Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara hiyo Mjini Dodoma leo. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Aloyce Nzuki.
Na Hamza Temba - Dodoma
.........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii,
Dk. Hamisi Kigwangalla leo Januari 25, 2018 mjini Dodoma ametaja majina ya
watuhumiwa wa ujangili ambao wengi wao ni wamiliki na washirika wa Kampuni za
uwindaji wa kitalii na kuwapa siku saba wawe wamefika kwa hiari yao wenyewe
katika ofisi za Wizara hiyo Mjini Dodoma, Swagaswaga House kwa ajili kutoa
maelezo kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kujibu tuhuma hiyo na nyingine
nyingi zinazowakabili mbele ya kamati atakayoiunda.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Dk. Kigwangalla ametaja baadhi ya tuhuma hizo ambazo ziko kinyume cha sheria na taratibu za uwindaji wa kitalii kuwa ni uwindaji
haramu, uhawilishaji wa umiliki wa vitalu vya uwindaji pasipo kufuata sheria, udanganyifu
kwenye kujaza fomu za uangalizi, rushwa,
uhalifu dhidi ya rasilimali za wanyamapori na uhujumu uchumi.
Alitaja tuhuma zingine kuwa ni
ukiukwaji wa kanuni za uwindaji (kupiga wanyama usiku, kuwinda wanyama bila
kujali umri, kupiga wanyama nje ya maeneo waliyopewa), kukutolipa tozo
mbalimbali za maendeleo za jamii kwenye vijiji jirani na maeneo wanaoendesha
biashara ya uwindaji, kushindwa kuendesha ipasavyo shughuli za kuzuia ujangili.
Dk. Kigwangalla aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni ndugu Pasanis na wenzake ambao wanamilikia
kampuni ya Berlette Safari Corporation Ltd na Ngugu Shein Ralgi na wakurugenzi
wenzake wa kampuni ya Game Frontiers of Tanzania Ltd.
Wengine ni Ndugu Howel na wakurugenzi wenzake wa kampuni ya
Mkwawa Hunting Sfaris Tanzania Ltd, Ndugu Thomas Fredikin na wenzake wa Kampuni
ya Mwiba Holdings Ltd, Wengert Windrose Safaris Tanzania Ltd na Tanzania Game Trackers Safaris Ltd, na
Ndugu Awadh na wenzake ambao wanamiliki kampuni ya Uwindaji wa Greenmiles
Safaris Ltd.
Aliwataja washirika wengine kuwa ni Ndugu ni Kwizema, Ndugu
Robert, Ndugu Solomon Makulu, Ndugu Siasa Shaban, Ndugu Hamis Abdul Ligagabile na
mtumishi wa Wizara Wizara ya Maliasili na Utalii, Alex Aguma.
Katika hatua nyingine Dk.
Kigwangalla ametoa Ilani ya siku 30 kwa watu mbalimbali ikiwemo Mawaziri Wakuu
Wastaafu waliovamia kiwanja chenye hati namba 4091 kilichopo Njiro Jijini
Arusha wafike kwa Kamishna Mkuu wa Ardhi waweze kuhakikiwa na kuthibitisha
umiliki wao halali ama sivyo wavirejeshe Serikalini viweze kumilikishwa kwa mmiliki
wake halali.
“Natoa ilani ya siku 30 kwa mtu
yeyote ambaye anajua alivamia kiwanja katika eneo hili ambalo lina hati namba
4091 kilichopo Njiro, Arusha, haraka sana ajipange kupeleka taarifa zake mbele
ya Kamishna wa Ardhi kabla hatujachukua hatua nyingine za kisheria, hati
iliyoko pale ipo katika jina la Bodi ya Utalii Tanzania japo wao wanadai wana
hati nyingine.
“Wengi wao wamejenga nyumba za
kudumu katika eneo lile, na wengine ni viongozi waliokuwa mawaziri wakuu
wastaafu nao wana viwanja katika eneo hilo na wamejenga nyumba zao katika eneo
hilo,” alisema Dk. Kigwangalla.
Alisema kiwanja hicho kilichokuwa
na ekari zaidi ya 40 kilikuwa kinamilikiwa na taasisi ya Serikali ambayo ni kampuni
tanzu ya Bodi ya Utalii Tanzania iliyokuwa inajulikana kama Serengeti Safari
Lodges na baadae kikauzwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla
ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi nchini kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa
wanne wanaojihusisha na mtandao wa ujangili pamoja na kupanga njama zilizopelekea
mauaji ya Mhifadhi wa Wanyamapori Ndugu Wayne Lotter, raia wa Afrika ya Kusini ambaye
alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni Pams Foundation, aliyeuawawa eneo la Chole Masaki
Jijini Dar es Salaam mwezi Agosti mwaka jana.
“Natoa siku saba kwa wenzetu wa
jeshi la Polisi wachukue hatua dhidi ya watu wanne, ambao mimi majina yao
ninayafahamu ambao miongoni mwao watatu wanahusika na kuendesha biashara ya
ujangili, na ni watu wakubwa, ni matajiri wakubwa na wana mitandao mikubwa ya
ujangili.
“Ninafahamu taarifa hizi polisi
wanazo lakini hawajachukua hatua za kuwakamata watu hawa na kuwafikisha kwenye
macho ya sheria, muda ni mrefu na sisi
wenye taarifa hizi sasa tumeanza kuchoka kusubiri.
“Hawa watu wanne walihusika kupanga njama ambazo zilipelekea
kusababisha mauaji ya kikatili ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Palm Foundation,
Ndugu Wayle Lotter mwezi Agosti mwaka jana eneo la Chole Masaki mwezi Agosti
mwaka jana.
“Nataka ndani ya siku hizi saba wawe wamechukua hatua na
kama hawatochukua hatua manaake tutajua wana vested interest (maslahi) kwahivo
tutaenda kuripoti kwa Amiri Jeshi mkuu ambaye ni Mhe. Rais aliyetutuma kazi ya
kusimamia sekta hii,”. Alisema Dk. Kigwangalla.
Dk. Kigwangalla akizungumza katika mkutano huo leo mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment