Thursday, August 17, 2017

TAARIFA KWA UMMA JUU YA ZOEZI LA KUONDOA MIFUGO NA MAKAZI NDANI YA HIFADHI YA TAIFA SERENGETI NA KWENYE MPAKA WA PORI TENGEFU LOLIONDO

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA

ZOEZI LA KUONDOA MIFUGO NA MAKAZI NDANI YA HIFADHI YA TAIFA SERENGETI NA KWENYE MPAKA WA PORI TENGEFU LOLIONDO

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngorongoro, kwa kushirikisha Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, inaendesha zoezi la kuondoa mifugo na makazi ndani ya hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo.

Zoezi hilo lililoanza tarehe 10  Agosti 2017  litadumu kwa siku kumi na nne na linashirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngorongoro, Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Serengeti na Hifadhi ya eneo la Ngorongoro.

Zoezi hilo linalenga kunusuru uhifadhi ndani ya hifadhi, ndani ya Pori Tengefu Loliondo, na ndani ya mfumo ikolojia wa Serengeti na pia kunusuru utalii katika mfumo ikolojia huo.

Aidha, hatua hii ya kuondoa makazi na mifugo kutoka katika maeneo ya mipaka ya Pori Tengefu Loliondo kutaongeza uhakika wa kupatikana malisho ya mifugo wakati wa kiangazi kwa kuwa hakutakuwepo na makazi ndani ya Hifadhi na ufugaji holela.

kimsingi zoezi hili linaendana na wito wa Serikali wa kuondoa mifugo ndani ya maeneo yote yaliyohifadhiwa nchini.

Katika kutekeleza zoezi hili, Mkuu wa Wilaya  Ngorongoro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngorongoro Bwana Rashidi Taka, alitoa maelekezo yafuatayo:

1. Zoezi litafanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo. Kwa upande wa mpaka wa Pori Tengefu Loliondo zoezi litaanzia kaskazini hadi kusini urefu wa kilometa 90, na upana wake utakuwa kilometa 5. Kwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti litafanyika upande wa mashariki kuanzia milima ya Kuka (kaskazini) hadi kigingi na. SNP 9 (kusini); 

2. Maboma yatakayokutwa ndani ya hifadhi yatateketezwa kwa moto na watu watakaokutwa na mifugo watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kupelekwa mahakamani;

3.  Maboma yaliyoko ndani ya mpaka wa Pori Tengefu Loliondo -  kwenye mpaka na ndani ya kilometa tano - wataondolewa ili warudi vijijini. Eneo hilo litabaki kwa ajili ya malisho na si kwa ajili ya makazi.  Uwepo wa makazi kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti umekuwa kichocheo kikubwa cha mifugo kuingizwa hifadhini.

Zoezi hili linalenga kuondoa changamoto kubwa ya mifugo kuingizwa Hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo, kupambana na uvamizi mkubwa uliofanywa na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani na kunusuru vyanzo vya maji kutokana na mifugo kulishwa kwenye vyanzo vya maji na hivyo kusababisha vyanzo hivyo kuharibika na kukosekana kwa maji kwa ajili ya mifugo na wanyamapori.

Hadi sasa zoezi hili la kuondoa mifugo na makazi ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo linaendelea vizuri likihusisha kuchoma moto maboma yote yaliyoachwa na wafugaji walioondoka wakati wa zoezi.

Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuufahamisha umma kuwa hakuna watu wanaopigwa katika zoezi hili.

Pia, Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuutaarifu umma kuwa habari zinazosambazwa mitandaoni ni upotoshaji wa ukweli wenye nia ovu ya kujenga chuki dhidi ya Serikali  kwa wananchi wa Loliondo na maeneo yanayopitiwa na zoezi hilo.

Aidha, Wizara ya Maliasili na Utalii, inapenda kuweka bayana kuwa, taarifa za kupigwa risasi Pormoson Losso mwenye umri wa miaka 23, mkazi wa Ololosokwan zilitolewa tarehe 8 Agosti 2017 na hazihusiani na zoezi tajwa kwani tukio hilo  lilitokea siku tano kabla ya kuanza zoezi la kuondoa mifugo na makazi ndani ya hifadhi wakati zoezi hili lilianza kutekelezwa Jumapili tarehe 13 Agosti 2017.

Hata hivyo Serikali inawapongeza wananchi wengi miongoni mwa wafugaji kwa kuunga mkono zoezi hili na kwa ushirikiano wanaotoa.
Serikali inatoa onyo kwa yeyote anayejihusisha na upotoshaji wa ukweli kuhusu zoezi hili lenye nia njema linalolenga kunusuru hifadhi, kuacha mara moja ili kujiepusha na hatua za kisheria zitakazochukuliwa pindi atakapobainika.

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

17/08/2017

Tuesday, August 15, 2017

ZIARA YA MANAIBU WAZIRI WATATU UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE NA MAMLAKA YA BANDARI TANZANIA

Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa tatu kulia), Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (wa nne kulia) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Edwin Ngonyani (wa tano kulia) wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Uzingatiaji wa Viwango wa Mamlaka ya Viwanja wa Ndege, Paul Rwegosha wakati wa ziara yao ya pamoja ya kukagua maeneo ya kuingilia wageni wa kimataifa hususan watalii katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam kwa ajii ya kubaini changamoto na kuziboresha ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya mapato ya Serikali yanayotokana na watalii wanaoingia nchini.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akizungumza katika kituo cha "terminal III" cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam kinachoendelea kujengwa wakati wa ziara ya pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni (wa tatu kulia) na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Edwin Ngonyani (kulia) kwa ajili ya kukagua maeneo ya kuingilia wageni wa kimataifa hususan watalii katika uwanja huo kwa ajii ya kubaini changamoto na kuziboresha ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya mapato ya Serikali yanayotokana na watalii wanaoingia nchini.
 Mkuu wa Kitengo cha Uzingatiaji Viwango wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini, Paul Rwegasha, akifafanua jambo wakati wa ziara iliyojumuisha  Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani(kushoto), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (wapili kushoto)  na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(kulia).Lengo la ziara hiyo ni kukagua masuala mbalimbali ikiwemo Ulinzi, Usalama, Miundombinu,Utolewaji wa visa, uingiaji na utunzaji kumbukumbu za Watalii wanaoingia nchini.
Meneja Huduma za Abiria wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Damas Temba, akielezea jinsi huduma ya kukagua mizigo inavyofanyika katika sehemu ya mizigo wakati wa ziara ya Manaibu Waziri, Mhandisi Hamad Masauni (Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi), Mhandisi Ramo Makani(Wizara ya Maliasili na Utalii) na Mhandisi Edwin Ngonyani(Wizara ya UIjenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), ikiwa na lengo kukagua masuala mbalimbali ikiwemo Ulinzi, Usalama, Miundombinu, Utolewaji wa visa, uingiaji na utunzaji kumbukumbu za Watalii wanaoingia nchini.
Meneja Mradi Ujenzi wa Uwanja Mpya wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Ray Blumrick, akizungumza na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni baada ya kumaliza kutembelea ujenzi huo.Lengo la ziara hiyo ni kukagua kukagua masuala mbalimbali ikiwemo Ulinzi, Usalama, Miundombinu, Utolewaji wa visa, uingiaji na utunzaji kumbukumbu za Watalii wanaoingia nchini.
Naibu Mkurugenzi Mamlaka ya Bandari Tanzania, Lazaro Twange (katikati), akiwaonyesha ramani ya bandari ya Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani(kulia) na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni wakati wa ziara ya viongozi hao lengo ikiwa ni kukagua masuala mbalimbali ikiwemo Ulinzi, Usalama, Miundombinu, Utolewaji wa visa, uingiaji na utunzaji kumbukumbu za Watalii wanaoingia nchini.
Naibu Mkurugenzi Mamlaka ya Bandari Tanzania, Lazaro Twange,  akifafanua jambo kwa  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani(wapili kulia) na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni (kulia), wakati wa ziara ya viongozi hao, lengo ikiwa ni kukagua masuala mbalimbali ikiwemo Ulinzi, Usalama, Miundombinu, Utolewaji wa visa, uingiaji na utunzaji kumbukumbu za Watalii wanaoingia nchini.Kushoto ni Mkuu wa Kikosi cha Polisi Bandarini,Matanga Mbushi.

Friday, August 4, 2017

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, PROF. JUMANNE MAGHEMBE AFANYA MABADILIKO MADOGO YA UONGOZI KWA BAADHI YA IDARA NA TAASISI ZA WIZARA HIYO

Image may contain: text
Image may contain: text

MHANDISI MAKANI ASISITIZA UHIFADHI SHIRIKISHI WA MALIASILI ZA TAIFA

Niabu Waziri wa Malisili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mshiri wilayani Moshi ,alipotembelea kijiji hicho kusikiliza Changamoto zinazo wakabili hususani katika eneo la Nusu Maili lililopo chini ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.
Mkazi wa Kijiji cha Mshiri akiwaslisha hoja yake kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.

NA HAMZA TEMBA -WMU
...............................................................................

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo makani amesema  jukumu la uhifadhi wa Maliasili za taifa sio la Serikali pekee kwakua Maliasili hizo ni urithi wa taifa na kila mwananchi anapaswa  kujua kuwa ana jukumu la kulinda urithi huo kutokana na umuhimu wake kwa taifa na jamii kwa ujumla.

Makani amesema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mshiri, Jimbo la Vunjo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro katika ziara yake ya siku mbili mkoani humo kwa ajili kuona changamoto za uhifadhi na kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.

Alisema askari pekee na mitutu ya bunduki haitoshi kulinda maliasili hizo kutokana na ukubwa wa maeneo yaliyopo ukilinganisha na rasilimali zilizopo. "Maliasili hizi zipo kwa faida ya kila mwananchi, tunawaomba muendelee kuiunga mkono Serikali katika kulinda Maliasili tulizonazo, tunahitaji kufanya uhifadhi shirikishi, utalii uimarike na nchi yetu ipate mapato zaidi tuweze kufikia uchumi wa kati", alisema Makani.

Akitaja miongoni mwa faida hizo, Makani alisema maliasili za misitu husaidia upatikanaji wa mvua, kuweka mazingira bora kwa ajili ya kilimo na upatikanaji wa hewa safi. Kwa upande wa faida za kiuchumi alisema sekta hiyo kupitia utalii inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimi 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, Betrita Loibooki alisema hifadhi hiyo imejenga mahusiano mazuri na wananchi wa vijiji jirani na kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kukabiliana na ujangili ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hakuna tukio lolote la ujangili wa tembo lililoripotiwa katika hifadhi hiyo.

Betrita alisema katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la uwekaji wa vigingi vya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi ili kuepuka migogoro na wananchi alisema jumla vigingi 290 vimewekwa kwa ushirikiano na wananchi kuzunguka hifadhi hiyo kwa urefu kwa kilomita 123 sawa na asilimia 100 ya lengo lililokusudiwa.


Kwa upande wa Wananchi wa kijiji hicho cha Mshiri ambacho kinapakana na Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro waliiomba Serikali iwalegezee masharti waweze kuingia na waume zao pamoja na vijana wao wa kiume katika eneo la Nusu Maili lililopo ndani ya hifadhi hiyo waweze kusaidiana kazi ya kukata majani ya mifugo na kuokota kuni.

