slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Tuesday, January 31, 2017

ASASI ZA KIRAIA LOLIONDO ZANYOOSHEWA KIDOLE...

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Waandishi wa habari jana  mjini Dodoma, kuhusiana na  uchochezi unaofanywana Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Loliondo na Ngorongoro ya kuwahimiza wananchi kuchunga, kulima na kukata miti katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo hali inayochangia kukausha vyanzo maji yanayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 

NA LUSUNGU HELELA - WMU
.......................................................
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inalaani vikali uchochezi unaofanywa na Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Loliondo na Ngorongoro ya kuwahimiza wananchi kuchunga, kulima na kukata miti katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo hali inayochangia kukausha vyanzo maji yanayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Akizungumza na Waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amesema maelfu ya mifugo kutoka nchi jirani ya Kenya imekuwa ikiingizwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti muda wa saa 11 jioni, 

Amesema katika kukabiliana na changamoto ya uharibu wa chanzo kikuu cha maji ya Serengeti kwa asilimia 47.2 ya maji yote, tayari mifugo 1700 imeshakamatwa

Mbali na mifugo hiyo.

Waziri Maghembe alisema kuwa maelfu ya Matrekta ya kutoka nchini Kenya yameletwa kulima katika maeneo yanayopakana na Serengeti

Aliongeza kuwa hivi karibuni kilimo kimeshamiri ambapo kipindi cha nyuma wakazi walikuwa wanalima na ng’ombe (maksai) ila sasa matrekta ya Kenya yanalima na kufungua mashamba makubwa.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Maghembe ameagiza kuwa raia wa Kenya wenye mifugo Loliondo warudi makwao mara moja, Mkoa na Wilaya uchukue hatua kuwaondoa mara moja

Pia, Matrekta yote ya nchi ya Kenya yawe na usajili wa kodi (Tax Clearance) toka TRA au yarudi kwao mara moja 

Aidha, ameagiza kuwa eneo la 1,5002km liwekewe alama mara moja na uwekaji alama ukamilike ifikapo tarehe 30 Machi, 2017. 

 Kwa upande wa Utalii, ameziagiza kampuni zote za utalii ambazo hazina usajili wa kitaifa zinazofanya biashara kwa mikataba ya vijiji ziripoti Wizarani ndani ya siku saba, Ikiwa pamoja na kuonyesha usajili wao, kuonyesha vitalu walivyopewa na Serikali pamoja kuiridhisha Serikali kama wanalipa kodi. 

 Awali, akizungumzia kuhusu mgogoro huo wa Pori Tengefu la Loliondo, Waziri Maghembe alisema anatambua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo anasimamia mazungumzo ya wadau wote ili kuleta utatuzi wa mgogoro huo.

‘’Nimeambiwa kuwa mwelekeo wa mazungumzo ni mzuri nahimiza mazungumzo yaendelee, lakini nimeona nikingoja hadi mazungumzo hayo yaishe Hifadhi ya Taifa ya Serengeti itakuwa haipo.’’ alisisitiza 

Saturday, January 28, 2017

WIZARA YAKANUSHA TAARIFA ILIYOANDIKWA NA GAZETI LA RAIA MWEMA KUHUSU KUONGEZWA MUDA WA LESENI ZA VITALU VYA UWINDAJI BILA KUFUATA TARATIBU

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUKANUSHA TAARIFA ILIYOANDIKWA NA GAZETI LA RAIA MWEMA KUHUSU KUONGEZWA MUDA WA LESENI ZA VITALU VYA UWINDAJI BILA KUFUATA TARATIBU

Wizara ya Maliasili na Utalii inakanusha taarifa iliyoandikwa na gazeti la Raia Mwema Toleo Na. 494 (ISSN 1821-6250) la Jumatano tarehe 25-31 Januari, 2017 ikiwa na kichwa cha habari “Waziri Maghembe Matatani”. Habari hiyo imeeleza kuwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe anadaiwa kuongeza muda wa leseni za vitalu vya uwindaji kwa kampuni za uwindaji wa kitalii kinyume na taratibu.

Aidha, habari hiyo imeeleza kuwa waziri hakufuata utaratibu uliowekwa katika kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ambayo inaweka utaratibu wa kufuatwa kabla waziri hajatoa leseni upya. Pa, habari hiyo imeeleza kuwa sheria hiyo inataka itangazwe kwenye magazeti utaratibu wa kuomba vitalu kwa waombaji pamoja na kufanyiwa tathmini.

Vilevile, habari hiyo imeeleza kuwa waziri anatakiwa kushauriwa na chombo ambacho ndicho hufanyia tathmini kampuni hizo. Taarifa hiyo imeripoti kuwa hapo awali kulikuwa na kamati ya kumshauri waziri ambayo ilivunjwa mwaka 2012 na aliyekuwa waziri wa Wizara hiyo, Khamis Kagasheki na hivyo kuhoji uhalali wa kufanya maamuzi bila kushauriwa na chombo hicho.

