slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Friday, February 24, 2017

VIFAA VYA OFISI VYA KUNDI LA KWANZA LA WATUMISHI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII WANAOHAMIA DODOMA VYASAFIRISHWA

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akiwa na baadhi ya watumishi wa wizara hiyo wakiaga msafara wa magari yaliyobeba vifaa vya ofisi vya kundi la kwanza la watumishi wa wizara hiyo wanaohamia Makao Makuu ya Nchi Mjini Dodoma nje ya jengo kuu la Wizara hiyo juzi.
Moja ya gari la jeshi lililokuwa limebeba vifaa vya ofisi vya watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii likiondoka rasmi makao makuu ya wizara hiyo juzi kuelekea mjini Dodoma.

Monday, February 20, 2017

FAO YATOA KIASI CHA SHILINGI MILIONI 280 KATIKA MCHAKATO WA KUPITIA UPYA SERA YA TAIFA YA MISITU YA MWAKA 1998


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) akiwa na Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) , Fred Kafeero (kulia) wakisaini hati ya makubaliano ya kupitia upya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikitumika kwa takribani miaka 19 hadi hivi sasa. ( Picha na Lusungu Helela- Maliasili) 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) akiwa na Mwakilishi Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Fred Kafeero (kulia) wakibadilishana hati ya makubaliano ya  kupitia upya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikitumika kwa takribani miaka 19 hadi hivi sasa.
Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa akionesha kitabu cha Sera ya Taifa ya Misitu ya Mwaka ya 1998 ambayo
imepitwa na wakati kutokana na mabadailiko mengi kutokea nchini. Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) akiwa na Mwakilishi Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Fred Kafeero (kulia).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) akizungumza kabla kutia saini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ya kupitia upya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikitumika kwa takribani miaka 19 hadi hivi sasa.

NA LUSUNGU HELELA - WMU

.........................................................................

Serikali ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) wameisaini makubaliano ya kupitia upya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998 ambayo imekuwa ikitumika kwa takribani miaka 19 hadi hivi sasa.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi amesema mpango huo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 280 ambazo zimetolewa na FAO kwa ajili ya kufanya utafiti wa kuongezea takwimu ambazo zitaboresha Sera ya Misitu ya Taifa ili iweze kufikia hadhi ya kimataifa.

Amesema hatua hiyo imekuja Kutokana na Sera ya Misitu ya Taifa ya mwaka 1998 inayotumika hadi hivi sasa kupitwa na wakati yakiwemo mabadiliko ya Kiuchumi, Kuongezeka kwa idadi ya watu pamoja na Mabadiliko ya tabia ya nchi.

Maj. Gen. Gaudence ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la ufyekaji misitu na hivyo kumechangia kupunguza uoto wa asili kutoka hekta milioni 55.9 kwa mwaka 1990 hadi kufikia hekta milioni 46 kwa sasa lakini Sera ya Misitu ni ile ile.

‘’ Sera ya Taifa ya Misitu ilishafanyiwa mapitio kuanzia mwaka 2009, Lakini kutokana na Sera hii kukaa kwa muda wa takribani Miaka 9 hadi hivi sasa tumegundua kuwa baadhi ya wadau wengi hawakupata nafasi ya kutoa mawazo yao. Hata wale waliotoa mawazo yao mengi yameshapitwa na wakati.’’ Alisema Maj. Gen. Milanzi

Naye Mwakilishi Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) , Fred Kafeero amesema kuwa Mradi huo utasaidia wananchi wengi kushiriki na kutoa mawazo mengi kuhusiana na Sera ya Misitu ikiwa pamoja na kuwajengea uwezo watumishi kuweza kukusanya taarifa nyingi ili ziwezeshe kuboresha sera kupitia tafiti. 

Aidha,Kafeero amesema kutokana na mabadiliko hayo FAO itasaidia katika kuhuisha sera mpya ambayo itatoa majibu kwa changamoto zinazoikabili nchi hivi sasa na kukidhi mikataba ya kimaifa kama vile mabadiliko ya tabia ya nchi

Monday, February 13, 2017

WANANDOA WAHUKUMIWA MIAKA 20 JELA KWA KUKUTWA NA MENO YA TEMBO

NA HAMZA TEMBA - WMU
...................................................................

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela Peter Kabi na Leonida Loi Kabi ambao ni wanandoa baada ya kukutwa na meno ya tembo 210 yenye uzito wa kilo 450.6 pamoja na mifupa mitano ya tembo.

