Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akipata maelezo ya eneo la kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha ambacho kimevamiwa na watu mbalimbali na kuanzishwa makazi yenye kaya 82 ndani ya eneo hilo kutoka Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Dk. Fredy Manongi (katikati). Eneo hilo ni mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na hati halisi ya eneo hilo ipo kwa jinala Bodi ya Utalii Tanzania.
Na Mwandishi Wetu
........................................................
Waziri
wa Malisili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla leo Januari 28, 2018 amekagua
eneo la kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha ambacho ni
mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kinachodaiwa kumegwa na
kuuzwa kinyume cha sheria kwa watu mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu
ambaye hata hivyo hakumtaja jina lake.
Akiwa
katika eneo hilo, Waziri Kigwangalla amepokea taarifa kutoka kwa Meneja wa Huduma
za Sheria wa mamlaka hiyo, Egidius Mweyunge ambaye alieleza kuwa, jumla ya hekta
20 (ekari 40) za eneo zilinunuliwa na mamlaka hiyo na kulipiwa Shilingi bilioni
1.8 kwa kamishna wa ardhi Mwaka, 2006 baada ya kuona tangazo la kuuzwa kwa eneo
hilo kupitia gazeti la Serikali.
Alisema
hata hivyo baada ya manunuzi hayo, Halmashauri ya Manispaa ya Arusha iliingilia na kumega
hekta 10 (ekari 20) ambazo waliuziwa watu mbalimbali ambapo hadi hivi sasa eneo
hilo lina kaya 83 zinazoishi watu.
"Mwaka
2016, tulipokagua eneo hili, tulibaini ni hekta 10 tu zilizobaki kutoka zile
20, na tulipouliza Halmashauri ya Manispaa ya Arusha walisema eneo ili liligawanywa toka 1996
na kupewa Kaya hizo 83. Lakini kwa upande wa Kamishna wa Ardhi, kule Moshi
Title iliyopo ni moja tu, tukajikuta kumbe kitu tulichokinunua hakikuwa ekari
40, ni ekari 20 tu na hapo ndipo tuliporejea kwenye mgogoro", alisema
Mweyunge.
Hata
hivyo, Waziri Kigwangalla alieleza kuwa hapo hakuna mgogoro na zaidi ni kutaka
kujua hao waliochukua hizo hekta 10, ni akina nani na walizipata kwa nani
kupitia utaratibu gani.
"Hapa
hakuna kumukunya maneno. hao wote hati zao ni feki na hazina msingi wowote kama
Kamishna anatambua hati yenu, hao wengine wapishe na waende wakamdai huyo
aliyewauzia hayo maeneo.
“Eneo
hili lirudi kwa Mamlaka ya Ngorongoro na Bodi ya Utalii wao watatafutiwa eneo
jingine. Watu hao kwenye hizo kaya 83 waliochukua hizo hekta 10, waende
wakamdai aliyewapa hizo Hati kwa hiyo sisi hatuna mgogoro wowote kwakuwa hakuna
mamlaka nyingine inayoweza kutoa hati zaidi ya Kamishna wa Ardhi. Hao
Halmashauri hawana mamlaka ya kutoa hati kwa mtu kama si Kamishina wa Kanda
kule Moshi" alieleza Dk. Kigwangalla.
Aidha,
Dk.Kigwangalla aliwataka wote waliojenga eneo hilo wakadai fidia kwa halmashauri
husika kwani mwenye mamlaka ya kutoa hati ni Kamishna wa Ardhi na si halmashauri.
Alisemwa kwa taarifa ambazo hazijathibitishwa eneo hilo waligawana Mawaziri wastaafu
ambao walitumia mamlaka zao vibaya wakiwa madarakani na maafisa wa mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro kwa kushirikiana na halmashauri kufoji hati.
Akijibu
maswali ya waandishi wa Habari waliokuwa wakitaka kujua ni Mawaziri gani hao,
Waziri Dk. Kigwangalla amesema kuwa, ametoa wito kwa wote waliuziwa maeneo hayo
kupeleka hati zao kwa Kamishina wa Ardhi na hapo watabainika majina yao na
watachukuliwa hatua kama watenda makosa wengine.
Kabla
ya kununuliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kiwanja hicho kilikuwa
kinamilikiwa na taasisi ya Serikali ambayo ni kampuni tanzu ya Bodi ya Utalii
Tanzania iliyokuwa inajulikana kama Serengeti Safari Lodges.
Hivi
karibuni, Waziri huyo akiwa Mjini Dodoma, alitoa ilani ya siku 30 kwa mtu
yeyote ambaye anamiliki kiwanja ndani ya eneo hilo kufika kwa Kamishina Mkuu wa
Ardhi waweze kuhakikiwa na kuthibitisha umiliki wao halali ama sivyo
wavirejeshe Serikalini viweze kumilikishwa kwa mmiliki wake halali.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua eneo la kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini Arusha ambacho kimevamiwa na watu mbalimbali na kuanzishwa makazi yenye kaya 82. Eneo hilo ni mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na hati halisi ya eneo hilo ipo kwa jinala Bodi ya Utalii Tanzania.
Meneja wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Egidius Mweyunge (kulia) akimuongoza Waziri Kigwangalla kukagua eneo hilo.
Dk. Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua eneo hilo.
No comments:
Post a Comment