slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Sunday, December 17, 2017

DK. KIGWANGALLA AFUNGA MAFUNZO YA 15 YA JESHI USU KWA MAAFISA WANYAMAPORI WA TAWA, TANAPA NA NGORONGORO MKOANI KATAVI


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwaongoza Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kupiga gwaride la ukakamavu muda mfupi baada ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi Usu jana katika kituo cha Mlele mkoani Katavi. 

Na Hamza Temba-  Mlele, Katavi
...........................................................................

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewaagiza wahifadhi wote nchini kushirikiana na wadau wengine hasa mamlaka za Mikoa na Wilaya katika maeneo yenye uvamizi wa mifugo na migogoro ya mipaka ya hifadhi ili kutatua changamoto hizo kwa namna shirikishi ikiwa ni pamoja na kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo.

Ametoa agizo hilo jana Disemba, 16, 2017 katika Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi wakati akifunga mafunzo ya 15 ya mabadiliko ya kuelekea mfumo wa Jeshi Usu kwa Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

“Kazi ya ulinzi wa rasilimali zetu za asili ni yetu na tutaiendeleza, Falsafa yetu ni kuwashirikisha wadau wote, kama kuna taasisi za kiraia kwenye eneo lako la kazi, taasisi za kijamii, mamlaka za mikoa na wilaya, wananchi, halmashauri husika mshirikiane nao ili kupunguza madhara ya operesheni zetu, na zoezi hili la uhifadhi liwe endelevu,” alisema Dk. Kigwangalla.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuheshimu Sheria za nchi na kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo kuingiza mifugo, kuanzisha kilimo, makazi na ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na matumizi mengineyo.

Awali akizungumzia mafunzo hayo alisema, lengo ni kubadilisha utendaji katika sekta ya uhifadhi kutoka ule wa kiraia kwenda wa jeshi usu ambao utaongeza nidhamu, uwajibikaji, uadilifu na maadili kwa watumishi wote wa sekta hiyo ili waweze kusimamia ipasavyo uhifadhi endelevu wa maliasili za taifa.

Alisema katika kuelekea mfumo huo, Jeshi hilo litakuwa moja bila kubagua taasisi yeyote ambayo ipo chini ya Wizara yake. “Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 inampa Waziri mamlaka ya kuunda Jeshi Usu, haikusema jeshi la TAWA, TFS, TANAPA au NGORONGORO na kwa vile hili jeshi ni langu nataka liwe moja, na tunakimbiza mchakato huu kwa haraka ukamilike kwa mujibu wa Sheria.

“Tunafarajika Mhe. Rais ameshaunga mkono na ameshatupa maelekezo, Mwenyekiti wa Kamati ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Ulinzi naye ameshasaini, ni sisi sasa tuendelee kujipanga vizuri ndani ya wizara, tuanze kuishi kwenye mfumo huo, kuanzia kwenye sare, uratibu wa mafunzo, uongozi na mfumo wa utawala,” alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema mfumo huo wa Jeshi Usu utakuwa na mnyororo mmoja wa mamlaka (chain of comand) na kwamba utahusisha taasisi zote za uhifadhi zilizopo chini ya wizara yake kwenye sekta ya wanyamapori, misitu na mali kale. “Sijawaona watu wa misitu hapa au mambo ya kale, wote hawa ni ni muhimu, rasilimali za mali kale nazo ni muhimu sana kulindwa kwani zikiharibika hazitengenezeki tena” alisema.

Katika hatua nyingine amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha kuwa mafunzo yote ya Jeshi Usu ambayo yanaendelea katika kituo cha Mlele, Mkoani Katavi yanaratibiwa moja kwa moja na Wizara tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo uratibu unafanywa na taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo.