Akitoa ombi hilo mbele ya Mhandisi Makani, mkazi wa kijiji hicho, Theresia Mtui alisema wanawake wa vijiji jirani na hifadhi hiyo wanaruhusiwa kuingia ndani ya eneo hilo kwa ajili ya kukata majani ya mifugo na kuokota kuni kavu lakini wanaume hawaruhusiwi.

Alisema wapo tayari kuhifadhi na kulinda mlima huo “Tunaomba mturuhusu na mtupe angalao miaka miwili au mitatu ya majaribio muone tutakavyolinda msitu huu”, alisema Mtui.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Estomi Benjamin Moshi alisema “Ombi letu turuhusiwe kuingia na kukata majani tu katika eneo hili, tupo tayari kuilinda hifadhi hii kwa taratibu tutakazopewa”.

Akijibu ombi hilo Naibu Waziri Makani alisema, ombi hilo litaenda kufanyiwa kazi kwa ushirikiano kati Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wakuu wa Wilaya zinazozunguka eneo hilo la hifadhi ambazo ni Moshi, Rombo, Hai na Siha, Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA ambapo wananchi watapewa mrejesho wa ombi lao hilo.

Sheria za uhifadhi zinakataza mtu yeyote kuingia na kulisha mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ikiwa ni pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu, kutokana na umuhimu wa eneo hilo kwa wananchi wanaolizunguka na katika jitihada za Serikali kujenga uhifadhi shirikishi, Mwaka 2014 Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro iliruhusu wanawake pekee kuingia ndani ya eneo hilo umbali wa mita 800 kutoka kwenye mpaka wa hifadhi hiyo kwa ajili ya kukata majani ya mifugo na kuokota kuni, wanaume walizuiliwa kutokana na kujihusisha na uharibifu wa eneo hilo. 

Nae mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia alisema ili uhifadhi uimarike ni lazima uwepo ushirikiano wenye tija kwa Serikali, Wananchi na Hifadhi huku akitoa rai ushirikiano huo uimarishwe kwa maslahi ya pande zote.

Wednesday, August 2, 2017

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI, MHANDISI RAMO MAKANI AKAGUA SHUGHULI ZA UTALII NA MFUMO WA UKUSANYAJI MAPATO KATIKA HIFADHI YA TAIFA YA MLIMA KILIMANJARO

Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kushoto) akizungumza na watalii kutoka Marekani wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utalii na mfumo wa ukusanyaji mapato katika geti la Machame ndani ya Hifadhi ya Taifa Mlima Kilimanjaro jana. Alipowauliza watalii hao ni wapi walipata habari za mlima huo, walijibu kuwa kila mtu anajua kuhusu mlima Kilimanjaro!. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa nne kushoto) akizungumza na watalii kutoka Marekani wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utalii na mfumo wa ukusanyaji mapato katika geti la Machame ndani ya Hifadhi ya Taifa Mlima Kilimanjaro jana. Alipowauliza watalii hao ni wapi walipata habari za mlima huo, walijibu kuwa kila mtu anajua kuhusu mlima Kilimanjaro!. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba, Mhifadhi Mkuu wa KINAPA, Betrita Loibooki na nyuma yake ni Mbunge wa Vunjo, James Mbatia.

Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa tatu kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhifadhi wa KINAPA, Steven Moshi (wa pili kulia) namna mfumo wa ukusanyaji mapato unavyofanya kazi katika Hifadhi ya Taifa Mlima Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utalii na mfumo wa ukusanyaji mapato katika geti la Machame jana. Kulia anayeshuhudia ni Mbunge wa jimbo la Vunjo, James Mbatia.
 Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (katikati) akipanda mlima Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utalii na mfumo wa ukusanyaji mapato katika geti la Machame jana. Kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba (kulia kwake), Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Zahoro Kimwaga (kushoto) na Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (kulia).
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa nne kulia) akipanda mlima Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utalii na mfumo wa ukusanyaji mapato katika geti la Machame jana. Wengine pichani ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo James Mbatia (wa tatu kulia), Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Zahoro Kimwaga (kushoto), Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TANAPA, Mtango Mtahiko (kulia), Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (wa pili kulia) na Mhifadhi wa KINAPA, Steven Moshi.  
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa tatu kulia) akipanda mlima Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utalii na mfumo wa ukusanyaji mapato katika geti la Machame jana. Wengine pichani ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo James Mbatia (wa nne kulia), Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba (kulia), Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TANAPA, Mtango Mtahiko (kushoto), Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (wa pili kushoto) na Mhifadhi wa KINAPA, Steven Moshi (wa pili kulia).  
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akipanda mlima Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utalii na mfumo wa ukusanyaji mapato katika geti la Machame jana. Wengine pichani ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia (kulia) na Mhifadhi wa KINAPA, Steven Moshi.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akisikiliza na kujibu kero mbalimbali za wapagazi wanaopandisha mizigo ya watalii katika mlima Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za utalii na mfumo wa ukusanyaji mapato katika geti la Machame jana
 Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, Betrita Loibook (kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na mtalii (katikati) pamoja na mhifadhi wa hifadhi hiyo wakati wa ziara hiyo.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, Betrita Loibook akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wahifadhi, mtalii na waongoza watalii.

Tuesday, August 1, 2017

MHANDISI MAKANI ASISITIZA UTALII WA MISITU YA ASILI NCHINI KAMA CHANZO MUHIMU CHA KUONGEZA PATO LA TAIFA NA JAMII KWA UJUMLA


Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akijibu kero mbalimbali za uhifadhi kwa wananchi wa Kijiji cha Shume Nywelo, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana. 

NA HAMZA TEMBA - WMU
.........................................................................................
Katika kuhakikisha sekta ya utalii nchini inaendelea kukua kwa kasi, Serikali imesema itaimarisha utalii wa Misitu ya Asili nchini iweze kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo hutegemea zaidi utalii wa wanyamapori.

Hayo yamesemwa jana wilayani Lushoto na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua migogoro mbalimbali ya uhifadhi.

Alisema sekta ya utalii nchini imekuwa ikitegemea sana wanyamapori na kusahau vivutio vingine kama vile misitu ya asili ambayo ndani yake kuna mimea na viumbe hai mbalimbali adimu duniani na ambavyo hupatikana Tanzania pekee.

“Tumezoea zaidi utalii wa wanyamapori, utalii wa misitu unaweza kuzidi hata wa wanyamapori, kwenye misitu yetu ya asili tunajivunia mimea adimu ya asili na viumbe hai mbali mbali kama vile ndege, vyura, vipepeo, mijusi nakadhalika, tunachotakiwa kufanya ni kutunza misitu yote ya asili, tuiboreshe na kuitangaza ili kupata watalii wengi zaidi na pato la taifa liendelee kukua”, alisema Makani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina jumla ya Hifadhi za Misitu ya Asili 100, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na hifadhi za taifa ambazo zipo 16 pekee, idadi hiyo kubwa pamoja na upekee wake inatoa fursa pana ya kuendeleza sekta ya utalii nchini.

Akizungumzia mafanikio, Makani alisema sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni. Alisema pamoja na faida hizo, sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa misitu ya asili ambayo ni muhimu kutafutiwa suluhu ya kudumu ili kunusuru misitu hiyo.

“Ni lazima tutafute njia endelevu ya ulinzi wa misitu, hatuwezi kuwa na askari wa kutosha, walinzi na mitutu, njia sahihi ni ulinzi shirikishi, tuwaelimishe wananchi umuhimu wa misitu na tuwaeleze watanufaikaje, tofauti na zile faida za ujumla za upatikanaji wa mvua na hali nzuri ya hewa, hii itasaidia sana kuwaleta karibu kwenye uhifadhi wa pamoja”, alisema Makani.