Meno hayo yanayodaiwa kuwa ni sawa na idadi ya tembo 93 waliouwawa yalikutwa nyumbani kwa washtakiwa hao tarehe 27 Oktoba, 2012 eneo la Kimara Stop Over Jijini Dar es Salaam.

Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shahidi amesema ametoa hukumu hiyo leo baada ya mahakama kujiridhisha na ushahidi wa upande wa Jamhuri ukiongozwa na mawakili Paul Kadushi na Elia Athanas ambao kwa pamoja umewatia hatiani washtakiwa hao.

Amesema katika kosa la kwanza katika kesi hiyo kila mtuhumiwa atatumikia kifungo cha miaka 15 jela, kosa la pili na la tatu miaka 20 kila moja na kwamba hukumu hizo zitaenda kwa pamoja.

Akielezea kuhusu adhabu hiyo, Wakili Kadushi alidai kifungu namba 11 cha Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, kinaelezea kuwa ni sharti la lazima kwa mahakama kutaifisha nyara zinazohusika na kesi hiyo ikiwemo meno ya tembo na mifupa mitano ya tembo.


Alieleza kuwa adhabu ya makosa hayo ni kifungo cha miaka 20 au 30 pamoja na faini inayoweza kuongezeka mara kumi ya thamani ya meno ya tembo waliyokutwa nayo washitakiwa.


Wakili wa utetezi wa washitakiwa hao, Bernard Mkagwa aliiomba mahakama itoe adhabu bila kumkomoa mshitakiwa na kwamba lengo la adhabu ni kurekebisha.


Pia aliomba mahakama ifikirie kuwa mtuhumiwa ni mke na mume ambao wanawatoto wawili wanaosoma pamoja na wazazi wazee ambao wanawategemea.

Akitoa ushahidi wa upande wa Jamhuri juu ya athari za ujangili nchini, Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Emmanuel Lymo amesema idadi ya tembo hapa nchini imepungua kwa kiasi kikubwa kwani sensa ya mwaka 2006 inaonyesha tembo walikuwa 134,000 tofauti na sesa ya mwaka 2012 ambayo ilionesha idadi hiyo kupungua na kufikia 43,000.Alisema sensa ya mwaka 2013 ilionesha idadi ya tembo kuongezeka na kufikia 50,000 ambayo ni matunda ya jitihada za Serikali katika kukabiliana na ujangili kwa kuongeza nguvu katika doria na mikakati mbalimbali ya kudhibiti ujangili.

Alidai tembo ni wanyama muhimu kwani ni miongoni mwa wanyama watano wenye thamani kubwa duniani na wanapowindwa kijangili kupunguza mapato ya serikali.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexandre Songorwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya hukumu hiyo amesema, kila mtanzania anapaswa kujifunza kupitia hukumu hiyo kwa kuwa binadamu wote hujifunza kutokana na makosa na kwamba ni jukumu la kila mtanzania kulinda na kuhifadhi rasilimali za taifa.

“Rasilimali hizi ni zetu sote watanzania, sio za Serikali, sio za Wizara ya Maliasili na Utalii, sisi ni vibarua wenu, tuwalindie watoto wetu na wajukuu zetu hizi rasilimali, wasijekututukana huko mwishoni kama hawatakuta chochote wakalazimika kupanda ndege kwenda kuangalia vitu vilivyokuwa hapa hapa, watatutukana hatuna sababu ya kusubiri matusi” alisema Songorwa. 
 Watuhumiwa wa Ujangili, Peter Kabi (wa pili kulia) na mke wake Leonida Loi Kabi (wa tatu kulia) wakielekea kusomewa mashtaka ya kukutwa na meno 210 na mifupa mitano ya tembo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam leo, wote wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela. 
 Mtuhumiwa wa Ujangili, Peter Kabi (wa pili kulia) akielekea kusomewa mashtaka ya kukutwa na meno 210 na mifupa mitano ya tembo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam leo, mtuhumiwa huyo na mke wake Leonida Loi Kabi (hayuko pichani) wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexandre Songorwa (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya hukumu hiyo leo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara hiyo anaeshuulikia Maendeleo ya Wanyamapori, Kanisius Karamaga.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexandre Songorwa akizungumza na wanahabari katika moja ya ukumbi mahakamani hapo.

