slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Wednesday, November 29, 2017

FULL VIDEO: SERIKALI YASISITIZA DESEMBA 31 KUWA UKOMO WA UWEKAGI WA VIGINGI (BEACONS) VYA MPAKA HIFADHININa Hamza Temba - Wizara ya Maliasili
..........................................................................
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga amesisitiza agizo la Serikali lililotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu kuhusu kukamilisha zoezi la uwekagi wa vigingi vya mpaka kwenye maeneo ya hifadhi nchini ifikapo Desemba 31 mwaka huu.

Amesema lengo la kukamilisha zoezi hilo ni kuiwezesha Serikali kufanya uamuzi wa mwisho wa kumaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu baina ya vijiji na maeneo ya hifadhi nchini.

Mhe. Hasunga ametoa kauli hiyo jana wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi ya msitu wa Isalalo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe ambapo aliziagiza taasisi zilizo chini ya Wizara yake kukamilisha zoezi hilo kabla ya tarehe hiyo ili kuiwezesha Serikali kubaini maeneo yenye mapungufu na kuyatolea uamuzi.

“Ifikapo tarehe 31 tuwe tumemaliza kuweka hizo beacon (vigingi) za mipaka, baada ya hapo hatua itakayofuata, Serikali tutakaa na kuangaliza ni vijiji vingapi au maeneo gani yameingia ndani ya hifadhi, tuangalie je tuwaachie hayo maeneo wananchi au tuwahamishe tuwapeleke maeneo mengine, maamuzi hayo yatakuja baada ya kufanya tathmini na kubaini penye mapungufu.

“Sasa ikitokea kwamba imefika tarehe 31 hatujatekeleza hili mimi kama Naibu Waziri nitakuwa sina kazi, maana sijatekeleza agizo la Serikali, kwahiyo lazima tulisimamie, na mimi sasa kabla halijanipasukia nitakupasukia bwana Meneja (Meneja TFS Wilaya ya Mbozi), nitakuja kukagua mipaka, na kabla ya tarehe 31 nitakuja kukagua tena,”alisema Naibu Waziri Hasunga.

Wakati huo huo amekemea vitendo vya baadhi ya wananchi wanaoingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini na kuwataka kufugia majumbani kwao au maeneo yaliyotengwa kwa ajili hiyo, amewatahadharisha pia juu ya ukali wa sheria za uhifadhi na kwamba endapo mifugo itakamatwa hifadhini sheria zilizopo zinaruhusu utaifishaji.

Aidha aliwataka wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo ya msitu wa Isalalo kuacha vitendo vya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti hovyo kwa ajili ya mkaa na uanzishaji wa maeneo ya kilimo. Pia alitoa wito kwa wananchi kulinda vyanzo vya maji na kuacha vitendo vya uchomaji moto misitu.

Katika hatua nyingine ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Nyanda za Juu Kusini kuwashirikisha wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hiyo ya msitu kwenye ulinzi wa hifadhi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha miche ya miti ya kutosha kwa ajili ya kupanda  kwenye maeneo yao yanayozunguka hifadhi hiyo.

Aidha ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kupima maeneo yao na kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa kuanisha maeneo kwa ajili ya kilimo, ufugaji na maeneo ya hifadhi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima ya wananchi

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni alisema katika kuimarisha mpaka wa hifadhi ya msitu huo wa Isalalo ambao una ukubwa wa hekta 11,552, jumla ya vigingi 30 vimewekwa kuzunguka hifadhi hiyo.

Alizitaja baadhi ya  changamoto katika hifadhi hiyo kuwa ni uvamizi wa wakulima na wafugaji, uvunaji haramu wa miti, uchomaji mkaa na moto, na ung'oaji wa vigingi vya mpaka na mabango.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo alisema ili kuimarisha uhifadhi wa msitu wa Isalalo ni vema wananchi wakashirikishwa ikiwemo kuanzishwa kwa vikundi vya vijana ambao watawezeshwa bodaboda zitakazowanufaisha kiuchumi na wakati huo huo zikatumika kwenye ulinzi wa hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akioneshwa ramani ya Hifadhi ya Msitu wa Isalalo na Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni (kulia) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua hifadhi hiyo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi mkoani Songwe jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo wakati wa kukagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo Mkoani Songwe kwenye ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na Mkuu wa Wilaya Mbozi, John Palingo (kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo uliopo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni (kulia) wakati akikagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo uliopo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana. Wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, John Palingo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Malolo wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana, alikagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo na kuagiza zoezi la uwekaji vigingi vya mpaka likamilike ifikapo Desemba 3l.

Sunday, November 26, 2017

CHUO CHA USIMAMIZI WA WANYAMAPORI-MWEKA KUANZA KUTOA MAFUNZO MAALUM KWA WAONGOZA WATALII NCHINI KUANZIA KESHO

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa tatu kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka, Brightone Mbilinyi kuhusu mafunzo ya silaha yanavyotolewa chuoni hapo katika mahafali ya 53 ya chuo hicho yaliyofanyika jana katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro. Zaidi ya asilimia 60 ya mafunzo chuoni hapo hutolewa kwa vitendo. Wengine Pichani ni Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Sahabi Dada (wa pili kushoto) na Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho (wa nne kulia).

 Na Hamza Temba-WMU
..................................................

Katika kutimiza azma ya Serikali kuboresha huduma za ukarimu kwenye sekta ya utalii nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii imekichagua Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka kilichopo mkoani Kilimanjaro kwa ajili kutoa mafunzo maalum kwa waongoza watalii nchini. 

Mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kuanza kesho (Jumatatu) chuoni hapo yatakuwa kwenye mfumo wa kujiendeleza na yamelenga kuwawezesha watoa huduma katika sekta hiyo kupata sifa za kusajiliwa na kupewa leseni ya kuendelea kutoa huduma hiyo kwa mujibu ya sheria ya utalii Na. 11 ya mwaka 2008 kifungu cha 48.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga katika mahafali ya 53 ya kuwatunuku vyeti wahitimu 224 wa chuo hicho katika kozi mbalimbali ikiwemo Shahada, Stashahada na Astashada kwenye Usimamizi wa Wanyamapori na Utalii.

"Katika kutambua utaalamu na uzoefu wa chuo chenu, Wizara yangu imeichagua Mweka kutoa mafunzo yatakayowawezesha waongoza watalii nchini kupata sifa ya kusajiliwa (cheti) na kupewa leseni," alisema Naibu Waziri Hasunga.

"Nimefurahi kusikia kuwa  mmeshajipanga tayari kuanza kutoa mafunzo hayo baada ya kufanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo na kuainisha mapungufu kwenye taaluma, ujuzi na mitazamo pamoja na kuandaa mtaala wa mafunzo hayo.

"Nitoe wito kwa waongoza watalii  nchini wajisaji ili wapate mafunzo haya muhimu kwakua katika miaka michache ijayo hawataruhusiwa kutoa huduma hiyo bila kutimiza masharti haya ya kisheria,” alisema Hasunga.

Alisema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watalii wengi wanaokuja nchini hupata taarifa kutoka kwa wenzao waliotembelea Tanzania ambao muda wao mwingi wanakuwa na waongoza watalii kwenye maeneo ya vivutio.

"Hivyo ni muhimu wapewe mafunzo  maalum waweze kutoa huduma bora zaidi zitakazowafanya watalii wafurahie ukarimu wao waweze kuwa mabalozi wazuri wa kuutangaza utalii wetu watakaporudi nchini kwao" alisema  Hasunga. 

Alisema licha ya Sekta ya utalii nchini kuchangia asilimia 17 ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni (watalii milioni 1.28 na bilioni 2 mwaka 2016), mchango wake unaweza kukua zaidi kupitia mikakati mbalimbali inayowekwa  na wizara yake ikiwemo hiyo ya mafunzo ambayo imelenga kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni mbili mwaka 2020 na watalii milioni 8 mwaka 2025 pamoja na mapato ya dola za kimarekani bilioni 20 mwaka 2025.

