Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akihutubia kikao cha mafunzo ya siku tano kwa watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na wakuu wa mapori ya akiba kilichofanyika Morogoro hivi karibuni.
Picha ya pamoja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (Kushoto) akiteta jambo na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Biswalo Mganga (wa pili kushoto) mara baada ya kufungua mkutano wa siku tano wa watendaji wakuu wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na wakuu wa mapori ya akiba kilichofanyika Morogoro hivi karibuni. Kulia ni Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki.
..........................................................
WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesema vitendo vya ujangili nchini vimepungua kwa mwaka uliopita ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Hali hiyo imetokana na kuwapo kwa ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama, mamlaka husika na wananchi katika kutoa taarifa na kufanikisha kukamatwa wahalifu wa ujangili wa tembo.
Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gaudence Milanzi hivi karibuni mjini Morogoro, alipotoa hotuba yake ya kufungua kikao cha mafunzo ya siku tano kwa watendaji wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na wakuu wa mapori ya akiba.
Alisema, ujangili umepungua na ukamataji wa meno ya tembo unaofanyika kwa hivi sasa unatokana na ujangili wa zamani ambayo baadhi ya wahalifu huo walikuwa wameyahifadhi kwa ajili ya usafirishaji kwenda katika masoko.
“Watu watasema, mbona ukamataji wa meno ya tembo unaendelea endapo ujangili umepungua? Meno haya ni yaliyokuwa yamehifadhiwa kwa kitambo na yanakuwa katika njia ya usafirishaji kwenda nje ya nchi na si meno mapya ya tembo,” alifafanua Milanzi.
Hata hivyo, alisema licha ya kupungua kwa ujangili tofauti na miaka ya nyuma, lakini bado unaendelea kufanyika kwa kiwango kidogo na kutokana na hali hiyo juhudi za pamoja zinahitajika katika suala la ukamataji na udhibiti kwenye maeneo ya hifadhi za taifa.
Alisema, “kazi ya sasa kwa mamlaka kwa kushirikiana na nyingine ni kazi ya kuhakikisha majangili hawawezi tena kuingia ndani ya mapori ya hifadhi kwa ajili ya kuua wanyamapori hasa tembo. Na hii itasaidia kukomesha biashara hii haramu,” alisema Milanzi.
Katibu Mkuu huyo aliwataka watendaji wa mamlaka hiyo na nyingine zinazosimamia rasilimali za hifadhi za wanyamapori kuongeza nguvu katika vita dhidi ya ujangili kwani mafanikio ya serikali yameanza kuonekana katika suala zima la mapambano ya vita vya ujangili.
Katika hatua nyingine ameipongeza Serikali ya China kwa kufunga biashara ya meno ya tembo nchini humo na kusema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza na kumaliza kabisa vitendo vya ujangili nchini.
Kwa upande wake Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Biswalo Mganga amesema watuhmiwa 200 walikamatwa katika kipindi cha mwaka jana kutokana makosa ya kukutwa na nyara mbali mbali za Serikali na kushtakiwa.
Alisema zaidi ya shilingi milioni 800 hadi 900 zilipatikana kutokana na faini walizotozwa na walioshindwa kulipa faini walifungwa kifungo cha miaka 20 hadi 25. "Endapo wote wangefanikiwa kulipa faini kiasi cha shilingi bililioni 164 zingekusanywa" .
Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Hamis Semfuko, kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu alisema kuwa ujangili, uharibifu wa mazingira na uvamizi wa mifugo na kujenga makazi ndani ya mapori ya hifadhi ya akiba ni mkubwa na mifugo mingi inatoka nje ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment