slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Thursday, April 12, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA AFUNGUA MKUTANO WA SITA WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU TANZANIA MJINI DODOMA LEO

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akishiriki kuimba wimbo wa mshikamano wa wafanyakazi wakati wa mkutano wa sita wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Huduma za Misitu TFS uliofanyika leo mjini Dodoma. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Aloyce Nzuki na Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo, Prof. Dos Santos Silayo (wa tatu kulia).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akihutubia baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania mjini Dodoma leo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo akihutubia baraza hilo.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Aloyce Nzuki akihutubia baraza hilo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania waliohitimu mafunzo ya Jeshi Usu hivi karibuni wakati wa mkutano wa sita wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala huyo uliofanyika leo mjini Dodoma. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kulia) akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Aloyce Nzuki muda mfupi baada ya kufungua baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania mjini Dodoma leo. 

Wednesday, April 11, 2018

DK. KIGWANGALLA AITAKA KAMATI INAYOCHUNGUZA TUHUMA ZA MAUAJI YA TEMBO KATIKA IKOLOJIA YA RUAHA-RUNGWA KUTENDA HAKI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla akisalimiana na Kamanda wa Polisi Mstaafu wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ambaye ni Mwenyekiti wa kamati inayochunguza tuhuma za mauaji ya tembo katika Ikolojia ya Rugwa-Ruaha ambazo zilitolewa hivi karibuni na kituo cha habari cha ITV LONDON cha nchini Uingereza, alipokutana na kamati hiyo leo ofisini kwake mjini Dodoma. Wengine pichani ni wajumbe wa kamati hiyo.

Na Hamza Temba-Dodoma
........................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameitaka kamati inayochunguza tuhuma za mauaji ya tembo katika Ikolojia ya Ruaha-Rungwa ambazo zilitolewa mwishoni mwa mwaka jana na kituo cha habari cha ITV London cha Uingereza kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa bila kumuonea mtu ili ukweli ubainike na Serikali iweze kuchukua hatua stahiki.

Dkt. Kigwangalla ametoa rai hiyo leo mjini Dodoma alipokutana na wajumbe wa kamati hiyo ambayo imewasilisha taarifa za awali za kazi ilizoanza kuzifanya za kupitia taarifa mbalimbali kuhusu tuhuma hizo kabla ya kwenda kuzifanyia uchunguzi maeneo husika.

Amewataka wajumbe hao kuchunguza ukweli wa tuhuma hizo ili kubaini kama kweli kuna watumishi wa Wizara waliohusika katika mauaji hayo pamoja na tuhuma kuwa mauaji ya tembo yalikuwa ni makubwa kama ilivyoripotiwa na chombo hicho cha habari.

Dkt. Kigwangalla pia ameitaka kamati hiyo kuchunguza ukweli wa tuhuma kuwa fedha za ufadhili wa mradi wa SPANEST zilizotolewa na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) zilitumika vibaya kufadhili mauaji hayo kama ilivyoripotiwa na chombo hicho cha habari.

“Msimtafute mtu, wala msimuonee mtu, fanyeni kazi hii kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ukweli ujulikane ili sisi kama Serikali tuweze kuchukua uamuzi unaostahili” alisema Dkt. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi Mstaafu wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema kamati yake itafanya kazi kwa uaminifu na weledi wa hali ya juu na kuleta taarifa za ukweli na mapendekezo yatakayoisaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi kuhusu tuhuma hizo.

Mapema mwezi Januari mwaka huu, Waziri Kigwangalla na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Natalie Boucly wakiwa katika ofisi ndogo ya wizara hiyo jijini Dar es Salaam walikubaliana kuunda kamati ya pamoja kuchunguza tuhuma hizo.

Kamati hiyo iliyoundwa mapema mwezi januari mwaka huu inajumuisha wajumbe sita wakiwemo wawili kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na wengine wanne kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla akisalimiana na Ndugu Robert Mande ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla akisalimiana na Bi. Getrude Lyatuu ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamisi Kigwangalla akisalimiana na wajumbe wa kamati inayochunguza tuhuma za mauaji ya tembo katika Ikolojia ya Ruaha-Rungwa ambazo zilitolewa hivi karibuni na kituo cha habari cha ITV LONDON cha nchini Uingereza, alipokutana na kamati hiyo leo ofisini kwake mjini Dodoma.