Thursday, February 2, 2017

MAKALA: MAFANIKIO YA KUKABILIANA NA UJANGILI KIMKAKATI YAANZA KUONEKANA

 Rais Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Meja Jenerali Gaudence Milanzi alipofanya ziara ya kushtukiza makao makuu ya hiyo (MPINGO HOUSE) jijini Dar es salaam Oktoba 29, 2016. (Picha na Ikulu)
Rais Dkt John Pombe Magufuli akikagua pembe za ndovu 50 zilizokamatwa katika operesheni maalum ya kusaka majangili alipofanya ziara ya kushtukiza makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (MPINGO HOUSE) jijini Dar es salaam Oktoba 29, 2016. (Picha na Ikulu)

NA HAMZA TEMBA - WMU
.....................................................................................

"Haiwezekani maliasili yetu ikawa inapotea hovyo hovyo kwasababu ya watu wachache wenye tamaa ya kupata utajiri wa harakaharaka, hakuna wa kumbakiza, awe mkubwa, awe nani, shikeni, wala msijali mtu cheo chake, umri wake, dini yake, kabila lake, umaarufu wake, sheria ni msumeno, watafuteni wote mpaka wakiona tembo wawe wanakimbia wenyewe".

Hiyo ilikua ni kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza katika makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House)  Jijini  Dar es Salaam tarehe 29 Oktoba, 2016 kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa operesheni ya kukabiliana na ujangili inayofanywa na kikosi kazi kilichoundwa na Wizara hiyo.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alishuhudia meno ya tembo 50 yaliyokuwa yamekamatwa katika kipindi cha siku mbili zilizopita Jijini Dar es Salaam, alioneshwa pia gari lililokuwa limebeba meno hayo na watuhumiwa wanane wanaotuhumiwa kujihusisha na mtandao wa biashara haramu ya meno ya tembo.

Rais Magufuli aliwapongeza askari wote waliopo katika kikosi cha kupambana na ujangili pamoja na raia wema wanaotoa ushirikiano katika mapambano hayo na kwamba anatambua kazi nzuri wanayofanya na anawaunga mkono.

Katika hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, Rais Magufuli alitoa vipaombele kadhaa vya kutekelezwa na wizara zake huku Wizara ya Maliasili na Utalii akiipa majukumu makuu matatu; kupambana na ujangili, kutatua migogoro ya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi na kuongeza mapato ya Serikali.

Wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Prof. Jumanne Maghembe; Naibu Waziri, Mhandisi Ramo Makani; Katibu Mkuu, Meja Generali Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki imejipanga kutekeleza majukumu yake makuu ya uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kuendeleza Utalii pamoja na vipaombele ilivyoelekezwa.

Mara tu alipoteuliwa kuingoza wizara hiyo, Prof. Maghembe alitangaza vita na majangili na kubainisha kuwa kipaumbele chake kikubwa kitakuwa ni kupambana nao. “Niwaambie majangili sasa wakafanye kazi nyingine ama wakae nyumbani, kiama kinakuja huko”, alisema.

Alisema kuwa atasimamia kwa uhakika maliasili za Watanzania kwa sababu mambo ya maliasili ndiyo eneo alilobobea kwenye usomi wake.
“Tutajitahidi pia kutangaza utalii na kuongeza mapato ya sekta hii kama tulivyofanya kwenye miaka ya 2006 hadi 2008, tuliongeza bei za vitalu na ada kwa mnyama mmoja mmoja anayewindwa,”  alisema Profesa Maghembe siku aliyoapishwa.

Mikakati ya Wizara kukabiliana na ujangili

Ni takribani mwaka mmoja na miezi miwili tangu uongozi wa Serikali ya awamu ya tano uingie madarakani, taarifa iliyotolewa na Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii, inaonyesha kuwa katika kipindi cha mwezi Novemba, 2015 hadi mwezi Oktoba 2016 Wizara hiyo imefanikiwa kuweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ujangili ikiwemo kuanzisha kikosi kazi maalum cha kupambana na ujangili.

Kikosi kazi hicho cha kudhibiti uhalifu wa Misitu na Wanyamapori nchini(Wildlife and Forest Crime Unit),kinasimamiwa na Watendaji wa Sekta ya Wanyamapori kwa ajili ya kukabiliana na majangili katika ngazi za juu za uwezeshaji (Facilitators) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini.

Kikosi hicho kiliundwa mwezi Julai, 2016 na Katika kipindi cha miezi mitatu (Agosti hadi Oktoba, 2016) kimefanikiwa kukamata majangili 107 na kesi 9 ziko mahakamani, upelelezi wa kesi nyingine unaendelea. Nyara mbali mbali, silaha na vifaa vya kufanyia ujangili pia vimekamatwa na kikosi kazi hicho.

Wizara imefanikiwa kuimarisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ilizinduliwa rasmi mwezi Novemba, 2015 na Rais wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na kuanza majukumu yake rasmi tarehe 1 Julai, 2016.

Mamlaka hii yenye jukumu la kuendeleza shughuli za ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori nchini kwa maeneo yote yaliyopo nje ya Hifadhi za Taifa na Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti ujangili kwenye maeneo hayo.

Mabadiliko ya mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu umenzishwa na Wizara kwa ajili ya kuimarisha nidhamu, ufanisi wa utendaji kazi za uhifadhi pamoja na mapambano dhidi ya ujangili. Katika kipindi hicho mafunzo kadhaa yametolewa kwa watumishi 425 wa TANAPA katika kuelekea mabadiliko hayo.

Watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania pia pia wamepatiwa mafunzo hayo. Lengo ni kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wote wa taasisi za uhifadhi nchini zikiwemo za wanyamapori na misitu.

Pamoja na mafunzo hayo, matumizi ya teknolojia ya ndege zisizokuwa na rubani (drones) kwa ajili ya doria na ulinzi wa mipaka na wanyamapori yamepewa kipaombele katika hifadhi mbalimbali za taifa na Pori la Akiba la Selous kama mkakati wa kukabiliana na ujangili.

Mkakati mwingine ulioanzishwa na kuimarishwa ni ukaguzi wa nyara katika viwanja vya ndege na bandari kwa kutumia mbwa maalum wa kunusa ili kutambua nyara na kufuatilia majangili.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa ushirikiano na nchi jirani katika kutatua changamoto za uhifadhi na biashara haramu ya ujangili umeimarishwa. Katika eneo hili Tanzania inashirikiana na nchi ya Msumbiji, Zambia, Uganda na Kenya kukabili ujangili unaovuka mipaka ya nchi hizo.

Ushirikishwaji wa wananchi katika uhifadhi na vita dhidi ya ujangili ni moja ya mkakati uliowekwa na wizara. Elimu ya uhifadhi kwa wananchi  imeendelea kutolewa katika  wilaya 11 na vijiji 57 vinavozunguka Pori la Akiba la Selous, Mapori ya Akiba  ya Lukwika/Lumesule na Msanjesi na eneo la Ardhioevu la Ziwa Natron.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa;

Katika kipindi cha mwezi Novemba, 2015 hadi Oktoba 2016, taarifa ya Idara ya Wanyamapori inaeleza kuwa Sekta ya Wanyamapori imefanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 5,894 kwa makosa mbalimbali ya uvunjaji wa Sheria za Uhifadhi na kuwafungulia mashitaka. Jumla ya kesi 859 zilifunguliwa. Kesi 136 zenye watuhumiwa 248 zilihukumiwa kifungo cha jumla ya miezi 8,295 na kesi 198 zenye watuhumiwa 234 walilipa faini jumla ya shilingi 387,985,063/=.

Imeeleza kuwa silaha 254 za aina mbalimbali zilikamatwa katika kipindi hicho, Nyara za aina mbalimbali zilikamatwa ikiwemo meno ya tembo vipande 848 vyenye uzito wa kilo 2,664.48, nyamapori yenye uzito wa kilo 7,790 za wanyama mbalimbali, meno 8 ya kiboko, magunia 67 ya magamba ya kakakuona, ngozi 16 na mikia 33 ya wanyamapori mbalimbali.

Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa katika kipindi hicho ni watu sita akiwemo mfanyabiashara Yusuf Ally (34) aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli kwa jina maarufu la ‘Mpemba’ kuwa ni kinara wa ujangili, watuhumiwa hao ambao kesi yao bado inaendelea walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya shilingi milioni 785.6.

Mtuhumiwa mwingine maarufu wa ujangili aliyewahi kukamatwa nchini ni mwanamke wa China anayedaiwa kuongoza genge kubwa zaidi la usafirishaji wa pembe za ndovu barani Afrika. Akipewa jina la utani “Ivory Queen”, Yang Feng Glan anadaiwa kusafirisha pembe za ndovu 706 kutoka nchini kwenda Mashariki ya mbali. Glan, 66, anadaiwa kuwa na ukaribu na majangili wa Afrika Mashariki na walanguzi wa China, kesi yake bado ipo mahakamani.

