Sunday, May 21, 2017

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YATOA SEMINA KWA WABUNGE JUU YA UMUHIMU WA UHIFADHI WA MALIASILI, MALIKALE NA MAENDELEO YA UTALII NCHINI

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta  Ndetiye (kushoto) akizungumza wakati wa semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kufanyika katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana. Kulia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Prof. Jumanne Maghembe. Semina hiyo ilihusu umuhimu wa uhifadhi wa Maliasili Malikale na Maendeleo ya Utalii nchini.
Baadhi ya viongozi na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakiwa ndani ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania muda mfupi kabla ya kuanza kuwasilishwa kwa mada mbalimbali katika semina hiyo. Mada zilizowasilishwa katika semina hiyo ni Kwanini Watanzania tuhifadhi uoto wa asili na Wanyamapori, Athari za Muingiliano wa Mifugo na Wanyamapori, Maendeleo ya Utalii na umuhimu wake katika uchumi wa Tanzania na Umuhimu wa Uhifadhi wa Misitu Nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jeneral Gaudence Milanzi akizungumza katika semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara kwa ajili ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkurugenzi wa Idara wa Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexander Songorwa askiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa Watanzania kuhifadhi uoto wa asili na Wanyamapori katika semina hiyo. Kushoto waliokaa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na baadhi ya viongozi na wakurugenzi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Prof. Songorwa akiwasilisha mada hiyo. 
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Dkt. Robert Fyumagwa akiwasilisha mada juu ya Athari za Muingiliano wa Mifugo na Wanyamapori katika semina hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo akiwasilisha mada juu ya Umuhimu wa Uhifadhi wa Misitu Nchini. Alieleza kuwa umuhimu wa misitu ni sawa na hewa safi ambayo inatoa uhai kwa mwanadamu na endapo misitu hiyo itatoweka kutokana na uharibifu unaoendelea basi maisha ya binadamu nayo yatakuwa hatarini kwa kuwa hewa hiyo chanzo chake ni misitu na mimea.
Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania, Richard Rugimbana akiwasilisha mada kuhusu Maendeleo ya Utalii na umuhimu wake katika uchumi wa Tanzania kwa wabunge hao.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta  Ndetiye (kushoto) wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika semina hiyo.
Aliyekuwa MC wakati wa semina hiyo, Meneja wa Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Paschal Shelutete akiteta jambo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Kabwa muda mfupi baada ya kuhitimishwa semina hiyo.
 Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Maliasili walioshiriki semina hiyo bungeni mjini Dodoma.
Bungeni wakati wa semina hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto), Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya (wa pili kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Alexander Songorwa na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Wizara ya Maliasili, Dkt. Ezeckiel Mwakalukwa wakitoka katika ukumbi wa bunge mara baada ya semina hiyo.

Tuesday, May 9, 2017

BREAKING NEWS: TEMBO WANNE WAONEKANA CHUO KIKUU CHA DODOMA (UDOM) LEO, ASKARI WA WANYAMAPORI WAANZA KAZI KUWARUDISHA HIFADHINI

