slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Monday, April 22, 2019

WAZIRI KANYASU AAGIZA MINADA YA MIFUGO ILIYOKAMATWA IFANYIKE NJE YA HIFADHI




Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameagiza minada yote ya mifugo iliyokamatwa Hifadhini baada ya Serikali kushinda kesi mahamakani ifanyike nje ya Hifadhi ili kuondoa dhana mbaya iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa  Wahifadhi hukamata mifugo hiyo ili waweze kujiuzia wenyewe.


Pia, Ameagiza minada hiyo itangazwe katika vijiji kabla ya tarehe ya kufanyika kwa lengo la kuwajulisha Wananchi hata kwa wale walioshindwa kesi hizo ili waweze  kushiriki katika minada hiyo huku Mkuu wa Wilaya husika ashirikishwe ipasavyo kwenye minada hiyo.

Akizungumza na viongozi wa vijiji 15 katika kijiji cha Kisondoko ambavyo ni miongoni mwa vijiji vilivyokutwa ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero lililopo katika wilaya ya Kondoa  Mkoani Dodoma, Mhe.Kanyasu amesema minada hiyo isifanyike kwa usiri badala yake iwe wazi nje ya Hifadhi ili kutoa fursa kwa yeyote kushiriki.

Akizungumzia kuhusu  ugumu wa kupata vibali vya kuingilia hifadhini wakati minada ilipokuwa ikifanyikia ndani,  Mhe.Kanyasu amesema kabla ya agizo hilo wananchi waliokuwa wakishiriki katika minada hiyo  walihitajika wawe na vibali vya kuingilia hifadhini  la sivyo walikuwa  wakikatwa kwa kosa la kuingia hifadhini bila kibali.

Amebainisha kuwa endapo minada hiyo itafanyika kwa uwazi na nje ya Hifadhi kutasaidia kuepusha shutuma nyingi zikiwemo za rushwa zinazowakabili  Wahifadhi kuwa wamekuwa wakishiriki kuwatafuta wanunuzi wa Ng'ombe kutoka mikoa ya mbali kwa makubaliano ya kulipwa mara baada ya mnada.


Amesema kitendo cha minada hiyo kuanza kufanyika nje ya Hifadhi  kutasaidia kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakidai kuwa pindi mifugo yao inapotaifishwa wamekuwa hata hawajulishwi lakini wafanyabiashara wakubwa ndo wamekuwa na taarifa.


Amesema wananchi ambao mifugo yao imekuwa ikikamatwa na baadaye kutaifishwa wamekuwa na chuki na Wahifadhi huku wakiwatuhumu kuwa wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara hao  kwa kuwajulisha ili wafike Hifadhini kwa ajili ya kuinunua.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewaonya askari wanyamapori wenye tabia ya kuvizia ng'ombe wakiwa mpakani kati ya  kijiji na Hifadhi na kisha kuwasukumia ng'ombe hao ndani ya Hifadhi ili wazikamate kuwa vitendo hivyo havikubaliki na sio kazi waliyotumwa na Serikali.

Akizungumza mbele ya Naibu Waziri huyo, Mwenyekiti wa kijiji cha Ikengwe, Ismail Hamis amesema licha ya huo utaratibu mpya wa kufanyia minada nje ya Hifadhi, anaiomba serikali iangalie upya sheria ya kutaifisha mifugo kwani imepelekea wafugaji wengi kuwa maskini.

Ameshauri kuwa mifugo ikikamatwa ndani ya Hifadhi, waruhusiwe kulipa fidia kwa sababu mifugo hiyo ndo imekuwa tegemeo lao kwa kuwasaidia kusomeshea watoto wao.


Kwa upande wake, Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania,( TAWA)Mabula Misungwi amemuahidi Naibu Waziri hiyo kuwa agizo lake litatekelezwa ipasavyo ili wananchi wa maeneo ya mifugo ilikokamatwa waweze kujulishwa.

Aidha, Misungwi amewataka watumishi hao kujiepusha na vitendo vya rushwa pindi wanapokamata mifugo kutoka kwa wafugaji kuwa yeyote atakayebainika atawajibishwa kikamilifu ili iwe funzo kwa wengine.