Ujangili waripotiwa kuanza kupungua;

Januari 17 mwaka huu (2017), akizungumza kwenye kikao cha kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii mkoani morogoro, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Generali, Gaudence Milanzi alisema ujangili hapa nchini kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba nyara zinazokamatwa kwa sasa ikiwemo meno ya tembo ni za zamani zilizokuwa zikisubiria kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Aliongeza kuwa mizoga ya wanyamapori imepungua ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo ni dalili pia ya kupungua kwa ujangili nchini, “mafanikio hayo yametokana na kazi kubwa inayofanywa na vikosi maalum vya Askari wa wanyamapori vya kudhibiti ujangili kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini”, alisema Milanzi.

Katika hatua nyingine alieleza kuwa kitendo cha Serikali ya China kupiga marufuku biashara ya meno ya tembo nchini humo ni jambo la kupongezwa na kwamba uamuzi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msukumo wa vitendo vya ujangili nchini kwa kuwa nchi hiyo ni miongoni mwa masoko makubwa ya meno hayo duniani.

Ujangili haukubaliki kwa kuwa unatishia kuathiri faida kubwa inayopatikana kupitia sekta ya utalii ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea uwepo wa wanyamapori katika hifadhi zetu, Sekta hii inachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na ni sekta inayoongoza kwa miaka mitatu mfululizo kwa kutoa mchango wa asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni nchini.

Ni jukumu la kila Mtanzania kuona umuhimu wa rasilimali hizi na kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa Maliasili zetu zinaendelea kuwepo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo, Tanzania bila Ujangili inawezekana, kila mmoja akitimiza wajibu wake.

Wednesday, February 1, 2017

MAADHIMISHO YA SIKU YA ARDHIOEVU DUNIANI KESHO TAREHE 2 FEBRUARI 2017

TAARIFA KWA UMMA

MAADHIMISHO YA SIKU YA ARDHIOEVU DUNIANI TAREHE 2 FEBRUARI 2017

Kesho tarehe 2 Februari, 2017 ni maadhimisho ya siku ya Ardhioevu Duniani. Siku hii inaadhimishwa duniani kote kwa kutoa elimu na kuwakumbusha watu wote kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za ardhioevu.
Ardhioevu ni maeneo ya ardhi yaliyopo kandokando na ndani ya Chemchem, Mito, Maziwa na mwambao wa bahari wenye kina cha maji yasiyozidi mita sita wakati wa kupwa. Ardhioevu pia hujumuisha Madimbwi, Mabwawa, Tingatinga na sehemu zote yanapokusanyika maji kipindi kirefu cha mwaka.
Tanzania hujumuika na nchi nyingine wanachama wa Mkataba wa “Ramsar” kuadhimisha siku ya ardhioevu duniani Februari 2 kila mwaka. Ujumbe wa mwaka huu wa Siku ya Ardioevu ni: "Ardhioevu Hupunguza Athari za Majanga” (Wetlands for Disaster Risk Reduction)". 
Tafsiri ya kauli mbiu hii ni kwamba, Ardhioevu huzuia majanga ya mafuriko yanayoweza kutokea katika pwani za bahari, hupunguza athari za kiafya zinazoweza kujitokeza kutokana na madini hatarishi kama Zebaki, hupunguza uwezekano wa kutokea kwa baa la njaa kwa kuwa maeneo okozi wakati wa kiangazi kama vyanzo vya maji na chakula kwa binadamu na wanyama. 
Ardhioevu pia ni maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa chakula kama vile mpunga na mbogamboga na chanzo cha maji yanayotumika kwenye kilimo cha umwagiliaji nchini. Arhioevu pia ni sekta endeshi ya uchumi wa nchi kwa kuwa ni chanzo cha maji yanayotumika kwenye kilimo, viwandani pamoja na uzalishaji wa umeme wa maji kwa gharama ndogo.

Inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya ardhi ya Tanzania ni ardhioevu ambayo ni muhimu kwa bioanwai, uchumi, shughuli za kijamii na kiikolojia. Maeneo haya ni makazi muhimu ya aina mbalimbali za viumbe hai wakiwemo samaki, viboko, mamba, ndege na viumbe wengine wasio na uti wa mgongo. Katika ikolojia ya ardhioevu tunapata bioanwai kubwa kuliko eneo lingine lolote duniani. Maeneo haya ni vyanzo vya maji kwa kipindi chote cha mwaka, huhifadhi maji na kupunguza mafuriko kwa maeneo ambayo ni hatarishi.