Tembo wakiwa wamejificha kwenye vichaka ndani ya eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) leo. Kwa mujibu wa taarifa za Wahifadhi wa Wanyamapori inaelezwa kuwa sehemu ya eneo hilo litakuwa ni njia ya tembo (maeneo ya mapito ya wanyamapori) ambayo ilipitika kwa miaka mingi iliyopita na kwamba tembo wana kumbukumbu hata kama walipita njia hiyo kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Imeelezwa kuwa njia hiyo ya mapito ya wanyamapori itakua ilitumiwa na wanyamapori kuhama eneo moja hadi jengine ikiwemo maeneo ya hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Ruaha, Serengeti, Pori Tengefu la Rugwa na maeneo mengine ya hifadhi na kwamba maeneo hayo mengi kwa miaka ya hivi karibuni yameshaingiliwa na shughuli za kibinadamu ambazo hazisababishi tembo hao kusahau njia hizo au kutokuzitumia tena.
Tembo hao wakiwa ndani ya eneo chuo kikuu hicho cha Dodoma leo. Hakuna madhara yeyote yaliyoripotiwa kusababishwa na tembo hao na taratibu za kuwarudisha kwenye maeneo yao ya hifadhi zimeshaanza kuchukuliwa na uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo Askari wa Wanyamapori wameanza zoezi la kuwafukuza kuwarudisha kwenye maeneo yao ya hifadhi.
Prof. Julius Nyahongo wa Chuo Kikuu cha Dodoma akitoa somo kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma namna ya kuchukua tahadhari juu ya ugeni wa tembo hao chuoni hapo. Aliwaeleza wanafunzi hao kuwa mazingira ya chuoni hapo yataendelea kuwa salama kwakuwa tembo hao wapo katika njia yao ya mapito na pengine kumewahi kukucha kabla ya wao kufika mwisho wa safari yao, hivyo kwa msaada wa askari wa wanyamapori ambao wamewasili chuoni hapo itasaidia  kuwaondoa tembo hao waweze kuendelea na safari yao hadi kwenye maeneo ya hifadhi.
Wanafunzi mbalimbali wa Chuo Kikuu cha Dodoma walikusanyika wakiwa na shauku ya kuwaona tembo hao.
Msafara wa viongozi mbali mbali wa Serikali ukiambatana na Askari Polisi na Askari wa Wanyamapori ukisogelea eneo walilokuwepo tembo hao kwa ajili ya kuanza kuwafukuza kutoka katika maeneo hayo ya chuo kwenda kwenye maeneo yao ya hifadhi.
Prof. Julius Nyahongo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (wa pili kulia), Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Paschal Shelutete (wa tatu kulia) na maafisa wengine wa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama wakiangalia eneo walilokuwa wamejificha tembo hao chuoni hapo.
Askari wa wanyamapori wakiingia ndani ya eneo walilokuwa wamejificha tembo hao kwa ajili ya kuanza kuwafukuza eneo hilo kuelekea kwenye maeneo yao ya hifadhi. Imeelezwa kuwa pindi tembo hao watakapofukuzwa kwa milio maalum ya risasi hutafuta njia wanazozijua wenyewe za kurudi kwenye maeneo yao ya hifadhi.
Tembo hao wakianza kuondoka katika eneo hilo baada ya askari wa wanyamapori kuanza kuwaondoa eneo hilo kwa kutumia milio maalum ya risasi.

Saturday, May 6, 2017

WANAHABARI WA ISRAEL WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA GOMBE, WAAHIDI KUTANGAZA VIVUTIO VYA TANZANIA NCHINI HUMO


Kundi la waandishi wa habari kumi kutoka nchini Israel wakiwa katika hifadhi ya Taifa ya Gombe kwa ajili ya kurekodi vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana katika hifadhi hiyo kwa ajili ya kuvitangaza nchini kwao ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na Hifadhi za Taifa (TANAPA). Kwa sasa soko la utalii la mashariki ya kati limeanza kufunguka kwa kasi ambapo hivi karibuni Waziri Mkuu Mstaafu wa Israel Ehud Barak ametembelea hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.

HAMZA TEMBA - WMU
.......................................................................

Kundi la wanahabari kumi akiwemo muigizaji mmoja na maofisa wa kampuni ya utalii ya Safari kutoka nchini Israel limetembelea hifadhi ya Taifa ya Gombe iliyopo mkoani Kigoma na kufurahia vivutio lukuki vya utalii vinavyopatikana katika hifadhi hiyo na kuahidi kuvitangaza watakaporudi nchini kwao ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TANAPA na Bodi ya Utalii kutangaza vivutio hivyo nchini humo.

Akizungumza hivi karibuni mara baada ya kukamilika kwa ziara hiyo ya siku mbili, Kiongozi wa kundi hilo, Ronit Hershkovitz alisema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa ambapo wamefurahia kuona vivutio vya kipekee katika hifadhi hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa vivutio hivyo nchini Israel. 

“Ni furaha kubwa kuwa hapa Gombe, tumeona makundi ya Sokwe na fukwe nzuri za Ziwa Tanganyika, tuko hapa kwa ajili ya kwenda kueleza kivutio hiki na vivutio vingine vya Tanzania nchini Israel, Waisrael wanaipenda Tanzania na wanapenda kutembelea Tanzania, tumeona ongezeko kubwa la watalii katika miaka ya hivi karibuni kutoka Israel baada ya kazi ngumu ya muda mrefu, sasa tuna furaha kuona watalii wengi wanaongezeka na tungependa kuona pia Watanzania wengi wakitembelea Israel,” Alisema Ronit.

Aliongeza kuwa, “Tunaenda kueleza taarifa hizi kwenye mitandao ya kijamii, magazeti, televisheni na popote tutakapoweza, lakini kubwa zaidi ni kuwaeleza marafiki zetu ana kwa ana uzuri wa Tanzania kwasababu tunaipenda Tanzania, nakupenda sana”.

