Waziri wa Maliasili
Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Ushirikiano wa
Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd
Muller alipowasili katika uwanja mdogo wa ndege wa Matambwe uliopo ndani ya
Hifadhi ya akiba ya Selous Mkoani Morogoro kwa ajili ya hafla ya makabidhiano
ya ndege maalum aina ya Husky A-1C kutoka Serikali ya Ujerumani itakayosaidia kufanya
doria za kupambana na ujangili katika hifadhi hiyo.
Waziri wa Maliasili
Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akizungumza na Waziri wa Ushirikiano wa
Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd
Muller (kushoto) katika hafla fupi ya makabidhiano ya msaada wa ndege
maalum aina ya Husky A-1C kutoka Serikali ya Ujerumani itakayosaidia kufanya doria
za kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous. Wengine ni Meneja
wa Hifadhi ya Selous Bw. Mabula Misungwi (wa pili kushoto), Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania Bw. Martin Laibooki (wa pili kulia) na
Bw. David Kanyatta Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Wanyamapori.
Waziri wa Maliasili
Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa ndege
maalum kutoka Serikali ya Ujerumani aina ya Husky A-1C kwa ajili ya kufanya
doria za kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous. Kutoka
kushoto ni Balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe. Egon Konchanke, Waziri wa
Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani
Dkt. Gerd Muller, Dkt. Christof Schenck Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Maendeleo la Uhifadhi la Kimataifa la FZS na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania Bw. Martin Laibooki.
Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller akizungumza katika hafla hiyo.
Waziri wa
Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani
Dkt. Gerd Muller (wa pili kushoto) akimkabidhi Waziri wa Maliasili Prof.
Jumanne Maghembe msaada wa ndege maalum aina ya Husky A-1C kwa ajili ya kufanya
doria za kupambana ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous. Wanaoshuhudia
Kulia ni Rubani wa Ndege hiyo Capt. Bernard Shayo, Dkt. Christof Schenck
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Uhifadhi la Kimataifa la FZS (wa
pili kulia) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA)
Bw. Martin Laibooki.
Waziri wa Maliasili
Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akifanya majaribio ya kupanda ndege maalum
aina ya Husky A-1C iliyotolewa na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kufanya
doria za kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya Selous. Wanaoshuhudia
ni Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya
Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller (wa pili kushoto), Capt. Bernard Shayo
(kulia), Bw. David Kanyatta Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Wanyamapori
(kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania Bw.
Martin Laibooki (wa tatu kushoto).
Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller akiwa na baadhi ya askari wa Wanyamapori katika Hifadhi ya Akiba ya Selous.
Waziri wa Maliasili
Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akiwasalimia askari wa Wanyamapori katika
Hifadhi ya Akiba ya Selous. Kulia anayeshuhudia ni Waziri wa Ushirikiano
wa Kiuchumi na Maendeleo kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd
Muller ambaye amemkabidhi Prof. Maghembe msaada wa ndege maalum aina ya Husky
A-1C ya kufanya doria za kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Akiba ya
Selous.
Sehemu ya kundi la Swala katika hifadhi ya akiba ya Selous.
Moja ya Twiga akiwa anakimbia katika hifadhi ya akiba ya Selous.
Sehemu ya wajumbe wa msafara wa Waziri Maghembe na Waziri wa Muller wakibadilishana mawazo katika hifadhi ya akiba ya Selous.
..............................................................
Serikali ya Ujerumani
imetoa msaada wa ndege maalum aina ya “Husky A-1C Aircraft” kwa Serikali ya
Tanzania kupitia Wizara ya Malisili na Utalii kwa ajili ya kusaidia katika doria
za kupambana na Ujangili katika Pori la Akiba la Selous.
Msaada huo wenye thamani
ya Euro 200,000 sawa na Tsh. 498,292,000, umekabidhiwa kwa Mhe. Waziri wa
Maliasili Prof. Jumanne Maghembe na Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na
Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani Dkt. Gerd Muller katika hafla
fupi iliyofanyika Matambwe ndani ya pori la Akiba la Selous.
Hafla hiyo
ilihudhuriwa na Maafisa wa Ubalozi wa Ujerumani hapa nchini wakiongozwa na
Balozi Mhe. Egon Konchanke, viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na
Utalii, Mamlaka ya Wanyamapori
Tanzania (TAWA), Mashirika ya Maendeleo ya Kimataifa ya FZS, WWF, GIZ na KFW.
