Serikali imepata mapato
ya Shilingi Milioni 30.9 kupitia mauzo meno ya viboko vipande 12,467 vyenye
uzito wa kilo 3,580.29 ambayo yameuzwa kupitia mnada wa hadhara uliofanyika
katika ofisi ndogo za Wizara ya Maliasili na Utalii katika Jengo la Mpingo
Jijini Dar es Salaam.
Mnada huo ulioratibiwa
na Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango ulijumuisha makampuni
19 yenye Leseni za Nyara Daraja la Kwanza ambapo kampuni ya On Tours Tanzania
Limited iliibuka mshindi kwa kutoa dau la Shilingi milioni 30.9.
Mwakilishi wa kampuni
hiyo, Grey Kilas alilipa asilimia 25 papo hapo kwa mujibu wa masharti ya mnada
huo na kuahidi kulipa asilimia 75 ya kiasi kilichobakia ndani ya siku 14 zijazo.
Kwa upande wake,
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA,
Mabula Misungwi alisema biashara hiyo haiwezi kuchochea ujangili kwa vile meno
hayo yanauzwa kwa wafanyabiashara maalum wenye leseni za nyara daraja la kwanza.
Mabula alisema meno hayo
yalianza kukusanywa tangu mwaka 2004 ambapo kipindi cha huko nyuma yalikuwa
yakiuzwa kwa makampuni yenye leseni za nyara kwa utarartibu tofauti na ulioanza
kutumika mwaka huu ambao ni kupitia mnada wa hadhara.
Naye Mwakilishi wa
Kampuni iliyonunua meno hayo, Grey Kilas aliwashukuru wasimamizi wa mnada huo kwa
kuuendesha kwa uwazi wa hali ya juu ambapo ulitoa fursa kwa kila mfanyanyabiashara
hatimaye ukamuwezesha kuibuka mshindi.
Akizungumzia kuhusu
soko, Kilas alisema meno hayo huuzwa nchini Japan, Marekani na Hongkong ambapo
hutumika kutengeneza mapambo, sanamu pamoja na vishikizo vya nguo.
Kwa mara mwisho biashara
hiyo ya kuuza meno ya viboko ilifanyika mwaka 2004.
No comments:
Post a Comment