Katibu Mkuu Wizara ya
Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi ametoa wito kwa wadau wa
uhifadhi nchini kukemea kwa nguvu zote tabia ya uingizaji wa mifugo ndani ya
hifadhi za Misitu na Wanyamapori nchini kwakuwa kufanya hivyo ni kinyume cha
sheria za nchi na kunahatarisha ustawi wa hifadhi hizo ambazo ni muhimu kiikolojia
na uchumi na wa taifa.
Milanzi ametoa wito
huo juzi wakati akifunga mafunzo maalum ya kijeshi katika kituo cha Mlele ndani
ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi, Mkoani Katavi kwa Mameneja wa Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro na Askari wa TANAPA kwa ajili kubadilisha mfumo wa utendaji katika
taasisi hizo kutoka wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu (paramilitary) kuboresha
utendaji wao wa kazi.
“Mifugo katika
hifadhi zetu sio sahihi ni kinyume kabisa cha sheria za nchi, endeleeni kulikemea
hili, tusipige siasa kufurahishana kwakua madhara yake ni mengi ikiwemo
uharibifu wa vyanzo vya maji, muingiliano wa magonjwa baina ya mifugo na
wanyamapori na kuharibu ubora wa vivutio vyetu” Alisema Milanzi.
Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka
2009 Ibara ya 18 (2) inakataza kabisa kuingiza mifugo ndani ya hifadhi, Sheria
hiyo inasema “Si ruhusa mtu yeyote kuingia na kulisha mifugo ndani ya Mapori ya
Akiba, Mapori Tengefu na Ardhioevu”.
Milanzi alisema kuwa hifadhi za taifa
nchini zina umuhifu mkubwa kwa uchumi wa taifa kwakuwa kupitia utalii
zinachangia asilimia 17.5 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya
fedha za nje (foreign currency). Aidha sekta hiyo inatoa ajira zaidi ya
milioni moja na nusu kupitia huduma za kitalii nchini.
Mbali na faida za kiuchumi hifadhi hizo pia
zina faida nyingi za kiikolojia ambazo ni uhifadhi wa vyanzo vya maji, kusaidia
upatikanaji wa mvua na hewa safi kwa viumbe hai ikiwemo binaadamu. Alisema
kuharibu hifadhi hizo kwa kulisha mifugo ndani yake ni jambo ambalo
halikubaliki kwa kuwa ni kuhatarisha pia maisha ya binaadamu ambayo yanategemea
hifadhi hizo.
Alieleza kuwa Serikali inaenda kulifanyia
kazi tatizo hilo pamoja na migogoro mingine ya ardhi kwa ajili ya kuyatafutia
suluhu kwa kushirikisha Wizara zinazohusika ambazo ni Ardhi, Kilimo na Mifugo,
Sheria na Katiba, Tamisemi, Maliasili na Utalii na Ofisi ya Makamu wa Rais
Mazingira.
Akizungumza na wahitimu wa mafunzo hayo, Milanzi
alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uadilifu, nidhamu, ujasiri, uaminifu
na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa muda mfupi na hivyo kuwataka kuyatumia
kuongeza ufanisi katika kulinda maliasili zilizopo kwenye maeneo yao.
Aliwataka pia wahitimu hao kutafsiri
mafunzo hayo na maendeleo ya sekta ya uhifadhi nchini na kuliongezea taifa
mapato kwa kuboresha huduma za utalii, kubuni bidhaa mpya za utalii na
kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Alan Kijazi aliwataka wahitimu
hao kutumia mafunzo waliyoyapata kuziba mianya yote ya ujangili na kwamba jamii
inategemea kuona kazi hiyo kwa vitendo.
Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa
na UNDP kupitia mradi wa “Spanest” yalifanyika kuanzia tarehe 15 Julai hadi
tarehe 13 Agosti, 2016 kwa kuwahusisha washiriki 69 kutoka Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro na Tanapa. Mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwa awamu yanatemewa
kuhusisha taasisi zote za uhifadhi wa wanyamapori nchini kuelekea kwenye
mabadiliko ya muundo wa utendaji kazi kutoka mfumo wa Kiraia kwenda mfumo wa Jeshi Usu (Paramilitary).
No comments:
Post a Comment