Akizungumza na wananchi wa kijiji Nywelo wilayani humo kuhusu mgogoro wa mpaka baina ya kijiji hicho na shamba la miti Shume, Makani alisema tatizo lililopo ni uelewa tofauti kuhusu mpaka huo baina ya pande hizo mbili,  hivyo akuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutuma wataalamu wa upimaji waliopima eneo hilo awali waje wafanye uhakiki wa mpaka huo kwa kushirikisha uongozi wa wilaya, halmashauri na kijiji hicho ili kuondoa tofauti hizo na kumaliza mgogoro huo ndani ya wiki mbili zijazo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Lugangika alisema wilaya yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti ya asili, uchimbaji wa madini kwenye maeneo ya hifadhi, uchomaji moto misitu na uhaba wa watumishi.

Katika ziara yake hiyo wilayani Lushoto, Naibu Waziri Makani alitembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba na Shamba la Miti la Shume, alifanya pia vikao vinne vya ndani na mkutano mmoja wa hadhara ambapo alijibu kero mbalimbali za wananchi.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kushoto) akisikiliza moja ya kero kuhusu uhifadhi kutoka kwa Abunio Abraham Shangali (wa pili kulia) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Shume Nywelo, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo. 
 Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akizungumza na viongozi wa kikundi cha uhifadhi na utalii cha Friends of Usambara kilichopo Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Sigareti Lugangika katika kijiji cha Shume Nywelo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Muwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mwalimu Elias Mkwilima akijibu baadhi ya hoja katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji cha Nywelo jana wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga.

Sunday, July 30, 2017

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MHANDISI RAMO MAKANI, AMUAGIZA MKUU WA WILAYA YA MUHEZA KUSHUULIKIA MGOGORO WA HIFADHI YA MSITU WA DEREMA WILAYANI HUMO

Na Hamza Temba - WMU - Muheza, Tanga
.............................................................................

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga kukutana na wakulima 879 wa vijiji vitano katika Tarafa ya Amani Wilayani humo kwa ajili kufanya uhakiki wa malipo ya fidia ya mazao waliyolipwa na Serikali ili kupisha eneo la hifadhi ya msitu wa Derema.

Mhandisi Makani ametoa agizo hilo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Msasa IBC, Tarafa ya Amani, Wilayani Muheza kufuatia malalamiko ya wananchi hao kupunjwa malipo yao wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 baina Serikali na wananchi wa vijiji hivyo vya Kisiwani, Kwemdim, Msasa IBC, Antakae na Kambi.

Akisoma risala ya wakulima hao mbele ya Naibu Waziri Makani, Mwenyekiti wa Kamati ya wakulima hao, Mohammed Rama Shesha alidai kuwa jumla ya wakulima 1,128 wa vijiji hivyo wanailalamikia Serikali kwa kuwalipa viwango pungufu vya malipo ya fidia ya mazao yao tofauti na viwango vilivyolipwa na Serikali mwaka 2002 kupitia mradi wa FINIDA. Aidha, alidai kuwa kuna baadhi ya mazao pia hayakulipiwa kabisa fidia hizo.

Akizungumzia viwango vya fidia hizo Shesha alisema wananchi walilipwa Shilingi 28,800 kwa mche mmoja wa iliki na Shilingi 11,000 kwa mche mmoja wa mgomba. Alidai viwango hivyo vilibadilika kuanzia mwaka 2005 ambapo walilipwa Shilingi 3,315 kwa kila mche mmoja badala ya Shilingi 5,100 kama ilivyoainishwa kwenye viwango vya Serikali hivyo akaomba walipwe kiasi kilichobakia cha shilingi 1,785.

Akitolea ufafanuzi wa malalamiko hayo, Naibu Waziri Makani alisema idadi kamili ya wananchi waliohakikiwa katika eneo hilo ni 879 na sio 1,128 kama alivyodai mwenyekiti huyo. Aidha, alisema viwango vilivyotumiwa kuwalipa wananchi hao mwaka 2002 sio vya Serikali na kwamba vilitumiwa na mradi wa FINIDA uliofadhiliwa na Serikali ya Finland kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa mpakani na hifadhi hiyo ili kufanikisha zoezi la kuanisha mpaka wa hifadhi hiyo na kusaidia Serikali kutimiza azma ya kuhifadhi eneo hilo.

