slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Friday, June 10, 2016

SERIKALI YA TANZANIA NA ZAMBIA ZASAINI MAKUBALIANO YA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA KUDHIBITI USAFIRISHAJI WA MAZAO YA MISITU NA MAGOGO KUPITIA MIPAKA YA NCHI HIZO

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (katikati) akisaini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Zambia,  jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususan magogo katika mipaka ya nchi hizo mbili. Wanaoshuhudia kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Wizara ya Maliasili, Gladynes Mkamba na Kaimu Mtendaji Mkuu TFS, Richard Kamwenda (kushoto). Waliosimama kulia ni Mwanasheria wa TFS, David Mung’ong’o na Mwanasheria wa Wizara ya Maliasili, Stephen Mwamasenjele. 
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda akisaini  makubaliano hayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda wakibadilishana hati ya makubaliano waliyosaini kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo katika mipaka ya nchi hizo. 
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi akizungumza katika hafla fupi ya kuweka makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Zambia jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo katika mipaka ya nchi hizo. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda. Maj. Gen. Milanzi alisema kuwa ushirikiano huo utaleta tija katika udhibiti wa biashara haramu ya uvunaji na usafirishaji wa magogo kutoka katika nchi hizo kwenda nchi nyingine kupitia mipaka ya nchi hizo na bandari ya Dar es Salaam. Aliwataka watanzania wanaojihusisha na biashara haramu ya uvunaji na usafirishaji wa magogo nje ya nchi waache mara moja kwani Serikali imejipanga kuhakikisha wanakamatwa na sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda wakiteta jambo wakati wakikagua Makontena 103 ya magogo (nyuma pichani) yaliyokamatwa hivi karibuni katika bandari ya Dar es Salaam kutoka nchini Zambia na DRC. Makatibu Wakuu hao wamesaini makubaliano ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo kwenye mipaka wa nchi hizo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto) na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Hifadhi ya Mazingira wa Serikali ya Zambia, Trevor Kaunda wakiangalia sehemu ya magogo yaliyokamatwa hivi karibuni katika bandari ya Dar es Salaam kutoka nchini Zambia na DRC. Makatibu Wakuu hao wamesaini makubaliano ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo kwenye mipaka wa nchi hizo.

........................................................................................... 

Serikali ya Tanzania na Zambia zimesaini makubaliano ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususani magogo katika maeneo ya mpakani kwa lengo la kulinda misitu na kuimarisha uhifadhi katika nchi hizo.

Makubaliano hayo yalitiwa saini jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili  na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya  Maliasili, Ardhi na Hifadhi ya Mazingira ya nchini  Zambia, Bw. Trevol Kaunda na kushuhudiwa na Wajumbe kutoka Zambia na Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mara  baada ya kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii  Maj. Gen. Gaudence Milanzi alisema hatua hiyo imefikiwa ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zilizopo za uharibifu wa misitu na usafirishaji wa mazao ya misitu na magogo kupitia mipaka ya nchi hizo.

Makubaliano hayo yalifikiwa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha siku tatu cha wajumbe kutoka nchi hizo mbili cha kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta misitu maeneo ya mpakani.

katika kikao hicho Tanzania iliwakilishwa na wajumbe kutoka taasisi za Serikali ambazo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  Mamlaka ya Bandari (TPA),  Ofisi ya Mwendesha Mashitaka  Mkuu wa Serikali na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Katika hatua nyingine mara baada ya kusaini makubaliano hayo, msafara wa Makatibu Wakuu hao ulitembelea Bandari ya Dar es Salaam kukagua shehena ya magogo yaliyokamatwa katika bandari hiyo kuanzia mwezi Novemba mwaka jana kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.

Maj. Gen. Milanzi alisema kuwa jumla ya makontena ya magogo hayo ni 103 ambapo makotena 56 yalikamatwa kuanzia mwezi Novemba mwaka jana yakidaiwa kutoka nchini Zambia na makontena mengine 47 yaliyodaiwa kutoka DRC ambayo yamekamwatwa kuanzia mwezi Januari mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada kukagua makontena hayo, Maj. Gen. Milanzi alisema "Napenda kuwaasa wananchi wanaojihusisha na biashara hii haramu ya kusafirisha magogo waache mara moja kwani inasababisha uharibifu mkubwa wa misitu na endapo tutawakamata tutawachukulia hatua kali za kisheria”.

Kwa upande wake  Katibu Mkuu wa  Wizara ya  Maliasili, Ardhi na Mazingira wa Zambia, Bw. Trevol Kaunda alisema kuwa “Ushirikiano baina ya pande hizi mbili utaleta ufanisi katika suala la uhifadhi wa misitu yetu kwa kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakisafirisha magogo na mazao ya misitu kwa kutumia njia danganyifu, umoja huu utatusaidia kuwabaini ni kuwachukulia hatua stahiki”.

Aliongeza kuwa makubaliano hayo ni mwanzo mzuri wa kuweza kufanya kazi kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika mpaka wa Tunduma ambako mazao ya misitu na magogo toka nchini Zambia yamekuwa yakipitishwa kwenda bandari ya Dar es Salaam na baadae nje ya nchi.

Akizungumzia hatima ya magogo hayo Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mohammed Kilongo alisema kuwa “Wafanyabishara wote waliokamatwa na magogo haya wametakiwa kuleta vielelezo halali vya uvunaji na usafirishaji wake jambo ambalo wameshindwa kutekeleza mpaka sasa, muda tuliowapa ukiisha utaratibu wa kuwafungulia mashitaka utafuata ili sheria ichukue mkondo wake”.


No comments:

Post a Comment