Habari hiyo siyo ya kweli, kwani Waziri hakutoa leseni za umiliki wa vitalu vipya bali ameongeza muda wa umiliki wa vitalu kwa mujibu wa kifungu cha 38 (8) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 sambamba na kanuni ya 16 ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2015. Sheria na Kanuni hiyo inaelezea utaratibu wa kuongeza muda wa umiliki wa vitalu kwa wale walioomba kuendelea na umiliki wa vitalu vya awali (renewal of hunting block).

Waziri kabla ya kuongeza muda wa umiliki wa vitalu (renewal) alikaribisha maombi kwa wale wanaotaka kuongezewa muda wa umiliki wa vitalu wanavyovimiliki kwa mujibu wa Sheria tajwa hapo juu kwa barua yenye Kumb. Na. CHA.79/519/47 ya terehe 22 Aprili, 2016. Aidha maombi hayo yalipitiwa na Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji ambayo ipo kisheria na iliteuliwa Septemba 2013, kinyume na madai ya mwandishi kuwa Kamati hiyo haipo. Baada ya tathmini ya maombi hayo, Kamati hiyo ilimshauri Waziri kwa mujibu wa sheria.

Kwa kufuata utaratibu ulioanishwa katika Kifungu cha 38 (8) na (9) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori, kifungu hiki kinampa Mamlaka Waziri kuongeza muda wa umiliki wa vitalu (Renew of hunting blocks). Kanuni ya 16 kanuni ndogo ya (1), (2), (3), (4), (5), (7), (8), (9) na (10) ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii  zinatoa utaratibu wa kufuatwa wakati wa kuongeza muda wa umiliki wa vitalu kwa muhula mwingine wa uwindaji na utaratibu huo umefuatwa.

Kwa kuzingatia utaratibu huo, wamiliki wa sasa wa vitalu kama Kanuni zinavyoelekeza, waliwasilisha maombi yao Wizarani. Idara ya Wanyamapori ilipitia maombi hayo na kuwasilisha kwenye Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji. Kamati hiyo ilipitia maombi hayo tarehe 26 hadi 27 Julai 2016 na tarehe 13 Januari 2017. Hivyo, baada ya Kamati kukamilisha taratibu zote na kujiridhisha iliwasilisha ushauri wake kwa Mhe. Waziri.

Kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori alichokitaja mwandishi wa gazeti hilo, kinaeleza utaratibu wa ugawaji wa vitalu kwa waombaji wapya na siyo kwa wale wanaoomba kuendelea na umiliki wa vitalu kwa msimu mwingine (renewal).
Uongezaji wa muda wa umiliki wa vitalu vya uwindaji ulifuata Sheria, Kanuni na Taratibu, Hivyo tunawoamba wananchi wapuuze habari hiyo kwani mwandishi alikusudia kuupotosha umma kwa kunukuu na kutafsiri vifungu vya Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori isivyo sahihi.

Imetolewa na,
KATIBU MKUU
29 Januari, 2017

Wednesday, January 25, 2017

TAARIFA KWA UMMA: KUWASILISHA MAOMBI YA LESENI YA BIASHARA YA NYARA (TROPHY DEALER’S LICENCE - TDL) KWA MWAKA 2017

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
 TAARIFA KWA UMMA

KUWASILISHA MAOMBI YA LESENI YA BIASHARA YA NYARA (TROPHY DEALER’S LICENCE - TDL) KWA MWAKA 2017

Wizara ya Maliasili na Utalii inawajulisha wananchi wanaotaka kufanya Biashara ya Nyara kuwasilisha maombi yao kwa Mkurugenzi kwa kujaza Fomu za Maombi ya Leseni zinazopatikana na kupitishwa na Maafisa Wanyamapori wa Wilaya husika.  Fomu hizo pia zinapatikana kwenye Ofisi ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori zilizopo Morogoro (Jengo la TAFORI), Dar Es Salaam, na Arusha.

Hakuna Leseni za Daraja lolote au Mnyama yeyote, kwa Mwaka 2017 zitakazotolewa kwa madhumuni ya ukamataji na usafirishaji wa Wanyamapori hai nje ya nchi.  Aidha, Tangazo hili linafuta Tangazo lililotolewa tarehe 06/12/2016 katika vyombo mbalimbali vya habari.

Fomu za mwombaji zinatakiwa kujazwa na kuwasilishwa kwa Maafisa Wanyamapori wa Wilaya ndani ya siku 45 tangu tarehe ya Tangazo hili.

