Waziri wa Maliasili na Utalii,
Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto) akisalimiana na Viongozi wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kagera katika ziara yake mkoani humo kuzungumzia operesheni
ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za
kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa kisheria na mahakama. Anayeongoza utambulisho huo
(kushoto) ni Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu.
Waziri wa Maliasili,
Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Kagera, mjini Bukoba kuhusu operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya
hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa
kisheria. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu na
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro.
NA HAMZA TEMBA - WMU
---------------------------------------------------------
Waziri wa Maliasili
na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Kagera unaongozwa
na Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu kwa kufanikisha operesheni
ya kuondoa mifugo katika maeneo ya hifadhi mkoani humo huku akitoa tahadhari
kwa watumishi wa hifadhi hizo kupoteza ajira zao endapo wataruhusu mifugo hiyo
kurudi tena katika hifadhi hizo.
Ametoa pongezi na
tahadhari hiyo jana mjini Bukoba wakati akizungumza na uongozi wa mkoa huo na
kusema kuwa, kazi hiyo ni ya kupongezwa sana kwakua imeleta matumaini ya
uhifadhi mkoani Kagera na taifa kwa ujumla.
“Napenda niwashukuru
kipekee kabisa kwa jinsi ambavyo mlifanya ile operesheni ya kuondoa mifugo
kwenye hifadhi zetu, tulifanya kwa ueledi uliotukuka, hata kama umesikia watu
wanalalamika lakini hakuna aliyesema kuku wangu waliuawa, walipigwa risasi,
tulinyang’anywa mifugo, kazi hii ilifanywa vizuri na kwa ueledi mkubwa sana”, alisema
Prof. Maghembe.
Aliongeza, “Hatutaruhusu
tena mifugo hiyo irudi huko ndani ya hifadhi, hili ni jambo kubwa ambalo ni
wajibu wa wahifadhi wote kuhakikisha
kwamba hakuna mifugo itakayokuwa inaingia humo ndani, Kuanzia sasa kama
tutakuta mtu ameingia kwenye hifadhi yako wakati tunamuondoa tunamuondoa yeye
na wewe na familia yako yote ili mbegu yako mbaya isibaki katika uhifadhi wa
wanyamapori”.
“Haiwezekani kwamba kila
siku Serikali yote inafunga kazi zingine zote tunahamia kuondoa wavamizi na
ninyi mpo na kazi yenu ni kuhakikisha kwamba wavamizi hawaingii humo, Kwahiyo
hii sio temporary na wala sio nguvu ya soda, hata kidogo, na kusema kila siku
inakua hivi hivi itaisha, tutaingia tu, hakuna hiyo, kwahiyo mfanye kazi yenu, mlinde, na wanyama
wakiingia humo itakua kazi imewashinda na itakua imewashinda “permanently” ni
vizuri mjue msije mkadhani kwamba hamkuambiwa, ndio maana nimekuja na
wakurugenzi wenu wote ili wasikie na walisimamie jambo hili” alisema.
Waziri Maghembe katika
ziara yake hiyo ya mkoani Kagera aliongozana na Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Hifadhi za Wanyamapori, Martin Loibooki na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo. Alitembelea pia mikoa ya Tabora na
Shinyanga ambapo alitoa maelekezo muhimu ya kuondoa mifugo kwenye hifadhi.
Alisema ili
kuimarisha ulinzi katika hifadhi hizo, utaratibu wa kutumia ndege maalum za doria
na “drones” (ndege zisizo na rubani) utawekwa ili kuwabaini wahalifu
watakaokuwa wamekaidia agizo hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.
“Tutakua tunarusha
ndege mara moja kila baada ya wiki tatu au wiki mbili kuhakikisha kwamba hakuna
mtu anaingia na mifugo humo ndani, lakini pili tutafanya doria na ndege zile
ambazo hazina marobani kuhakikisha kwamba tunaangalia kinachotokea humo ndani
wakati wote.
“Najua wanaweza
kubadilisha “system” (utaratibu) ikawa ya usiku na hawa askari hawa tutawapa
mafunzo maalum chini ya jeshi la wananchi wa Tanzania, kuanzia miezi sita mpaka
tisa, wajifunze namna ya kuhangaika na hawa ambao wanaingia kwenye hifadhi zetu”,
alisema.
Akizungumzia
operesheni hiyo, alisema ulitolewa muda maalum kwa watu kutoa mifugo yao kwa
hiari katika mapori ya akiba na hifadhi za misitu mkoani humo ambapo wale wote
waliotii hakuna mashtaka yeyote yalifunguliwa dhidi yao ispokuwa wale
waliokaidi walifikishwa mahakamani na mifugo yao ikataifishwa kwa mujibu wa
Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kifungu namba 111 sehemu ya kwanza ambayo inaruhusu kutaifisha mali itakayokutwa hifadhini.
