hayo na hivyo kujitengenezea kipato kupitia utalii wa Kiutamaduni.

Pamoja na Maporomoko hayo kivutio vingine kinachopatikana ukanda wa kusini ni Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni ya kwanza kwa ukubwa nchini ikifuatiwa na hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hifadhi hii inasifika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo.

Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ni kivutio kingine katika ukanda huu ambacho sifa yake kubwa ni uwepo wa aina nyingi za maua ndwele ya asili ambayo hayapatikani kwingineko duniani, sifa hiyo imesababisha wenyeji kuita hifadhi hiyo 'Bustani ya Mungu'. Wataalamu wa uhifadhi wanasema endapo maua yaliyopo Kitulo yangekuwa ni wanyamapori basi hifadhi hiyo ingeizidi wanyama waliopo Serengeti.

Vivutio vingine ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambayo ni ya tatu kwa ukubwa nchini, Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa, Mikumi, Mahale, Gombe, Pori la Akiba la Selous, Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Mlima Rugwe, Kimondo cha Mbozi n.k.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) akiteta jambo na Katibu Tawala Wilaya ya Kalambo Frank Schalwe wakati akishuka kwenye ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. 
Meneja wa TFS Wilaya ya Kalambo, Joseph Chezue (kushoto) akimuonyesha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18.
 Muonekano wa ngazi hizo kuelekea kwenye Maporomoko ya Mto Kalambo.
Muonekano wa ngazi hizo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukagua ujenzi wa ngazi maalum zinazojengwa kwa ajili ya kuwawezesha watalii kushuka hadi kwenye kina cha Maporomoko ya Mto Kalambo wakati wa ziara yake mkoani Rukwa. Maporomoko hayo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika baada ya TUGELA yaliyopo Afrika ya Kusini yana kina cha mita 235 na upana kati ya mita 3.6 hadi 18. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura. 
Baadhi ya washiriki wa ziara hiyo wakishuka kwenye ngazi ambazo ujenzi wake bado unaendelea. Ujenzi huo ukikamilika ngazi hizo zitakuwa na urefu wa mita 227.
Ngazi hizo zimejengwa kwenye ukingo wa korongo la Mto Kalambo.
Sehemu ya juu ya Maporomoko ya Mto Kalambo.
 Muonekano wa mto Kalambo ambao unaotengeneza Maporomoko ya Mto Kalambo (Kalambo Falls)
Taswira ya maporomoko ya mto Kalambo kutokea angani (Picha hii ni kwa hisani ya Mtandao)

TAMKO LA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, DK. HAMISI KIGWANGALLA KUHUSU MIFUGO LOLIONDO


Saturday, October 28, 2017

FALSAFA YA 'UHIFADHI ENDELEVU NI UHIFADHI SHIRIKISHI JAMII'

Na. Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii.
.......................................................................
Katika kuleta uhifadhi endelevu, tatizo letu la msingi si wananchi kuvamia hifadhi kwa maksudi, wala si chuki ya wahifadhi dhidi ya wananchi, ni kwamba idadi ya watu imeongezeka, idadi ya mifugo imeongezeka, eneo limebaki lile lile, na kuna mabadiliko ya tabia nchi.

Hivyo hakuna sababu ya kupambana na matokeo yanayotokana na uwepo wa tatizo kubwa la msingi, badala yake ni busara kuanza kutatua tatizo la msingi.

Ujumbe wangu kwa wananchi umekuwa huu. Kwamba, tuanze kushughulika na tatizo la msingi, tena kwa pamoja na kwa umoja wetu.

Mfano, eneo la hifadhi ya Ngorongoro mwaka 1959 kulikuwa na wakazi 8,000 wakiishi humo, ikatungwa sheria kwamba wanaweza kuishi pamoja (co-exist). Leo kuna wananchi 92,000 kwenye eneo lile lile la kilometa za mraba 8292. Idadi ya watu imekua zaidi ya mara 10. Kwa utamaduni wa wafugaji, kila anayezaliwa na kukua atakuwa na boma lake na mifugo yake.

Pamoja na mabadiliko haya, bado wananchi hawajabadilika na sisi wahifadhi hatujabadilika.