Akizungumzia kuhusu mafunzo ya jeshi usu chuoni hapo, Naibu Waziri Hasunga aliuagiza uongozi wa chuo hicho kuendesha mafunzo hayo muda wote wa masomo tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo hutolewa kwa wiki mbili katika kila 'semister'.

"Mafunzo haya yasiishie tu kwa muda wa wiki mbili, ni matarajio yangu kuona yanaendeshwa katika kipindi chote cha mafunzo ikiwemo wanafunzi kuvaa sare za heshima za jeshi usu, kuwa na nidhamu ya kijeshi na muhimu zaidi kuonyesha utayari na uwezo wa kukabiliana na wahalifu ikiwemo majangili," alisema Hasunga.

Aidha, alizitaka taasisi zilizopo chini ya Wizara yake kuajiri wananfunzi wanaomaliza chuoni hapo ikiwa ni pamoja na kutumia fursa ya chuo hicho mahiri kuwaongezea ujuzi wafanyakazi waliopo makazini.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho alimueleza Naibu Waziri Hasunga kuwa Chuo chake kimeshafanya maandalizi yote ya kuanza kutoa mafunzo kwa waongoza watalii nchini kama ilivyoagizwa na wizara yake ambapo tathmini ya mahitaji ya mafunzo hayo imeshafanywa kwa kuainishwa mapungu katika taaluma, ujuzi na mitazamo. 

"Tumeshaandaa pia mitaala ya mafunzo ambayo imezingatia kuondoa mapungufu tuliyoyabaini, na tunatarajia kuanza mafunzo yetu ya kwanza kwa wapagazi 100 kwa muda wiki tatu kuanzia jumatatu ijayo (leo)," alisema Prof. Kideghesho.

Alisema ili kufanikisha mafunzo hayo chuo chake kimepokea msaada wa Shilingi milioni 110 kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wapagazi wanaotoa huduma katika mlima Kilimanjaro, fedha ambazo zitatumika kwa ajili ya mafunzo na tafiti mbalimbali.

Mahafali hayo ya 53 yalihudhuriwa pia na Balozi wa Nigeria nchini,  Balozi Sahabi Dada, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo hicho, Prof. Faustin Bee, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba, Mkuu wa Wilaya ya Same, Harun Mbogo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Nebo Mwina, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo na baadhi ya wawakilishi wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda.

Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka kilianzishwa mwaka 1963 baada ya azimio la Arusha mwaka 1961 ambalo lilitaka uwepo wa watu waliopewa mafunzo kwa ajili ya kulinda na kusimamia urithi wa rasilimali za Afrika. 

Chuo hicho ambacho huendesha mafunzo yake kwa vitendo kwa zaidi ya asilimia 60 kimepata ongezeko la wanafunzi kutoka 25 mwaka 1963/1964 hadi zaidi ya wanafunzi 550 mwaka 2016/2017 kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi na Cameroon.

Aidha, katika kipindi cha miaka 54 iliyopita chuo hicho kimeweza kufundisha zaidi ya mameneja wa wanyamapori 8,000 kutoka nchi zaidi ya 50 duniani.

