slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Friday, September 30, 2016

WAKALA WA HUDUMA ZA MISITU NCHINI WATOA MICHE YA MITI 600 KATIKA SHULE YA SEKONDARI MAMA SALMA KIKWETE KUUNGA MKONO KAMPENI YA UPANDAJI WA MITI JIJINI DAR ES SALAAM

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina akipanda mti katika Shule ya Sekondani ya Mama Salma Kikwete, Jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni kuunga mkono kampeni ya upanadaji miti Jijini Dar es Salaam iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa huo Paul Makonda, Kampeni hiyo ijulikanayo kama "Mti Wangu"  itazinduliwa kesho Oktoba Mosi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania umechangia miche ya miti 600 katika shule hiyo na miche ya miti mingine 3,000 itatolewa kesho wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo kwa ajili ya Jijiji la Dar es Slaam, katika awamu ya pili watachangia tena miche ya miti 5,000.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina (wa pili kulia) akimkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mama Salma Kikwete, Elestina Chanafi (wa pili kushoto) baadhi ya miche ya miti kati ya miche 600 iliyotolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa ajili ya shule hiyo kuunga mkono Kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya upandaji wa miti Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo (kulia) akimkabidhi Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina (wa pili kulia) miche 600 ya miti iliyotolewa na ofisi yake kwa ajili ya shule ya Sekondani ya Mama Salma Kikwete Jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono Kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya upandaji wa miti Jijini Dar es Salaam ijulikanyo kama “Mti Wangu” . Katika uzinduzi huo TFS imechangia miche ya miti 3,000 kati ya miche 8,000 ambayo imepanga kutoa kwa ajili ya kupandwa katika Jiji la Dar es Salaam. 
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo.

Msanii wa Filamu nchini, Jackline Wolper (katikati) akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo kuhusu kampeni yake ya "Think Green" katika kuunga mkono Kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ijulikanayo kama "Mti Wangu" ambayo itazinduliwa kesho Oktoba Mosi na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan . Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo (kushoto) akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Mama Salma Kikwete Jijini Dar es Salaam leo katika hafla fupi ya upandaji wa miti shuleni hapo kuunga mkono Kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ya upandaji wa miti, Prof. Silayo amewaasa wanafunzi hao kuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti. Katika hafla hiyo TFS wamekabidhi jumla ya miche ya miti 600.
Picha ya pamoja kati ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Luhaga Mpina (wa tano kushoto), Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo (wa sita kushoto), Msanii Jackline Wolper, Watumishi na baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Mama Salma Kikwete.

Wednesday, September 28, 2016

TANGAZO KWA UMMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA  MALIASILI NA UTALII




WAFANYABIASHARA WA UTALII KUSAJILI NA KULIPIA ADA YA LESENI YA MWAKA 2016

Wizara ya Maliasili na Utalii inawakumbusha wafanya biashara za utalii wasiokuwa na leseni ya biashara hiyo inayotolewa kwa mujibu wa sheria ya Utalii Na. 29 ya Mwaka 2008 Vifungu Na.10 na 31, kuwa wanatakiwa kusajili na kulipia ada ya leseni kwa mwaka 2016 ifikapo tarehe 31 Oktoba, 2016.

Biashara za Utalii husika ni hizi zifuatazo:

1
Kampuni za kusafirisha watalii
10
Vivutio vya kuuza bidhaa za urithi (Cultural heritage centres)
2
Kampuni za uwindaji wa kitalii
11
Wajasiriamali wa utalii wa utamaduni (Cultural tourism enterprises)
3
Wawindaji Bingwa
12
Kampuni za kukodisha vifaa vya utalii