Monday, April 9, 2018

JENGO LA MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO KUWA KIVUTIO CHA KIHISTORIA CHA UTOAJI WA HUDUMA ZA UTALII JIJINI ARUSHA



Na Hamza Temba - WMU
........................................................
JENGO la kitega uchumi la Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro jijini Arusha ambalo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi juni mwaka huu litakuwa kivutio cha kihistoria cha utoaji wa huduma za utalii hapa nchini.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla muda mfupi baada ya kukagua jengo hilo ambalo linasemekana kuwa refu kuliko majengo yote jijini Arusha likiwa na jumla ya ghorofa 18.

Alisema jengo hilo ambalo linatizamana na Round About ya AICC katikati ya jiji hilo, limekusudiwa kuwa Kituo Kimoja (One Stop Centre) cha shughuli zote za utoaji wa huduma za utalii jijini humo kuanzia uwekezaji, utangazaji na menejimenti kwa ujumla.

Alisema jengo hilo litatoa fursa kwa wadau mbalimbali wanaotoa huduma za utalii kuweka ofisi zao ikiwemo mabenki, watoa huduma za usafiri, mashirika ya ndege, mawakala wa safari za utalii na huduma, maduka ya bidhaa za utalii na mahoteli.

"Tutapamba pia jengo hili na" live screen" (Mabango ya Video Mubashara) za vivutio, hivyo wanyama wakiwa wanapita huko porini watakuwa wanaonekana "LIVE" (Mubashara) kwenye jengo hili kupitia LED Screen ambazo zitakuwa zimezunguka jengo hili" alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema huduma nyingine zitakazotolewa katika Jengo hilo ni pamoja na zile za kuangalia jiji la Arusha kupitia darubini, huduma za burudani ikiwemo kumbi za starehe na migahawa.

Kwa upande wake Mkandarasi wa jengo hilo, Mhandisi Bismas Meela wa Kampuni ya Inter-Consult limited alisema ujenzi wa jengo hilo ambalo ulianza mwezi Novemba, 2013 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu.

Alisema jengo hilo ambalo lina uwezo wa kupaki magari 67 kwa wakati mmoja katika ghorofa za chini linagharimu shilingi za Kitanzania bilioni 45.

Katika ziara hiyo ya siku moja ya ukaguzi wa jengo hilo, Dk. Kigwangalla aliongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Dk. Fredy Manongi na Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka hiyo, Asangye Bangu. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asangye Bangu kuhusu jengo la kitega uchumi la mamlaka hiyo lililopo katikati ya Jiji la Arusha ambalo limekusudiwa kuwa Kituo Kimoja cha shughuli zote za utoaji wa huduma za utalii jijini humo kuanzia uwekezaji, utangazaji na menejimenti kwa ujumla. Kulia ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Fredy Manongi.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia mandhari ya Jiji la Arusha akiwa juu ya Jengo la kitega uchumi la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Kutoka kulia ni Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka hiyo, Asangye Bangu na  Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Fredy Manongi. 
Dk. Kigwangalla akiendelea kupata maelezo kuhusu jengo hilo kutoka kwa Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa mamlaka hiyo, Asangye Bangu. 

 Dk. Kigwangalla na msafara wake wakiangalia umbo la uso wa simba uliotengengenezwa katika moja lango la kuingilia kwenye lift ndani ya jengo hilo. Milango yote ya kuingilia kwenye lift ndani ya jengo hilo itapambwa kwa taswira mbalimbali za wanyamapori.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akishuka kwenye ngazi maalum zinazotumia nishati ya umeme ndani ya Jengo hilo. Kulia ni Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asangye Bangu na nyuma yake ni Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Fredy Manongi. \
Waziri Kigwangalla akikagua kabati la kuhifadhia vitu katika moja ya Hotel Aprtment ndani ya jengo hilo. Kulia ni Naibu Mhifadhi wa Huduma za Uendeshaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asangye Bangu.
Muonekano wa jengo hilo kutokea barabara ya Makongoro Jijini Arusha.

Friday, April 6, 2018

AGIZO ALILOTOA WAZIRI KIGWANGALLA WILAYANI KISHAPU WAKATI WA KILELE CHA MAADHIMISHO YA UPANDAJI MITI KITAIFA



WAZIRI KIGWANGALLA AAGIZA KILA KIJIJI KUTENGA ENEO LA UHIFADHI WA MISITU, ATOA SIKU 7 KWA TFS KUWASILISHA MPANGO WA UVUNAJI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakipanda mti wa kumbukumbu wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Na Hamza Temba, WMU, Kishapu, Shinyanga
.......................................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewaagiza Wakuu wa Mikoa nchini kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinatenga maeneo katika kila kijiji kwa ajili ya uhifadhi wa misitu ikiwa ni pamoja na vijiji hivyo kuunda kanuni na taratibu zao wenyewe za kusimamia maeneo hayo. 