Maeneo haya ni muhimu kwa kuchuja kemikali zilizopo kwenye maji yaliyochafuka hususani kutoka kwenye kilimo, viwanda na matumizi ya nyumbani. Madini yanayochujwa kwa wingi  na ardhioevu ni pamoja na madini ya Nitrojen, Phosphorus na madini ya Aluminium na Chuma. Madini ya Nitrojen na Phosphorus husababisha kupungua kwa hewa muhimu ya oxygen kwa viumbe wa majini.

Hii hutokana na kumea kwa wingi kwa mimea aina ya mwani (Algae) ambayo ikiota kwa wingi kwenye uso wa maji husababisha ukijani unaozuia mwanga wa jua kufika kwenye kina cha maji na kuzuia “photosynthesis” kutokea. Hewa ya “oxygen” itapungua majini  na viumbe maji kama samaki hufa kwa wingi.

 Ardhioevu pia huzuia mmomonyoko wa udongo kwenye fukwe/kingo za mito na mifereji unaoweza kusababishwa na mawimbi ya bahari. Ardhioevu pia ni vyanzo vya umeme, na huchangia huduma ya usafirishaji na ni maeneo mazuri kwa ajili ya kubarizi.

 Maeneo ya ardhioevu yanasimamiwa na mkataba wa “Ramsar” ambayo Tanzania imeweka saini, Sheria ya Usimamizi wa Wanyamapori na Mazingira yake, na ndio msingi wa usimamizi na matumizi endelevu ya ardhioevu duniani. Mkataba huu ulisainiwa na nchi wanachama kwa mara ya kwanza katika mji wa Ramsar nchini Iran mwaka 1972. 

Lengo la kuanzishwa kwa  mkataba huu ni kuhifadhi Ndege maji kwa mfano Korongo Taji, Korongo Nyangumi Bungunusu, Herroe Mkubwa, Heroe Mdogo. Ndege hawa ni muhimu kwa utalii na uhifadhi wa mazingira na mwingiliano wa bianuwai. Pia ni dalili ya afya ya mazingira. Tanzania iliweka saini makubaliano haya mwaka 2000.

 Tanzania kuna maeneo ya Ardhioevu  manne ambayo ni; Ziwa Natron yenye umuhimu wa kuhifadhi ndege aina ya Heroe Wadogo-(Lesser flamingo), Malagarasi Muyovosi  ina umuhimu wa kuhifadhi ndegemaji aina ya  Korongo Domkiatu (Shoebill Stork), Bonde la Mto Kilombero yenye umuhimu wa uhifadhi wa Puku na Rufiji mafia Kilwa uhifadhi wa Mikoko na Mazao ya Baharini.

Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa ardhioevu nchini. Hata hivyo, ardhioevu nyingi nchini zinaharibika na zingine kutoweka kutokana na ongezeko la shughuli za kimaendeleo zisizo endelevu kama vile ujenzi kwenye vyanzo vya maji, ufugaji holela, kilimo kisichozingatia kanuni za kilimo cha kisasa na kukata miti ovyo. 

Athari zingine zinazotokana na matumizi mabaya ya ardhioevu ni pamoja na vifo vya mimea maji na wanyama wanaotegemea maji kuishi na kunywa kutokana na matumizi yasiyoendelevu, ukosefu wa mapato kwa jamii kutokana na kuathiriwa kwa sekta za uvuvi, utalii, kilimo cha umwagiliaji na ufugaji. Binadamu, mimea na wanyama wakiwemo samaki pia huathirika kwa kukosa maji.

Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania inawakumbusha wananchi kuwa maeneo ya ardhioevu ndio vyanzo vya maji ambayo binadamu wanatumia kila siku. Mimea na Wanyama pia hutegemea maji kutoka kwenye ardhioevu. Mamlaka inatoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Ardhioevu, kushirikiana na Serikali na Taasisi zake pamoja na Taasisi zisizo za Kiserikali katika kuyatunza maeneo haya. 

Mamlaka inatoa wito kwa  wananchi kutekeleza sheria mbalimbali za uhifadhi ikiwemo Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Sheria nyingine za kisekta kama ya Maji na Uvuvi na kuwahimiza wale wote wanaoishi kwenye maeneo ya ardhioevu na hifadhi kuhama bila shuruti.


         Martin T. Loibooki
KAIMU MKURUGENZI MKUU-TAWA
1 Februari 2017