Meombi ya Leseni kwa Mwaka 2017 ni kwa Daraja zifuatazo:-

DARAJA
MAELEZO
1.
Biashara ya Meno ya Kiboko au Ngiri ambayo hayajatengenezwa, nzima au kipande
2.
Biashara ya ngozi za wanyamapori isipokuwa ngozi za Pimbi na Mbega
3.
Biashara ya ngozi ya Pimbi
5.
Biashara ya kukata na kutengeneza ngozi za Chui, Simba, Mondo au ngozi nyingine za wanyamapori jamii ya Paka.
6.
Biashara ya kukata na kutengeneza ngozi za wanyamapori isipokuwa za Pimbi na Mbega pamoja na kutengeneza vitu kutokana na nyara hizo.
7.
Biashara ya nyara zilizotengenezwa
8.
Biashara ya kuhifadhi nyara mbalimbali ili zisiharibike mapema
10.
Biashara ya mikia ya wanyamapori isipokuwa ya Tembo, Faru, na Mbega na vitu vinavyotokana na nyara hizo.
11.
Wakala wa kusafirisha nyara kwa ujumla isipokuwa Wanyama hai.
17.
Bustani ya Wanyamapori
18.
Mashamba ya kufuga wanayamapori (isipokuwa kwa nia ya kusafirisha Wanyamapori hai nje ya nchi).
19.
Vituo vya Karantini (isipokuwa kwa nia ya kusafirisha wanyama hai nje ya nchi).
20.
Ranchi za wanyamapori (isipokuwa kwa ajili ya kusafirisha wanyamapori hai nje ya nchi)
21.
Aina yoyote ya biashara ya nyara ambayo haikutajwa kwenye daraja la 1-20 isipokuwa kusafirisha wadudu na viumbe wengine hai nje ya nchi.


Mwombaji anatakiwa kuwasilisha fomu ya maombi ya leseni pamoja na uthibitisho wa yafuatayo:-

1.                  Endapo mwombaji ni mtu binafsi anatakiwa awasilishe hati ya usajili  wa jina la biashara (Certificate of Registration of Business name) au iwapo mwombaji ni Kampuni awasilishe Katiba ya Kampuni (Memorandum and Articles of Association) na Hati ya utambulisho wa mlipa kodi (Tax payer Identification Number).

2.                  Uthibitisho wa kuwa na Wakamataji wenye elimu ya Uhifadhi wa Wanyamapori kutoka kwenye Chuo kinachotambulika na Serikali.

3.                  Uthibitisho kwamba biashara ina leseni kutoka kwenye Mamlaka husika.

4.                  Mpango wa biashara (business plan) unaoruhusu biashara inayotarajiwa kufanywa na uthibitisho wa mtoaji.

5.                  Uthibitisho wa malipo ya Ada ya maombi ya leseni ya (TZS. 5,000/=) ambayo haitarudishwa (Non-Refundable).  Fedha hizo zilipwe kupitia Benki ya NBC Samora Avenue, Akaunti Na. 012103011903 ya “SELOUS GAME RESERVE au CRDB Tanzania Wildlife Management Authority Akaunti Na. 0150319566100 TAWA”

6.                  Mwombaji asiwe na rekodi ya kupatikana na hatia ya kuvunja Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na

7.                  Kwa mwombaji wa shughuli za ufugaji wa Wanyamapori, Ada ya Maombi ya Leseni ya Ufugaji itategemea aina ya ufugaji kama ifuatavyo:-

i)                    Bustani ya Wanyamapori; Ada ya Maombi ni Dola za Kimarekani 150 kwa mzawa, mzawa kwa kushirikiana na Mgeni Dola za Kimarekani 250.

ii)                  Mashamba ya Ufugaji Wanyamapori; Ada ya Maombi ni Dola za Kimarekani 200 kwa mzawa na kwa mzawa akishirikiana na mgani ni Dola za Kimarekani 500.

iii)                Ranchi za Wanyamapori Ada ya Maombi ni Dola za Kimarekani 500 kwa mzawa na kwa kushirikiana na mgeni ni Dola za Kimarekani 1000.
  