4
Kampuni za kusafirisha watalii kwa ndege
13
Maeneo ya michezo ya burdani (Theme parks, wildlife forms. Zoo, snake parks etc)
5
Kampuni za kusafirisha watalii kwa Maputo (hot air balloon)
14
Kampuni za kukodisha magari kwa watalii
6
Kampuni za kusafirisha watalii kwa farasi
15
Kampuni za kukatisha tiketi za ndege
7
Kampuni za kusafirisha watalii kwa boti
16
Wakala wa kutoa huduma kwa watalii (tourist handling agents)
8
Kampuni za kupandisha watalii Milimani
17
Nyumba za huduma za malazi (hoteli, loji, kambi za kitalii)
9
Kampuni za utalii wa michezo ya kusisimua (tourism adventure sports)
18
Maduka ya zawadi za kitalii (Curio Chops)



i.      Wizara inachukua nafasi hii pia kusisitiza kwamba ni kosa linalostahili adhabu  kisheria kufanya biashara ya utalii bila ya kusajili na kulipia ada ya leseni kwa  mwaka husika.

ii.        Vilevile, tunapenda kuwafahamisha kuwa maombi kwa ajili ya leseni ya kufanya  biashara ya utalii kwa mwaka 2017 yameanza kupokelewa katika Ofisi zetu zilizopo Dare s Salaam, Arusha, Mwanza na Iringa.

iii.    Orodha ya wafanyabiashara ya utalii waliosajiliwa na kulipia ada za leseni  inapatikana katika tovuti ya Wizara (www.mnrt.go.tz), na katika ofisi za Wizara  zilizotajwa hapo juu.

Angalizo: Umma unatahadharishwa kutofanya biashara na kampuni za biashara za utalii ambazo hazina Leseni ya Biashara ya Utalii ya mwaka 2016, kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha Sheria.


Imetolewa na:

KATIBU MKUU
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Simu: +255 22 2864230

Barua pepe: ps@mnrt.go.tz

Friday, September 23, 2016

JESHI LA POLISI MKOANI PWANI KWA KUSHIRIKIANA NA MAOFISA WA MALIASILI WAKAMATA VIROBA VYA BANGI NDANI YA MAGUNIA YA MKAA

Askari polisi wa kituo cha polisi cha Chalinze akionesha viroba viwili vya bangi vyenye uzito wa kilo 50 kila kimoja vilivyokuwa ndani ya Magunia mawili ya mkaa yaliyokamatwa jana katika Operesheni ya kuthibiti utoroshaji wa mazao ya Misitu yasiyo na kibali katika kata ya Vigwaza tarafa ya Chalinze mkoani Pwani katika Bara bara kuu ya Morogoro wakitokea Tunduma wakiwa kwenye gari lenye namba za usajili T876 DDL aina ya DAF Leyland
Moja ya Kiroba kilichojaa bangi chenye uzito wa kilo 50 kilichokuwa ndani ya gunia la mkaa lililokamatwa jana katika Operesheni ya kuthibiti utoroshaji wa mazao ya Misitu yasiyo na kibali katika kata ya Vigwaza tarafa ya Chalinze mkoani Pwani katika Bara bara kuu ya Morogoro kikitokea Tunduma kikiwa kwenye gari lenye namba za usajili T876 DDL aina ya DAF Leyland.
Kaimu wa Kanda ya Pwani ya Wakala wa Hudumza Misitu Tanzania (TFS) Bw. Jonathan Mpangala akiwaonesha waandishi wa habari gari lililokuwa limebeba magunia mawili ya mkaa ambayo ndani yake kulikuwa na viroba viwili vilivyojaa bangi vyenye uzito wa kilo 50 kila kimoja ( Picha na Lusungu Helela- Afisa Habari Maliasili na Utalii)
_____________________________________
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Maofisa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) inamshikilia Dereva Bw. Emanuel Bisama (37) ambaye ni mkazi wa Kimara Suka Dar es Salaam,kwa kosa la kusafirisha magunia mawili ya mkaa ambayo baada ya kupekuliwa ndani yake kulikutwa na viroba viwili vyenye uzito kilo 50 kila kimoja vikiwa vimejaa bangi.

Akizungumza jana na Waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Pwani , ACP. Bonaventura Mushongi alisema Mtuhumiwa ambaye ni dereva wa gari lenye namba za usajili T876 DDL aina ya DAF Leyland Bw. Emanuel Bisama (37) alikamatwa Septemba 21 saa 4.00 asubuhi katika kata ya Vigwaza tarafa ya Chalinze mkoa wa Pwani katika Bara bara kuu ya Morogoro akitokea Tunduma na kwa sasa yupo mbaroni kwa mahojiano licha ya kukana kuwa hakujua kilichomo ndani ya magunia hayo.


