Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Generali Gaudence Milanzi (kulia) akizungumza kwenye Mkutano wa Kamati ya Uwezeshaji Utalii (Tourism Facilitation Committee- TFC) uliofanyika hivi karibuni Mpingo House Jijini Dar es Salaam. Wapili kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utalii Leseni na ubora wa huduma Bw. Deogratius Mdamu.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi (kulia) akizungumza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya Wajumbe wa kamati ya Uwezeshaji Utalii (Tourism Facilitation Committee- TFC) ambao walikutana kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Utalii nchini kwa kutoa maoni, ushauri na ufumbuzi wa changamoto ikiwa na kuchangia mikakati mbalimbali itakayowezesha kusaidia kuhamasisha Utalii wa ndani.
.....................................................................................................
.....................................................................................................
Wizara ya
Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau wa utalii nchini, imejipanga
kuhakikisha inaendelea kukuza utalii wa ndani ambao utakua na uhakika zaidi wa
kuliingizia taifa mapato tofauti na hivi sasa ambapo utegemezi upo kwa watalii
kutoka nje ya nchi ambapo wakati mwingine hupelekea uhaba kutokana na athari za
majanga ya kimataifa.
Baadhi ya
Majanga hayo yaliyoathiri Sekta ya Utalii katika kipindi cha hivi karibuni ni
milipuko ya magonjwa kama Ebola, matukio ya Ugaidi nchini Kenya na kushuka kwa thamani
ya Euro ya Ulaya dhidi ya Dola ya Marekani.
Akizungumza
kwenye Mkutano wa Kamati ya Uwezeshaji Utalii ijulikanayo kama Tourism
Facilitation Committee (TFC) uliofanyika hivi karibuni Mpingo House jijini Dar
esSalaam, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja. Generali. Gaudence
Milanzi amesema maendeleo ya Utalii yanahitaji sana Utalii wa ndani kuimarika
badala ya kudhani kuwa vivutio vya utalii vilivyopo ni kwa ajili ya wageni
kutoka nchi za nje.
Meja Generali
Milanzi amesema Utalii ni sekta nyeti sana katika kuliingiza Taifa pesa za
kigeni lakini hata hivyo ni sekta ambayo imekuwa inaathirika kwa haraka sana
pindi majanga yanapotokea nchi jirani hivyo ni lazima jamii ijengewe utamaduni
wa kutembelea vivutio vya Utalii ili kuweza kujihakikishia Watalii wa ndani
wanakuwa wengi.
Baadhi ya
mikakati iliyopendekezwa na Wajumbe wa kamati ya Uwezeshaji Utalii (TFC) ni
kuwawezesha maafisa Utalii wa Halmashauri wanatengewa bajeti ya kutosha,
wanajengewa uwezo kuhusu ya vivutio vya utalii vilivyopo kwenye maeneo yao
pamoja na Idara ya Utalii kufungua ofisi kila kanda ili kuweza kutimiza majukumu
yake ipasavyo.
Mkakati
mwingine uliopendekezwa ni kwa viwanja vya ndege vilivyopo nchini kuimarishwa
ikiwa ni pamoja na nchi kuwa na ndege zake kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya
na Rwanda.
Awali, Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bi. Uzeeli Kiangi alisema Mkutano wa TFC hutoa
fursa ya kuibua na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Utalii
hivyo Sekta Binafsi zinawajibu mkubwa wa kuhakikisha changamoto zinazoikabili
sekta zinatafutiwa ufumbuzi
Aliongeza kuwa
Idara ya Utalii imekuwa ikishiriki katika maonesho mbalimbali ya kitaifa lengo
likiwa ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutembelea vivutio vya Utalii
nchini.
Mdau wa
Utalii, Prof Wineastor Anderson amesema sekta ya Utalii imekuwa ikikua lakini
si kwa kiwango cha kuridhisha hivyo jitihada za kutangaza utalii ndani na nje
nchi upewe uzito unaostahili kwa kuiwezesha Bodi ya Taifa ya Utalii kuwa na
bajeti ya kutosha kujitangaza ndani na nje ya nchi.
Wakati huo
huo, Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya Utalii Tanzania (TCT) Bw. Richard
Rugimbana, amesema Utalii wa ndani ili uweze kukua suala la elimu linahitajika
kutolewa ili kuweza kuibadilisha jamii ipende kutembelea vivutio vya Utalii vya
ndani ya nchi.
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi (ACP) Ndaki anayeshughulikia dawati la Utalii (Tourism
Police Unit) amewahakikishia usalama watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea
vivutio vya Utalii bila kuwa na hofu yoyote kwa kuwa Jeshi la Polisi nchini
lipo macho muda wote.
No comments:
Post a Comment