Chuo hicho pia kimepewa tuzo na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kama Kituo cha Ubora wa Taaluma ya Usimamizi wa Wanyamapori (Centre of Excellence).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mmoja ya Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, Leonard Mgamba kuhusu mafunzo ya taaluma ya wanyamapori yanavyofanywa kwa vitendo chuoni hapo. Wengine pichani ni Balozi wa Nigeria nchini, Sahabi Dada (wa tatu kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Harun Mbogo (kushoto) na Mtenaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu, Prof. Dos Santos Silayo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiwa ndani ya handaki linalotumika kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu 224 wa kozi mbalimbali chuoni hapo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akikagua gwaride la wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu 224 wa kozi mbalimbali ikiwemo Shahada, Astashahada na Stashada katika taaluma za usimamizi wa wanyamapori na utalii katika mahafali ya 53 yaliyofanyika chuoni hapo jana katika Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro. Zaidi ya asilimia 60 ya mafunzo chuoni hapo hutolewa kwa vitendo na wahitimu 224 wa kozi mbalimbali walitunukiwa vyeti.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda ambao walishiriki kwenye mahafali ya 53 ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka jana.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Prof. Faustin Bee (kulia), Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Harun Mbogo (kushoto) wakiteta jambo wakati wa mahafali ya 53 ya chuo hichao ambayo yalifanyika jana mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, Prof. Jafari Kideghesho (kulia) akiwasilisha taarifa fupi kuhusu chuo hicho kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) wakati wa mahafali ya 53 ya chuo hicho ambayo yamefanyika jana mkoani Kiliamanjaro. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chuo hicho, Prof. Faustin Bee (wa pili kushoto) na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Sahabi Dada.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka, Prof. Faustin Bee (kulia), Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba (wa pili kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Harun Mgogo wakati wa mahafali ya 53 ya chuo hicho ambayo yamefanyika jana mkoani Kilimanjaro. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Sahabi Dada.
Mkuu wa Chuo chaUsimamizi wa Wanyamapori Mweka, Prof. Jafari Kideghesho (kulia) akiteta jambo na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Sahabi Dada.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori, Mweka, Ebenezer Mollel kuhusu mafunzo ya taaluma ya wanyamapori yanavyofanywa kwa vitendo chuoni hapo. Wengine pichani ni Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho (wa pili kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba.
Sehemu ya taswira ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga akipanda mti wa kumbukumbu chuoni hao.
Baadhi ya wanafunzi wa chuo cha Usimamizi ya Wanyamapori Mweka, pembeni yao ni mifupa ya miguu ya tembo katika chumba maalum cha mafunzo ya wanyamapori.
Sehemu ya wananfunzi 224 waliopewa vyeti vya kuhitimu mafunzo mbalimbali katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka wakiwasili katika viwanja kwa ajili ya mahafali ya 53 yachuo hicho yaliyofanyika jana katika viwanja vya chuo hicho wilayani Moshi Mkoa wa Kiliamanjaro. Vyeti hivyo vilitpolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga. 
Gwaride la wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka wakitoa heshma mbele ya mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (hayuko pichani)

Naibu Waziri wa Maliasi na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akimtunuku cheti Mhitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori, katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka, Valentina Fiasco ambaye ni raia wa Italia katika mahafali ya 53 yaliyofanyika jana chuoni hapo katika wilaya ya Moshi mkoani Kiliamanjaro. Kulia ni Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho. Jumla ya wahitimu 224 wa kozi mbalimbali walitunukiwa vyeti.
Naibu Waziri wa Maliasi na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akimtunuku cheti mmoja ya wahitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori, katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-Mweka wakati wa mahafali ya 53 yaliyofanyika jana chuoni hapo katika Wilaya ya Moshi Mkoani Kiliamanjaro. Kulia ni Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho. Jumla ya wahitimu 224 wa kozi mbalimbali walitunukiwa vyeti. 
 Naibu Waziri wa Maliasi na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akitoa tamko la kuwatunuku kozi mbalimbali wananfunzi 224 wa chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka katika mahafali ya 53 ya chuo hicho ambacho yamefanyika jana mkoani Kilimanjaro. Kulia ni Mkuu wa chuo hicho, Prof. Jafari Kideghesho, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Prof. Faustin Bee (wa tatu kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (mwenye tai) na washiriki wengine katika mahafali hayo.

Thursday, November 23, 2017

HAYA NDIYO MAAJABU YA KIMONDO CHA MBOZI KILICHOPO MKOANI SONGWE

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akiwa ameshikilia kivutio cha utalii cha Kimondo leo wakati wa ziara yake ya kikazi katika kijiji cha Ndolezi wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.

Kimondo hicho kinachokadiriwa kuwa na tani 12 kiligunduliwa wilayani Mbozi mwaka 1930 na kimeundwa kwa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.

Aidha, kimondo hiki ni cha pili kwa ukubwa kati ya 35 vilivyopo barani Afrika na cha nane kati ya 578 vilivyopo duniani kote ambavyo vimeundwa kwa chuma. Sifa kuu ya kimondo hiki ni kuwa na ubaridi wakati wote hata mchana wa jua kali.

Pamoja na mambo mengine katika ziara hiyo, amekagua ujenzi unaoendelea wa jengo la kituo cha taarifa (Information Centre) katika kivutio hicho ambalo linagharimu Shilingi milioni 400. 

Alisema Serikali kupitia wizara yake ina mpango thabiti wa kuendeleza kivutio hicho pamoja na vivutio vya ukanda wa kusini ambapo kupitia Benki ya Dunia imepata mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 150 sawa na shilingi bilioni 340 kwa ajili ya kuendeleza vivutio vya ukanda wa kusini ikiwemo kuimarisha miundombinu.

Vivutio vingine vya utalii vinavyopatikana Mkoani Songwe ni pamoja na chemchem ya maji moto, vitalu vya uwindaji vyenye wanyamapori mbalimbali, mifupa ya shingopana songwensis, unyayo wa mtu wa kale, mapango ya popo, maporomoko ya maji, mbega weupe, kituo cha kwanza cha polisi Tanzania, mabaki ya nyumba za kufua chuma,  na ziwa Rukwa
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Muhifadhi wa Mambo ya Kale, Winnie Msacky kuhusu kivutio cha utalii cha Kimondo wakati wa ziara yake ya kikazi katika kijiji cha Ndolezi wilaya ya Mbozi Mkoani wa Songwe jana. 
Jengo la kituo cha taarifa katika eneo la kivutio hicho (Information Center) ambacho ujenzi wake unaendelea. Ujenzi wa kituo hiki unagharimu Shilingi Milioni 400.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na baadhi ya watumishi wa kituo hicho na wananchi wa vijiji jirani.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga akizungumza na watumishi pamoja na wananchi hao. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akipata maelezo kutoka Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale, Bi. Digna Tilya kuhusu jengo la kituo hicho cha taarifa katika kivutio hicho. (Picha na Hamza Temba-Wizara ya Maliasili na Utalii)

Tuesday, November 21, 2017

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, MHE. JAPHET HASUNGA AAGIZA KUUNDWA KWA CHOMBO CHA KUDHIBITI UBORA WA MAZAO YA MISITU NCHININa Hamza Temba – WMU
..........................................................
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kubuni utaratibu mpya ikiwemo kuanzishwa kwa chombo kitakachosimamia upangaji wa madaraja ya ubora wa mbao zinazozalishwa hapa nchini ziweze kukidhi viwango vya mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Ametoa agizo hilo jana kwenye kikao cha majumuisho na watumishi wa Shamba la Miti la Serikali la Kiwira ambalo linasimamiwa na wakala huyo wakati anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.

“Kuna changamoto kubwa kwenye soko la mbao, kwa kiwango kikubwa mbao zetu nyingi tunaziuza hapa nchini, Lazima tufike mahali hizi mbao tuwe tunaziexport (uza nje) kwa kiwango kikubwa. Lakini ili tufikie malengo hayo mbao zetu lazima ziwe kwenye kiwango kinachokubaliwa.

“Mbao zinazokuwepo kwenye soko letu la ndani huwezi kuzitenganisha kwamba hizi ni za TFS au za mwananchi wa kawaida, nyingine zina ubora nyingine hazina, agizo langu kwenu kaeni chini kama watendaji tuje na utaratibu utakaotuwezesha kuzipanga kwenye madaraja, daraja la kwanza, la pili, la tatu au la nne ili mnunuzi ajue ananunua mbao ya ubora wa aina gani,” alisema Hasunga.

Alisema amepata taarifa kuwa baadhi ya wananchi wanavuna miti ambayo haijakomaa jambo ambalo linaathiri ubora wa mbao kwenye soko kwa kutokidhi mahitaji ya wateja, hivyo akaagiza Wakala huyo kubuni mbinu mpya za kuwalinda wateja ikiwemo kuanzishwa kwa chombo maalum cha udhibiti wa ubora wake.

"Kwa maeneo mengine tuna TBS, kwenye chakuka tuna TFDA, kwenye mbao je? Nani anaregulate?(dhibiti), ni lazima tufike mahali tuwe na mdhibiti atakayetusaidia kuhakikisha kwamba ubora unakuwepo,” alisema Hasunga.

Aidha alitoa wito kwa taasisi hiyo kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuvuna miti ikiwa imeshakomaa ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa miche ya miti na kuhamasisha wananchi wapande miti zaidi kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia nidhamu kwenye Utumishi wa Umma, Naibu Waziri Hasunga alisema Serikali ya awamu ya tano haitomvumilia mtumishi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa, uzembe au uvivu kwenye kutekeleza majukumu ya Serikali kwa kua sifa hizo ni chanzo kimojawapo kikubwa cha umasikini nchini.

Kwa upande wa kampeni ya upandaji miti kitaifa, alisema Serikali itafuatilia nchi nzima kuona utekelezaji wa agizo hilo ambalo linaitaka kila Wilaya kupanda miti milioni moja na laki tano kwa mwaka ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha miti mingi zaidi inapandwa kwa kuwashirikisha zaidi wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Zawadi Mbwambo alisema taasisi hiyo imewahi kupokea malalamiko juu ya ubora hafifu wa baadhi ya mbao zinazopatikana kwenye soko ambazo baadhi ya wananchi hutumia jina la Shamba la Miti Sao Hill kuziuza na hivyo kuharibu sifa ya shamba hilo.

Alisema maagizo yote aliyoyatoa Naibu Waziri Hasunga yatafanyiwa kazi kupitia vikao halali vya kiutendaji vya taasisi hiyo ikiwemo vile vya kuandaa mikakati ya utekelezaji wa majukumu yake ya uhifadhi.

Awali Meneja wa Shamba la Miti Kiwira, William Dafa akiwasilisha taarifa yake kwa Naibu Waziri Hasunga, alisema shamba hilo ambalo lilianzishwa mwaka 1964 likiwa na hekta 2,713 limekuwa na maendeleo mazuri ambapo mwaka 2016/2017 lilivuka malengo ya makusanyo ya mapato ya Serikali kutoka bilioni 1.3 hadi bilioni 1.7.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja (wa pili kushoto) alipofika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo akiongozana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza (wa pili kulia) kwa ajili ya kujitambulisha wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi mkoani humo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akimsikiliza Meneja wa Shamba la Miti Kiwira, William Dafa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi katika shamba hilo jana katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akimsikiliza Meneja wa Shamba la Miti Kiwira, William Dafa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi katika shamba hilo jana katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Zawadi Mbwambo (kushoto) wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi kwenye Shamba la Miti Kiwira lililopo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya jana.

Mti huu wa kumbukumbu ulipandwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1965 katika shamba la miti la Serikali  la Kiwira katika Wilaya ya Rugwe Mkoani Mbeya.
 Mti alipanda Mwalimu Nyerere mwaka 1965 katika shamba la miti Kiwira.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga akizungumza na watumishi wa Shamba la Miti Kiwira  wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi kwenye Shamba hilo katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya jana.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Zawadi Mbwambo akizungumza katika kikao hicho.
Baadhi ya watumishi wa shamba la miti Kiwira.

Monday, November 20, 2017

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, MHE. JAPHET HASUNGA AKABIDHI MSAADA WA MABATI KWA SHULE YA MSINGI ILIYOATHIRIKA NA KIMBUNGA MKOANI IRINGA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela wakitwanga Kinu wakati wa ziara yake katika Makumbusho ya Utamaduni wa Mkoa wa Iringa (Boma) jana Mkoani humo.

