slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Thursday, January 5, 2017

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAOKOA WAFUGAJI 50 WALIOKUWA WAKIPITISHA MIFUGO YAO NDANI YA PORI LA AKIBA LA SELOUS

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence  Milanzi (katikati) akipata taarifa kutoka kwa  Meneja wa Pori la Akiba la Selous,  Enock Msocha (wa tatu kushoto)  mara baada ya  kuwasili kwa ajili ya kuwatembelea  Wafugaji 50 waliokolewa na Askari wanyamapori baada ya kutelekezwa  na mtu mmoja waliyemtaja kwa  jina la Mzigua. ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)
lus1
  Baadhi wa Wafugaji wakiwa wanakunywa maji na juisi walizopelekewa kama msaada baada ya kuokolewa na Askari wanyamapori wa Pori la Akiba la Selous,  Kanda ya Kaskazini Mashariki  Kingupira  baada ya kutelekezwa kwa muda wa  siku tano na mtu mmoja waliyemtaja kwa  jina maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya Pori hilo ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii) 

NA LUSUNGU HELELA - WMU
.................................................................
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Askari wa Wanyamapori wa Pori la Akiba la Selous, Kanda ya Kaskazini Mashariki  Kingupira imewaokoa wafugaji 50 waliokuwa wakiwapitisha jumla ya ng’ombe 1780, kondoo  200 na punda 6  baada ya kutelekezwa kwa muda wa  siku tano na mtu mmoja aliyetajwa kwa  jina  la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya Pori hilo wao bila kujua na kuamua kuwakimbia.
Bw. Lisasi Cherehani ambaye ni mmoja wa wafugaji hao alisema ‘’tulimpa Mzigua kiasi cha zaidi ya shilingi 5,000,000 kutoka kwa wafugaji  kama malipo ya kutufikisha eneo la Ilonga mkoani Morogoro tukitokea vijiji vya Ndundunyekanza, Kipungila  na Chumbi vilivyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani kwa makubaliano  kuwa  atatupitisha  njia fupi ya mkato tutakayotembea kwa muda wa siku tano tu, hatukujua anatutupitisha ndani ya pori hili. ‘’
Baada ya kutelekezwa,  wafugaji hao ambao walikuwa katika hali mbaya waliomba msaada kwa ndugu zao  ambao waliwasiliana na Uongozi wa Pori la Akiba la Selous ambao kwa haraka walifanya jitihada za kuokoa maisha yao  ikiwa ni kuwapa huduma ya kwanza,  maji, uji pamoja na kuwakimbiza hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence  Milanzi aliwatembelea wafugaji hao jana kwa ajili ya  kuwapa pole na kuwapelekea  chakula yakiwemo maji pamoja na  unga.
Aidha, Milanzi  aliagiza Wafugaji hao  waachiwe huku akitoa wito kwa wananchi kuacha kupita maeneo ya Hifadhi kwa vile ni kosa kisheria na wale wote watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria na kuahidi kuwa mtu huyo aliyewa danganya kwa  kuwapitisha ndani ya Hifadhi hiyo ni lazima akamatwe kwa udi na uvumba.
‘’Sisi kama Serikali kitu cha kwanza ni ubinadamu tumewahudumia  na  hivyo natoa tamko la kuwaachia wafugaji wote waliopotea ndani ya Pori hili kwa vile mateso  waliyoyapata na mali waliyoipoteza ni kubwa sana  baada ya kudanganywa kwa na kupitishwa ndani ya Pori la Akiba la Selous.’’ Alisema Milanzi
Mmoja wa  wafugaji aliyekuwa katika msafara huo na aliyekuwa akiwasiliana kwa njia ya simu  , Bw. Lisesi Cherehani akielezea namna walivyotelekezwa  katika pori hilo,  alisema kuwa walianza safari hiyo  siku ya jumatano ambapo walikuwa wakitembea usiku na mchana  kwa muda w siku tano bila kujua wanapitishwa ndani ya Hifadhi hiyo ndipo wakaanza kushikwa na kiu kwa vile maji waliyokuwa nayo yaliwaishia na kila walipokuwa wakijaribu kumuuliza aliyewapitisha njia hiyo alikuwa akiwambia baada muda mfupi watakutana na maji hata hivyo waliendelea na safari bila mafanikio ndipo walipoanza kuanguka na baadhi ya wafugaji walianza kunywa mikojo yao pamoja na damu za kondoo kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Aliongeza kuwa, wasingekuwa Askari wanyamapori ambao walikuja kuwapa msaada wa kibinadamu kwa kuwapatia maji pamoja na kuwanyesha uji wangeweza kufa wote.‘’Nawashukuru sana askari wanyamapori kwa kutuhudumia bila wao leo hii msingemkuta mtu yeyote hapa tungekuwa tayari tumeshakufa.’’ Alisema Bw. Cherehani.
Mfugaji mwingine, Mbaga Mahila aliwashukuru sana Askari wanyampori  kwa utu waliouonesha tokea mwanzo walipowaokoa hadi hapo walipofikia na kuitaka jamii ibadilishe mtazamo wa kuwaona askari wanyamapori kama watu katili jambo ambalo halina ukweli wowote.
Pia, Masanje Hambe aliiomba Serikali iwasamehe kwa kuwa wametambaua  kosa la kuingia ndani ya Pori la Akiba la Selous kinyume cha sheria lakini hata hivyo hawakujua kuwa wanapitishwa ndani ya hifadhi hiyo.
Awali,  Mkuu wa Kanda ya Mashariki Kingupira, Bw. Paschal Mrina alisema wamepata  taarifa za wafugaji hao kutoka kwa Wasamaria wema na Uongozi wa wilaya ya Rufiji kuwa  kuna wafugaji  wamepotelea ndani ya hifadhi hiyo  na kwa bahati nzuri kulikuwa na mfugaji mmoja aliyekuwa na simu ndipo wakaanza kuwasiliana naye na kuunda kikosi maalum cha doria kwa ajili ya kuwaokoa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kanda hiyo alisema  wamefanikiwa kuwaokoa wafugaji wote na  ilionekana mizoga saba na wengine ambao hawakuonekana taratibu za kuanza kutafuta zimeandaliwa  
Alielezea njia walizotumia kuokoa wafugaji hao ni kuwa waliunda vikosi vitatu vya doria ambapo kikosi cha kwanza kilifanya doria kwa njia za miguu, kikosi cha pili kilfanya doria kwa njia za magari na kikosi cha tatu kilifanya doria  kwa kutumia ndege kwa ajili ya kubaini walipo.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafugaji, Bw. Magembe Makoye alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuacha kuwafukuza wafugaji katika maeneo waliyopo badala yake  wawatafutie maeneo mbadala ili kuthibiti matukio kama hayo ambayo yamepelekea hasara na mateso makubwa kwa wafugaji.
Pori la Akiba la Selous lina ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 na limegawanywa katika kanda nane huku Kanda ya Mashariki  Kipungira ikiwa moja kati  ya kanda kubwa yenye kilomita za mraba 7,650, Shughuli zinazofanyika  katika Pori hilo ni Utalii wa picha na pamoja na uwindaji

No comments:

Post a Comment