Ametoa agizo hilo jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wakati wa kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika mkoani humo kuanzia Aprili 03 mwaka huu.

Katika kufanikisha zoezi hilo ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuchagua mikoa 10 ya kuanza utekelezaji wa agizo hilo ikiwemo mikoa ya Shinyanga na Tabora ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa misitu.

Ameugiza pia we uongozi huo wa TFS kuweka mpango wa uhifadhi wa misitu ya asili katika maeneo hayo kwa kushirikiana na vijiji kupanga maeneo yanayostahili kuhifadhiwa sambamba na kuwapa elimu ya umuhimu wa uhifadhi wa maeneo hayo.

Wakati huo huo Dk. Kigwangalla ametoa siku saba kwa uongozi huo wa Wakala wa Huduma za Misitu kuwasilisha kwake mpango wa tathmini ya uvunaji wa mazao ya misitu wa nchi nzima kwa kuzingatia kiasi cha rasilimali misitu kilichopo na kiwango halisi kitakachotakiwa kuvunwa ambacho hakitazidi robo ya rasilimali iliyopo.

"Hatuwezi kuendelea tu kutoa vibali vya kuvuna misitu hatujui tunavuna wapi, tuna rasilimali kiasi gani, wavune kiasi gani, hapana, mnitengenezee mpango laa sivyo nitasitisha uvunaji, nikisema nasitisha uvunaji nitapeleka waraka kwa Wakuu wa Mikoa, na nina uhakika kwa nguvu walinayo hawashindwi kuzuia uvunaji. 

"Kwahiyo TFS nawapa siku saba mniletee mpango wa tathmini ya namna ambavyo tuna rasilimali kwenye kila mkoa, tujue mkoa flani una miti cubic mita kadhaa ya mbao kadhaa, ya kuni kadhaa, ya mkaa kadhaa na kwa mwaka huu tutaruhusu wavune kwenye msitu fulani  kiasi kadhaa, twende kisayansi, sio Meneja wa TFS anakaa Wilayani anatoa vibali watu wanaenda kuvuna,".

Dk. Kigwangalla amesema  takwimu za uharibifu wa misitu hapa nchini zinatisha jambo ambalo likiachwa liendelee bila kuchukua hatua nchi itageuka kuwa jangwa.

"Kwa mwaka tunakata miti kwa mahitaji mbalimbali kati ya ekari 800,000 na 1,200,000.
Ili kurejesha walau nusu ya miti tunayokata kwa mwaka tunahitaji kupanda miti 3,000,000 kwa mwaka mfululizo kwa miaka 17 ili kufidia kiasi cha uharibifu tunachofanya kwa nusu mwaka" alisema Dk. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Ezekiel Mwakalukwa ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alisema kumekuwepo na jitihada za kuandaa programu kubwa za kitaifa za uhifadhi wa mazingira katika maeneo mahususi yaliyoonekana kuzidiwa na tatizo la uharibifu wa mazingira. 

Alitaja Programu hizo kuwa ni Hifadhi Ardhi Dodoma (HADO), Hifadhi Ardhi Shinyanga (HASHI), na Hifadhi Mazingira Iringa (HIMA).

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema mkoa wake kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Tabora umeanza kuchukua hatua za kurejesha uoto wa asili katika maeneo yao ikiwemo kuanzisha utaratibu wa kugawa miche ya miti kwa kila kaya pamoja na kuimarisha kamati za uhifadhi wa mazingira.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Taboba, Aggrey Mwanri alisema ushirikiano huo ni muhimu kwani utawezesha kukabiliana na changamoto zilizopo katika mikoa hiyo kwa kuweka mikakati ya pamoja wa kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyopo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakipanda mti wa kumbukumbu wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwahutubia wananchi wakati wa kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Upandaji Miti Kitaifa yaliyofanyika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakiteta jambo wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akiwahutubia wananchi wakati wa maadhimisho hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakiwasalimu wananchi wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
  Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Ezekiel Mwakalukwa ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo akitoa maelezo kuhusu maadhimisho hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakielekea eneo la tukio la kupanda miti wakati wa kilele cha kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa iliyofanyika jana katika kijiji cha Mhunze wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akishiriki kucheza ngoma wakati wa maadhimisho hayo.