slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Friday, December 30, 2016

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, MHANDISI RAMO MAKANI ATOA UFAFANUZI WA UTOAJI WA TAARIFA ZA FARU JOHN, AUNDA KAMATI YA KUSULUHISHA MGOGORO WA MUDA MREFU WA PORI TENGEFU LA LOLIONDO

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akizungumza katika kikao cha wadau wanaohusika na mgogoro wa pori tengefu la Loliondo alichokiitisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa ya Loliondo wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha jana. Kupitia kikao hicho aliunda kamati maalum ya kutatua mgogoro wa muda mrefu wa pori tengefu la Loliondo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mfaume Taka.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akizungumza katika kikao hicho.
Baadhi ya wadau wanaohusika na mgogoro wa pori tengefu la Loliondo wakiwa kwenye mkutano huo.

NA HAMZA TEMBA - WMU
.......................................................................

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani amesema hakuna mamlaka nyingine ya Serikali chini ya ofisi ya waziri mkuu yenye mamlaka ya kutoa tamko au ufafanuzi kuhusiana na Faru John kwa sasa kwakua jambo hilo bado lipo kwenye uchunguzi.

Amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku mbili wialayani humo kwa ajili ya kufuatilia changamoto za uhifadhi pamoja na utekelezaji wa maagizo wa Waziri Mkuu aliyoyatoa hivi karibuni akiwa ziarani mkoani Arusha.

Amesema miongoni mwa maagizo aliyoyatoa Waziri Mkuu katika ziara hiyo ni kuwasilishwa kwa taarifa ya inayoelezea utaratibu uliotumika kumuhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti pamoja na kuwasilishwa kwa pembe zake ambapo baadae aliunda tume ya kuthibitisha ukweli wa taarifa hiyo.
.
"Ripoti hii ya uchunguzi ni mali ya Waziri Mkuu atakayeweza kutoa ripoti hii nje kwa ajili ya matumizi  ya kila mmoja wetu ni Waziri Mkuu, kwa maana ya mamlaka, kwa hiyo hakuna mamlaka nyingine yeyote ya Serikali chini ya Waziri Mkuu yenye uhalali wa kutoa tamko au ufafanuzi wa jambo hili, mpaka pale Waziri Mkuu atakapokamilisha kusoma ripoti kwa kina kwa kutumia wataalam wake, kufanya vipimo kama ambavyo tunasikia amevipeleka kwa mkemia mkuu wa Serikali, pamoja na udadavuzi wa ripoti.

"Kwa kipindi hiki nnapozungumza, zaidi ya kwamba tunasubiri maagizo au maelekezo au muelekeo sasa juu ya jambo hili kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, hakuna jambo jingine ambalo Wizara inaweza kufanya wala kusema kuhusiana na suala la Faru John, hatuna mamlaka hiyo", amesema.

Akizungumzia tukio la hivi karibuni la baadhi ya watumishi wa wizara kuonekana kwenye chombo kimoja cha habari wakitoa ufafanuzi juu ya jambo hilo amesema "Mimi kwa sasa nnachoweza kusema kwa chochote kilichofanyika kama kuna utaratibu umetumika kuwafanya waweze kwenda mbele ya vyombo vya habari, kwenda kutoa taarifa hizo, lakini pia tukijua kabisa kwamba wao sio wasemaji wa wizara na wala kwa level  (hatua) ya jambo lenyewe pale lilipofikia wao hawana mamlaka ya kuweza kutosha kulizungumzia jambo hilo, sasa kwanini limekua hivo jana ni jambo ambalo tunalifanyia kazi, bila shaka walipoitwa pengine hawakuambiwa sawasawa wanaenda kuzungumzia nini",.

"Kama wizara tutachukua sasa muda wa kuweza kuzungumza nao tujue nini kilitokea lakini kimsingi baada ya hiki nnachokisema hapa sasahivi ieleweke hivo na taifa zima kwa ujumla kuwa hakuna tunachoweza kusema sasa hakuna tunachoweza kufanya sasa mpaka uchunguzi unaofanyika chini ya ofisi ya waziri mkuu ukamilike mpaka waziri mkuu asome aridhike na taarifa yetu na aweze kuina taarifa ile inafaa kwa namna gani na kama kuna maagizo mengine atayatoa baada ya hatua hiyo.

Wakati huo huo ametoa wito kwa wananchi kuwa na subira juu ya taarifa sahihi za faru John "Unaweza kusikiliza habari kutoka vyanzo vingi tu, lakini ukishapata habari usiifanyie kazi haraka haraka bila ya kujiridhisha juu ya ubora wa taarifa unayoipata, wawe na subira, wananchi waendelee kusubiri, si waliapata taarifa ya faru John kupitia kwa Waziri Mkuu?, busara ya kawaida inasema kwamba wangesubiri kutoka kwa Waziri Mkuu au mtu atakayekasimiwa madaraka na Waziri Mkuu atasema kitu kingine kinachofuatia baada ya pale na si vinginevyo".

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Makani ameunda kamati maalum ya kuushulikia mgogoro wa muda mrefu katika  pori tengefu la Loliondo baina ya wananchi, wawekezaji na hifadhi hiyo. Hatua hiyo imekuja ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya waziri mkuu ya kuwakutanisha wadau katika eneo hilo kumaliza mgogoro huo.

Kamati hiyo imehusisha taasisi za serikali, asasi za kiraia, viongozi wa dini, wazee wa kimila (Leigwanan), viongozi wa vijiji, wajumbe wa kamati teule za vijiji, wawakilishi wa wanawake na vijana. Ameunda pia kamati ya kuandaa kanuni za kundesha vikao  vya kamati hiyo.

"Kuna watu humu ndani na hata nje ambao hawataki tumalize migogoro Loliondo, nitoe rai kwao, waache chokochoko. Wananchi muone umuhimu wa jitihada za Serikali kumaliza changamoto hii na kutuunga mkono", alisema Makani.

Thursday, December 29, 2016

MHANDISI MAKANI ATOA WIKI MBILI KWA WAFANYAKAZI NGORONGORO KUWASILISHA TAARIFA ZA MIFUGO NA MAJENGO YA KUDUMU WANAYOMILIKI NDANI YA HIFADHI HIYO

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati) akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha jana katika ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu. Kulia ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Freddy Manongi na Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha (kushoto). 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha jana katika ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu,  ametoa wiki mbili kwa watumishi wenye mifugo na majengo ndani ya eneo la mamlaka ya hifadhi hiyo kujiandikisha kwa uongozi wa mamlaka hiyo ikiwa ni mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu. 

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha akichangia katika mkutano huo. Alieleza kuwa salama ya Hifadhi ya Ngorongoro itategemea uwekaji wa mizania sawa baina ya uhifadhi na maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.
 Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Freddy Manongi (katikati) akizungmza katika mkutano huo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexandre Songorwa (kulia).
 Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Mfaume Taka (kushoto) akizungumza kwenye mkutano huo.
 Sehemu ya watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiwa kwenye mkutano huo.

NA HAMZA TEMBA - WMU
....................................................

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani ametoa wiki mbili na siku tano kwa watumishi wote wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wenye mifugo na majengo ya kudumu  ndani ya eneo la hifadhi hiyo kuorodhesha majina yao kwa uongozi wa mamlaka hiyo  na kusalimisha taarifa ya kile wanachokimiliki ndani ya eneo hilo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa utekelezaji maagizo ya Waziri Mkuu  aliyoyatoa kwa uongozi wa mamlaka hiyo.

Ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na Ngorongoro katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa makao makuu ya NCAA yaliyopo katika wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa ajili ya kufuatilia changamoto za uhifadhi na utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoyatoa kwa mamlaka hiyo hivi karibuni akiwa ziarani mkoani Arusha.

Anasema miongoni mwa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu ambayo yameshaanza kufanyiwa kazi ni pamoja na kuondolewa mifugo yote maeneo ya Kreta, kuhakikisha upatikanaji wa maji na chumvi kwa ajili ya mifugo na wananchi, idadi ya mifugo kutambuliwa na kupigwa chapa pamoja na kutambua idadi ya wananchi ndani ya eneo la mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kupewa hati za utambuzi.

“Mpaka ikifika wiki ya pili ya mwezi januari, tarehe 15, kila mtumishi ambaye yeye binafsi ana mifugo ndani ya eneo hili, maana tunaanzia nyumbani, Conservator (Mhifadhi) uweke utaratibu wa kupokea taarifa kutoka kwao, kila mmoja aweze kudeclare (kutangaza) umiliki wake wa mifugo ndani ya eneo la hifadhi, ng’ombe, mbuzi, kondoo.

"Lakini pia kila mtumishi ambaye ana nyumba ya kudumu ndani ya hifadhi, iliyojengwa kwa matofali, mabati, zege nakadhalika atuambie, na mimi nishauri tu kuwa muwazi itakusaidia. Kwasababu haiwezekani sisi tuanze kuwaambia watu wengine, wewe kwanini umejenga nyumba ya kudumu hapa, wakati tunapowaonyesha vidole na wengine sisi tunazo, hatuwezi kwenda kuwaambia wengine, wewe kwanini una mifugo humu 200,000, 2000, 1000 au 500 wakati wengine sisi humu tuna mifugo zaidi yao hata mara mbili", alisisitiza Makani.

Alisema kuwa, kwa wale waajiriwa wapya wapewe elimu juu ya malengo na majukumu mahsusi ya taasisi hiyo pamoja na miiko yake ambayo ni pamoja na uwepo wa maeneo maalum ya uhifadhi yasiyoruhusiwa mifugo na majengo ya kudumu.

Amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kusoma kwa makini madhumuni ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo pamoja na majukumu makhsusi iliyopewa ili kufanya vizuri zaidi katika uhifadhi endelevu wa Hifadhi hiyo huku wakitambua kuwa wao ndio wenye jukumu la kwanza la kuhakikisha kuwa taasisi hiyo inastawi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Makani ametoa muda wa wiki mbili kwa uongozi wa NCAA kumkabidhi taarifa ya mpango mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu. "Zile wiki mbili nilizozisema, ule mpango mkakati wa utekelezaji wa maagizo ya waziri mkuu, sina maana kwamba tutaanza kutekeleza kwenye wiki mbili, hivi tunavyoendelea kutekeleza kwa maana yapo mambo mengine hapa utekelezaji wake ni wa muda zaidi ya hizo wiki mbili, nataka nipate mpango kazi wa utekelezaji wa maagizo hayo tuujadili na kuufanyia kazi kwa haraka".

Alisema miongoni mwa changamoto kubwa za uhifadhi katika eneo hilo kwa sasa ni wingi wa mifugo pamoja na majengo ya kudumu ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro jambo lililohatarisha uhifadhi endelevu wa hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Freddy Manongi amesema jukumu kuu la kuazishwa kwa mamlaka hiyo ni kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori na malikale, utalii na jamii iliyopo ndani ya Eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Akizungumzia changamoto  alisema kuna uhaba wa chakula kutokana na wananchi wa eneo hilo kuzuiliwa kulima kisheria, malalamiko kuhusu wanyama wakali kuwashambulia wananchi na ongezeko la magonjwa mbalimbali huku mengi yakisababishwa na muingiliano wa wananchi na  wanyamapori. 

Wednesday, December 21, 2016

SERIKALI YATOA UFAFANUZI WA KUFUNGIA BIASHARA YA USAFIRISHAJI WANYAMAHAI NJE YA NCHI.NA HAMZA TEMBA - WMU
........................................................................

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa ufafanuzi wa uamuzi wake wa kuzuia biashara ya usafirishaji wa wanyamahai nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo na kusema kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa lengo la kupanga vizuri biashara hiyo kwa faida ya serikali na wafanyabiashara wenyewe.

Ufafanuzi huo umetolewa jana na Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Jumanne Maghembe katika kikao alichokiitisha wizarani hapo na wafanyabiashara wa wanyamahai wa makundi ya wadudu, vyura, mijusi, ndege, nyani na tumbili ambao walitaka kupata ufafanuzi wa hatima ya biashara yao kutoka serikalini.

Katika risala iliyosomwa na kiongozi wa wafanyabiashara hao, Adam Rashid Warioba kwa Waziri Maghembe, aliiomba Serikali kutoa ufafanuzi wa hatma ya biashara yao iliyofungiwa ambayo imekuwa tegemeo pekee katika kuendesha maisha yao huku wakitaka kujua hatma ya wanyamahai waliohifadhiwa na gharama zao walizolipia Serikalini.

Akitoa ufafanuzi wa uamuzi wa Serikali kufungia biashara hiyo kwa wafanyabiashara hao, Prof. Maghembe amesema wanyamahai wengi kutoka nchini Tanzania wamekuwa wakisafirishwa nje ya nchi bila ya kufuata utaratibu maalum ikiwemo vibali vya kukamata na kuwasafirisha wanyama hao jambo ambalo limekuwa likiikosesha serikali mapato mengi.

“Wapo kati yenu ambao walikuwa wanasafirisha wanyamahai kinyume cha sheria, bila vibali vyovyote, na wanyama wa Tanzania walikuwa wakimatwa kwenye bandari na viwanja vya ndege, ambao wanasafirishwa kinyume cha sheria, wengi tu, na ndio maana Serikali ikasema hii biashara tusimamae kwanza tuwekwe utaratibu ambao kila mtu ataufuata, na ambao hautaweza kututia aibu huko nje”, alisema.

Alisema sababu nyingine iliyopelekea serikali kufunga biashara hiyo kwa muda ni bei ndogo inayouzwa wanyama hao nje ya nchi ambayo haiwanufaishi wafanyabiashara na Serikali ukilinganisha na thamani yake kwa kile wanachoenda kufanyiwa, alitolea mfano tumbili ambao hufanyiwa utafiti wa madawa mbali mbali na baadae kuuzwa mabilioni ya fedha huku tumbili huyo akiuzwa kwa dola 25 tu.