Akizungumza katika
hafla hiyo Waziri Maghembe amesema ndege hiyo itasaidia jitihada za Serikali za
kupambana na Ujangili kwa kufanya doria katika anga ya hifadhi ya Akiba ya Selous
na kusaidia kutoa taarifa za kiuhalifu pale itakapobainika na kuchukuliwa hatua
stahiki za kukabiliana na uhalifu huo.
“Ndege hii
tunayoshuhudia mapokezi yake leo ni ukombozi kwa Wanyamapori katika Pori hili
la Akiba la Selous kwani itasaidia na kuimarisha doria za kupambana na ujangili
ndani na kuzunguka eneo zima la hifadhi”. Alisema Prof. Maghembe.
Waziri Maghembe
ameishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia kwa Waziri Muller kwa msaada huo na
mingine ambayo wamekuwa wakiitoa kusaidia uhifadhi wa Wanamapori hapa nchini, Amebainisha
kuwa misaada hiyo imekuwa na tija kubwa katika kuendeleza uhifadhi wa
Wanyamapori ikilinganishwa na kipindi cha nyuma kabla ya kuwepo kwa misaada
hiyo.
Waziri Maghembe
alieleza kuwa sera ya Wanyamapori Tanzania inatambua ushirikiano wa wahisani na
watu binafsi katika kuisaidia Serikali Kifedha na Kitaaluma kwenye eneo la
uhifadhi, hivyo amewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuipa ushirikiano Serikali
katika jitihada zake za kuendeleza Uhifadhi wa Wanyamapori nchini.
Kwa upande wake
Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani Dkt. Gerd Muller alimueleza
Prof. Maghembe kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika
kuendeleza uhifadhi hapa nchini. Waziri huyo pia aliwapongeza Askari wa Wanyamapori
kwa kazi nzuri wanayofanya ya kulinda Wanyamapori katika mazingira magumu ya
porini.
Akizungumza kwa lugha
ya Kijerumani huku ikitafsiriwa kwa Kiingereza na Mkalimani wake Dkt. Muller alisema
ipo haja kubwa ya kuendelea kuwalinda Wanyamapori kwa nguvu zote kwa kuwa hawana
hatia na kwamba walikuwepo katika mazingira yao ya asili kabla hata ya binadamu
kuwepo hapo.
“Hawa viumbe hai
wanaowindwa walikuwepo katika mazingira haya kabla ya sisi binadamu kuja hapa,
Sote tunahitaji kuwalinda na kuishi kwa amani na viumbe hawa ndio kutakuwa na
amani duniani kote” Alieleza Dkt. Muller.
Mapema akizungumza
kabla ya tukio la kukabidhiwa ndege, Meneja wa Pori hilo la Akiba la Selous Bw.
Mabula Misungwi alieleza baadhi ya changamoto kuu zinazoikabili hifadhi hiyo
kuwa ni ujangili, miundombinu mibovu ya barabara kwa ajili ya doria na vifaa
ikiwemo magari ya doria.
Msafara wa Waziri
Maghembe na ugeni wake kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani walipata
fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi ya Selous ikiwemo Matambwe na
Behobeho ambayo inajulikana kama Serengeti ndogo na kujionea Wanyamapori
mbalimbali wakiwemo Tembo, Twiga, Pundamilia, Swala, Nyani, Ngiri, Nyumbu na
mandhari mazuri ya mto behobeho.
Pori la Akiba la Selous
ni moja ya Pori kubwa duniani ikiwa na ukubwa wa zaidi ya Kilomita za mraba
50,000. Pori hili lipo ndani ya Mikoa mitano ya Tanzania ambayo ni Pwani,
Morogoro, Lindi, Mtwara na Songea. Pori hili limeathiriwa kwa kiasi kikubwa na
ujangili kwani katika Sensa ya mwaka 2013 ilionesha idadi ya tembo katika
pori hilo kuwa 13,000 idadi ambayo ni ndogo sana ikilinganishwa na ile ya
mwaka 2003 ambayo ilikuwa 70,000.
No comments:
Post a Comment