slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Sunday, May 28, 2017

TANAPA, NGORONGORO, TAWA NA TAWIRI KUUNGANISHWA KUWA TAASISI MOJA - PROF. MAGHEMBE

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijibu hoja mbalimbali wakati akihitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018 bungeni mjini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo makani akijibu hoja mbalimbali wakati wa kuhitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018 bungeni mjini Dodoma.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, Viongozi wakuu na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo wakiwa nje ya lango la Bunge mara baada ya kikao cha Bunge kupitisha bajeti ya Wizara hiyo.

Na Hamza Temba - WMU 
---------------------------------------------------------------------
Serikali inafikiria kuunganisha taasisi zote zinazohusika na sekta ya uhifadhi wa wanyamapori nchini kuwa chombo kimoja chenye nguvu  kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi hizo pamoja na kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika sekta hiyo muhimu hapa nchini.

Akizungumza mwishoni mwa wiki bungeni mjini Dodoma wakati akihitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alisema anaunga mkono ushauri uliotolewa na wabunge mbalimbali ukiwemo wa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Atashasta Nditiye juu ya umuhimu wa kuunganisha taasisi hizo za uhifadhi.

"Wakati umefika sasa, tusiwe na makampuni (taasisi) zaidi ya manne ndani ya sekta hii ya wanyamapori, tuwe na kampuni (taasisi) moja tu ambayo itapunguza gharama katika uendeshaji, tutaunganisha jeshi la wahifadhi na jeshi hilo tutakalolitengeneza ni jeshi moja tu ambalo litakua na malezi chini ya jeshi la wananchi wa Tanzania, ili kujenga nidhamu, kuheshimu haki za binadamu na kufanya kazi kwa mujibu wa maslahi ya taifa,". alisema Maghembe. 

Aliongeza kusema "Jeshi hilo ambalo tunaliandaa kisasa, jeshi usu litakua na "chain ya comand" moja na litawajibika kijeshi kwa makosa ya haki za kibinadamu na usaliti wa taifa au usaliti wa uchumi wa nchi yetu".

Awali akiwasilisha bungeni hapo hotuba ya makadidirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake, Prof. Maghembe alizitaja taasisi hizo kuwa ni Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na  Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).  

Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura 282 na kupewa dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yaliyoanzishwa kisheria kuwa Hifadhi za Taifa. Hifadhi hizo ambazo zipo 16 zina jumla ya kilometa za mraba 57,365.80. 

Kwa upande wake, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) ilianzishwa kwa Sheria Sura 284 na kupewa jukumu la kusimamia eneo la kilometa za mraba 8,292 kwa ajili ya kuhifadhi, kuendeleza utalii na wafugaji wenyeji wa eneo hilo ambapo wakati mamlaka ikianzishwa walikua takriban 8,000 mwaka 1959 na idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia zaidi ya wakazi 90,000 mwaka uliopita, 2016. 

Nayo, Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na.135 la tarehe 9 Mei, 2014 chini ya Kifungu cha 8 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Sura 283 ikisomwa pamoja na marekebisho yake yaliyotolewa katika Tangazo la Serikali Na.20 la tarehe 23 Januari 2015. Mamlaka hiyo ilianza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2016. 

Mamlaka hiyo ina jukumu la kusimamia uhifadhi wa wanyamapori kwenye Mapori ya Akiba 28, Mapori Tengefu 42  na maeneo ya wazi yenye mazalia ya wanyamapori, mtawanyiko na shoroba. Aidha, Mamlaka inashirikiana na jamii katika kusimamia maeneo 22 ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori na maeneo manne ya ardhioevu yenye umuhimu wa kimataifa (Ramsar Sites).

Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ilianzishwa kwa Sheria Sura 260 kwa lengo la kusimamia, kufanya na kuratibu utafiti wa wanyamapori nchini. Taasisi hiyo ina wajibu wa kutoa ushauri kuhusu uhifadhi endelevu wa wanyamapori kwa kutumia matokeo ya utafiti wa kisayansi. Aidha, TAWIRI inawajibu wa kufanya Sensa ya makundi mbalimbali ya Wanyamapori ili kushauri Wahifadhi na Serikali.

Akizungumzia umuhimu wa uhifadhi wa Wanyamapori, Prof. Maghembe alisema sekta ya maliasili kwa ujumla inachangia asilimia 21.4 ya pato lote la taifa, ambapo mchango wa wanyamapori kupitia utalii ni asilimia 17.5 na misitu asilimia 3.9. Aliongeza kuwa wanyamapori pia husaidia katika tafiti mbalimbali duniani kwa ajili ya utafutaji wa dawa za kutibu maradhi ya binadamu.

Katika mwaka huu wa fedha 2017/2018, Bunge limeidhinisha Sh. bilioni 148.597 kwa ajili ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo Sh. bilioni 96.794 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh. bilioni 51.803 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 

1 comment:

  1. Hizo bilioni 148 zilizoidhinishwa ni bajeti ya Wizara nzima pamoja na taasisi zake? Yaani Tanapa, Tawa, NCAA, na TFS?

    ReplyDelete