Alisema kuwa kumekuwepo
na malalamiko mbalimbali juu ya utaratibu wa upigaji mnada mifugo
iliyotaifishwa ikiwemo minada hiyo kufanyika ndani ya maeneo ya hifadhi, wenye
mifugo kutoruhusiwa kuingia na wakati mwingine kuwepo kwa malalamiko ya idadi
tofauti ya mifugo iliyotaifishwa na inayopelekwa mnadani.
Ili kuondoa
malalamiko hayo alielekeza kuwa baada ya amri ya mahakama kutoka ni lazima mamlaka
ya Wilaya husika ijulishwe na zoezi hilo lifanyike katika maeneo ya wazi ili
kila mwananchi anayehitaji aweze kushiriki mnada husika.
“Minada hii ifanywe
kwa maelekezo ya mamlaka, hukumu ikitoka mkuu wa wilaya ajulishwe, na kwamba
mifugo kadhaa itapigwa mnada, na yeye ataamua mnada ufanyike wapi na lini, na
iwe sehemu ambayo kila mtu anaweza kufika, minada hiyo iwe ya wazi na matangazo
yatolewe ili malalamiko yasiwepo ndio maana maelekezo yametoka minada isitishwe
kwa muda wa siku saba mambo haya yawekwe sawa”, alisema Maghembe.
Kwa upande wake Mkuu
wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu alishukuru kwa ushirikiano
alioupata kutoka Wizara ya Maliasili katika kipindi chote cha utekelezaji wa
operesheni hiyo ambayo amaeielezea kuwa na mafanikio makubwa ikiwemo
wanyamapori kuanza kurudi kwenye maeneo yao katika Mapori ya Akiba ya
Biharamulo Burigi na Kimisi.
Waziri wa Maliasili,
Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Kagera, mjini Bukoba kuhusu operesheni ya kuondoa mifugo kwenye maeneo ya
hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyotaifishwa
kisheria. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu,
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro (kulia), Katibu Tawala Mkoa wa
Kagera, Diwani Athuman (wa pili kushoto) na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori,
Prof. Alexander Songorwa.
Waziri wa Maliasili,
Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa
Kagera, mjini Bukoba.
Picha ya pamoja
kati ya Waziri wa Maliasili (katikati waliokaa) na kamati ya ulinzi na usala ya
Mkoa wa Kagera muda mfupi baada ya kikao cha kujadili operesheni ya kuondoa
mifugo kwenye maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada
ya mifugo iliyotaifishwa kisheria.
Picha ya pamoja kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii (katikati waliokaa), Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu (wa pili kulia waliokaa), Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro (wa pili kushoto waliokaa), Katibu Tawala Mkoa huo, Diwani Athuman (kulia waliokaa), Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa (kushoto waliokaa), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Laibooki (katikati waliosima) na maofisa wa Mamlaka hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mst. Salum Kijuu (kushoto) akizungumza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Laibooki (wa pili kushoto) Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Kudhibiti ujangili, Faustine Masalu (kulia).
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa (kulia), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo (katikati) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Laibooki (kushoto).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akisalimiana na uongozi wa Wilaya ya Biharamulo alipotembelea wilayani humo kwa ajili ya kutoa maelekezo ya Serikali kuhusu operesheni ya kuondoa mifugo katika maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo iliyokamatwa na kutaifishwa na mahakama. Anayeongoza utambulisho huo (kulia) ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Sada Malunde.
Waziri wa Maliasili,
Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na usala ya
Wilaya ya Biharalamulo na watumishi wa sekta ya wanyamapori wilayani humo.
Waziri wa Maliasili
na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na Kamati ya Ulinzi na usala ya
Wilaya ya Biharalamulo na watumishi wa sekta ya wanyamapori wilayani humo. Kulia ni Mkuu wa
Wilaya hiyo, Sada Malunde na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Diwani Athuman
(kushoto).
Baadhi ya askari na watumishi wa Idara ya Wanyamapori wa Wilaya ya Biharamulo.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, viongozi wa mamlaka za uhifadhi, watumishi na kamati ya ulinzi na usala ya Wilaya.
Waziri wa Maliasili,
Prof. Jumanne Maghembe akiagana na Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Diwani Athuman
pamoja na viongozi wengine wa chama na Serikali wa Wilaya ya Biharamulo baada
ya kumaliza ziara yake Mkoani humo ya kujadili operesheni ya kuondoa mifugo kwenye
maeneo ya hifadhi pamoja na taratibu sahihi za kuendesha minada ya mifugo
iliyotaifishwa kisheria.
No comments:
Post a Comment