Na Hamza Temba - WMU
....................................................................
Katika jiihada za Serikali za kuendeleza ushirikiano na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa msaada wa mabati sitini kwa ajili ya kuezeka madarasa ya shule ya msingi Kipanga baada ya kuezuliwa na kimbunga hivi karibuni katika kijiji cha Ubwachana Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.

Msaada huo umetolewa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga alipotembelea kituo cha Malikale cha Isimila mkoani humo ambacho kinapakana na shule hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Mkoani humo.

Akikabidhi mabati hayo, Naibu Waziri Hasunga alisema  Serikali inatambua mchango wa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi kwenye uhifadhi shirikishi hivyo ni jukumu la Serikali kuwaunga mkono pale wanapopatwa na majanga ya aina mbalimbali.

Aidha, aliwataka baadhi ya wananchi wanaochimba mchanga kwenye maeneo ya vivutio katika kituo hicho waache mara moja kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria kwakuwa wanahatarisha uhai wa kingo za miamba ya kale ambayo na kivutio kikubwa cha utalii wa asili katika ukanda wa kusini.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya mambo ya Kale wa Wizara hiyo, Bi. Digna Tillya alitoa rai kwa wananchi wanaozunguka kituo hicho kushirikiana na Serikali katika uhifadhi na ulinzi wa kituo hicho na kujiepusha na vitendo vya uharibifu wa mazingira.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiwa amevaa “musk’ mfano wa vazi la kabila la wahehe wa Mkoa wa Iringa wakati wa ziara yake katika Makumbusho ya Utamaduni wa Mkoa wa huo (Boma) jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa tatu kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Kijiji cha Ubwachana, Donatus Lihoha mabati 60 kwa ajili ya kuezeka vyumba vya madarasa vya shule ya msingi Kipanga ambayo iliezuliwa na kimbunga hivi karibuni ikiwa ni kutambua mchango wa wananchi katika uhifadhi shirikishi wa Kituo cha Mali Kale cha Isimila jana Mkoani Iringa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (wa pili kushoto) akimsikiliza Mhadhiri wa Chuo Kikuu Iringa, Jimson Sanga ambaye pia ni Meneja Msaidizi wa Mradi wa Fahari Yetu unaojishughulisha na Uhuishaji, Uendelezaji na Utangazaji wa utalii Nyanda za Juu Kusini kuhusu Makumbusho ya Utamaduni wa Mkoa wa Iringa (Boma) wakati wa ziara yake jana Mkoani humo. Anayeshuhudia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela (wa tatu kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale wa Wizara hiyo Digna Tillya.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akimsikiliza Mhadhiri wa Chuo Kikuu Iringa, Jimson Sanga ambaye pia ni Meneja Msaidizi wa Mradi wa Fahari Yetu unaojishughulisha na Uhuishaji, Uendelezaji na Utangazaji wa utalii Nyanda za Juu Kusini wakati akitoa maelezo kuhusu Makumbusho ya Utamaduni wa Mkoa wa Iringa  (Boma) wakati wa ziara yake jana Mkoani humo. Anayeshuhudia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela (kulia kwake).

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na watumishi wa Makumbusho ya Utamaduni wa Mkoa wa Iringa (Boma) alipotembelea Makumbusho hiyo jana wilayani Iringa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (wa pili kulia) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela kuhusu Makumbusho ya Utamaduni wa Mkoa wa Iringa (Boma) wakati wa ziara yake jana Mkoani humo. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (wapili kushoto) akisalimiana na wafanyakazi wa  (Kituo cha Mali Kale cha Isimila) alipotembelea kituo hicho jana mkoani Iringa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) akimpa maelekezo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya (kulia) alipotembelea Kituo cha Mali Kale cha Isimila mkoani Iringa jana.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Digna Tilya akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kukabidhi mabati.

Baadhi wa washiriki wa hafla hiyo.

Baadhi ya washiriki wa hafla hiyo.