KATIBU MKUU
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

23 JANUARI, 2017

FARU FAUSTA AWEKA REKODI NGORONGORO

MNYAMAPORI aina ya faru anayesadikiwa kuwa na umri mkubwa kuliko faru wote duniani, anaishi katika hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Faru Fausta mwenye umri wa miaka 54, ni miongoni mwa faru weusi ambao asili yao ni kusini mwa Afrika na kutokana na umri mkubwa, kwa sasa amepoteza uwezo wa kuona.
Tofauti na faru wengine wenye umri mkubwa duniani, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Fausta anaishi katika mazingira ya asili, lakini wengine katika nchi tofauti duniani, ikiwamo Kenya wanaishi katika mazizi maalumu (zoo) au maeneo yaliyotengwa kwa faru yajulikanayo kama “Rhino Sanctuary”.
Akizungumza na MTANZANIA, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk. Fred Manongi, alisema kwa sasa Fausta amehifadhiwa katika banda maalumu, baada ya kujeruhiwa na kundi la fisi.
Alisema wataalamu wa wanyamapori na uhifadhi walikuwa wanatafakari kumwachia kutoka katika banda hilo, ili arejee na kuishi kwenye mazingira yake ya asili baada ya afya yake kuimarika.
“Huyu faru amekaa katika banda kwa takribani mwezi mmoja sasa, tunaangalia uwezekano wa kumwachia aendelee kuishi kwenye mazingira yake ya asili baada ya majeraha yake kuanza kupona,” alisema.
Mhifadhi huyo, alisema Fausta ambaye ni miongoni mwa faru zaidi ya 50 wanaoishi Ngorongoro, hakuwahi kuzaa katika maisha yake yote.
“Fisi waliomjeruhi walifanikiwa kufanya hivyo kutokana na udhaifu alionao unaotokana na umri mkubwa, lakini tumejipanga kuhakikisha anaishi miaka mingi zaidi, na kuacha historia ya kipekee,” alisema Mhifadhi bingwa wa faru wa NCAA, Cuthbert Lemanya.
Matukio mawili yaliyotokea Desemba, mwaka jana nchini Tanzania na Kenya, yaliibua mijadala mizito na kuwafanya faru kutawala mijadala kadha wa kadha.
Nchini Tanzania, ziliibuka taarifa zilizodai kupotea kwa faru maarufu kwa jina la John, aliyekuwa akiishi Ngorongoro, ambaye awali ilidaiwa aliuzwa kwa mwekezaji Kampuni ya Grumeti.
Lakini baadae ilibainika kuwa John hakuuzwa, bali alihamishwa baada ya taratibu zote kufuatwa kutoka Ngorongoro na kupelekwa eneo la Sasakwa, Grumeti, ambako Agosti 21, mwaka jana alifariki dunia kutokana na maradhi na umri. Kwa kawaida umri wa faru kuishi ni miaka 35 hadi 38.
Kwa upande nchi jirani ya Kenya, Desemba 5, mwaka jana, faru mzee kuliko wote nchini humo aliyejulikana kwa jina la Solio (42), alifariki dunia.
Solio alikuwa amehifadhiwa eneo maalumu la uhifadhi (wildlife conservancy), liitwalo Lewa, ambalo linatajwa kuwa hifadhi kubwa maalumu (si ya asili) ya faru barani Afrika. Katika hifadhi hiyo kuna faru weusi 84 na weupe 72.
Faru ni miongoni mwa wanyamapori ambao wapo katika tishio la kutoweka duniani, kutokana na majangili kuwaua kisha kuuza pembe zao kwa bei kubwa, soko kubwa likiwa Mashariki ya Mbali.
Tangu mwaka 1998, Tanzania imekuwa na mpango mkakati maalumu wa kuongeza idadi ya faru, ili kuwa na zaidi ya faru 100 ifikapo 2018.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Save the Rhino ya nchini Uingereza, kulikuwa na faru 500,000 barani Afrika na Asia mwanzoni mwa karne ya 20, lakini kwa sasa wanakadiriwa kusalia 29,000. (SOURCE - MTANZANIA)

Tuesday, January 24, 2017

WIZARA YA MALIASILI YAWASILISHA TAARIFA YA MAENDELEO YA SEKTA YA UTALII KWA KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII MJINI DODOMA

Mkurugenzi wa Idara ya Utalii Wizara ya Maliasili na Utalii, Zahoro Kimwaga (wa pili kushoto) akiwasilisha taarifa ya hali ya sekta ya utalii nchini kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii mjini Dodoma tarehe 24 Januari, 2017.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto), Naibu waziri, Mhandisi Ramo Makani (wa tatu kushoto), Katibu Mkuu, Meja Generali Gaudence Milani (kushoto mstari wa nyuma), Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki (wa pili kushoto mstari wa nyuma), viongozi wengine wa Wizara na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi ya Maliasili na Utalii wakifuatilia uwasilishaji wa Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara na Taasisi zake kwa Mwaka wa fedha 2016/2017 kwa Kamati hiyo.
Kamati ya Bunge ya kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii ikipokea Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara na Taasisi zake kwa Mwaka 2016/17 mjini Dodoma. 
Wajumbe wa kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakiwa na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ( wengine hawapo pichani) wakisikiliza taarifa ya Utekelezaji iliyowasilishwa na Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro - NCAA, Dkt. Fredy Manongi tarehe 23 Januari 2017. 
 
  Katibu Mkuu, Meja Generali Gaudence Milani (kushoto), Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki, Viongozi wengine wa Wizara hiyo na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakiwa kwenye kikao cha pamoja mjini Dodoma. 
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dr. Fredy Manongi akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji ya mamlaka hiyo kwa kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii mjini Dodoma tarehe 23 Januari 2017. (Picha na Dorina Makaya-WMU)

