slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Wednesday, December 30, 2015

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHE. PROF. JUMANNE MAGHEMBE AONANA NA BODI YA TAWA LEO

Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kulia mstari wa mbele), Naibu Waziri Mhe. Eng. Ramo Makani (wa tatu kushoto mstari wa mbele), Katibu Mkuu Dkt. Adelhelm Meru (wa pili kulia mstari wa mbele) na Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wa bodi ya Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) mara baada ya mkutano wa pamoja uliofanyika leo tarehe 30 Desemba 2015 Makao Makuu ya Wizara hiyo Mpingo House Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta ya Wanyamapori na Utalii kwa ujumla. 

Tuesday, December 29, 2015

SERIKALI KUPITIA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, TAMISEMI NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS MAZINGIRA NA MUUNGANO KUANZISHA PROGRAMU YA PAMOJA WA UPANDAJI MITI KWA AJILI YA UHIFADHI NA UNDELEZAJI WA MAZINGIRA NCHINI

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akizungumza kwenye kikao cha pamoja kati yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Mhe. Januari Makamba (kulia) leo tarehe 29 Desemba 2015 katika ukumbi wa Selous Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii  Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuipa majukumu Kamati Maalum ya Wataalam ya kutengeneza andiko maalum litakalotumika kuandaa Programu ya pamoja ya kitaifa ya upandaji miti nchi nzima kuanzia mijini hadi vijijini kwa lengo la kuhifadhi na kuendeleza mazingira ikiwemo misitu. Kwa mujibu wa Prof. Maghembe Kamati hiyo imepewa wiki mbili kukamilisha kazi. Mpango huo utashirikisha pia Wizara ya TAMISEMI.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Mhe. Januari Makamba (kulia) akizungumza katika kikao hicho. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akifafanua jambo katika kikao hicho.

...............................................................................

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, Tamisemi na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano inategemea kuanzisha programu ya pamoja wa upandaji miti nchini kwa ajili ya uhifadhi na undelezaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

 

Akizungumza katika mkutano wa pamoja uliwakutanisha Mawaziri wa Wizara ya Maliasili, Utalii na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano na jopo la wataalamu, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe amesema Serikali ya awamu ya tano imekusudia kuboresha uhifadhi wa mazingira.

 

Prof. Maghembe. Ameongeza kuwa Wizara ina maeneo makubwa yaliyotengwa kwa ajili ya kupanda miti ili kuzuia uharibifu wa Mazingira ikiwa ni pamoja na kuzuia ukataji miti hali inayotishia nchi kuwa jangwa kama hatua stahiki hazitachukuliwa mapema.

‘’Tupo tayari tumejiandaa na tunaweza ikiwa nia yetu ni kuhakikisha nchi nzima inapandwa miti kwa wingi na kwa usimamizi wa hali ya juu kwa kuwashirikisha wananchi’’ Prof. Maghembe alisisitiza.

 

Mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Mhe. January Makamba ulikuwa na lengo la kuipa kazi kamati maalum kwa ajili ya kuandaa andiko maalum litakalotumika kuandaa mpango mkakati huo.

 

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano Mhe. January Makamba Kamati hiyo imepewa wiki mbili kuhakikisha inakamilisha kazi hiyo ambapo utekelezaji wake unategemewa kuanza mara moja ukiwa na mbinu mpya zaidi.


‘’Oparesheni panda miti ni lazima ibadilishwe kwa kuwa kumekuwa hakuna utaratibu mzuri ni lazima tuhakikishe idadi ya miti itakayopandwa inatunzwa ipasavyo’’ Mhe. Makamba alisisitiza.