“Nimefurahi yule bwana aliyesema tumbili mmoja ni dola 25, lakini akasema hao ndio wanafanya medical research (utafiti wa madawa) yote duniani, sasa sisi tunapata dola 25 na wenzetu wanafanya research (utafiti) wanatuuzia madawa yote billions of dollars (mabilioni ya dola za kimarekani), tuweke utaratibu na ninyi mtakapokuwa mnafanya hii biashara mpate sio lazima serikali ndio lazma ipate, mpate kilicho sawa na thamani ya wanyama mnaowauza”, alisema Prof. Maghembe.

Aliwahakikishia wafanyabiashara hao kuwa Serikali ya awamu ya tano ni sikivu hivyo kuahidi kushuulikia changamoto walizoziwasilisha hadi kufikia Januari 10, mwakani (2017), aliwaeleza kuwa hatma ya wanyamahai ambao wamewahifadhi pamoja gharama za vibali walizowalipia serikalini zitashuulikiwa.

“Ambacho ninaweza kuwaambia hapa leo, kwamba tumepata hii taarifa, tunayo ile idadi ambayo imepitiwa na wataalamu huko kwenye mazizi, tunazo zile permit (vibali) za serikali ambazo mmepewa na leseni, vyote vile mlivyonavyo na sisi tunavyo, tutavipitia vyooote kabisa, alafu tutaona ni namna gani tutawainua kwa kuwafuta jasho”, alisema.

Aliongeza kuwa “Tutaangalia kila mfanyabiashara ameilipa nini serikali, kwa wanyama hawa ambao wapo, ambao katazo lilipofanywa walikuwa nao kwenye mazizi yao na wanyama hao tunawafanyia tathmini tukishakamilisha tutaamua sasa wanyama hao wanapelekwa wapi, na maeneo yenyewe ni machache tu, ama kwenye mazoo, ili waweze kutunzwa na kuendelezwa kwa vile ni vigumu kuwarudisha tena maporini.

 “Na kutokana na vibali na risiti mbalimbali ambazo wameilipa serikali katika kuwapata hao wanyama basi tutaviangalia na kuangalia utaratibu wa kuwarudishia wale wafanyabiashara hela zao”.

Akizungumzia lalamiko la wafanyabiashara hao kuwa wao wamezuiliwa kufanya biashara hiyo huku mfanyabiashara mmoja kutoka nje akiruhusiwa kufanya biashara hiyo kwa tangazo la serikali, Prof. Maghembe anasema “Na hilo tangazo mnalosema lina mtu amebebwa hamna ruhusa ya mtu kubebwa hapa, na mtu atayempa huyo mtu kibali mnafahamu kitakachotokea, hakuna ruhusu, ndivyo serikali ilivyosema”.

Mei 26, mwaka huu, akifanya majumuisho ya hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2016/17, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, alitangaza kuwa ni marufuku kusafirisha wanyamahai wote nje ya nchi kwa miaka mitatu mfululizo.


“Kuanzia sasa (saa moja na dakika tano usiku) kwa miaka mitatu serikali imepiga marufuku usafirishaji wa wanyamahai wote kwenda nje ya nchi, hata chawa wa Tanzania hawataruhusiwa kusafirishwa nje, Na katika kipindi hiki cha miaka mitatu, idara ya wanyamapori itafanya kazi ya kuishauri serikali namna gani biashara hiyo itakavyoendeshwa”, alisema Prof. Maghembe.

Wednesday, December 14, 2016

RAIS DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AWAAPISHA VIONGOZI MBALIMBALI AKIWEMO NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

4.Aloyce
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Ikulu jijini Dar es Salaam.
5
 Viongozi walioapishwa wakila kiapo cha Maadili mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam. Wakwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Itifaki Balozi Grace Alfred Martin, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki, Katibu Mkuu Mawasiliano Dkt. Maria Sasabo, Katibu Mkuu Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe pamoja na Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olonyokie Ole-Sendeka
7.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi pamoja na viongozi walioapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam Wakwanza kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki, Katibu Mkuu Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olonyokie Ole Sendeka, Wakwanza kutoka kulia ni Mkuu wa Itifaki Balozi Grace Alfred Martin pamoja na Katibu Mkuu wa Mawasiliano Dkt. Maria Sasabo.
6
 Viongozi walioapishwa waki weka saini katika viapo vya maadili Ikulu jijini Dar es Salaam. Wakwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Itifaki Balozi Grace Alfred Martin, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mali asili na utalii Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki, Katibu Mkuu Mawasiliano Dkt. Maria Sasabo, Katibu Mkuu Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe pamoja na Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olonyokie Ole Sendeka.

