Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Machi, 2016. Kulia ni Naibu Waziri Eng. Ramo Makani.
Sehemu ya waandishi wa habari na wajumbe mbalimbali walioshiriki Mkutano huo.
........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe
amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini, (TFS)
Bw. Juma Mgoo pamoja na Wakurugenzi wawili wa Taasisi hiyo ili kupisha
uchunguzi kutokana na mwenendo usioridhisha wa ukusanyaji wa maduhuri ya
Serikali na usimamizi mbovu wa rasilimali za misitu nchini.
Prof. Maghembe ametaja majina ya Wakurugenzi hao aliowasimamisha
kazi kuwa ni Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Bw. Zawadi Mbwambo pamoja na Kaimu
Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi endelevu ya Misitu, Bw. Nurdin Chamuya
Baada ya kuwasimamisha hao amewateua watu
wengine kushika nafasi zao wakati mchakato wa kuwapata watendaji wapya
ukifanyika na walioteuliwa kukaimu nafasi hizo ni Kaimu Mtendaji Mkuu TFS,
Gerald Kamwendo, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Misitu, Mwanaidi Kijazi, na Kaimu
Mkurugenzi wa Matumizi Rasilimali Misitu, Haji Mpya.
Wengine waliosimamishwa kazi
na kanda zao katika mabano ni Hubert Haule (Kusini), Bakari Rashid (Mashariki),
Cuthbert Mafipa (Kaskazini), Emmanuel Minja (Magharibi), Haji Khatibu (Ziwa) na
Bruno Mallya (Nyanda za Juu Kusini).
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Prof.
Maghembe amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini mapungufu mbalimbali
katika ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali na usimamizi usioridhisha wa
rasilimali za misitu.
Alisema kuwa hivi karibuni
walibaini shehena kubwa za magogo aina ya mninga katika Mkoa wa Rukwa wilayani
Kalambo yakiwa yamekatwa na kuwekwa ndani ya makontena ndani ya msitu pamoja na
kutengenezewa nyaraka feki zinazoonesha magogo hayo yanatoka nchini Zambia
tayari kwa kusafirishwa kupelekwa nchini China.
Amesema kuwa baada ya kubaini tukio hilo na kulitolea maamuzi alipata
taarifa kuwa shehena ya Magogo hayo yenye thamani ya shilingi milioni 500 za
Kitanzania yaliyotakiwa kupelekwa Makao makuu ya Wilaya ya Kalambo yamemwagiwa
petroli na kuchomwa moto wakati wiki mbili kabla alishatoa agizo la magogo hayo
kusafirishwa kupelekwa Matai ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo.
Aliongeza kuwa kumekuwa na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa
ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika
Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.
“Pesa zitokanazo na makusanyo hayo zimekuwa hazipelekwi benki
kwa wakati na hata zikipelekwa benki zimekuwa zikipelekwa pungufu na muda
mwingine pesa hizo zimekuwa hazipelekwi kabisa”. Alisema Prof. Maghembe.
Katika tukio lingine, Waziri Maghembe amemsimamisha kazi
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dkt. Charles
Mulokozi kwa kosa la kukaidi agizo la kusaini vibali vya kusafirisha
Wanyamapori nje ya nchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya
kukamatwa watu katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro wakitaka
kusafirisha nyani 61 “velvety monkeys” na kubaini kuwa Idara ya Wanyamapori
ndio iliyotoa vibali vya kusafirisha nyani hao na vibali hivyo kusainiwa na
Mkurugenzi huyo.
Alisema watu hao kutoka Ulaya
Mashariki na washirika wao wa hapa nchini, walikodisha ndege ili kuwaondoa
tumbili hao kwenda Ulaya Mashariki. Alisema harakati za kukamata tumbili hao
porini zilianza wiki iliyopita na jumla ya idadi yao ni 450 ilhali kuna taasisi
zinazolinda hayo mapori bila walinzi wa mapori hayo kujua
Prof. Maghembe alisema nyani hao
walikamatwa maeneo ya Upareni, Hanang Manyara na Kiliamanjaro ambapo aliwaita
wasimamizi na kuwapa taarifa juu ya watu hao na kuwakataza kutotoa kibali
chochote cha kusafirisha wanyama hao.
“Nikiwa Moshi katika Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa nilimuita Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori Matumizi
Endelevu, Dk Charles Mulokozi na kumuarifu juu ya kamata kamata hiyo na
kumuagiza kutotoa kibali cha kusafirisha wanyama ili tuwakamate watu hao,
lakini baadaye tukagundua yeye ndio amesaini kibali hicho kutoka Dar es
Salaam,” alisema Maghembe.
Ameongeza kuwa ndege iliyokamatwa ilikuwa imekodiwa kutoka Afrika ya Kusini kwa
ajili ya kusafirisha nyani hao kwenda Ulaya ya Mashariki, Ndege hiyo imeshikiliwa
pamoja na rubani wake kwa mahojiano zaidi.
Prof. Maghembe ametoa onyo kali kwa wale wote wanaohujumu
rasilimali za nchi na kusema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali.
“Hatutasita kumfukuza kazi mtu yeyote ambaye atashiriki katika
suala hili la kuiibia nchi mali zake au anakaa anaangalia kando wakati fedha za
nchi, mali za nchi zinaporwa” Alisema Prof. Maghembe kwa ukali.
No comments:
Post a Comment