Ufugaji kwenye zama hizi hauwezi kuwa ule ule wa 1959. Lazima tuendeleze maeneo ya malisho, maeneo ya maji, masoko ya uhakika ya mifugo, wafugaji wabadilike waanze kuvuna mifugo yao, kuwe na kanuni za kijamii za kuongoza uvunaji, kuwe na mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuwa na mbegu bora za mifugo yenye tija kwa kutoa maziwa mengi ama kuwa na nyama nyingi na hivyo kuvutia bei kubwa zaidi.

Sisi wahifadhi lazima tuwe na namna ya kushirikiana na wananchi kutekeleza azma hii. Tutoe dira na mwongozo huu ili atakayekiuka sasa naye awe mchokozi na akutane na adhabu kali! Hii ndiyo falsafa yangu ya uhifadhi endelevu.

Maana hata kama tukisema tuache kuhifadhi maeneo haya, miaka mitatu haitozidi, wananchi hawatokuwa na malisho wala maji ya mifugo yao. Inawezekana hii sayansi hawaielewi sana, lakini sisi kama serikali tukiwashirikisha na kuwapa motisha wanaweza kubadilika na kuona tija ya uhifadhi.

Uhifadhi chini ya uongozi wangu kwenye Wizara hii utakuwa shirikishi. Ni lazima tuwekeze kwa wananchi wanaotuzunguka kama tunataka hifadhi zibaki salama na wananchi watupe ushirikiano kwenye kazi yetu ya msingi - uhifadhi.

Wananchi wanahitaji malisho ya mifugo, maji ya kunywesha mifugo, maji ya kumwagilia mashamba yao, elimu ya ufugaji wa kisasa/kilimo cha kisasa, soko la uhakika la mifugo yao, soko la uhakika la mazao yao, na taarifa sahihi za umuhimu wa hifadhi ya uoto wa asili na wanyamapori kwa maisha yetu sisi tunaoishi leo na dhamana tuliyonayo kwa vizazi vijavyo.

Sisi, Wizara ya Maliasili na Utalii, tutatoa mfano wa kuwekeza kwenye jamii inayotuzunguka; wenzetu wa Halmashauri, Ardhi, Mazingira, Kilimo na Mifugo nao wafanye kwa upande wao.

Tuandae mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo yote nyeti jirani na hifadhi zetu, tuwekeze kwenye kutenga na kuendeleza maeneo ya malisho ya mifugo na maeneo kwa ajili ya kilimo, tuwekeze kwenye kutoa elimu ya ufugaji wa kisasa, kilimo rafiki kwa mazingira na kuwawezesha wananchi kuuza mifugo yao na mazao yao kwa bei nzuri.

Tumehangaika sana kukamata mifugo ya wananchi, kuendesha operesheni za kuwaondoa wananchi kwenye maeneo ya hifadhi mpaka tukasahau kazi yetu ya msingi ya 'uhifadhi', kupambana na majangili, kutangaza vivutio vyetu vya utalii, kuendeleza sekta yetu. Sasa basi. Tubadilike. Sisi hatuna jukumu la kuchunga ng'ombe wa wananchi, ama kupambana nao mahakamani. Jukumu letu ni uhifadhi endelevu.

Turudi kwenye kazi yetu ya msingi, tupambane na majangili, tushirikishe wananchi kwenye uhifadhi. Tuondoe uadui na uhasama baina yetu na wananchi, tujenge ujirani mwema. Tutafanikiwa zaidi.

Sambamba na hilo, tutaongeza adhabu kwa wavamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa na tutakuwa wakali zaidi baada ya hapo. Wananchi pia wanapaswa waelewe kuwa kuna maeneo si ya kusogelea!

Kwa hakika, 'uhifadhi endelevu ni uhifadhi shirikishi jamii'.

Thursday, October 26, 2017

NAIBU WAZIRI ATIMUA WANANCHI WALIOVAMIA HIFADHI YA KATAVI, AAGIZA WATUMISHI WALIOPIMA VIWANJA NDANI YA ENEO LA HIFADHI WACHUKULIWE HATUA ZA KISHERIA


Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kushoto) akipokea taarifa ya Serikali ya Mkoa wa Katavi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo Mej. Jen. Mst. Rafael Muhuga baada ya kusomwa mbele yake jana alipotembelea mkoa huo kwa ajili ya kutatua migogoro ya hifadhi na wananchi.