Monday, December 12, 2016

WAZIRI MKUU APOKEA TAARIFA YA FARU JOHN NA PEMBE ZAKE...............................................

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti.


Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay leo mchana (Ijumaa, Desemba 9, 2016) na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu amesema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake. 

"Nilipokea taarifa yenu jana saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo tukimaliza sherehe za 
maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana kuhusu taarifa yenu,”amesema. 

Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema hadi kufikia Desemba 
2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) 
ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.

“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.

Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John 
ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo 
iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru. Kamati hiyo inaundwa 
na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa 
NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.

Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo
cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande alimweleza kwamba 
pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na 
uzito wa kilo 2.3.

Watendaji wa wizara waliohudhuria kikao hicho ni Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Iddi Mfunda; 
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Bw. Freddy Manongi; 
Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Bw. Simon Mduma; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, 
Bw. Alexander Songorwa na Mkuu wa Pori la Akiba la Ikorongo/Grumeti, Bw. 
Nollasco Ngowe. 

Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa 
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika 
kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo 
Alhamisi, Desemba 8.

Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani 
Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na 
Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani 
humo.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

IJUMAA, DESEMBA 9, 2016.


Wednesday, December 7, 2016

RAIS MAGUFULI AFANYA MABADILIKO YA MAKATIBU WAKUU, NAIBU KATIBU WAKUU NA WAKUU WA MIKOA - MABADILIKO HAYO YAIGUSA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Desemba, 2016 
amefanya uteuzi wa Katibu Mkuu mmoja na Mkuu wa Mkoa mmoja na pia amefanya 
mabadiliko madogo katika Wizara na Mikoa kama ifuatavyo;

Dkt. Magufuli amemteua 
Prof. Faustin Kamuzora kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais.Kabla ya uteuzi 
huo, Prof. Kamuzora alikuwa Katibu Mkuu Mawasiliano.

Rais Magufuli 
amemteua Mhandisi Mathew Mtigumwe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi 
na Mifugo anayeshughulikia Kilimo. Mhandisi Mathew Mtigumwe anachukua nafasi ya 
Dkt. Frolence Turuka ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na 
Jeshi la Kujenga Taifa.

Kabla ya uteuzi 
huo Dkt. Frolence Turuka alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na 
Uvuvi aliyekuwa akishughulikia Kilimo. Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. 
Job Masima ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Rais Magufuli 
amemteua Dkt. Maria Sasabo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na 
Mawasiliano na atakuwa akishughulikia Mawasiliano. Dkt. Maria Sasabo anachukua 
nafasi iliyoachwa wazi na Prof. Faustin Kamuzora ambaye ameteuliwa Katibu Mkuu 
Ofisi ya Makamu wa Rais.

Pia Rais Magufuli 
amemteua Mhandisi Angelina Madete kuwa Naibu Katibu Mkuu Katika Wizara ya 
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mhandisi Angelina Madete anachukua nafasi 
iliyoachwa wazi na Dkt. Maria Sasabo aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya 
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano.

Aidha, Rais 
Magufuli amemteua Dkt. Aloyce K. Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya 
Maliasili na Utalii.

Wakati 
huo huo, Rais Magufuli amemteua Bw. Christopher Ole 
Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe.Bw. Christopher 
Ole Sendeka anachukua nafasi ya Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kituo 
cha kazi na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Dkt. Rehema 
Nchimbi anajaza nafasi iliyoachwa na Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye ameteuliwa 
kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo anayeshughulikia Kilimo.Katika 
hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Dkt. Osward
J. Mashindano kuwa Msajili wa Hazina. 

Dkt. Osward J. 
Mashindano anachukuwa nafasi ya 
Bw. Lawrence Mafuru ambaye atapangiwa kazi 
nyingine

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais,
IKULU

Dar es Salaam

07 Desemba, 2016

JARIDA LA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA (TFS) - ONLINE EDITIONThursday, November 24, 2016

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AZUGUMZA NA VIONGOZI NA WATENDAJI WAKUU WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao alichokiitisha kati yake na  Watendaji Wakuu wa  Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakuu wa Mapori  ya Hifadhi za Mistitu, Ofisini kwake mjini Dodoma Novemba 21, 2016.  Kulia kwake ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kushoto kwake) na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akizungumza katika Mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  Ofisini kwake mjiniDodoma Novemba 21, 2016.
  Baadhi ya Watendaji Wakuu  wa Wizara ya Maliasili na Utalii  wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao Ofisini kwake mjini Dodoma, Novemba 21, 2016.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (kulia) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati) baada ya kuongoza kikao kati yake na Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisini kwake mjini Dodoma Novemba 21, 2016.
____________________________

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi na siku tisa kwa Wakuu wa Mapori ya Hifadhi za Misitu kuhakikisha wanaweka mawe ya alama (beacons) kwenye mipaka yao ili kuepusha migogoro na wanavijiji wanaowazunguka.

Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatatu, Novemba 21, 2016) wakati akizungumza na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakuu wa Mapori ya Hifadhi za Misitu nchini katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.

“Tatizo la migogoro baina ya wafugaji, wakulima na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya ni lazima lifanyiwe kazi. Mkitoka hapa rudini katika maeneo yenu mkawaambie wananchi mipaka yenu iko wapi. Ninyi mnatambua mipaka yenu iko wapi kwa hiyo waelewesheni wananchi kwa kuweka alama,” amesema.

“Wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akizindua bunge tarehe 20 Novemba, 2015 aliwapa maeneo makuu matatu ambayo ni kuanisha mipaka, kupambana na ujangili na kukusanya mapato. Alizungumzia suala la mipaka kwa sababu iliyopo haieleweki, mkiulizwa mnajibu kuna buffer zone. Hivi mwananchi wa kawaida anajua buffer zone ni nini?,” alihoji.

“Sasa ninawapa muda hadi Januari 31, 2017 kazi ya kuweka beacons kwenye hifadhi zote za misitu iwe imekamilika. Kila pori nenda mkatengeneze alama zenu kama TANROADS walivyofanya. Kaeni mpige hesabu ni kiasi gani cha saruji na kokoto kinahitajika. Tutarudi hapa Dodoma kupeana taarifa ya utekelezaji. Katibu Mkuu niletee taarifa ya kila mkoa na wilaya kuna mapori mangapi tutakutana hapahapa kupeana mrejesho,” alisisitiza.

Alisema kama TANROADS waliweza kuweka alama za barabarani kwa nchi nzima ni kwa nini Wizara ya Maliasili na Utalii imeshindwa kuchukua hatua kama hizo. “Ni lazima tuweke hizo alama kila katika pori lake, tusipofanya hivyo, migogoro hii itaendelea,” alisema.

“Nendeni mkaweke alama za mipaka mkishamaliza sasa muwaeleze wananchi ni umbali wanapaswa waache kutoka kwenye hizo alama zenu na muwaelimishe kwamba hiyo ndiyo buffer zone. Suala la beacons ni serious na ninatarajia nikute hizo beacons kwenye maeneo yenu”

“Kila mmoja anayo fursa ya kuitisha mkutano na wananchi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuwa na mapori ya akiba. Pandeni kwenye majukwaa, muelezee mipaka hiyo mipya na wananchi watawaelewa kwa sababu mwenye dhamana ya kwanza katika kutoa elimu hii ni wewe Mkuu wa Pori,” alisistiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuanzia leo Ofisi ya Rais TAMISEMI haina budi kusitisha usajili wa vijiji hadi zoezi la kuweka alama kwenye mipaka mapori ya hifadhi za misitu litakapokalimika.

“Kuanzia leo ninasimamisha zoezi la usajili wa vijiji unaofanywa na TAMISEMI hadi wizara ya Maliasili na Utalii ikamilikshe zoezi la kuainisha na kuweka alama kwenye mipaka mapori ya hifadhi za misitu. Tusipofanya hivyo tutaendelea kuwa na Taifa la walalamikaji,” alisema huku akishangiliwa na watendaji hao.

“Wakuu wa mapori tambueni ni vijiji vingapi ambavyo Serikali ilifanya makosa na kuvisajili wakati viko ndani ya hifadhi na vijiji vingapi bado havijasajiliwa. Pia onyesheni ni vijiji vingapi ambavyo ni hatarishi,” alisema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemtaka Mkurugenzi wa Idara ya Utalii katika wizara hiyo, Bw. Zahoro Kimwaga pamoja na Bodi ya Utalii nchini wabadilike na kuanza kufanya kazi kibiashara zaidi.

“Mkurugenzi wa Utalii na Bodi yako ya Utalii bado hamjajitangaza vya kutosha. Promosheni ya utalii hapa nchini bado haitoshi na mgeweza kuoata mapato makubwa zaidi kwa kujitangaza. Mabango ya barabarani yamejaa matangazo ya Vodacom na Airtel badala ya kuwa na picha za wanyama ili kila mtu akiona atamani kwenda mbugani,” alisema.