Thursday, January 19, 2017

KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YATEMBELEA MAKUMBUSHO YA TAIFA NA KIJIJI CHA MAKUMBUSHO

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Eng. Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) akizungumza na wabunge na baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakati walipokuwa wakiangalia sanamu mtu wa kabila la Kimasai iliyochongwa kwa kutumia mti aina ya Mpingo kabla ya Wabunge wa kamati hiyo kuanza kutembelea Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam, wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Eng. Ramo makani.
Mwenyekiti wa Wabunge wa Kamati ya Maliasili, Ardhi na Utalii, Eng. Atashasta Nditiye ( watatu kushoto) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng.Ramo Makani (watatu kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (wa pili kulia) akizungumza na wabunge na baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakati walipokuwa wakiangalia zana za mawe zilizotumiwa na binadamu wa kale wakati Wabunge wa kamati ya Maliasili, Ardhi na Utalii walipokuwa wakitembelea Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Wabunge wa Kamati ya Maliasili, Ardhi na Utalii, Eng. Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) akitia saini kwenye kitabu cha Wageni akishuhudiwa na baadhi ya Wabunge wa Kamati ya Maliasili, Ardhi na Utalii pamoja na baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwa kwenye chumba maalumu ( strong room) cha kuhifadhia urithi wa utamaduni wa thamani kubwa kama zamadamu (hominine remains), masalia ya akiolojia, historia pamoja na sanaa ya ethnografia) leo walipotembelea Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam, 
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Eng. Ramo makani (kushoto) akitia msisitizo jambo kwa Mwenyekiti wa Wabunge wa Kamati ya Maliasili, Ardhi na Utalii, Eng. Atashasta Nditiye (katikati) akiwa pamoja na Mbunge wa kamati hiyo, Mhe, Shabani Shekilindi ( wa kwanza kulia) mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea kijiji cha Makumbusho cha Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi akizungumza na Mwenyekiti wa Wabunge wa Kamati ya Maliasili, Ardhi na Utalii, Eng. Atashasta Nditiye wakati wakielekea kuangalia Nyumba ya wahehe iliyopo kijiji cha Makumbusho cha Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, ( Picha na Lusungu Helela- WMU)

Wednesday, January 18, 2017

KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YATEMBELEA MAKAO MAKUU YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, MPINGO HOUSE

NA HAMZA TEMBA - WMU
...........................................................................

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetembelea makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mpingo House jijini Dar es Salaam leo na kuzuru ghala la nyara za Serikali kuona utunzaji wa meno ya tembo na changamoto zake.

Kabla ya kutembelea ghala hilo kamati hiyo ilipokea taarifa maalum ya wizara juu ya mchakato mzima wa taratibu za ukusanyaji wa meno ya tembo, usafirishaji, uhakiki, usajili kwenye mfumo maalum wa kielektroniki, uhifadhi wake na ulinzi thabiti wa ghara hilo.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Robert Mande alisema meno yanayohifadhiwa katika ghala hilo ni yale yanayotokana na vifo asilia, kuuawa kutokana na uharibifu wa mali na maisha ya binadamu na yale yanayotokana na ujangili.

Waziri wa Maliasili na utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijibu moja ya swali la wajumbe wa kamati hiyo ambao walitaka kujua uwezekano wa kuuza meno hayo ya tembo yaliyohifadhiwa ili kulipatia taifa mapato,  amesema msimamo wa Serikali ya Tanzania kwa sasa sio wa kuuza wala wa kuchoma meno hayo.

"Msimamo wetu ni kama ule wa nchi za Kenya, Uganda, Zambia, Malawi na Msumbiji wa kutokuuza meno haya kwa sasa kwasababu mbalimbali za kimsingi kabisa, moja ikiwa ni sababu za kiutafiti ambapo vinasaba vya meno ya zamani vinaweza kutumika kubaini mambo mbalimbali ikiwemo utafutaji wa dawa ya magonjwa ya tembo”, alisema.

Alisema kitendo cha kuuza meno hayo pia ni kuchochea zaidi biashara hiyo kwakuwa kitaongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo kwenye masoko hivyo kuendelea kuipa uhai biashara hiyo haramu duniani.

Hapo awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Generali, Gaudence Milanzi akizungumza kwenye kikao cha kamati hiyo mkoani morogoro kilichohusisha uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) alisema ujangili hapa nchini kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba nyara zinazokamatwa kwa sasa ikiwemo meno ya tembo ni za zamani zilizokuwa zikisubiria kusafirishwa nje ya nchi.

Alisema hatua hiyo ya kupungua kwa uhalifu huo imefanikiwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa vikosi maalum vya Askari wa wanyamapori vya kudhibiti ujangili kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini.

Alisema hatua ya Serikali ya China kupiga marufuku biashara ya meno ya tembo nchini humo ni jambo la kupongezwa na kwamba uamuzi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msukumo wa vitendo vya ujangili nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Naye mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye amewapongeza viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii namna walivyojipanga katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo na kuwaahidi ushirikiano kutoka kwa kamati yake.

Aliahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi wa wizara hiyo katika kuhakikisha kuwa wanaikabili changamoto kubwa ya uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. "Sisi tunaungana na nyie, hatukubali mifugo kwenye hifadhi zetu, kwakuwa zinaharibu ubora wa hifadhi hizo, tunawaahidi ushirikiano wa kukabiliana ma changamoto hiyo"