Kamanda Mushongi alisema walifanikiwa kumkamata wakiwa katika Operesheni ya Ukaguzi wa mazao ya Misitu katika Barabara kuu ya Morogoro hadi Dare Salaam, aliongeza kuwa Dereva huyo wa gari amefunguliwa kesi CHA/RB/3039/2016 kwa kosa la kupatikana na bangi

Kwa upande Wakala wa Hudumza Misitu Tanzania (TFS) Kaimu wa Kanda ya Pwani Bw. Jonathan Mpangala alisema kuwa Mtuhumiwa huyo amefunguliwa kesi ya pili yenye CHA/RB/5113/2016 kwa kosa la kumiliki na kusafirisha mazao ya misitu bila kibali kwa sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2012 kifungu 88 na 89.

Alisisitiza kuwa Operesheni ya kukamata usafirishaji wa mazao ya misitu bila vibali itakuwa ya kudumu baada ya kuona magari mengi hasa makubwa yakiwa yamepakiwa magunia ya mkaa kuanzia mawili hadi matano ambayo yamekuwa yakioneka waziwazi hata ukiwa barabarani namengi yakiwa hayalipiwa ushuru wa Serikali kuu na hata magari mengine yakiwa hayajalipiwa ushuru wa Halmashauri

SHAMBA LA MITI SAO HILL, NGUZO YA MAENDELEO NA MKOMBOZI WA MAZINGIRA WILAYA YA MUFINDI NA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI

Displaying DSC_7362.JPG
Meneja wa Shamba la Miti Sao Hill, Salehe Beleko (kulia) akionesha sehemu ya madawati 4,112 yanayotengenezwa na shamba hilo kwa ajili kuunga Mkono Mpango wa Serikali ya awamu ya tano wa kuhakikisha Shule zote nchini zinakuwa na madawati ya kutosha. Wengine pichani ni watendaji katika shamba hilo.
Displaying DSC_7399.JPG
Moja ya kitalu cha miche ya miti aina ya Misindano ambacho kipo katika Kituo cha Ilundi ndani ya Shamba la Miti Sao Hill. Kitalu hicho kina jumla ya miche milioni tatu kwa ajili ya kupandwa katika shamba hilo na mingine watapewa wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hilo kwa ajili ya kuhamasisha upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.
Displaying DSC_7386.JPG
Uchakataji wa asali katika shamba la miti Sao Hill ukiendelea. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Ufugaji wa Nyuki, Joseph Sondi na kulia ni Happyness Nandonde, Msaidizi.
_________________________________________________

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ina jukumu la Kuanzisha na kusimamia mashamba ya miti na manzuki za Serikali kuu, Kuna jumla ya mashamba 18 ya miti ambayo yanaendeshwa na Serikali kupitia Wakala huyo na kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa.

Mashamba hayo ni Buhindi, Kawetire, Kiwira, Korongwe, Longuza, Mbizi, Meru/USA, Mtibwa, North Kilimanjaro, North Ruvu, Rondo, Rubare, Rubya, Sao Hill, Shume, Ukaguru, West Kilimanjaro na Wino.

Shamba la Miti Sao Hill ndilo shamba kubwa zaidi kati ya mashamba hayo 18 ya Serikali ambayo yanasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Kwa sehemu kubwa Shamba hilo lipo katika Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa na baadhi ya eneo katika Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro.

Shamba hilo lilianzishwa kwa majaribio mwaka 1939 hadi 1951 na upandaji wa miti kwa kiwango kikubwa kuanza rasmi mwaka 1960 hadi 1990, Ukubwa wa shamba hilo ni Hekta 135,903 ambazo zimehifadhiwa kwa ajili ya Upandaji wa Miti (Plantation)  na Hifadhi ya Misitu Asilia (Nature Reserve).

Katika shamba hilo Jumla ya hekta 55,617.22 zimepandwa miti aina ya misindano na mikaratusi, hekta 48,200 ni maeneo ya misitu ya asili ambayo sehemu kubwa ni kwa ajili ya vyanzo vya maji, hekta 29,933 ni kwa ajili ya upanuzi wa upandaji miti na hekta 1,700 ni maeneo ya makazi na matumizi mengineyo.