NA HAMZA TEMBA -WMU-KATAVI
..............................................................
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, amewataka  wananchi wa Kitongoji cha Situbwike ambao wamevamia Hifadhi ya Taifa ya Katavi na kuanzisha shughuli za kibinadamu kinyume cha sheria waondoke kwa hiari ndani ya wiki mbili zijazo kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Naibu Waziri Hasunga amesema hayo jana katika Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi baada ya kutembelea kitongoji hicho chenye kaya zaidi ya 82 ndani ya hifadhi hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi nchini.

"Naagiza, mamlaka husika muhakikishe wananchi hawa wanahama ndani ya wiki mbili zijazo, lazima sheria ziheshimiwe, ifikapo tarehe 10 Novemba, hatutaki tukute mtu hapa, atakayekaidi kitakachompata asitulaumu" aliagiza Naibu Waziri Hasunga.

Kwa upande wa wananchi wa kitongoji hicho ambao wamevamia hifadhi hiyo na kuanzisha shughuli za kilimo, makazi na ufugaji walikiri kuwa wapo ndani ya hifadhi na kwamba walipewa eneo hilo bila ya wao kujua na uongozi wa kijiji cha Stalike ambao kwa sasa haupo madarakani.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga alisema Serikali ya Wilaya hiyo ilitoa notisi ya siku 30 kwa wananchi hao waondoke jambo ambalo halijatekelezwa huku taarifa zikieleza kuwa baadhi yao wamekaidi kuondoka kwa madai kuwa mpaka waone polisi ndio watakusanya virago vyao.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Hasunga ameuagiza uongozi wa TANAPA kuendelea na zoezi la uwekaji wa vigingi vya mpaka katika eneo hilo la hifadhi lenye mgogoro ikiwa ni pamoja na kupima umbali wa mita 500 kutoka kwenye mpaka huo na kuweka mabango yanayoonyesha kuwa eneo hilo haliruhusiwi kwa shughuli za kibinadamu kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mwailwa Pangani kuwatafuta maafisa ardhi waliohusika kuwapimia wananchi wa kitongoji cha Mgolokani eneo la makazi ndani ya hifadhi ya msitu wa Msanginya kinyume cha sheria.

"Nakuagiza Mkurugenzi wa halmashauri, wale wote waliopima eneo hili ndani ya hifadhi hii watafutwe wahojiwe, labda walikuwa na sababu, wakikutwa na makosa wachukuliwe hatua stahiki za kisheria, hawa wanapaswa kuwajibika" alisema Naibu Waziri Hasunga.

Aidha, alimuagiza mkurugenzi huyo kutafuta maeneo kwa ajili ya kuwagawia wananchi waliondolewa katika hifadhi hiyo ya msitu pamoja na wale walioondolewa hifadhi ya taifa ya Katavi waweze kuanzisha makazi mapya, kilimo na ufugaji.

Mwisho alitoa wito kwa watumishi wa Serikali, taasisi na mamlaka zote za Serikali kufanya kazi kwa ushirikiano kuepuka migogoro isiyo ya lazima inayosababishwa na mkanganyiko wa maamuzji baina ya viongozi wa Serikali.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mej. Jen. Mst. Rafael Muhuga (kulia) alipotembelea mkoa huo jana kwa ajili ya kutatua migogoro ya hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga akizungumza katika kikao na Mkuu wa Mkoa wa Katavi alipotembelea mkoa huo jana kwa ajili ya kutatua migogoro ya hifadhi.
Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mej. Jen. Mst. Rafael Muhuga, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Katavi na viongozi wa watumishi wa TANAPA,TFS na TAWA. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kushoto) akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mej. Jen. Mst. Rafael Muhuga (kulia) baada ya mazungumzo mafupi ofisini kwake alipotembelea mkoa huo jana kwa ajili ya kutatua migogoro ya hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kulia) akikagua eneo lililovamiwa na wananchi wa Kitongoji cha Situbwike na kuanzisha makazi na shughuli za kilimo na ufugaji ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi,  aliagiza wananchi hao kuondoka kwa hiari ndani ya siku 14 kabla ya kuondolewa kwa nguvu alipotembelea hifadhi hiyo jana mkoani Katavi. Kushoto ni Diwani wa Kata ya Stalike, Adam Chala.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (wa nne kushoto) akikagua moja ya kigingi cha mpaka kilichovunjwa na wananchi wa Kitongoji cha Situbwike ambao wamevamia Hifadhi ya Taifa ya Katavi na kuanzisha makazi na shughuli za kilimo na ufugaji, aliagiza wananchi hao kuondoka kwa hiari ndani ya siku 14 kabla ya kuondolewa kwa nguvu alipotembelea hifadhi hiyo jana mkoani Katavi. Kulia na Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Martin Loibooki.
Baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Situbwike ambao wamevamia hifadhi ya Taifa ya Katavi na kuanzisha makazi na shughuli za kilimo na ufugaji kinyume cha sheria wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (hayupo pichani) wakati akiwapa maelekezo ya kuondoka hifadhini hapo kwa hiari ndani siku 14 zijazo kabla ya kuondolewa kwa nguvu alipotembelea hifadhi hiyo jana mkoani Katavi.