Akizungumzia mafanikio ya vita dhidi ya ujangili na matunda ya mafunzo hayo alisema, “Katika siku za hivi karibuni tumepiga hatua kubwa ya kupambana na ujangili hasa wa tembo, Kwa dhati napongeza jitihada zinazofanywa na zinazoendelea kufanywa na wahifadhi, maaskari watumishi wengine na wadau wetu wote kwa ujumla ambazo zimeimarisha hali ya uhifadhi wa maliasili zetu”. 

Alisema kwa kiasi kikubwa matukio ya ujangili yamepungua na kwamba nyara nyingi zinazokamatwa katika kipindi hiki ni za zamani ambazo zilikuwa zimefichwa na majangili kwa ajili ya kuzitafutia masoko au kukimbia mikono ya sheria.

Alisema Wizara yake itaendelea kutumia mbinu za kisasa za kiitelijensia za kukabiliana na ujangili ikiwemo kutumia ndege zisizo na rubani kwa ajili ya doria na kuweka mifumo ya kisasa ya mawasiliano ambayo haitaweza kuingiliwa na majangili au watu wengine wenye nia ovu na uhifadhi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo, Dk. Nebo Mwina akitoa nasaha zake kwa wahitimu wa mafunzo hayo ya Jeshi Usu, aliwataka kuishi kwenye viapo vyao kwa kudumu katika ukakamavu, uhifadhi, maadili mema na nidhamu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Dk. James Wakibara aliwataka wahitimu hao kutumia mafunzo waliyopewa kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu kwa kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali, kujiepusha na rushwa na kudhibiti vitendo vya ujangili.

Mhifadhi Gloria Bidebeli kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA akisoma risala ya wahitimu hao alisema mafunzo hayo yatawawezesha kuboresha ufanisi wa shughuli za uhifadhi kwa kutii amri na kutekeleza maagizo kwa wakati.

Mafunzo hayo ya wiki nne ambayo yalianza Novemba, 20 mwaka huu yalihusisha Mameneja wa Mapori ya Akiba na Tengefu 20, Wakuu wa Kanda wa Kikosi Dhidi ya Ujangili wanane, Maafisa Wanyamapori 29 kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Wahifadhi Wanyamapori watano kutoka TANAPA na Wahifadhi Wanyamapori 26 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Mafunzo hayo yalihusisha matumizi sahihi ya silaha, mbinu mbalimbali za kupambana na uhalifu, huduma ya kwanza, ukakamavu, sheria mbalimbali zinazosimamia maliasili, ukamataji na upekuzi wa wahalifu na jinsi ya kuwafungulia hati za mashtaka.

Tangu kuanzishwa kwa mafunzo hayo Septemba 2015 jumla wahifadhi 1468 wakiwemo Askari wa Wanyamapori na Viongozi mbalimbali kutoka TAWA, TANAPA na NGORONGORO wameshapatiwa mafunzo hayo katika kituo hicho cha Mlele.  
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kushoto) akikagua gwaride la Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi Usu jana katika kituo cha Mlele mkoani Katavi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi Usu jana katika kituo cha Mlele mkoani Katavi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Dk. James Wakibara wakati wa hafla hiyo. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akimkabidhi cheti mmoja ya wahitimu wa mafunzo ya Jeshi Usu kati ya Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro jana katika kituo cha Mlele mkoani Katavi.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Dk. James Wakibara akitoa nasaha zake kwa wahitimu wa mafunzo hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (katikati) akipokea salamu za Jeshi Usu wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akipokea salamu za Jeshi Usu wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo. Kulia ni Mkufunzi Mwandamizi wa Mafunzo hayo, Fidelis Kapalata.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akiangalia onesho la kulenga shabaha liliofanywa na Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro muda mfupi kabla ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi Usu jana katika kituo cha Mlele mkoani Katavi. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Dk. James Wakibara. 
Maonesho ya klenga shabaha.
Maonesho ya klenga shabaha.
Maonesho ya klenga shabaha.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo.
Mhifadhi Gloria Bidebeli kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA akisoma risala ya wahitimu hao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiaga baada ya hafla hiyo.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.

No comments:

Post a Comment