NA HAMZA TEMBA - WMU
........................................................................
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa ufafanuzi wa uamuzi wake wa kuzuia biashara ya usafirishaji wa wanyamahai nje ya nchi kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo na kusema kuwa uamuzi huo ulitolewa kwa lengo la kupanga vizuri biashara hiyo kwa faida ya serikali na wafanyabiashara wenyewe.
Ufafanuzi huo umetolewa
jana na Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Jumanne Maghembe katika kikao alichokiitisha
wizarani hapo na wafanyabiashara wa wanyamahai wa makundi ya wadudu, vyura,
mijusi, ndege, nyani na tumbili ambao walitaka kupata ufafanuzi wa hatima ya
biashara yao kutoka serikalini.
Katika risala iliyosomwa na
kiongozi wa wafanyabiashara hao, Adam Rashid Warioba kwa Waziri Maghembe,
aliiomba Serikali kutoa ufafanuzi wa hatma ya biashara yao iliyofungiwa ambayo
imekuwa tegemeo pekee katika kuendesha maisha yao huku wakitaka kujua hatma ya
wanyamahai waliohifadhiwa na gharama zao walizolipia Serikalini.
Akitoa ufafanuzi wa uamuzi
wa Serikali kufungia biashara hiyo kwa wafanyabiashara hao, Prof. Maghembe
amesema wanyamahai wengi kutoka nchini Tanzania wamekuwa wakisafirishwa nje ya
nchi bila ya kufuata utaratibu maalum ikiwemo vibali vya kukamata na
kuwasafirisha wanyama hao jambo ambalo limekuwa likiikosesha serikali mapato
mengi.
“Wapo kati yenu ambao
walikuwa wanasafirisha wanyamahai kinyume cha sheria, bila vibali vyovyote, na
wanyama wa Tanzania walikuwa wakimatwa kwenye bandari na viwanja vya ndege,
ambao wanasafirishwa kinyume cha sheria, wengi tu, na ndio maana Serikali
ikasema hii biashara tusimamae kwanza tuwekwe utaratibu ambao kila mtu
ataufuata, na ambao hautaweza kututia aibu huko nje”, alisema.
Alisema sababu nyingine
iliyopelekea serikali kufunga biashara hiyo kwa muda ni bei ndogo inayouzwa
wanyama hao nje ya nchi ambayo haiwanufaishi wafanyabiashara na Serikali
ukilinganisha na thamani yake kwa kile wanachoenda kufanyiwa, alitolea mfano
tumbili ambao hufanyiwa utafiti wa madawa mbali mbali na baadae kuuzwa
mabilioni ya fedha huku tumbili huyo akiuzwa kwa dola 25 tu.
“Nimefurahi yule bwana
aliyesema tumbili mmoja ni dola 25, lakini akasema hao ndio wanafanya medical
research (utafiti wa madawa) yote duniani, sasa sisi tunapata dola 25
na wenzetu wanafanya research (utafiti) wanatuuzia madawa
yote billions
of dollars (mabilioni ya dola za kimarekani), tuweke utaratibu na ninyi
mtakapokuwa mnafanya hii biashara mpate sio lazima serikali ndio lazma ipate,
mpate kilicho sawa na thamani ya wanyama mnaowauza”, alisema Prof. Maghembe.
Aliwahakikishia
wafanyabiashara hao kuwa Serikali ya awamu ya tano ni sikivu hivyo kuahidi kushuulikia
changamoto walizoziwasilisha hadi kufikia Januari 10, mwakani (2017), aliwaeleza
kuwa hatma ya wanyamahai ambao wamewahifadhi pamoja gharama za vibali
walizowalipia serikalini zitashuulikiwa.
“Ambacho ninaweza kuwaambia
hapa leo, kwamba tumepata hii taarifa, tunayo ile idadi ambayo imepitiwa na
wataalamu huko kwenye mazizi, tunazo zile permit (vibali) za serikali
ambazo mmepewa na leseni, vyote vile mlivyonavyo na sisi tunavyo, tutavipitia
vyooote kabisa, alafu tutaona ni namna gani tutawainua kwa kuwafuta jasho”,
alisema.
Aliongeza kuwa “Tutaangalia
kila mfanyabiashara ameilipa nini serikali, kwa wanyama hawa ambao wapo, ambao katazo
lilipofanywa walikuwa nao kwenye mazizi yao na wanyama hao tunawafanyia
tathmini tukishakamilisha tutaamua sasa wanyama hao wanapelekwa wapi, na maeneo
yenyewe ni machache tu, ama kwenye mazoo, ili waweze kutunzwa na kuendelezwa
kwa vile ni vigumu kuwarudisha tena maporini.
“Na kutokana na vibali na risiti mbalimbali
ambazo wameilipa serikali katika kuwapata hao wanyama basi tutaviangalia na
kuangalia utaratibu wa kuwarudishia wale wafanyabiashara hela zao”.
Akizungumzia lalamiko la
wafanyabiashara hao kuwa wao wamezuiliwa kufanya biashara hiyo huku
mfanyabiashara mmoja kutoka nje akiruhusiwa kufanya biashara hiyo kwa tangazo
la serikali, Prof. Maghembe anasema “Na hilo tangazo mnalosema lina mtu
amebebwa hamna ruhusa ya mtu kubebwa hapa, na mtu atayempa huyo mtu kibali
mnafahamu kitakachotokea, hakuna ruhusu, ndivyo serikali ilivyosema”.
Mei 26, mwaka huu, akifanya
majumuisho ya hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa
mwaka 2016/17, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe,
alitangaza kuwa ni marufuku kusafirisha wanyamahai wote nje ya nchi kwa miaka
mitatu mfululizo.
“Kuanzia sasa (saa moja na
dakika tano usiku) kwa miaka mitatu serikali imepiga marufuku usafirishaji wa
wanyamahai wote kwenda nje ya nchi, hata chawa wa Tanzania hawataruhusiwa
kusafirishwa nje, Na katika kipindi hiki cha miaka mitatu, idara ya wanyamapori
itafanya kazi ya kuishauri serikali namna gani biashara hiyo itakavyoendeshwa”,
alisema Prof. Maghembe.
No comments:
Post a Comment