Alisema viwango halali vya Serikali vilivyopo kisheria kwa ajili ya kulipa fidia ya mimea hiyo ni kuanzia Shilingi 5,100 kwa kiwango cha juu kwa mmea uliokoma kufikia kiwango cha uzalishaji, Shilingi 3,315 kwa mmea wenye mwaka mmoja na Shilingi 2,040 kwa mmea wenye mwezi mmoja. Alisema viwango vingine vya malipo kwa kiwango cha chini ni Shilingi 204, Shilingi 102 na Shilingi 51.

Alisema Serikali iliamua kulipa kiwango cha Shilingi 3,315 kwa mazao yote ikiwemo yale yaliyostahili kulipwa kiwango cha chini kabisa cha Shilingi 51 ili kuweka uwiano na kurahisha zoezi hilo la malipo. Alihoji kama kuna mwananchi yeyote aliyelipwa chini ya kiwango hicho japokuwa kulikuwepo na wengine mazao yao yalistahili kulipiwa viwango hivyo, hakuna aliyejitokeza.

Kufuatia ufafanuzi huo aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Muheza kutumia kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo Jumatatu kuonana na wakulima hao ili kuhakiki malipo yao na hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kama kuna yeyote aliyezulumiwa apewe haki yake. 

"Kwa wale ambao tayari wana kumbukumbu zao vizuri wazilete mbele ya Serikali, kupitia wao pengine tunaweza kupata picha ya jumla pengine kulikua na mapungufu kwenye malipo. Kuanzia jumatatu ijayo Mhe. DC tulitekeleze hilo la kukusanya nyaraka kwa wale walizonazo tuweze kuzilinganisha na zile tulizokua nazo Serikalini tujadiliane nao kwamba ni kitu gani kimebaki tofauti katika maeneo yale yale mliyofanyiwa uhakiki", alisema Mhandisi Makani.

Alisema kwa wale ambao wamepoteza nyaraka zao za malipo wataandaliwa utaratibu maalum wa uhakiki kwa kuwa kumbukumbu zote za malipo zipo kwenye Kompyuta za halmashauri ya Wilaya ya Muheza.

Alisema lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inamaliza kabisa migogoro ya ardhi nchini. “Tutahakikisha tunaboresha zaidi usimamizi wa uhifadhi wa rasilimali zetu za misitu, wanyamapori na nyinginezo kuhakikisha migogoro hiyo inapungua kwa kasi kuelekea kwenye sifuri, zero rate", alisema Makani.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo alisema, Serikali ya Wilaya imepokea maelekezo hayo na itayafanyia kazi na kwamba maafisa wa Halmashauri watafika katika kila kijiji siku ya Jumatatu na Jumatano kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo la uhakiki.

Akizungumzia zoezi la fidia Mkuu huyo wa Wilaya alisema pamoja na wananchi hao kulipwa fidia za mazao yao ambayo yalilipwa kwa awamu tatu, asilimia 50 mwaka 2005, asilimia 25 mwaka 2006 na asilimia 25 mwaka 2008, pamoja na asilimia 23 kama fidia ya ucheleweshaji wa deni, Serikali pia itawapa maeneo ya fidia ambapo kila mwananchi aliyeathirika eneo lake atapewa ekari tatu.

