Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewataka
wananchi wafuate sheria kwa kujiepusha
kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya Hifadhi ili kujenga mahusiano mazuri
baina yao na Wahifadhi.
Pia, amewataka wananchi kuwachukulia Wahifadhi hao kama rafiki wa umma na watendaji waliotumwa
na Serikali kulinda Maliasili kwa niaba
yao.
Akizungumza na Watumishi
wa Pori la Akiba la Swagaswaga katika wilaya ya Chemba jijini Dodoma, Mhe. Kanyasu amesema Wahifadhi wamepewa
jukumu la kulinda hifadhi za Taifa na wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya kuifanya Tanzania
iendelee kuwa na maeneo mazuri yaliyohifadhiwa.
''Sisi ni wa moja hakuna haja ya
kujengeana uhasama kati yetu, Wananchi wafuate sheria za Uhifadhi na Wahifadhi fuateni sheria wakati
mnapokabaliana na Wananchi'' amesisitiza Kanyasu.
Amesema Wahifadhi wa Wanyamapori na
Misitu wanazilinda rasilimali hizo kwa ajili wote, vitu kama mvua, hali ya hewa
safi pamoja na mvua ni moja ya faida za moja kwa moja zinazopatikana kutokana
na maeneo yaliyohifadhiwa vizuri.
Amesema Wahifadhi hao wameajiriwa kwa
mujibu wa sheria hivyo hutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya kazi
zao na pale wanapokiuka sheria mamlaka zinazohusika huwachukulia hatua.
“Sisi kama Wizara tunaamini kwamba
wahifadhi wetu wanafanya kazi nzuri, pale ambapo wamekuwa wakilaumiwa kwa
kuwapiga na kuwanyanyasa watu kwa namna yoyote ile tumetuma Tume maalum
kuchunguza na kuchukua hatua” Amesema
Mhe, Kanyasu amesema uchunguzi
unapofanyika na ikathibitika kuwa tukio lililofanyika halikuongozwa na matumizi
ya sheria na kuwepo kwa haki wizara imekua ikichukua hatua.
Ameeeleza kuwa Wahifadhi ni watu
muhimu saba kwa vile bila wao hakuna uhifadhi unaoweza kuendelea nchini
akibainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakipinga juhudi za uhifadhi kwa
kuwatetea watu wanaovunja sheria.
Kuna watu wanatamani kuona misitu na wanyamapori wote tunawamaliza ili
wapate maeneo ya malisho na kilimo, Nawambieni tukithubutu kufanya hivyo huu
ndo utakuwa mwisho wetu wa maisha" Amesisitiza Mhe.Kanyasu
Amesema yapo madhara makubwa
yanayoweza kutokea kama hakutakuwa na uhifadhi imara ikiwemo maeneo mengi ya
nchi kugeuka kuwa jangwa kutokana na uharibifu wa misitu, ukosefu wa mvua,
ukosefu wa maji, chakula na ukosefu wa hewa safi.
Kwa upande wake, Meneja wa Pori la
Akiba la Swagaswaga, Alex Choya amesema
kuwa kumekuwa na tuhuma za vitendo vya ukatili dhidi ya raia vinavyofanywa na
baadhi ya askari wa hifadhi za Taifa na kutoa wito kwa wananchi wote wenye
ushahidi na taarifa juu ya vitendo hivyo kuziwasilisha ili hatua stahiki
zichukuliwe.
Amesisitiza kuwa Mamlaka ya Usimamizi
wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) hairuhusu askari kufanya vitendo vya ukatili na
unyanyasaji dhidi ya raia badala yake imekua ikiwahamasisha wananchi kushiriki
kikamilifu katika ulinzi wa rasilimali zinazowazunguka.
Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungumza na watumishi wa Pori la Akiba la
Swagaswaga mara baada ya kutembelea michoro ya mapangoni iliyochorwa zaidi ya
miaka 1000 na kabila la Wasandawe katika
wilaya ya Chemba mkoani Dodoma
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (wa tatu ) akiangalia baadhi michoro ya mapangoni iliyochorwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita na kabila la Wasandawe ambayo ni miongoni mwa vivutio vya Utalii katika ziara yake ya kikazi wilayani Chemba jijini Dodoma. Wa kwanza kulia ni Meneja wa Pori hilo, Alex Choya.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu (wa tatu) akiwa na baadhi ya watumishi wa Pori la Akiba la SwagaSwaga wakitoka kuangalia michoro ya miambani ambayo imechorwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita
Baadhi ya watumishi wa Pori la Akiba la SwagaSwaga wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe, Constantine Kanyasu wakati alipokuwa akizungumza nao.
Meneja wa Pori la SwagaSwaga , Alex Choya akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe, Constantine Kanyasu, Kushoto ni Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)