Akizungumza na Mwandishi wa Makala hii, Meneja wa Shamba hilo, Salehe Beleko alisema pamoja na kazi hiyo ya upandaji wa miti pia wanashughulika na ufugaji wa nyuki kama mkakati wa kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha ulinzi wa misitu na mazingira.

“Shamba letu lina jumla ya mizinga 1,298 ya nyuki na kwa mwaka 2015/16 tulivuna asali kilo 379 na baada ya kupima sampuli ya asali hiyo vipimo vya maabara vilionesha kuwa asali inayotoka kwenye hifadhi ya msitu wetu ni asali halisi isiyokuwa na kemikali (pure organic honey)” Alisema Beleko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Ufugaji wa Nyuki wa Shamba hilo, Joseph Sondi alisema katika kipindi cha Mwezi July – August, 2016 jumla ya kilo 700 za asali zimeshavunwa katika shamba hilo.

Akizungumzia dhumuni la kuanzishwa shamba hilo, Meneja Salehe Beleko alisema ilikuwa kwa ajili ya Kupunguza utegemezi wa misitu ya asili kama chanzo cha malighafi ya miti kwa matumizi mbalimbali na Kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda vinavyotumia malighafi ya miti, kwa mfano viwanda vya mbao, karatasi, viberiti, nguzo za umeme na simu.

Alisema kuwa malengo mengine yalikuwa ni pamoja na Kuboresha hali ya mazingira kwa ujumla na uoto wa asili, Kuhifadhi ardhi na vyanzo vya maji, Kuwapatia wananchi ajira zinazotokana na kazi za msimu za mashambani na kutokana na viwanda tegemezi vya mazao ya misitu pamoja na kuwa Chanzo cha mapato ya Serikali.

Akizungumzia mafanikio juu ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika shamba hilo, alisema katika mwaka wa fedha 2015/16 makusanyo yaliongezeka na kuvuka malengo yaliyowekwa ya kukusanya shilingi bilioni 31.35 na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 36.14, makusanyo ambayo ni ya juu kabisa ukilinganisha na makusanyo ya miaka ya nyuma toka kuanzishwa kwa shamba hilo.

Beleko alisema shamba la Miti Sao Hill limekuwa na faida kubwa kwa jamii ambapo kwa sasa limekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya viwanda vidogo na vikubwa vya uchakataji wa mbao katika Wilaya ya Mufindi na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hatua hiyo inaunga mkono mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kujenga uchumi wa viwanda.

Pamoja na faida hiyo alisema “Shamba hili limesaidia sana kuongezeka kwa ari ya upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwa wananchi wanaozunguka shamba na ukanda wote wa nyanda za juu kusini jambo ambalo limesaidia kupunguza matukio ya moto kupitia ulinzi shirikishi, Aidha limepelekea pia kupanda kwa thamani ya ardhi katika maeneo haya”.

Meneja huyo alisema Shamba hilo pia lina mchango mkubwa katika maendeleo ya Wilaya za Mufindi na Kilombero na jamii jirani ambapo wamekuwa wakipatiwa gawio la asilimia 5 ya mrahaba kila mwaka. Kumbukumbu zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 2000 mpaka 2016 jumla ya Mrahaba wa shilingi bilioni 4.8 umeshatolewa kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo katika jamii hizo.

Pamoja na Mrahaba shamba hilo pia hutoa ajira mbalimbali za muda mrefu na mfupi zinazokadiriwa kufikia 34,000, ajira hizo ni katika shamba lenyewe, viwanda vya kuchakata mbao pamoja na ujasiriamali. Sehemu kubwa ya wananchi katika ajira hizo ni wakazi wa Wilaya ya Mufindi.

Akizungumzia miradi ya maendeleo, Beleko alisema Shamba hilo huchangia uendelezaji wa miradi ya maendeleo (afya, elimu, ujenzi wa ofisi za vijiji) kwa jamii zinazozunguka msitu pamoja na miradi ya upandaji wa miti na ufugaji nyuki kwenye vijiji vinavyozunguka msitu. Katika kipindi cha mwaka 2010 mpaka 2016 jumla ya shilingi milioni 110 zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo vijiji kadhaa vilinufaika.

