slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Monday, December 12, 2016

WAZIRI MKUU APOKEA TAARIFA YA FARU JOHN NA PEMBE ZAKE



...............................................

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti.


Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay leo mchana (Ijumaa, Desemba 9, 2016) na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu amesema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake. 

"Nilipokea taarifa yenu jana saa 7 usiku lakini nikaahidi kuwa leo tukimaliza sherehe za 
maadhimisho ya Uhuru tukutane na kujadiliana kuhusu taarifa yenu,”amesema. 

Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Maghembe alisema hadi kufikia Desemba 
2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) 
ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.

“Kati ya faru 37 waliokuwepo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26 sawa na asilimia 70.2. Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.

Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John 
ilianza kudorora na alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo 
iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru. Kamati hiyo inaundwa 
na Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Mkurugenzi Mkuu wa 
NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.

Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo
cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande alimweleza kwamba 
pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na 
uzito wa kilo 2.3.

Watendaji wa wizara waliohudhuria kikao hicho ni Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Iddi Mfunda; 
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Bw. Freddy Manongi; 
Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Bw. Simon Mduma; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, 
Bw. Alexander Songorwa na Mkuu wa Pori la Akiba la Ikorongo/Grumeti, Bw. 
Nollasco Ngowe. 

Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa 
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika 
kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo 
Alhamisi, Desemba 8.

Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani 
Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na 
Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani 
humo.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU

IJUMAA, DESEMBA 9, 2016.


No comments:

Post a Comment