Walfson Noa, ambaye ni Mwandishi wa Mitandao ya Kijamii na Meneja Masoko wa Kampuni ya Utalii ya Safari ya Israel alisema, “Tulifanya matembezi kuwaona Sokwe wanaovutia sana huku wakiishi katika mazingira yao ya asili, hili ziwa ni la maajabu sana (Ziwa Tanganyika), hata nyani nao walikuwa wakijaribu kuingia kwenye mahema yetu ni jambo la kuvutia, katika mtizamo wa kimasoko hili ni eneo ambalo nitawashauri wateja wangu watembelee, ni kitu ambacho watu wanatakiwa kukifahamu, kugundua siri ya uzuri wa hifadhi ya Taifa ya Gombe” 

Kwa upande wake Meneja wa Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Paschal Shelutete ambaye alikuwa kiongozi wa msafara huo akishirikiana na Meneja Mawasiliano TTB, Geofrey Tengeneza, Meneja Mawasiliano wa TFS, Glory Mziray na Afisa Mawasiliano wa Wizara ya Maliasili, Hamza Temba alisema ujio wa wanahabari hao utaleta chachu ya kuongezeka kwa watalii wengi kutoka Israel pamoja na kupanua soko la utalii kwa hifadhi za mikoa ya magharibi mwa Tanzania ikiwemo hifadhi ya Gombe.

“Tumekuja na kundi hili la wanahabari ambao wameamua kama mlivowasikia kwa dhati kabisa kwamba watakaporudi nyumbani watatumia mitandao ya kijamii, radio mbalimbali, Televisheni lakini kubwa zaidi magazeti, wataandaa makala na vipindi mbalimbali hivyo tunaamini kwa dhati kabisa watakaporudi nyumbani na kuzifanyia kazi taarifa zote walizozipata katika hifadhi ya Taifa ya Gombe ama kwa hakika tutashuhudia ongezeko kubwa la watalii kutoka nchini Israel katika siku chache zijazo,” Alisema Shelutete.

Aliongeza kuwa, “Ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha rasilimali hizi za hifadhi zinazopatikana katika hifadhi za taifa zinaendelea kutunzwa kwa ajili ya kizazi hiki na vizazi vijavyo, watalii hawaji kuangalia ng’ombe kwenye hifadhi zetu, nasisitiza kuwa mifugo haikubaliki kwenye hifadhi zetu”.

Msafara huo ulikuwa na wanahabari kutoka vyombo maarufu nchini humo ikiwemo kituo cha Televisheni cha Channel 2, Jarida la Atmosphere, Jarida la National Geographic, Jaria la wiki la Yediot Acharanot -7 Yamim na waandishi wawili wa mitandao ya kijamii. Wengine ni maofisa wawili wa kampuni ya Utalii ya Safari ya nchini humo.