Alisema programu  ya kupanda miti hiyo  itahakikisha Wananchi wanashiriki kikamilifu kwani kwa sasa miti imekuwa ni biashara kubwa miongoni wa Wananchi hivyo itawasaidia pia kuwaongezea kipato.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Eng. Ramo Makani amewataka watalaamu hao wasiishie tu kwenye kuandika na badala yake wawe mstari wa mbele kuhakikisha malengo ya upandaji miti yanafikiwa kwa kuweka mipango hiyo katika vitendo.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII PFOF. JUMANNE MAGHEMBE AKABIDHIWA RASMI OFISI LEO NA ALIYEKUWA WAZIRI WA WIZARA HIYO LAZARO NYALANDU

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto) akikabidhiwa taarifa ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Lazaro Nyalandu (wa pili kulia) leo tarehe 29 Desemba 2015 ofisini kwake Mpingo House. Wanaoshuhudia makabidhiano hayo ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Ndugu Selestine Gesimba (kulia).
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kushoto) akizungumza na Waziri wa sasa wa Wizara hiyo Mhe. Prof. Jumanne Maghembe na Katibu Mkuu Dkt. Adelhelm Meru (kulia) wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika leo tarehe 29 Desemba 2015 katika ofisi za Wizara hiyo Mpingo House. Katika salamu zake Mhe. Nyalandu amepongeza uteuzi wa Prof. Maghembe ambapo amesema Mhe. Rais amefanya chaguo sahihi kwani Prof. Maghembe anao uwezo wa kufanya kazi nzuri katika Wizara hiyo.  
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akizingumza na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kulia) muda mfupi baada ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika ofisini kwake leo. Mhe. Prof. Maghembe amempongeza Mhe. Nyalandu kwa kazi nzrui aliyoifanya akiwa Waziri wa Wizara ya Malisili na kuahidi kuanzia alipoishia katika kuhakikisha Maliasili za nchi zinatunzwa ipasavyo ikiwemo kupambana na changamoto zilizopo za ujangili na uharibifu wa misitu na maliasili kwa ujumla.

.............................................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri kabla yake Mhe. Lazaro Nyalandu, Makabidhiano hayo yamefanyika leo Makao Mkuu ya Wizara hiyo, Mpingo House jijini Dar es Salaam.

Katika makabidhiano hayo Mhe. Nyalandu amekabidhi taarifa rasmi ya makabidhiano kwa Mhe. Waziri Prof. Jumanne Maghembe kama ishara ya kukabidhi rasmi Ofisi ya Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Makabidhiano hayo ambayo ni utaratibu wa kiserikali wa kukabidhi ofisi umeshuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Selestine Gesimba,  baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo na waandishi wa habari.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo Mhe. Nyalandu amempongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Prof. Maghembe kuwa Waziri wa Wizara ya Maliasili kwa kuwa ana sifa stahiki za kuongoza Wizara hiyo nyeti.

Aliongeza kwa kusema kuwa Prof. Maghembe ana sifa ya kuwa mhifadhi kwa kusomea na pia ni mhifadhi kwa asili yake hivyo Wizara imepata mtu makini kwenye masuala ya Uhifadhi.



“Natambua umahiri wako katika masuala ya uhifadhi nina imani utapambana na ujangili  pamoja na usafirishaji haramu wa magogo kwa kasi inayotarajiwa na wananchi”. Alisema Mhe.  Nyalandu.

Kwa upande wake, Waziri aliyechukua nafasi yake  Prof. Jumanne Maghembe amempongeza Mhe. Nyalandu kwa kazi nzuri na juhudi aliozoonesha wakati  akiwa Waziri wa Wizara hiyo katika kuhakikisha Maliasili zilizopo zinaendelea kuwepo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Prof. Maghembe ameongeza kuwa kwa sasa vita kubwa iliyoko mbele yake ni vita dhidi ya ujangili na uharibifu wa misitu ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa rasilimali za misitu kinyume cha sheria. Ameomba ushirikiano kwa wadau wote wa Maliasili nchini kumpa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha anafanikiwa katika vita hiyo.


Pamoja na mambo mengine taarifa hiyo ya makabidhiano inaelezea kazi zilizokwisha kufanyika katika kipindi cha utawala uliopita, kazi zinazoendelea na zilizopo kwenye mpango wa utekelezaji pamoja na changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya Maliasili na Utalii ikiwemo Ujangili na uvunaji pamoja na usafirishaji wa magogo. 