Kamati hiyo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilitembela pia makao makuu ya Wakala ya Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) zote za mkoani Morogoro.
 Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki (kulia) akisalimiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye baada ya kuwasili makao makuu ya Wizara hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam jana huku akiongozana na wajumbe wa kamati hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto) akizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii  katika ukumbi wa Ngorongoro wizarani hapo jana. Kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Ramo Makani, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kemilembe Lwota, Mwenyekiti wa Kamati, Mhandisi Atashasta Nditiye, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki.
Kikao kikiwa kinaendelea katika ukumbi wa Ngorongoro, Makao Makuu ya Wizara hiyo, Mpingo House, Jijini Dar es Salaam.
 Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Robert Mande akiwasilisha taarifa kuhusu taratibu za uhifadhi wa ghala la meno ya tembo kwa Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii katika ukumbi wa Ngorongoro makao makuu ya Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam leo.
 Baadhi ya wajumbe wa kamati ya bunge Ardhi, Maliasili na Utalii katika kikao hicho. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki.
 Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo.
Baadhi ya wakurugenzi wa Idara katika Wizara ya Maliasili na Utalii, wakifuatilia mjadala kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge.
 Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge.

Tuesday, January 17, 2017

KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YATEMBELEA MAKAO MAKUU YA TTSA, TAWA NA TAFORI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto) na Katibu Mkuu wa Wizaya hiyo, Meja Generali Gaudence Milanzi (kushoto) wakiwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipowasili katika ofisi za Wakala ya Miti za Mbegu Tanzania (TTSA) mjini Morogoro jana kwa ajili ya kuona kazi na miradi ya wakala huyo. Kushoto ni wajumbe wa kamati hiyo, Silafi Maufi ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa na Godwin Molel (wa pili kushoto), Mbunge wa jimbo la Siha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mohammed Kilongo alipowasili na kamati yake katika ofisi za Wakala wa Miti za Mbegu Tanzania mkoani Morogoro jana. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii, Marry Faini na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa (wa pili kulia).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akiwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika ofisi za makao makuu ya Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA). Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Atashasta Nditiye.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Edigar Masunga (wa pili kulia) akiwasilisha taarifa ya wakala huyo kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi ya Maliasili na Utalii mkoani Morogoro jana. Alisema wakala huyo huzalisha aina 195 za mbegu, kati ya hizo asilimia 60 ni miti ya kienyeji na asilimia 40 ni miti ya kigeni. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Nditiye.
Katibu Mkuu wa Wizaya ya Maliasili na Utalii, Meja Generali Gaudence Milanzi (kulia) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Aloyce Nzuki wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Edigar Masunga kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii mkoani Morogoro jana. Meja Generali Milanzi alisema Ujangili nchini kwa sasa umepungua kutokana na kasi ya udhibiti wa vitendo hivyo inayofanywa na askari wa wanyamapori kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama. Alisema nyara nyingi zinazokamatwa kwas sasa ni zile za zamani na kwamba uamuzi wa China kuzuia biashara ya meno ya tembo utasaidia kupunguza zaidi ujangili nchini.
Mtaalam wa Baiolojia ya mbegu wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania, Fandey Mashimba (kulia) akitoa ufafanuzi wa namna ya uaandaaji wa mbegu na miche ya miti kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipotembelea wakala huyo jana Mkoani Morogoro kwa ajili ya kuona shughuli na miradi ya wakala huyo. Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe.
Meneja wa Kanda ya Mashariki na Kati wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania, Frida Mngulwi (kulia) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii namna mashine za kuandaa mbegu za miti zinavyofanya kazi. Wa pili kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe.
 Wajumbe wa Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii wakikagua vitalu vya miche ya miti vya wakala wa mbegu za miti Tanzania (TTSA) walipotembelea makao makuu ya wakala huyo mkoani Morogoro jana.
 Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Edigar Masunga (mbele kushoto) akiongoza wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kukaga shamba la miti la wakala huyo mkoani Morogoro jana. 
Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mohammed Kilongo (kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) wakati wa kukagua shamba la miti la Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA) mkoani Morogoro jana.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Laurence Mbwambo (kushoto) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii namna taasisi hiyo ilivyojipanga kuendesha tafiti zake na kuhifadhi taarifa za utafiti kwa njia ya mtandao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisistiza jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walipotembelea ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) mkoani Morogoro jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wanne kushoto) akitoa maelezo ya mtandao (kulia) wa kugundua matukio ya moto kwenye maeneo ya misitu nchini unavyofanya kazi kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Mtambo huo upo chini ya usimamizi na utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI).
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Martin Laibooki akiwasilisha taarifa ya mamlaka hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo mkoani Morogoro jana. Katika taarifa yake ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Agosti 2016 mamlaka hiyo ilitoa jumla ya shilingi bilioni 2.2 kama faida ya mgao wa mapato ya utalii kwa Halmashauri za Wilaya, vijiji pamoja na Jumuiya za Uhifadhi wa Wanyamapori nchini (WMAs). Hata hivyo alisema changamoto kubwa ya mamlaka hiyo kwenye uhifadhi kwa sasa ni uvamizi wa mifugo ndani ya maeneo ya hifadhi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utali, Dkt. Aloyce Nzuki (kulia) akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa wakati kamati ya bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea makao makuu ya TAFORI NA TAWA mkoani Morogoro jana.