Baadhi ya nyumba za makazi zilizojengwa ndani ya hifadhi ya Taifa ya Katavi kinyume cha sheria. Akiwa Mkoani Katavi jana, Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga ameagiza wananchi waliovamia hifadhi hiyo wahamishe makazi yao kwa hiari ndani ya wiki mbili zijazo kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

DK. KIGWANGALLA ATUA LOLIONDO, AFANYA KIKAO NA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA YA WILAYA YA NGORONGORO

NA MWANDISHI WETU
.................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amewasili Makao makuu ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha na kufanya mkutano maalum na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo ambapo pia atatembelea maeneo yenye migogoro. 

Waziri, Dkt.Kigwangalla amewasili katika uwanja mdogo wa Wasso uliopo tarafa ya Loliondo na kisha kukutana na viongozi hao wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Rashid Mfaume Taka. 

Dk Kigwangalla baada ya kumaliza kikao hicho maalum na wakuu hao, anatarajia kutembelea maeneo yenye migogoro ili kupata picha halisi na kubaini kiini cha mgogoro wa eneo hilo la Pori Tengefu Loliondo.

Aidha, anatarajia kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Tarafa ya Loliondo kwa ajili ya kusikiliza kero zao mbalimbali. 

Waziri, Dkt.Kigwangalla yupo Mkoani Arusha kwa ajili ya ziara ya kikazi ambapo awali alianza kutembelea Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ambapo pia aliweza kukutana na jamii ya wafugaji wanaoishi kwenye hifadhi ya Ngorongoro.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akishuka kwenye ndege wakati akiwasili Loliondo kufuatilia kwa kina mgogoro unaoendelea Loliondo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiongozana na na viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro kwenye uwanja wa ndege wakati akiwasili Loliondo kufuatilia kwa kina mgogoro unaoendelea wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya hiyo Mh. Rashid Mfaume Taka akimwakilisha Waziri Dk.Kigwangalla katika mkutano huo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama

Wednesday, October 25, 2017

DK. KIGWANGALLA AFANYA ZIARA MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.  Dkt. Hamisi Kigwangalla amefanya ziara ya kikazi katika ofisi za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambapo amezungumza na viongozi na watumishi wa Mamlaka hiyo. Katika ziara hiyo ametembelea pia maeneo ya hifadhi yenye mgogoro kwa ajili kuyatafutia ufumbuzi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akipokelewa na viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro alipowasili makao makuu ya hiyo leo Oktoba 25,2017

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (kushoto)  akipata maelezo kutoka Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk. Fredy Manongi (wapili kulia)

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (kulia) akipata maelezo kuhusu eneo la hifadhi ya Ngorongoro kutoka kwa Naibu Mhifadhi wa Mamlaka hiyo, Assangye Bangu.

Waziri wa Maliasili na Utalii,  Dkt. Hamisi Kigwangalla akisikiliza maoni kutoka kwa viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro .

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dk. Freddy Manongi akizungumza wakati wa kumkaribisha Waziri wa Maliasili, Dkt. Hamisi Kigwangalla aweze kuzungumza na watumishi.

Tuesday, October 24, 2017

WIZARA YA MALIASILI, ARDHI NA TAMISEMI KUMALIZA MGOGORO WA MPAKA WA HIFADHI YA NORTH UGALA NA VIJIJI JIRANI

NA HAMZA TEMBA- WMU- URAMBO, TABORA
...................................................................................
Naibu Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema Wizara yake itashirikiana na Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kutoa uamuzi wa pamoja wa kumaliza mgogoro wa mpaka baina ya Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja wilayani Urambo .