Saturday, April 20, 2019

NAIBU WAZIRI KANYASU ATOA ONYO KWA WAHIFADHI NCHINI KUHUSU WANANCHI




Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amezionya na kuzitaka Taasisi za Uhifadhi kuacha tabia ya kuwabughudhi wananchi wanaoishi katika vijiji na vitongoji 366 vilivyokutwa ndani ya Hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini mpaka hapo maamuzi ya Kamati ya Mawaziri saba iliyoundwa kushughulikia suala hilo itakapokamilisha kazi iliyopewa na kuwasilisha ripoti  kwa Mhe. Rais.


Hatua hiyo ni kufuatia  malalamiko kutoka  kwa baadhi ya  wananchi wakiwemo wakulima na wafugaji  wanaoishi katika vijiji na vitongoji hivyo kudai kuwa wamekuwa wakisumbuliwa  na mifugo yao kukamatwa mara mara kwa madai ya kukutwa imeingia ndani ya Hifadhi.

 Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisondoko ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyomo ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Mhe. Kanyasu amezitaka taasisi hizo kufuata na kuzingatia  maelekezo yaliyotolewa na Serikali kuhusu wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

 Aidha, Mhe. Kanyasu ametumia fursa hiyo kuwaonya wananchi  ambao wamekuwa wakivamia maeneo mapya ya Hifadhi  kwa kisingizio cha kauli aliyoitoa Mhe. Rais kuacha mara moja na kwamba yeyote  atakayekamatwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.


" Wananchi ninao walenga ni wale tu ambao walikuwa wakiishi Hifadhini  kabla ya kauli ya Rais aliyoitoa mwanzoni mwa mwaka huu" Alisisitiza.


 Hata hivyo, Mhe Kanyasu amebainisha kuwa Kamati ya Mawaziri saba iliyoundwa na kuzunguka nchi nchi nzima imebaini kuwa kuna zaidi ya vijiji 820 ambavyo vimo ndani ya Hifadhi mbali ya vile 365 vilivyobainishwa awali na kuwasihi wananchi  wasiendelee kuvamia maeneo mengine.


 Mhe.Kanyasu  ameowanya baadhi ya askari wa wanyamapori  wanaoomba rushwa Kutoka kwa wafugaji pindi wanapokamata  mifugo yao ili waweze kuiachia waache mara moja tabia hiyo akisisitiza kwamba  askari yeyote atakayethibitika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa Sheria za utumishi wa Umma.


Mkuu wa wilaya ya Kondoa, Mhe. Sezaria Makota  amewataka wananchi hao kuendelea kuwa walinzi wa maeneo hayo huku wakisubili hatma ya taarifa ya kamati ya Mawaziri saba itakayotolewa hivi karibuni.

" Baada ya taarifa hiyo  mtajua hatma yenu na kama hapa mtabaki au mtahamishwa na kama mtahamishwa tutajua tutawapeleka eneo gani kwa ajili ya malisho na kilimo." Alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Wananchi, Mwenyekiti wa kijiji cha Kisondoko, Ismail Said amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa baadhi ya askari wa wanyamapori wamekuwa wakikamata mifugo yao na kuomba rushwa na pale makubaliano yanaposhindikana huondoka na mifugo yao.

Amesisitiza kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikichochea chuki baina ya wananchi na askari hao jambo linalorudisha nyuma jitihada za Uhifadhi nchini.



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine  Kanyasu wa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisondoko ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyomo ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma ambapo ameagiza wananchi hao wasibughuziwe hadi hapo maamuzi yatakapotolewa juu ya hatma yao. Wengine ni kmati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo pamoja na Maafisa wa kutoka  Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo, Sezaria Makota.



  Mkuu wa wilaya ya Kondoa, Sezaria Makota akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisondoko kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu katika kijiji  ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyoomo ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma ambapo ameagiza wananchi hao wasibughuziwe hadi hapo maamuzi yatakapotolewa juu ya hatma yao.  



.Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kisondoko wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akizungumza nao kuhusu mifugo yao kukamatwa mara kwa mara na askari wanyamapori wa Pori la Akiba la Mkungunero katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.


 Diwani wa kata ya Kisondoko, Mhe. Ismail Juma akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kisondoko kabla ya kumkaribisha Mkuu wa wilaya  Mhe. Sezaria Makota katika kijiji  ambacho ni miongoni mwa vijiji vilivyoomo ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.