Miongoni mwa vijiji vilivyonufaika ni Kitasengwa, Ihalimba, Itimbo, Nyololo, Mninga, Mkalala, Vikula, Wami, Nundwe, Ibatu, Mwitikilwa, Kasanga, Changarawe, Ugesa, Ludilo na Usokami.

Katika kuboresha dhana ya ushirikishaji jamii kwenye ulinzi wa msitu, Beleko alisema “Shamba limetoa vibali kadhaa kwa vijiji na kata za Wilaya ya Mufindi katika kipindi cha miaka mitano mfululizo (2012-2016). Jumla ya miti yenye mita za ujazo 78,000 ambayo thamani yake kwa bei ya soko baada ya kuchakatwa ni shilingi bilioni 3.9, fedha hizo zimekusudiwa kwa ajili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii hiyo na shughuli za maendeleo”.

Beleko alisema, kwa kuwa Shamba hilo limezungukwa na vijiji vingi, wamekuwa wakitoa mitambo ili kusaidia matengenezo ya barabara kwenye vijiji hivyo. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 jumla ya kilometa 66 za barabara zimelimwa kwenye vijiji vya Kinyanambo, Itimbo-Lyasa, Ihalimba-Igomtwa-Usokami, Ugesa-Wami na Ludilo.

Aliongeza kuwa shamba hilo linatekeleza dhana ya Kilimo Mseto ambapo Wafanyakazi wa shamba na wanavijiji hugawiwa maeneo ya kulima katika maeneo yaliyovunwa miti.

“Kilimo hiki hufanyika kwa msimu mmoja tu wakati wa kupanda miti upya katika maeneo hayo. Wastani wa watu 600 hufaidika na huduma hiyo ambapo takribani tani 2,000 za mahindi yanayokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 800 huvunwa kila mwaka” Alisema Beleko.

Aidha Beleko alisema, jamii zinazozunguka mashamba zinasaidiwa kwa kupatiwa mahitaji muhimu ya kuanzisha vitalu vya miche ya miti na ufugaji nyuki kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo.

“Ili kutekeleza azma hii, Shamba hugawa miche ya miti kwa jamii inayotuzunguka ambapo kwa mwaka 2014/15 jumla ya miche ya miti 300,000 yenye thamani ya shilingi milioni 120 iligawanywa na mwaka 2015/16 jumla ya miche 600,000 yenye thamani ya shilingi milioni 240 inatarajiwa kugawanywa” Alisema.

Mchango mwingine wa shamba hilo kwa Wananchi waishio jirani na shamba hilo ni fursa ya kuokota kuni kavu bure kwa ajili ya matumizi ya majumbani. Vilevile wananchi wanaruhusiwa kuvuna bure mazao yasio timbao kama vile uyoga, mbogamboga na matunda. Tafiti iliyofanyika mwaka 2010 inaonesha kuwa zaidi ya kilo 80,000 za matunda aina ya pesheni (passion) yenye thamani ya shilingi milioni 240 huvunwa kila mwaka kutoka maeneo ya Shamba hilo.

Katika kutoa mchango wa huduma za afya alisema “Shamba lina zahanati moja na vituo vitatu vya huduma ya kwanza kwa ajili ya huduma ya matibabu kwa wafanyakazi na wanavijiji wanaozunguka shamba hili. Shamba huchangia katika ununuzi wa dawa kwa ajili ya zahanati na vituo hivyo”.

Alisema baadhi ya vijiji vinavyonufaika na huduma hiyo ni Kihanga, Mninga, Matanana, Sao Hill, Ihalimba, Iheka, Mwitikilwa, Nundwe, Vikula, Kitasengwa na Makungu. Kwa wastani jumla ya wananchi 2,000 kutoka kwenye vijiji vinavyozunguka Shamba hupata huduma ya matibabu kutoka kwenye zahanati ya Shamba na vituo vyake.

Katika mchango wa elimu, Shamba lina shule ya msingi moja ambayo hutoa elimu kwa watoto wa wafanyakazi wa shamba, kiwanda cha mbao cha Sao Hill na jamii inayozunguka shamba. Shamba kwa kushirikiana na uongozi wa kiwanda cha mbao cha Sao Hill linahudumia shule kwa kuwapatia walimu nyumba za kuishi, madarasa ya wanafunzi na ukarabati wa majengo yote pamoja na huduma nyingine muhimu kama vile maji, umeme, usafiri na matibabu.

Aidha Beleko alisema kuwa katika kuunga mkono sera ya Serikali ya awamu ya tano ya elimu bure, jumla ya madawati 4,112 yanatengenezwa kwa ajili ya kutatua changamoto ya uhaba wa madawati katika Wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa kwa ujumla. Alisema madawati hayo yakikamilika yatakabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi.

Akizungumzia kuhusu kukua kwa uchumi wa Mji wa Mafinga Beleko alisema Biashara ya Magogo na Mbao imepelekea Mji wa Mafinga kukua kwa kasi kiuchumi hadi kupewa hadhi ya Mamlaka ya Mji Mdogo. Takribani asilimia 62 ya watu wenye vibali vya kuvuna miti na kuchakata magogo katika shamba la miti la Sao Hill ni wenyeji wa wilaya ya Mufindi kutoka katika vijiji vinavyozunguka msitu.

Beleko alisema kuwa pamoja na faida zote hizo shamba linahitaji gharama kubwa za uendeshaji ili liweze kuzalisha ipasavyo ambapo bajeti yake kwa mwaka ni takribani shilingi bilioni 10 mpaka 15.

Kuhusu fursa za uwekezaji katika shamba hilo, Beleko alisema uwepo wa shamba umeipa fani ya Misitu umaarufu mkubwa Wilayani Mufundi na Ukanda wote wa Nyanda za Juuu Kusini, Hivyo kutoa fursa ya uwekezaji katika viwanda na vyuo mbalimbali vya Misitu kwa ajili ya kuzalisha wataalamu katika fani hiyo.

Alisema fursa nyingine ni pamoja na ufugaji wa nyuki kutokana na uwepo wa misitu ya asili, ya kupandwa pamoja na vyanzo mbalimbali vya maji. Alieleza kuwa asali inayozalishwa katika shamba hilo ilipimwa katika moja ya maabara ya kimataifa nchini Ujerumani na kuthibitika kuwa haina kemikakali yeyoye (pure organic).

“Fursa ya kuwekeza katika viwanda vya maji pia inapatikana katika shamba hili kutokana na uwepo wa chem chem na vyanzo mbalimbali vya maji. Yapo pia maporomoko ambayo yanafaa kwenye nishati ya umeme wa maji pamoja na mabwawa kwa ajili ya ufugaji wa samaki, tunawakaribisha wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta hizo” Alisema Beleko.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Ufugaji wa Nyuki, Joseph Sondi alisema pamoja na shughuli za uzalishaji wa mazao ya misitu na asali, Sao Hill pia ni Kituo cha Mafunzo kwa vitendo ambapo kila mwaka hupokea wanafunzi mbalimbali kutoka vyuo vikuu vya Sokoine (SUA), Dar es Salaam (UDSM) na Mipango Dodoma. Vilevile mashamba mapya ya miti yaliyoanzishwa kama vile Wino na Mbizi hujifunza katika shamba hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Festo Elia Mgina alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia mahusiano baina ya shamba la Sao Hill na Halamshauri yake alisema, uwepo wa shamba hilo umeongeza mzunguko mkubwa wa fedha na ajira katika Halmashauri hiyo.

“Siasa za Mufindi ni Sao Hill, mtu mmoja anayenunua mita za ujazo 200 ambazo ni kiwango cha chini kabisa anaajiri watu wasiopungua 40 katika mfumo mzima wa uchakataji jambo ambalo linaongeza ajira kwa wakazi wa mufindi na wakati huo huo mzunguko mkubwa wa fedha” Alisema Mgina.