Alisema eneo ambalo limeanishwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi hao ni lililokuwa shamba la mkonge Kibaranga ambalo lina ukubwa wa hekta 1370 sawa na ekari 3425 na lilikua likimilikiwa na Bodi ya Mkonge, eneo hilo lilitolewa tamko ya kufutiwa umiliki wake na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mwezi Julai, 2016.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa hifadhi ya msitu wa Derema. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati), akimuonesha mwenyekiti wa kamati ya wakulima wa vijiji vitano vya tarafa ya Amani, Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Mohammed Ramadhani Shesha viwango halali vya serikali vya kulipia fidia za mazao kwa wananchi waliondolewa katika eneo la hifadhi ya msitu wa Derema wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua migogoro wa hifadhi hiyo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo.  
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa hifadhi ya msitu wa Derema.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani, (wa tatu kushoto), akiangalia eneo la Msitu wa hifadhi ya Derema na viongozi wa wilaya ya Muheza Muheza wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua mgogoro wa hifadhi hiyo. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia), akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza Mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua mgogoro ya hifadhi ya msitu wa Derema. 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kushoto), akimuonesha mwenyekiti wa kamati ya wakulima wa vijiji vitano vya tarafa ya Amani, Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Mohammed Ramadhani Shesha (kulia) viwango halali vya serikali vya kulipia fidia za mazao kwa wananchi waliondolewa katika eneo la hifadhi ya msitu wa Derema wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua migogoro wa hifadhi hiyo. 

Friday, July 28, 2017

NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII INJINIA RAMO MAKANI AFUNGA RASMI MKUTANO WA SITA WA TANAPA KWA WAHARIRI NA WANAHABARI WAANDAMIZI MKOANI TANGA


Naibu Waziri Maliasili na Utalii Injinia  Ramo Makani akimkabidhi
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006)Ltd, Absalom Kibanda cheti cha ushiriki wa Mkutano wa Mwaka na Wahariri na Wanahabari Waandamizi nchini uliohitimishwa jioni ya leo jijini Tanga.Katika hatua hiyo ya kukabidhiwa vyeti,washiriki wote walikabidhiwa vyeti vya ushiriki wao kwa ukamilifu katika mkutano huo.

Mgeni rasmi,Naibu Waziri Maliasili na Utalii Injinia  Ramo Makani(wanne kulia) akiwa katika picha ya pmoja na washiriki wa Mkutano wa Sita wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa Wahariri na Waandishi waandamizi ulioanza kufanyika jana kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Tanga ,ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni 'Utalii na Tanzania ya Viwanda'. 
Naibu Waziri Maliasili na Utalii Injinia Ramo Makani leo akizungumza jambo wakati akifunga rasmi Mkutano wa Mwaka na Wahariri na Wanahabari Waandamizi nchini jijini Tanga.

Sehemu ya Meza kuu,kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF),Theophil Makunga,Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO),Dkt.Hassan Abbas,Mkurugenzi wa Utalii na Masoko wa TANAPA,Bwa.Ibrahim Mussa ,Mgeni rasmi-Naibu Waziri Maliasili na Utalii Mhe. Ramo Makani,Mkuu wa Wilaya ya Tanga,Mhe.Thobis Mwilapa.

Baadhii ya washiriki wa mkutano huo wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri ukumbini humo kabla ya kufungwa rasmi jioni ya leo.
Mkurugenzi wa Utalii na Masoko wa TANAPA,Bwa.Ibrahim Mussa akiwashukuru washiriki wa Mkutano wa Sita wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa Wahariri na Waandishi waandamizi ulioanza kufanyika jana kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Tanga ,na kuhitimishwa rasmi jioni ya leo na Naibu Waziri Maliasili na Utalii Mhe. Ramo Makani .
Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mh.Thobias Mwilapa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mh.Martin Shigella wakati wa kutoa salamu za shukurani kabla ya kufungwa rasmi kwa Mkutano wa Sita wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa Wahariri na Waandishi waandamizi ulioanza kufanyika jana kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Tanga ,ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni 'Utalii na Tanzania ya Viwanda'.

 Meneja Mahusiano wa TANAPA,Pascal Shelutete akizungumza jambo kabla ya mgeni rasmi kufunga Mkutano wa Sita wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa Wahariri na Waandishi waandamizi ulioanza kufanyika jana kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Tanga.