Hifadhi ya Taifa ya Gombe ilianzishwa mwaka 1968 kwa ajili ya tafiti za kisayansi, hususani katika kuwalinda na kuwahifadhi wanyamapori adimu wa jamii ya Sokwe Mtu (chimpanzees) ambao wapo hatarini kutoweka. Hifadhi hii inaelezwa kuwa na Sokwe wasiopungua mia moja ambao huishi kwa makundi na kuwa kivutio kikubwa na adimu katika hifadhi hiyo ambayo ina ukubwa wa kilomita za mraba 52.
Timu maalum ya wanahabari kutoka nchini Israel ikiwa na wajumbe kumi ilipowasili katika uwanja wa ndege wa Kigoma tayari kwa ajili ya ziara ya kitalii ya siku mbili katika hifadhi ya Taifa ya Gombe. Ziaza hiyo iliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa kushirikiana na Shirika ya Hifadhi za Taifa Tanzani (TANAPA) kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Israel ikiwa ni mkakati maamlum wa kukamata soko la Mashariki ya Kati. Kutoka kulia wanaongoza msafara huo ni Meneja Mawasiliano TANAPA, Paschal Shelutete na Meneja Mahusiano wa TTB, Geofrey Tengeneza.
Wanahabari kutoka Israel wakipanda kwenye boti kwa ajili kunza safari kuelekea hifadhi ya Taifa ya Gombe. Msafara huo ulikuwa na wanahabari kutoka vyombo maarufu nchini humo ikiwemo kituo cha Televisheni cha Channel 2, Jarida la Atmosphere, Jarida la National Geographic, Jaria la wiki la Yediot Acharanot -7 Yamim na waandishi wawili wa mitandao ya kijamii. Wengine ni maofisa wawili wa kampuni ya Utalii ya Safari  ya nchini humo.
Msafara wa Wanahabari wa Israel wakiwa kwenye boti tayari kwa safari ya kuelekea hifadhi ya Taifa ya Gombe ambapo kutoka Kigoma mjini hadi kwenye hifadhi hiyo ni mwendo wa saa moja na nusu hadi masaa mawili.
Mhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Gombe, Elihuruma Wilson (kushoto) akitoa maelezo mafupi kwa wanahabari kutoka nchini Israel kuhusu hifadhi hiyo kabla ya kuanza ziara ya kutembelea vivutio vilivyopo. Alieleza kuwa hifadhi hiyo ina vivutio vingi wakiwemo  Sokwe zaidi 100, Nyani, Kima, maporomoko ya maji, ndege aina mbalimbali na fukwe nzuri za kuogelea za ziwa Tanganyika. 
Meneja Mawasiliano wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete (kulia), Meneja Mahusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (Geofrey Tengeneza) na Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Glory Mziray) wakiongoza msafara wa wanahabari wa Israel kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Timu ya wanahabari wa Israel wakianza safari ya kuingia ndani ya msitu wa hifadhi ya Taifa ya Gombe kwa ajili ya kuona makundi mbalimbali ya Sokwe. Lengo kuu la ziara hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii na TANAPA ni kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Israel.
Wanahabari kutoka Israel wakipata maelezo kutoka kwa mhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Gombe kuhusu utarartibu wa kuzingatia wawapo ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo kutokupiga kelele na kuepuka matumizi ya mwanga wa kamera (Flash Lights).
Mmoja ya wanahabari wa Israel, Gerald Eddie wa Jarida la National Geographic akiwa katika harakati za kupata taswira mwanana ya picha za Sokwe ndani hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Wanahabari wa Israel wakiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Sokwe akirukia matawi ya miti akiwa na mtoto wake ndani ya hifadhi ya Taifa ya Gombe wakati wa ziara ya wanahabari wa Israel kwenye hifadhi hiyo.
Taswira mwanana ya Sokwe Mtu ndani ya hifadhi ya Taifa ya Gombe wakati wa ziara hiyo.
Mtoto wa Sokwe akila matunda yanayopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Gombe wakati wa ziara ya wanahabari wa Israel katika hifadhi hiyo. Lengo kuu la ziara hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii na TANAPA ni kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania nchini Israel.
Sokwe akiwa kapumzika kwenye maeneo yake ya kujidai ndani ya hifadhi ya Taifa ya Gombe wakati wa zaira ya wanahabari wa Israel katika hifadhi hiyo. Wanahabari hao walifurahia kuwaona sokwe hao wanaoelezewa na wanasayansi kuwa wanakaribiana na binaadamu kwa takribani asilimia 80.
Meneja Mawasiliano wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete (wa pili kulia) akionesha kifaa maalum cha kupigia picha za angani (drone) kilichorushwa na mmoja wa mwanahabari ambaye ni mpigapicha kutoka Israel katika fukwe za Ziwa Tanganyika pembezoni mwa hifadhi ya Taifa ya Gombe wakati wa zaiara ya wanahabari hao hifadhini hapo.   
Kifaa hicho maalum cha kupiga picha za angani kijulikancho kama 'drone' kikiwa angani kupata taswira pana ya hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Wanahabari hao wakipiga picha za mwanahabari mwenzao na nyani wanaopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Gombe katika fukwe za Ziwa Tanganyika.
