Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe.Constantine Kanyasu ametoa muda wa miezi mitatu kwa wananchi waliovamia na
kuanzisha shughuli za kibinadamu ndani ya Shamba la miti la Biharamulo kuondoka
mara moja kwa hiari yao bila shuruti kabla ya mwezi Juni mwaka huu.
Ametoa muda huo ili wananchi waliolima
mazao mbalimbali yakiwemo mahindi
na pamba waweze kuvuna mazao yao kabla ya kuanza kwa oparesheni maalum ya
kuwaondoa, iliyopangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu
itakayofanywa na Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania ( TFS) kwa kushirikiana na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo.
Mhe.Kanyasu ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya
kikazi ya kutembelea shamba la miti
Biharamulo lililopo katika wilaya ya Chato mkoani Geita.
Amesema Oparesheni hiyo haitasubiri
taarifa ya Wizara tano inayoendelea kufanyiwa kazi kwa kuwa eneo hilo
halihusiani na vile vijiji 366
vilivyokutwa ndani ya Hifadhi.
Amesema haiwezekani wananchi waliovamia eneo hilo
waendelee kuachwa kwa kisingizio cha Kauli ya Rais aliyoitoa Januari 15 mwaka
huu kuhusiana na vijiji 366 vilivyokutwa ndani ya maeneo ya Hifadhi.
Amebainisha kuwa wananchi waliovamia
eneo hilo wameitafsiri visivyo Kauli hiyo na kuongeza kuwa baada tu ya tamko la
Mhe. Rais , baadhi ya wananchi hata wale waliokuwa wakiishi katika maeneo mengine nje ya hifadhi
waliendelea kuvamia na kuanza
kujimilikishia maeneo makubwa wakidai kuhalalishwa na tamko la Rais.
Amefafanua kuwa taarifa inayoendelea
kufanyiwa kazi na timu ya Mawaziri na
Makatibu Wakuu kutoka Wizara tano imebainisha kuwa mpaka sasa zaidi ya vijiji
700 vimekutwa ndani ya Hifadhi badala 366 vilivyoripotiwa awali.
Kufuatia hali hiyo amesema baadhi ya
wavamizi wa Hifadhi katika maeneo mbalimbali wataendelea kuondolewa bila
kusubili kukamilika kwa zoezi linaloendelea kwa kuwa walieendelea kuvamia
maeneo ya Hifadhi kwa kisingizio cha tamko la Rais huku maeneo hayo yakizidi
kuharibiwa kwa miti kukatwa na shughuli nyingi za kibinadamu
Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu
ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) kutenga Bajeti ya
kugharamia operesheni ya kuwaondoa
wavamizi ndani ya Shamba hilo.
Ameitaka TFS kuendesha oparesheni za
mara kwa mara ili wavamizi hao wajue Serikali ipo kazini kulinda rasilimali za
Taifa muda wote.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mtemi Simeoni akizungumza katika ziara
hiyo alisema kuwa baadhi ya wananchi kutoka nje ya wilaya hiyo
wamekua wakivamia na kuanzisha shughuli za kibinadamu ndani ya Shamba hilo,
suala ambalo ni kinyume cha sheria.
Mkuu huyo wa wilaya amebainisha kuwa
wananchi katika maenro hayo wana mahitaji makubwa ardhi na kuiomba Wizara
iangalie namna ya kuwasaidia hekari 5000 ili wapate maeneo ya kulima na kuchungia
mifugo yao.
Kwa upande wake Meneja wa Shamba hilo
Bw. Thadeus Shirima amemweleza Naibu
Waziri huyo kuwa hadi sasa zaidi ya hekari 900 zimepandwa miti licha ya Shamba
hilo kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi pamoja na
vitendea kazi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Mtemi Simeoni (kushoto) alipotembelea Shamba la Miti la Biharamulo mara baada ya kukagua maendeleo ya miti iliyopandwa katika shamba hilo kwa ukubwa hekari 900 katika wilaya ya Chato mkoani Geita. Wengine ni watumishi pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungumza na wananchi pamoja na watumishi wa shamba la miti la Biharamulo ambalo mara baada ya kukamilika kwa kupandwa miti katika eneo lote litakuwa ndio shamba la pili kwa ukubwa kati ya mashamba 20 yanayomilikiwa na Wakala wa Hudumza Misitu Tanzania lililopo wilayani Chato mkoani Kagera.
Mkuu wa wilaya ya Chato, Mhe. Mtemi Simeon akipanda mti wakati alipotembelea Shamba la Miti la Biharamulo mara baada ya kukagua maendeleo ya miti iliyopandwa katika shamba hilo lenye ukubwa wa hekari 900 katika wilaya ya Chato mkoani Geita
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa wilaya na watumishi wa Shamba la Miti la Biharamulo lililopo katika wilaya ya Chato mkoani Geita.
.Baadhi ya watumishi wa Shamba la Miti
la Biharamulo wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii
wakati Naibu Waziri huyo alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika shamaba
hilo hukuakiwasisitizan umuhimu wa kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi wanaoishi
karibu na shamba hilo.
No comments:
Post a Comment