Na. Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii.
.......................................................................
Katika kuleta uhifadhi endelevu, tatizo letu la msingi si wananchi kuvamia hifadhi kwa maksudi, wala si chuki ya wahifadhi dhidi ya wananchi, ni kwamba idadi ya watu imeongezeka, idadi ya mifugo imeongezeka, eneo limebaki lile lile, na kuna mabadiliko ya tabia nchi.
Hivyo hakuna sababu ya kupambana na matokeo yanayotokana na uwepo wa tatizo kubwa la msingi, badala yake ni busara kuanza kutatua tatizo la msingi.
Ujumbe wangu kwa wananchi umekuwa huu. Kwamba, tuanze kushughulika na tatizo la msingi, tena kwa pamoja na kwa umoja wetu.
Mfano, eneo la hifadhi ya Ngorongoro mwaka 1959 kulikuwa na wakazi 8,000 wakiishi humo, ikatungwa sheria kwamba wanaweza kuishi pamoja (co-exist). Leo kuna wananchi 92,000 kwenye eneo lile lile la kilometa za mraba 8292. Idadi ya watu imekua zaidi ya mara 10. Kwa utamaduni wa wafugaji, kila anayezaliwa na kukua atakuwa na boma lake na mifugo yake.
Pamoja na mabadiliko haya, bado wananchi hawajabadilika na sisi wahifadhi hatujabadilika.
Ufugaji kwenye zama hizi hauwezi kuwa ule ule wa 1959. Lazima tuendeleze maeneo ya malisho, maeneo ya maji, masoko ya uhakika ya mifugo, wafugaji wabadilike waanze kuvuna mifugo yao, kuwe na kanuni za kijamii za kuongoza uvunaji, kuwe na mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuwa na mbegu bora za mifugo yenye tija kwa kutoa maziwa mengi ama kuwa na nyama nyingi na hivyo kuvutia bei kubwa zaidi.
Sisi wahifadhi lazima tuwe na namna ya kushirikiana na wananchi kutekeleza azma hii. Tutoe dira na mwongozo huu ili atakayekiuka sasa naye awe mchokozi na akutane na adhabu kali! Hii ndiyo falsafa yangu ya uhifadhi endelevu.
Maana hata kama tukisema tuache kuhifadhi maeneo haya, miaka mitatu haitozidi, wananchi hawatokuwa na malisho wala maji ya mifugo yao. Inawezekana hii sayansi hawaielewi sana, lakini sisi kama serikali tukiwashirikisha na kuwapa motisha wanaweza kubadilika na kuona tija ya uhifadhi.
Uhifadhi chini ya uongozi wangu kwenye Wizara hii utakuwa shirikishi. Ni lazima tuwekeze kwa wananchi wanaotuzunguka kama tunataka hifadhi zibaki salama na wananchi watupe ushirikiano kwenye kazi yetu ya msingi - uhifadhi.
Wananchi wanahitaji malisho ya mifugo, maji ya kunywesha mifugo, maji ya kumwagilia mashamba yao, elimu ya ufugaji wa kisasa/kilimo cha kisasa, soko la uhakika la mifugo yao, soko la uhakika la mazao yao, na taarifa sahihi za umuhimu wa hifadhi ya uoto wa asili na wanyamapori kwa maisha yetu sisi tunaoishi leo na dhamana tuliyonayo kwa vizazi vijavyo.
Sisi, Wizara ya Maliasili na Utalii, tutatoa mfano wa kuwekeza kwenye jamii inayotuzunguka; wenzetu wa Halmashauri, Ardhi, Mazingira, Kilimo na Mifugo nao wafanye kwa upande wao.
Tuandae mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo yote nyeti jirani na hifadhi zetu, tuwekeze kwenye kutenga na kuendeleza maeneo ya malisho ya mifugo na maeneo kwa ajili ya kilimo, tuwekeze kwenye kutoa elimu ya ufugaji wa kisasa, kilimo rafiki kwa mazingira na kuwawezesha wananchi kuuza mifugo yao na mazao yao kwa bei nzuri.
Tumehangaika sana kukamata mifugo ya wananchi, kuendesha operesheni za kuwaondoa wananchi kwenye maeneo ya hifadhi mpaka tukasahau kazi yetu ya msingi ya 'uhifadhi', kupambana na majangili, kutangaza vivutio vyetu vya utalii, kuendeleza sekta yetu. Sasa basi. Tubadilike. Sisi hatuna jukumu la kuchunga ng'ombe wa wananchi, ama kupambana nao mahakamani. Jukumu letu ni uhifadhi endelevu.
Turudi kwenye kazi yetu ya msingi, tupambane na majangili, tushirikishe wananchi kwenye uhifadhi. Tuondoe uadui na uhasama baina yetu na wananchi, tujenge ujirani mwema. Tutafanikiwa zaidi.
Sambamba na hilo, tutaongeza adhabu kwa wavamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa na tutakuwa wakali zaidi baada ya hapo. Wananchi pia wanapaswa waelewe kuwa kuna maeneo si ya kusogelea!
Kwa hakika, 'uhifadhi endelevu ni uhifadhi shirikishi jamii'.
No comments:
Post a Comment