Mwanahabari maarufu nchini Israel, Dana Spector, wa Jarida la Yediot  Acharonot (kushoto) akiigiliza mkao wa nyani katika hifadhi ya Taifa ya Gombe wakati wa ziara hiyo. Matukio hayo yataonekana katika jarida hilo nchini Israel kwa ajili kutangaza vivutio vya Tanzania. Anayepiga picha ni Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa, Paschal Shelutete.
Mpiga picha wa Jarida la National Geographic la nchini Israel, Gerald Eddie akipiga picha nyani wanaopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Gombe ambao pia ni kivutio cha utalii katika hifadhi hiyo kwa ajili ya kuvitangaza katika jarida hilo.
Nyani akiwa kambeba mtoto wake katika  hifadhi ya Taifa ya Gombe tukio ambalo pia sehemu ya vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hiyo.
Wanahabari hao hawakutaka kupitwa na tukio lolote katika ziara yao hiyo, hapo wakipiga picha boti ambayo hufanya safari za kawaida kwa wananchi wa vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika na Manispaa ya Kigoma.
Mwanahabari maarufu nchini Israel, Dana Spector, wa Jarida la Yediot  Acharonot (wa pili kushoto) na Mtangazaji maarufu wa Radio na Televisheni nchini humo, Ran Sarig wakiigiliza mkao wa nyani dume na jike katika fukwe za ziwa Tanganyika kwenye hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Mwanahabari maarufu nchini Israel, Dana Spector, wa Jarida la Yediot  Acharonot (wa pili kushoto) na Mtangazaji maarufu wa Radio na Televisheni nchini humo, Ran Sarig wakifurahia matukio mbali mbali yaliyokuwa yakifanywa na nyani wa hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Wanahabari hao pia walipata fursa ya kuogolea katika fukwe za kitalii za ziwa Tanganyika pembezoni mwa Hifadhi hiyo ya Taifa ya Gombe, Fukwe hiyo ni kivutio kikubwa cha utalii katika hifadhi ya Taifa ya Gombe. 
Wanahabari hao wakiwa wanaogelea katika fukwe za kuvutia za ziwa Tanganyika kwenye hifadhi ya Taifa ya Gombe huku wakipiga picha za tukio hilo kwa ajili kutangaza kivutio hicho nchini Israel.
Wanahabari hao pia walipata fursa kutembelea jamii ya kijiji cha Mwamgongo ambacho kinapakana na hifadhi ya Taifa ya Gombe, hapo wakimpiga picha mtoto aliyekuwa na mpira wa makaratasi ambao ni sehemu ya utalii wa kiutamaduni.
Mwandishi wa habari kutoka Israel ambaye ni mpiga picha wa kituo cha Televisheni cha Chanel 2, Roni Dahabari Kuban akiwapiga picha watoto katika kijiji cha Mwamgongo jirani na hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Mtangazaji maarufu wa Radio na Televisheni nchini Israel, Ran Sarig akifungwa shuka aliyoinunua na wananchi wa Kigoma katika ziara hiyo. Shuka hizo zinazofumwa kwa mikono ni maarufu Mkoani Kigoma na sehemu ya utalii wa Kiutamaduni unaopatikana katika Mkoa huo. 
Mtangazaji maarufu wa Radio na Televisheni nchini Israel, Ran Sarig akipiga picha ya "Selfie" na baadhi ya watoto wa kijiji cha Mwamgongo kilichopo jirani na hifadhi ya Taifa ya Gombe wakati wa ziara hiyo.
Wanahabari hao walipotembelea kijiji cha Mwamgongo kilichopo jirani na hifadhi hiyo ya Taifa ya Gombe walipata kujionea na kushiriki katika ngoma za asili ambazo pia ni sehemu ya utalii wa kiutamaduni.
Mwanahabari maarufu nchini Israel, Dana Spector, wa Jarida la Yediot  Acharonot  akijaribu kuwasiliana na wanakikundi cha ngoma za asili wa kijiji cha Mwamgongo kinachopakana na hifadhi ya Taifa ya Gombe na kushudia kazi zao za mikono na ngoma ambazo ni sehemu ya utalii wa kiutamaduni.
Mwandishi wa habari wa mitandao ya kijamii nchini Israel, Walfson Noa akifurahia michezo na jamii ya watoto wa kijiji cha Mwamgongo wakati wa ziara hiyo.
Watalii wa ndani nao pia walikuwemo kufurahia vivutio vya utalii vinavyopatikana katika hifadhi hiyo na kutoa wito kwa watanzania wengi zaidi kuvitembelea. Meneja wa Shirika la Hifadhi za Taifa, Paschal Shelutete (wa pili kushoto waliosimama) akiongoza mahojiano na watalii hao wa ndani.
Picha ya pamoja ya wanahabari wa Israel, wahifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Gombe na waongoza msafara huo ambao ni Meneja Mawasiliano wa TANAPA, Paschal Shelutete (wa pili kulia), Meneja Mahusiano wa TTB, Geofrey Tengeneza (katikati waliosimama), Meneja Mawasiliano TFS, Glory Mziray (wa tatu kulia) na Afisa Mawasiliano wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Hamza Temba (wa nne kulia).
Baada ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Gombe msafara wa wanahabari hao ulipanda boti kwa ajili ya safari ya kurudi Kigoma Mjini.