Picha ya pamoja ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania na Taasisi ya Utafiri wa Misitu Tanzania (TAFORI).
Mtaalamu wa maabara wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) akieleza namna tafiti za misitu zinavyofanywa kwenye maabara ya taasisi hiyo kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) wakiwa kwenye mkutano wa kamati hiyo ya bunge.

Friday, January 13, 2017

NAIBU WAZIRI MAKANI ALIVYOPANIA KUMALIZA MGOGORO ULIODUMU ZAIDI YA MIAKA 25 LOLIONDO

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kushoto) akioneshwa Ramani ya Kijiji cha Ololosokwan na Diwani wa Kata hiyo, Yanick Ndoinyo alipotembelea kijiji hicho hivi karibuni kuona changamoto za uhifadhi. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Ololosokwan, Emmanuel Salteimoi. 
Kundi la mifugo likiwa ndani ya Pori Tengefu la Loliondo, karibu kabisa na mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akizungumza katika kikao cha wadau wa mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo alichokiitisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo mkoani Arusha hivi karibuni.

NA HAMZA TEMBA - WMU
............................................................................

Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli mara tu ilipoingia madarakani mwezi Oktoba mwaka juzi ilitoa vipaombele vyake kadhaa vya kutelezwa na wizara zake mbalimbali huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikikabidhiwa majukumu mazito matatu ya kutekeleza katika kipindi cha uongozi wake. 


Majukumu hayo yaliyotolewa na Rais Magufuli wakati wa hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, ni yale ya kuhakikisha kuwa wizara hiyo inakomesha vitendo vya ujangili, kuongeza mapato ya serikali na kushuulikia utatuzi wa migogoro ya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi nchini. 

Wizara ya Maliasili na Utalii, imesema kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa malengo yake ya uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kuendeleza Utalii pamoja na utekelezaji wa vipaombele ilivyopewa na Serikali ya awamu ya tano kuwezesha kufikia malengo hayo yanatimia kwa wakati.

Kwa upande wa utatauzi wa migogoro kwenye maeneo ya hifadhi nchini, Wizara hiyo imejipanga kuwashirikisha wadau wote wanaohusika na migogoro hiyo kwa kukaa nao pamoja kwenye vikao vya majadiliano na kuweka mikakati ya pamoja ya kufikia suluhu ya migogoro hiyo kwa faida ya Serikali na wadau wote wanaohusika.

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alifanya ziara ya kiutafiti katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Pori Tengefu la Liliondo, lengo kuu la ziara hiyo ikiwa ni kuona uhalisia wa changamoto zilizopo pamoja na kupata taarifa sahihi kutoka kwa wadau husika, alifanya hivyo bila ya kujitambulisha kwa lengo la kupata taarifa sahihi kuhusiana na migogoro hiyo.

Akiwa katika Tarafa ya Loliondo alitembelea kijiji cha Ololosokwan, Pori Tengefu la Liliondo, sehemu ya mpaka wake na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na eneo la muwekezaji, kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) na kampuni ya &Beyond (Kleins Camp).


Akiwa katika eneo hilo alizungumza na viongozi wa kijiji cha Ololosokwan ambao waliwasilisha changamoto kadhaa ikiwemo ongezeko la mifugo kutoka nchini Kenya na vijiji jirani hususani wakati wa kiangazi kwa ajili ya kutafuta malisho na uelewa tofauti wa mpaka baina ya vijiji na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Diwani wa Ololososkwan, Yanick Ndoinyo alisema uhifadhi umekuwa ukiwanufaisha kwa kiasi kikubwa kwa kuwa kupitia utalii kijiji hicho hupata fedha taslim zaidi ya shilingi milioni 300 kwa mwaka kupitia mikataba ya wawekezaji na mgao kutoka Serikalini.

Pamoja na mchango huo amesema “wawekezaji wa eneo hili wamekuwa wakitekeleza miradi ya jamii ambapo wamechimba visima vinne, wamejenga madarasa mawili na kisima kingine kinajengwa jirani na kata hii, lakini kampuni zote kwa ujumla zinatoa ajira kwa wanavijiji, kwahiyo kwakweli sisi ni kijiji ambacho tumeona manufaa ya utalii “

Ndoinyo alisema fedha hizo zimekuwa zikisaidia kusomesha watoto masikini kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu, kusaidia ujenzi wa zahanati na huduma nyingine za jamii.

Kwa upande wa kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) ambao wamewekeza katika pori hilo kupitia Afisa Mahusiano wao, William Parmat walisema changamoto kubwa inayowakabili ni ya wananchi kuingiza mifugo katika eneo la uwekezaji jambo linalosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo wanyamapori kutoweka.

Muwekezaji huyo alisema wapo tayari kuweka makubaliano ya uhifadhi na wananchi pamoja na kusaidia kujenga miundombinu ya huduma za jamii. Alisema changamoto ya mifugo imesababishwa na msukumo wa baadhi ya asasi za kiraia kwa wananchi kwamba Serikali inataka kuchukua pori hilo hivyo waingize mifugo yao kwa ajili ya kulilinda.

