JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI
NA UTALII
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
KUKANUSHA TAARIFA ILIYOANDIKWA
NA GAZETI LA RAIA MWEMA KUHUSU KUONGEZWA MUDA WA LESENI ZA VITALU VYA UWINDAJI BILA
KUFUATA TARATIBU
Wizara
ya Maliasili na Utalii inakanusha taarifa iliyoandikwa na gazeti la Raia Mwema
Toleo Na. 494 (ISSN 1821-6250) la Jumatano tarehe 25-31 Januari, 2017 ikiwa na
kichwa cha habari “Waziri Maghembe
Matatani”. Habari hiyo imeeleza kuwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.
Jumanne Maghembe anadaiwa kuongeza muda wa leseni za vitalu vya uwindaji kwa
kampuni za uwindaji wa kitalii kinyume na taratibu.
Aidha,
habari hiyo imeeleza kuwa waziri hakufuata utaratibu uliowekwa katika kifungu
cha 38 (6) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ambayo
inaweka utaratibu wa kufuatwa kabla waziri hajatoa leseni upya. Pa, habari hiyo
imeeleza kuwa sheria hiyo inataka itangazwe kwenye magazeti utaratibu wa kuomba
vitalu kwa waombaji pamoja na kufanyiwa tathmini.
Vilevile,
habari hiyo imeeleza kuwa waziri anatakiwa kushauriwa na chombo ambacho ndicho
hufanyia tathmini kampuni hizo. Taarifa hiyo imeripoti kuwa hapo awali kulikuwa
na kamati ya kumshauri waziri ambayo ilivunjwa mwaka 2012 na aliyekuwa waziri wa
Wizara hiyo, Khamis Kagasheki na hivyo kuhoji uhalali wa kufanya maamuzi bila kushauriwa
na chombo hicho.
Habari
hiyo siyo ya kweli, kwani Waziri hakutoa leseni za umiliki wa vitalu vipya bali
ameongeza muda wa umiliki wa vitalu kwa mujibu wa kifungu cha 38 (8) cha Sheria
ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 sambamba na kanuni ya 16 ya Kanuni
za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2015. Sheria na Kanuni hiyo inaelezea utaratibu
wa kuongeza muda wa umiliki wa vitalu kwa wale walioomba kuendelea na umiliki
wa vitalu vya awali (renewal of hunting block).
Waziri
kabla ya kuongeza muda wa umiliki wa vitalu (renewal) alikaribisha maombi kwa
wale wanaotaka kuongezewa muda wa umiliki wa vitalu wanavyovimiliki kwa mujibu
wa Sheria tajwa hapo juu kwa barua yenye Kumb. Na. CHA.79/519/47 ya terehe 22
Aprili, 2016. Aidha maombi hayo yalipitiwa na Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa
Vitalu vya Uwindaji ambayo ipo kisheria na iliteuliwa Septemba 2013, kinyume na
madai ya mwandishi kuwa Kamati hiyo haipo. Baada ya tathmini ya maombi hayo,
Kamati hiyo ilimshauri Waziri kwa mujibu wa sheria.
Kwa
kufuata utaratibu ulioanishwa katika Kifungu cha 38 (8) na (9) cha Sheria ya
Kuhifadhi Wanyamapori, kifungu hiki kinampa Mamlaka Waziri kuongeza muda wa
umiliki wa vitalu (Renew of hunting blocks). Kanuni ya 16 kanuni ndogo ya (1),
(2), (3), (4), (5), (7), (8), (9) na (10) ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii zinatoa utaratibu wa kufuatwa wakati wa
kuongeza muda wa umiliki wa vitalu kwa muhula mwingine wa uwindaji na utaratibu
huo umefuatwa.
Kwa
kuzingatia utaratibu huo, wamiliki wa sasa wa vitalu kama Kanuni
zinavyoelekeza, waliwasilisha maombi yao Wizarani. Idara ya Wanyamapori
ilipitia maombi hayo na kuwasilisha kwenye Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa
Vitalu vya Uwindaji. Kamati hiyo ilipitia maombi hayo tarehe 26 hadi 27 Julai
2016 na tarehe 13 Januari 2017. Hivyo, baada ya Kamati kukamilisha taratibu
zote na kujiridhisha iliwasilisha ushauri wake kwa Mhe. Waziri.
Kifungu cha 38 (6) cha
Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori alichokitaja mwandishi wa gazeti hilo,
kinaeleza utaratibu wa ugawaji wa vitalu kwa waombaji wapya na siyo kwa wale
wanaoomba kuendelea na umiliki wa vitalu kwa msimu mwingine (renewal).
Uongezaji wa muda wa
umiliki wa vitalu vya uwindaji ulifuata Sheria, Kanuni na Taratibu, Hivyo
tunawoamba wananchi wapuuze habari hiyo kwani mwandishi alikusudia kuupotosha
umma kwa kunukuu na kutafsiri vifungu vya Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori
isivyo sahihi.
Imetolewa na,
KATIBU MKUU
29
Januari, 2017
Waandishi wa namna hii wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria. Tutaendelea kuchapa kazi.
ReplyDeleteHapa kazi tu