Aliongeza kuwa shamba hilo limehamasisha kwa kiwango kikubwa upandaji wa miti kwa jamii inayolizunguka ambapo pia hutoa msaada wa mafunzo na miche ya miti kwa ajili ya kupandwa. “Hamasa ya kupanda miti imekuwa kubwa kutokana na thamani inayoonekana Sao Hill kiasi kwamba imefikia hatua sasa tunawaelimisha watu wetu waache baadhi ya maeneo kwa ajili ya kilimo cha mazao mengine ya chakula na biashara” Alisema Mgina.

Akizungumzia misaada mingine inayotoka Sao Hill alisema ni pamoja na elimu ya kukabiliana na moto ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuondoa tatizo hilo, Msaada wa mitambo ya kutengeneza barabara na vifaa mbali mbali vya ujenzi, zahanati na mashule.

Thursday, September 22, 2016

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI ENG. RAMO MAKANI AONANA NA VIONGOZI NA WADAU WA RAFIKI WILDLIFE FOUNDATION KUZUNGUMZIA KAMPENI YA KUPIGA VITA UJANGILI NCHINI

Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Eng. Ramo Makani (kushoto) akizunumza na viongozi na wadau shirikishi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Rafiki Wildlife Foundation kuhusu Kampeni ijulikanayo kama "Jitokeze Tuongee, Piga Vita Ujangili Afrika na Wizara ya Maliasili na Utalii" iliyoandaliwa na shirika hilo kwa ushirikiano na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wengine ofisini kwake Dar es Salaam jana, tarehe 21 Septemba, 2016. Kampeni hiyo imepangwa kuzinduliwa Jijini Arusha tarehe 07 Oktoba, 2016. Kaulimbiu ya Kampeni hiyo ni "Fursa ya Elimu ya Uhifadhi na Utalii ni Haki ya kila Mtanzania ili kupiga vita Ujangili, Idai". Kulia ni mdau wa kampeni hiyo ambaye pia ni Mbunge Mstaafu wa Viti Maalum , Al-Shaymaa Kwegyir.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na viongozi na wajumbe shirikishi wa Rafiki Wildlife Foundation ofisini kwake jana. Alieleza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kupiga vita ujangili na kuimarisha uhifadhi wa Maliasili nchini. Alitoa wito kwa watanzania kuwa wazalendo kwa nchi yao na kupenda Malisili za taifa na kujenga utaratibu wa kuzitembelea ili kukuza utalii wa ndani ambao Wizara imejipanga kuuendeleza kuhakikisha unakuwa kwa kasi ili kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa.
 Mkurugenzi wa Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya Rafiki Wildlife Foundation, Mchungaji Clement Matwiga (wa tatu kulia) akizungumza katika kikao hicho, Mchungaji huyo alitoa wito kwa watanzania kuwa mstari wa mbele katika ulinzi wa wanyamapori hususani Tembo na Faru kwa kuwa wana faida kubwa kwao kiuchumi na kijamii, alisema kuwa kwa sasa jamii inaona  jukumu hilo ni la Serikali pekee kupitia Wizara ya Maliasili na Taasisi zake jambo ambalo sio sahihi. Akielezea kuhusu kampeni ya "Jitokeze Tuongee, Piga Vita Ujangili Afrika na Wizara ya Maliasili na Utalii"  itakayozinduliwa Jijini Arusha na Waziri wa Maliasili na Utalii alisema, itahusisha fursa mbalimbali ikiwemo kutembelea hifadhi ya Taifa ya Arusha kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani, Semina mbalimbali kuhusu uhifadhi pamoja na michezo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (wa tatu kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi na wajumbe shirikishi wa Rafiki Wildlife Foundation ofisini kwake jana.

Wednesday, September 14, 2016

MAKALA: MATUMIZI YA NISHATI MBADALA YA GESI NA MAKAA YA MAWE SULUHISHO LA UHARIBIFU WA MISITU NCHINI

 Sehemu ya makaa ya mawe yaliyotengenezwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la Mbalawala Women Organization (MWO) la Mkoani Ruvuma kwa ajili ya matumizi ya majumbani.
 Moja ya mashine inayotumiwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la Mbalawala Women Organization (MWO) kuchakata makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi ya majumbani. 
Jengo ambalo ndani yake kuna tanuri la kuchakata makaa ya mawe ambalo limejengwa kwa msaada wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ikiwa moja ya mkakati wake wa kushirikiana na wadau mbalimbali katika  kuanzisha na kutumia nishati mbadala kunusuru Misitu nchini. Jengo hilo linatumiwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la Mbalawala Women Organization (MWO).