Naibu Waziri Makani aliuahidi uongozi wa kijiji cha Ololosokwan pamoja na wawekezaji hao kuwakutanisha wadau wote wanaohusika na mgogoro wa pori hilo kwa ajili kujadili changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.


Akiwa kwenye Pori Tengefu la Loliondo na kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti alishuhudia makundi ya mifugo ikiwa ndani ya pori hilo na mingine ikizagaa maeneo ya mpakani na Hifadhi hiyo. Alielezwa na Viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro kuwa, mifugo hiyo huingizwa kwa ajili ya malisho wakati wa usiku kwenye hifadhi ya Serengeti. 

Inaelezwa kuwa eneo la Pori Tengefu la Loliondo lina umuhimu wa pekee katika uhifadhi kwa sababu ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori, mapito ya wanyamapori na vyanzo vya maji. Kutokana na sababu hizo, eneo hilo linapaswa kuendelea kuhifadhiwa ipasavyo, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti.

Siku chache baada ya ziara hiyo ya kiutafiti, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kikazi mkoani Arusha na kuwaagiza viongozi wa Serikali kukaa pamoja na wadau wanaohusika na migogoro ya ardhi katika Tarafa ya Loliondo na kuitafutia suluhu ya kudumu.

Baada ziara hiyo ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Makani aliendelea na ziara yake katika tarafa ya Loliondo ambayo aliikatisha kupisha ziara Waziri Mkuu. Mara hii ziara hiyo ikihusisha pia ufuatiliaji wa maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa kwenye ziara yake mkoani Arusha.

Aliwasili Loliondo kwa ajili ya kuweka mkakati wa kumaliza changamoto ya mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 25 kati ya mwekezaji, wanavijiji, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), suala la mifugo, uharibifu wa mazingira na utata wa mpaka wa Hifadhi ya Serengeti na Loliondo.  

Tarehe 29 Desemba, 2016 alifanya mkutano na wadau wanaohusika moja kwa moja na mgogoro wa Loliondo, mkutano huo ulifanyika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo, Kupitia mkutano huo aliunda kamati maalum ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.

Kamati hiyo inahusisha taasisi za serikali, asasi za kiraia, viongozi wa dini, wazee wa kimila (Leigwanan), viongozi wa vijiji, wajumbe wa kamati teule ya vijiji 15 ya mpango bora wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa uhifadhi na wawakilishi wa wanawake na vijana. Aliunda pia kamati ya kuandaa kanuni za kundesha vikao vya kamati hiyo.

Naibu Waziri huyo aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Mfaume Taka akateuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.  

“Kamati ya kanuni itumie muda wa wiki mbili hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2017 iwe imeshakamilisha rasimu ya kanuni ili tarehe 18 Januari, 2017 tuzipitie, tuzijadili na kuzipitisha. Hatua itakayofuata ni mawasilisho ya taarifa mbalimbali kutoka kwa wadau pamoja na majadiliano”, alisema Makani.

Aliagiza pia taarifa mbalimbali za kamati zilizowahi kushuulikia mgogoro huo miaka ya nyuma na mapendekezo yake pamoja na taarifa mbalimbali za sheria za uhifadhi na vijiji kwa ajili ya kusaidia majadiliano hayo ziwasilishwe.

Kikao hicho kilikubaliana kazi hiyo ifanyike ndani ya miezi mitatu hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2017 iwe imekamilika na muafaka upatikane kwa ajili ya kuishauri Serikali namna bora ya kumaliza mgogoro huo.

Wadau wote walikubaliana kushiriki vikao vya majadiliano huku wengine wakipongeza hatua iliyofikiwa na Serikali ya kutaka kumaliza mgogoro huo, hata hivyo Naibu Waziri Makani alitoa angalizo kwa wadau hao; "Kuna watu humu ndani na hata nje ambao hawataki tumalize migogoro Loliondo, nitoe rai kwao, waache chokochoko.

“Wafikishiwe salamu, tutawabaini, tutawakamata na kuwashitaki kwa kosa la kukwamisha jitihada za Serikali kuwaletea wananchi maendeleo yao, Wananchi muone umuhimu wa jitihada za Serikali kumaliza changamoto hii na kutuunga mkono”, alisema Makani.

Akizungumza katika mkutano huo, mchangiaji mmoja ambaye hakutambulisha jina lake alisema “Eneo hili Loliondo lenye kata saba na vijiji 15 lilikosekana dawati la pamoja, kwa mfumo huu tutaenda mbele, Taasisi nyingi zimekuwa zikipotosha umma kuhusiana na taarifa za Loliondo, tutashukuru kuona tunapata muafaka kupitia kamati hii iliyoundwa leo”

Changamoto ya Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo ni mkwamo kwa maendeleo ya wananchi wa Loliondo na Taifa kwa ujumla, Kila mwananchi wa Loliondo ana nafasi kubwa  ya kuhakikisha mgogoro huu unafikia tamati kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine. Kila mmoja atimize wajibu wake mgogoro huu utakuwa historia na Loliondo itakua salama na kupiga hatua kimaendeleo.