slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Tuesday, November 14, 2017

TUTAWEKA MIKAKATI MIPYA WA KUNADI VIVUTIO VYA UTALII NCHINI CHINA - DK. KIGWANGALLA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke ofisini kwake mjini Dodoma jana Novemba, 14 ambapo walijadili mikakati ya kuongeza idadi watalii na wawekezaji katika sekta hiyo kutoka nchini China.

Na Hamza Temba - WMU
................................................................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema Serikali kupitia Wizara yake inakusudia kuandaa mkakati maalum wa kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini China ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ya Serikali.

Dk. Kigwangalla amesema hayo jana ofisini kwake mjini Dodoma akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke ambaye alimtembelea kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta ya Uhifadhi na Utalii.

“Moja ya mkakati wangu kama Waziri mpya wa Wizara hii kukuza utalii ni kuweka mkakati wa kuleta watalii wengi kutoka China, China ni Taifa Kubwa lenye watu wengi, tunalenga zaidi kuwafikia watu wanaoishi maisha ya kati ambao ndio wanaopenda kutumia fedha zao kufurahia maisha” alisema Dk. Kigwangalla.

Katika mazungumzo hayo alimuomba Balozi huyo kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa njia ya ushauri wa kitaalamu au wa kifedha kwa ajili ya kuandaa mkakati mahususi wa kulifikia soko la utalii la China kwa kuainisha vivutio na aina ya huduma ikiwemo hoteli ambazo zitakuwa kivutio kwa watalii kutoka China kuweza kutembelea Tanzania.

Miongoni mwa mikakati waliojadiliana ni uwezekano wa kutumia fursa ya uwepo wa wawakilishi wa Televisheni ya CCTV ya China nchini Tanzania ambao wanaweza kutumika kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini ikiwemo kuambatana na Waziri Kigwangalla kwenye ziara zake za kikazi kwenye maeneo ya vivutio na baadaye kuvitangaza nchini China na Duniani kote.

Walijadili pia uwezekano wa kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege baina ya nchi hizo mbili kwa lengo la kurahisisha Safari za Utalii pamoja na kuanzisha mtandao wa pamoja wa watoa huduma za utalii wa mataifa hayo mawili.

Aidha, Dk. Kigwangalla alimuomba balozi huyo kuleta wawekezaji katika sekta ya Hoteli za kitalii na kuahidi kuwapa maeneo ya kujenga hoteli hizo ili kukuza huduma na soko la utalii nchini kwa kurahisisha upatikanaji wa watalii wa China kutembelea Tanzania.

Kwa upande wake Balozi Wang Ke alimueleza Waziri Kigwangalla kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali ambapo mwezi Februari mwakani (2018) itaandaa Maonyesho ya Kimataifa ya Kuuza Nje na Kuingiza Bidhaa na Huduma (International Export and Import Fair) ambapo watu mashuhuri kutoka China watashiriki akiwemo mcheza  Filamu mashuhuri kwenye filamu ya kichina kwa Lugha ya Kiswahili maarufu kama Maododo.

Alisema kupitia Maonyesho hayo Tanzania itaweza kujenga mtandao wa utalii na China kwa kunadi vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini kwa watu maarufu watakaoshiriki maonyesho hayo wakiwemo wafanyabiashara na watoa huduma za utalii na ukarimu. 

No comments:

Post a Comment