   

Monday, December 28, 2015

WAZIRI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII PROF. JUMANNE MAGHEMBE AWASILI MAKAO MAKUU YA WIZARA HIYO MPINGO HOUSE MARA BAADA YA KUAPISHWA IKULU LEO

 
Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (mbele kulia) akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Selestine Gesimba wakati wa mapokezi yake leo tarehe 28 Desemba 2015 katika ofisi yake mpya Mpingo House mara baada ya kuapishwa Ikulu mapema asubuhi ya leo. Nyuma yake kulia ni naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Eng. Ramo Makani na anaeongoza utambulisho katikati yao ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru.
 Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akisaini kitabu cha wageni mara tu baada ya kuingia katika ofisi yake mpya iliyopo Mpingo House mapema leo tarehe 28 Desemba 2015 baada ya kuapishwa Ikulu na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Wanaoshuhudia kulia ni Naibu Wazari wa Wizara hiyo Mhe. Eng. Ramo Makani na Katibu Mkuu Dkt. Adelhelm Meru (kushoto).
Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akiongea na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru (kushoto) na Naibu Waziri Mhe. Eng. Ramo Makani (kulia) mara baada ya kusaini kitabu cha wageni ofisini kwake mapema leo tarehe 28 Desemba 2015.
Picha ya pamoja kati ya Mhe. Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) na Naibu Waziri wake Mhe. Eng. Ramo Makani (wa pili kushoto), Katibu Mkuu wa Wziara hiyo Dkt. Adelhelm Meru (wa kwanza kulia) na Naibu Katibu Mkuu Ndugu Selestine Gesimba(kushoto). 
Sehemu ya wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwa tayari kwa mapokezi ya Waziri wao mpya Mhe. Prof. Jumanne Maghembe aliyeapishwa Ikulu leo na Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania Mhe. John Pombe Magufuli.

Sunday, December 27, 2015

PROF. JUMANNE MAGHEMBE ATEULIWA KUWA WAZIRI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, KUAPISHWA LEO IKULU

Mhe. Prof Jumanne Maghembe (pichani) ameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kujaza nafasi ya uteuzi wa nafasi ya Waziri wa Wizara ya Maliasi na Utalii aliyokuwa ameibakiza pamoja na Wizara zingine chache wakati akitangaza baraza lake la mawaziri la kwanza katika awamu ya tano ya uongozi wake. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ikulu tarehe 23 Desemba 2015 Mawaziri hao wateule wataapishwa leo Jumatatu Desemba 28, 2015 Ikulu, Dar es Salaam.

Monday, December 14, 2015

NAIBU WAZIRI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII ENG. RAMO MATALA MAKANI AAZA KAZI RASMI LEO KATIKA OFISI YAKE MPYA MPINGO HOUSE

Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Eng. Ramo Matala Makani 
(kushoto) akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru (katikati) ofisini kwake leo tarehe 14 Desemba 2015 baada ya kufika kwa mara ya kwanza toka kuteuliwa kwake na Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli kuwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo. Katika salam zake kwa uongozi na watumishi wa Wizara hiyo amewaomba ushirikiano wa dhati kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake kwa wakati ili kuleta maendeleo katika sekta ya Maliasili na Utalii nchini. Ameongeza kuwa yeye binafsi hawezi kuleta maajabu Wizarani hapo bila kupewa ushirikiano katika kazi. Pichani kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Ndugu Selestine Gesimba.   
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adelhelm Meru (kulia) akitoa taarifa fupi ya muundo pamoja na shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mhe. Naibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Ramo Matala Makani muda mfupi baada ya kuwasili katika ofisi yake mpya iliyopo Mpingo House Jijini Dar es Salaam.
 Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Eng. Ramo Matala Makani 
(kushoto) akimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru wakati akimpa taarifa fupi ya muundo wa Wizara hiyo leo tarehe 14 Desemba 2015 . 

