Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi
Kigwangalla (kulia) akizungumza na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka
Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya
kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya
nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini.
Na Hamza Temba - Dodoma
..............................................................
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Dk. Hamisi Kigwangalla ameipongeza Serikali ya Finland kwa ushirikiano na
misaada mbalimbali ambayo imekuwa ikiitoa kuunga mkono juhudi za Serikali
katika uhifadhi wa maliasili na uendelezaji wa misitu nchini.
Dk. Kigwangalla ametoa pongezi
hizo leo Januari 16, 2018 kwa Balozi wa nchi hiyo hapa nchini, Mhe. Peka Huka
ambaye amemtembelea ofisini kwake mjini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha na
kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo katika
uhifadhi na maendeleo ya misitu nchini.
“Napenda kutoa pongezi zangu za
dhati kwa Serikali ya Finland, mmekuwa washirika
wetu wakubwa wa maendeleo kwa muda mrefu ambao mmetusaidia mambo mbalimbali
ikiwemo kuendeleza misitu nchini, kuendeleza Chuo cha Mafunzo ya Misitu
Olmotonyi na hata mapitio ya Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998, ni
matumaini yetu kuwa mtaendelea kudumisha ushirikiano huu”, alisema Dk.
Kigwangalla.
Alimueleza balozi huyo kuwa
Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika uhifadhi wa misitu nchini
ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha na teknolojia kwa ajili ya kuwezesha uhifadhi
endelevu. Alisema changamoto nyingine ni uvunaji haramu wa mazao ya misitu ambayo
husababisha eneo la hekta 372,000 za misitu kupotea kila mwaka.
Alisema mbali na nguvu kubwa
inayotumiwa na Serikali katika udhibiti wa uvunaji holela wa mazao ya misitu Wizara
yake kwa kushirikiana na taasisi zilizoko chini yake inaendelea kuweka mikakati
thabiti kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kiserikali kwa ajili ya kutafuta
nishati mbadala pamoja na kuanzisha mashamba kwa ajili ya uzalishaji wa miti ya
mkaa kwa njia endelevu.
Akizungumzia umuhimu wa misitu
nchini, Dk. Kigwangalla alisema takribani kila kitu hapa nchini kinategemea
uwepo wa misitu. Alisema zaidi ya asilimia 80 ya chanzo cha nishati ya umeme nchini
ni maji ambayo hutegemea uwepo wa misitu, alitaja pia kilimo na ufugaji ambao
pia hutegemea mvua na maji ambayo hutegemea pia uwepo wa misitu.
Kutokana na umuhimu huo, Dk.
Kigwangalla amemuomba Balozi huyo kuhamasisha wawekezaji wa Finland kuja kuwekeza Tanzania katika uzalishaji na
matumizi endelevu ya rasilimali za misitu nchini na kuahidi kuwapa ushirikiano.
Kwa upande wake Balozi Huka,
alimueleza Dk. Kigwangalla kuwa nchi yake imekua ikifadhili miradi mbali mbali
ya uendelezaji wa misitu katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo mikoa ya
nyanda za juu kusini na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo.
Alimueleza Waziri Kigwangalla
kuwa changamoto iliyopo ya uharibifu wa misitu nchini inahitaji uwepo wa
nishati mbadala ambayo mchakato wa upatikanaji wake unatakiwa kushirikisha
wadau na Mamlaka nyingine za Kiserikali ikiwemo Wizara ya Nishati.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi
Kigwangalla (kulia) akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka
ofisini kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya
kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya
nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini kwake mjini Dodoma leo alipotembelewa na balozi huyo kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo katika uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi
Kigwangalla (kulia) akimsikiliza Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka ofisini
kwake mjini Dodoma leo.
Balozi Peka Huka akimsikiliza Waziri Kigwangalla katika kikao hicho.
Waziri Kigwangalla akifafanua jambo kwa Balozi Peka Huka (hayuko pichani) katika kikao hicho mapema leo mjini Dodoma.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi
Kigwangalla (kulia) akimuaga Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Peka Huka baada ya mazungumzo ofisini
kwake leo mjini Dodoma .
No comments:
Post a Comment