“Tumieni mabango ya kieletroniki (electronic screens) kurusha picha za wanyama. Mfano pale nje ya uwanja wa Taifa, au uwanja wa ndege hata kwenye njia kuu  za mikoani wekeni mabango ya iana hiyo. Ombeni vipindi kwenye televisheni nyingine, kile cha TBC1 peke yake hakitoshi,” alisisitiza.

KUKUZA UCHUMI KUPITIA SEKTA YA UTALII KUNAHITAJI WAFANYAKAZI WENYE SIFA - MAGHEMBE

Waziri wa Maliasili na utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akisikiliza maelezo ya mmoja wa wahitimu wa mafuzo ya upishi katika hoteli za kitalii wakati wa mahafali ya sita ya Chuo cha Hoteli na Utalii Njuweni kilichopo Kibaha, mkoani Pwani hivi karibuni. 
_______________________________

Waziri wa Maliasili na utalii, Prof. Jumanne Maghembe amesema  ili Tanzania iendelelee kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii inahitaji wafanyakazi wa kada hiyo  wawe na sifa zinazostahili ikiwemo nidhamu na uaminifu.


Ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya  6 ya Chuo cha Hotel na Utalii  cha Njuweni kilichoko  Kibaha mkoani Pwani ambayo yalifanyika kwenye viwanja vya Chuo hicho.

Alisema kuwa  pamoja na vyanzo mbalimbali vya mapato vinavyokuza uchumi wa taifa taifa,  Wizara ya Maliasili na Utalii ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi huo hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha watu wanaopewa dhamana ya kufanyakazi kwenye Wizara hiyo wanafanya kazi kwa weledi.

"Napenda kuwakumbusha kuwa nidhamu na uaminifu ndiyo siri itakayowawezesha ninyi kufika mbali katika utendaji wenu wa kazi, lakini mkiingiza tamaa na udokozi hamtafika mbali na badala yake mtalitia taifa kwenye sifa mbaya" alisema

Alisema kuwa Serikali imekuwa ikikuza uchumi wa nchi kila mwaka kupitia Sekta ya utalii ambapo idadi ya  watalii  imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 23.7 kutoka watalii 867,994 mwaka 2011 hadi kufikia watalii 1,137,182 mwaka 2015. Aidha sekta hiyo inachangia asilimia 17 ya pato la taifa.

"Mapato yatokanayo na  shughuli za utalii yaliongezeka  kwa asilimia 28.8 kutoka dola za Marekani mil. 1,353.29 mwaka 2011 hadi kufikia dola za Marekani mil. 1,901.1 mwaka 2015" alisema

kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Nditi Rashid alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana kwa miaka kadhaa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho lakini bado kuna changamoto kadhaa zinazowakabili ikiwemo upungufu wa vifaa vya kisasa vya kuendeshea masomo ya TEHAMA

"kutokana na ufinyu wa bajeti tulionao tunakuomba mheshimiwa mgeni rasmi utusaidie kupata msaada wa vifaa vipya vitakavyotusaidia kuendesha masomo ya TEHAMA kwa ufanisi zaidi" alisema

Mahafari hayo ambayo ni ya sita tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 200o  yalihusisha jumla ya wanafunzi 350 waliohitimu kwa ngazi ya stashahada ambao walipata vyeti na zawadi mbalimbali .

Wednesday, November 23, 2016

HAKUNA KIONGOZI WA JUU WA SERIKALI ANAYEPINGA ZOEZI LA UHIFADHI NCHINI – MAJALIWANA HAMZA TEMBA - WMU
......................................................................

Kufuatia malalamiko ya wahifadhi juu ya kauli na vitendo mbalimbali za baadhi ya wananchi na viongozi wa kisiasa vyenye lengo la kukwamisha shughuli za uhifadhi nchini kwa maslahi yao binafsi kwa visingizio kuwa ni maagizo kutoka juu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa tamko na kusema kuwa hakuna kiongozi wa juu wa Serikali anayepinga zoezi la uhifadhi wa maliasili nchini.
Majaliwa ameyasema hayo juzi wakati akizungumza na viongozi na watendaji wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wakuu wa taasisi za uhifadhi zilizopo chini ya wizara hiyo na wakuu wa hifadhi za taifa pamoja na mapori ya akiba katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.
“Wapo watu wanaotumia majina ya viongozi wakuu kukwamisha mazoezi yanayoendeshwa na wahifadhi nchini. Hakuna kiongozi wa juu anaeweza kuzuia zoezi muhimu kama hili. Na Kama kuna mtu anakuja kukuambia wewe fulani kasema, mwambie niunganishe na yeye mwenyewe.  Tumeona maeneo mengi sana, watu wanafanya madudu wanasema huyu kaagizwa kutoka juu, juu ni wapi, kwa Mkurugenzi wako? kwa Katibu Mkuu?  Naibu Waziri au Waziri? Au huku kwa Waziri mkuu? Makamu wa Rais au Rais?,” alihoji.
“Fanyeni, bora ukosee halafu tuseme hapo umekosea utarekebisha, kuliko kuogopa kufanya kwa sababu mtu kakukwamisha, kwani ulivokuwa unaimplement (unafanya) alikuambia nani? si kutokana na na sheria na taratibu, muhimu zaidi ni kuzingatia sheria na taratibu, usije ukafanya mambo ya ajabu,” aliongeza.
Ili kufanikisha zoezi hilo aliwaagiza pia kuhakikisha wanaweka alama za mipaka (beacons) katika hifadhi zao hadi kufikia januari 31, 2017 ili kuepusha migogoro na wananchi wanaovamia maeneo hayo kwa makusudi au kwa kutokujua maeneo ya mipaka husika.
“Nendeni mkawaambie mwisho ni hapa weka na beacon kabisa, na sheria zitachukua mkondo wake kwa yeyote ambaye hatafata maelekezo yenu. Tatizo la migogo iliyozungumzwa kati wa wafugaji na wahifadhi au wafugaji na kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mikoa ni lazma likafanyiwe kazi, lazima tuendelee kudhibiti kuingia mifugo ndani ya mapori,” alisisitiza.
Aliwaagiza pia kusimama kwenye majukwaa na kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo yao ya hifadhi. “Namba moja wa utoaji elimu ni wewe mkuu wa pori, ni lazma utoe maelezo ya pori lako ni wapi linakoishia, kama mpaka huo ni wa kisheria muwaambie, nini umuhimu wa kutoingia, wananchi wapate elimu namna ya kuhifadhi pori na faida zake,” alisema.
Akizungumzia changamoto iliyoibuliwa katika kikao hicho kuhusu mgongano uliopo katika usimamizi wa misitu baina Wakala wa Huduma za misitu Tanzania na Serikali za Mitaa alisema Serikali inaenda kuliangalia upya suala hilo ili ione namna bora ya kutoa majukumu ya kusimamia rasilimali zote za misitu kwa chombo kimoja tofauti na ilivyo hivi sasa, hatua ambayo inaelezwa kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto za uharibifu wa misitu nchini.
“Kama ilivyoelezwa kuwa kuna mgongano wa majukumu kwenye kitengo cha misitu, baina ya TFS na DFO (Ofisa misitu wa Wilaya), DFO anauza bila hata kumconsult (kumtaarifu) TFS na anagonga na nyundo…, kwa hiyo tutaliangalia tuone majukumu yale na namna ambavyo tunaweza tukayapa chombo kimoja ili kisimamie lakini TFS mmeperform (mmefanya) vizuri endeleeni kufanya hivyo vizuri kwa sasa,” alisema huku akipigiwa makofi na watendaji hao.
Changamoto nyingine iliyoibuliwa katika kikao hicho ni matukio ya kuingizwa kwa mifugo katika maeneo ya hifadhi yaliyoko mpakani huku asilimia kubwa ya mifugo hiyo ikielezwa kutoka nje ya nchi, Waziri Mkuu Majaliwa amekemea kitendo hicho na kuagiza mifugo hiyo iondolewe mara moja. “Hatutaki ng'ombe wa nje ya nchi kuingia ndani ya nchi, mifugo ya ndani imetutosha,” alisema.
Aidha ameutaka uongozi wa Wizara kuimarisha doria za mara kwa mara, kuongeza ajira za makamanda (askari wa wanyamapori) na vitendea kazi muhimu vya kuimarisha doria ikiwemo magari.
Kwa upende wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alisema ipo changamoto kubwa ya tishio la kutoweka kwa mvua na kukauka kwa vyanzo muhimu vya maji nchini kutokana na uharibifu wa maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na muingiliano wa mifugo na wanyamapori kama vile kimeta na homa ya bonde la ufa.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utalii wa Wizara hiyo, Zahoro Kimwaga alisema, umuhimu wa uhifadhi una faida mtambuka  ambapo sekta ya utalii pekee inachangia asilimia 17 ya pato la taifa huku ikitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja takriban milioni 1.5. Alisema sekta hiyo pia inachangia asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni ikiwa ni sekta kiongozi kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.
Aliongeza kuwa hadi kufikia Novemba 20 mwaka huu takwimu zinaonyesha kuwa maendeleo ya sekta ya utalii yameongezeka kwa asilimia 5 licha ya malalamiko mbalimbali kuhusu sekta hiyo baada ya Serikali kuweka kodi ya VAT katika huduma za kitalii nchini.