Thursday, November 26, 2015

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAFANYA MKUTANO NA WADAU WA SEKTA YA MALIASILI NCHINI KUJADILI MAENDELEO YA SEKTA HIYO

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adelhelm Meru akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Maliasili nchini leo tarehe 26 Novemba 2015 katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Kampasi ya Bustani Jijini Dar es Salaam. Mkutano huo umeshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wa Wizara zenye muelekeo wa Maliasili, Sekta binafsi, NGOs, Waandishi wa habari na wadau wengine. Mada mbalimbali kutoka katika Sekta ndogo za Wanyamapori, Misitu, Utalii, Mambo ya Kale na Uvuvi zimewasilishwa. 
Baadhi ya Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adelhelm Meru wa pili kulia akiwa kwenye picha ya pamoja na balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe. Egon Kochanke wa pili kushoto muda mfupi baada ya kufungua Mkutano huo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mkambusho ya Taifa Prof. Audax Mabula.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adelhelm Meru akihojiwa na Mwandishi wa Habari wa Azam TV, Jamal Hashim muda mfupi baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Maliasili nchini uliofanyika leo tarehe 26 Novemba 2015 katika Ukumbi wa Chuo cha Maliasili Jijiji Dar es Salaam. Mkutano huo umejadili mambo mbalimbali ikiwemo mafanikio, changamoto na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo muhimu inayochangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa. Miongoni mwa changamoto kubwa alizozieleza Katibu Mkuu huyo ni Ujangili na Uharibifu wa misitu jambo ambalo amesema Serikali na Wizara imejiapanga kupambana nalo na kuwaomba wadau kushirikiana na Serikali katika vita hiyo.   
 Baadhi ya wadau walioshiriki Mkutano huo.
Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Sera Bi. Mary Faini kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii akiwasilisha mada kuhusu Mafanikio, Changamoto na Fursa zinazopatikana katika Sekta ya Maliasili nchini Tanzania. 
Picha ya pamoja.

Tuesday, November 24, 2015

TANZANIA YACHAGULIWA NA UNESCO KUWA MJUMBE WA KAMATI YA URITHI WA DUNIA

 
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adelhelm Meru akizungumza na Waandishi wa Habari (hawako pichani) leo tarehe 23/11/2015 katika Ofisi za Wizara hiyo ambapo amesema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia kwa kipindi cha miaka minne. Uchaguzi huo umefuatia uamuzi wa Mkutano Mkuu wa 20 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) unaohusu Urithi wa Dunia uliofanyika mjini Paris, Ufaransa tarehe 18-20 Novemba 2015. (Habari Kamili SOMA TAARIFA KWA UMMA HAPO CHINI)
 
 Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adelhelm Meru kushoto akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na Tanzania kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia. Alieleza kuwa katika Kamati hiyo Tanzania itawakilishwa na Bw. Donatius Makamba ambaye ni Mkurugugenzi Idara ya Mambo ya Kale Wizara ya Maliasili na Utalii akisaidiwa na Dkt. James Wakibara, Mwikolojia Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA) na Dkt. Mohammed Juma, Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji kutoka Zanzibar.
 Bi. Eliwasa Maro Mkurugenzi Msaidizi Utafiti Mafunzo na Takwimu Wizara ya Maliasili na Utalii akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo katika Mkutano huo na Waandishi wa Habari.
 Sehemu ya washiriki wa Mkutano huo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wakinukuu baadhi ya mambo muhimu.

KOBE 201 WALIOKUWA WAKISAFIRSHWA NJE YA NCHI WAKAMATWA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA J.K NYERERE

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Adelhelm Meru akikagua mabegi matano yenye Kobe 201 yaliyokamatwa usiku wa kuamkia leo na askari wanyamapori kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika uwanja wa Kimataifa wa J.K. Nyerere jijini Dar es Salaam.  

Watuhumiwa hao wa usafirishaji wa wanyamapori wametajwa kuwa ni David Mungi mkazi wa Muheza Mkoani Tanga na Mohammed Suleiman (43) mkazi wa Zanzibar ambao katika tukio hilo walishafanikiwa kupita kwenye mitambo ya ukaguzi lakini mbwa maalum (sniffer dogs) wakasaidia kugundua uhalifu huo. Kwa pamoja watuhumiwa hao walikamatwa na tiketi za kusafiria kuelekea nchini Malaysia. 
Kobe wapatao 201 waliokamatwa na askari wanyamapori kwa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutumia mbwa maalum (sniffer dogs).   
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Dorina Makaya kulia na Mmoja wa Askari wanyamapori wakiangalia kobe 103 waliotelekezwa eneo la Tabata hivi karibuni baada wahalifu waliohusika kuhofia kukamatwa na vyombo vya dola.