Naibu Waziri Hasunga amesema hayo mkoani Tabora jana wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo. Akiwa mkoani humo alitembelea eneo lenye mgogoro, akafanya mkutano wa hadhara na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali kwa ajili ya kutafuta majibu ya kutatua mgogoro huo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme, Mkazi wa Kijiji hicho, Ramadhan Rashid alisema wananchi wa vijiji hivyo wanailalamika Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu kwa kusogeza mpaka wa hifadhi hiyo hadi ndani ya ardhi ya vijiji wakati wa uwekaji wa vigingi vipya vya mpaka. Alisema eneo hilo ni la vijiji hivyo tangu mwaka 1988.

Naye, Mkuu wa Kanda ya Magharibi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Peter Maiga alisema hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 1956 ikiwa na hekta 165,282 huku mipaka yake halisi ikiwa haijabadilishwa. Alisema zoezi la uwekaji wa vigingi vipya vya mpaka lilizingatia mipaka halisi kwa kutumia mfumo wa GPS.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Urambo, Magreth Sitta akizungumza kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo kwenye mkutano huo, alisema idadi ya wananchi inaongezeka huku maeneo yakiwa hayaongezeki hivyo akaiomba Serikali ione uwezekano wa kuwaongezea wananchi maeneo ya kulima na kuendeshea maisha yao.

Akijibu malalamiko na maombi ya wananchi hao wa Urambo, Naibu Waziri Hasunga alisema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutatua kero za wananchi sambamba na kuwaletea maendeleo.

“Baada ya kukagua eneo hili na kusikiliza pande zote, tunaenda kukaa pamoja na Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi tuangalie ramani zote zilizopo, Matangazo ya Serikali (GN) na taarifa mbalimbali ili tujiridhishe ni ipi mipaka halali tufikie ufumbuzi wa mwisho, migogoro ya namna hii haiwezi kuisha bila kushirikisha wizara hizi.

“Nawaagiza watendaji wangu kwenye taasisi mshirikiane na wananchi muwaelimishe na mzuie wasiendelee na uharibifu hadi hapo tutakapopata suluhu ya mgogoro huu”. alisema Naibu Waziri Hasunga.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo aliwataka wananchi wa vijiji hivyo kujiepusha na vitendo vya kuingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. “Mkiingiza mifugo tukaikuta tutaitaifisha kwa mujibu wa sheria” alisema Naibu Waziri Hasunga.  

Aidha aliwataka wananchi hao kujikita kwenye shughuli za ufugaji nyuki kibiashara kwa kutumia mizinga ya kisasa ambayo huongeza uzalishaji. “Asali ina soko zuri duniani kwa sasa, bei yake ni nzuri, kila mtu afuge tuchangie uchumi wa taifa letu” alisema Hasunga.

Naibu Waziri Hasunga ataendelea na ziara yake ya kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi katika mikoa wa Katavi, Rukwa na Songwe.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kangeme kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo
 Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kulia) akijibu kero mbalimbali za wananchi wa kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (katikati) akisikiliza maelezo ya Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kigwa (kushoto) kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (katikati) akiteta jambo Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kigwa (kulia) na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Urambo, Mussa Mohammed (kushoto) kuhusu mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (wa pili kushoto) akikagua ramani ya eneo lenye  mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja alipokagua eneo hilo katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana. Alisema Wizara yake itakutana na Wizara ya TAMISEMI na Ardhi kwa ajili kutoa uamuzi wa kumaliza mgogoro huo
 Mbunge wa Jimbo la Urambo, Magreth Sitta akizungumza katika mkutano huo.
 Mmoja ya wananchi akitoa kero yake katika mkutano huo.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kangeme wakimpongeza kwa kumpigia makofi, Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (hayuko pichani) baada ya kutoa ahadi ya kutatua mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Msitu wa North Ugala na vijiji jirani vya Kangeme, Utenge na Mtakuja kwa kushirikisha Wizara ya TAMISEMI na Ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kangeme wilaya ya Urambo mkoani Tabora jana.

Mkutano ukiwa unaendelea.