----------------------------------------------------------------------

Misitu ni uhai kwa kuwa hukidhi mahitaji mbalimbali ya binadamu, kama vile kuhifadhi vyanzo vya maji, kuboresha hali ya hewa, kuzuia mmomonyoko wa ardhi, upatikanaji wa kuni, mbao, madawa, malisho ya mifugo, kuboresha shughuli za kilimo na kuboresha mandhari ya nchi yetu mijini na vijijini. Aidha, misitu pia ni chanzo muhimu cha mapato kwa wananchi wengi wa vijijini na mijini.

Ni kutokana na umuhimu huo wa Misitu ndio maana Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) akapewa jukumu la kusimamia misitu na rasilimali zake kwa niaba ya Serikali Kuu ili iweze kuwanufaisha watanzania wa leo na wa vizazi vijavyo kupitia matumizi endelevu.

Iko wazi kuwa kuna utegemezi mkubwa wa misitu kama chanzo rahisi na kikuu cha nishati nchini, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya nishati inayotumika Nchini inatokana na miti. Uvunaji mkubwa wa mkaa umeathiri sana ubora wa misitu. Kuni zinatumika zaidi vijijini na mkaa unatumika zaidi mijini.

Matumizi ya nishati mbadala yanatajwa kama moja ya suluhisho la tatizo hilo, Katika kukabiliana na tatizo la uharibifu wa Misitu Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) inafanya ushirikiano na wadau wa sekta mbalimbali hasa  Wizara ya Nishati na madini na jamii kwa ujumla ili kupunguza utegemezi wa misitu kama chanzo kikuu cha nishati.

Miongoni mwa asasi za kiraia ambazo Wizara inashirikiana nazo katika kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ni Shirika Lisilo la Kiserikali (NGO) la Mbalawala Women Organization (MWO) ambalo lipo katika wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, Makao yake makuu yakiwa katika kijiji cha Ruanda eneo maarufu kwa jina la Center D.

Shirika hilo limejikita katika uwezeshwaji wa vikundi vya wanawake kiujisiliamali ili waweze kujikwamua kiuchumi hasa wanawake ambao wanazunguka mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka uliopo Kata ya Ruanda wilayani Mbinga, wengi wao wameshindwa kuajiriwa na mgodi huo kutokana na ugumu wa shughuli husika ambazo hufanywa na wanaume.

Likiwa limejikita na shughuli za miradi ya utengenezaji wa vitofali vya kupikia vya makaa ya mawe pia lina lengo la kutunza mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti kwa kutengeneza na kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya nishati hiyo mbadala.

Akizungumza na Mwandishi wa Makala hii, Meneja wa Uzalishaji wa shirika hilo, Harid Kapinga aliitaja miradi mingine ambayo inafanywa na shirika hilo kuwa ni huduma ya chakula na usafi katika kambi ya mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka, programu ya shule, bustani ya mboga na matunda, shamba la mpunga na ufinyanzi wa vyungu.

Akizungumzia uongezaji wa thamani wa makaa ya mawe ili yaweze kutumika kwa matumizi ya majumbani, Meneja huyo wa Uzalishaji alisema, awali wananchi walikuwa wanaokota makaa ya mawe pembezoni na mgodi na kwenda kupikia bila kujua madhara yake kwa maisha ya binadamu na uharibifu wa vyombo ambavyo walikuwa wanavitumia katika kupikia vyakula vyao.

“Kutokana na umuhimu wa jambo hilo Kampuni ya Tancoal Energy kwa kushirikiana na Mbalawala waliamua kuchukua hatua ya kuongeza thamani ya makaa ya mawe kupitia wataalam na maabara ya mgodi ili yaweze kufaa kwa kupikia majumbani” alisema Kapinga.

Alisema kuwa huwa wanatumia vumbi ambalo linatokana na kukatwa kwa mkaa wa mawe na kupelekwa maabara ili kuweza kubaini kiasi cha athari ya joto lililopo kabla ya kuongezewa thamani kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya majumbani.

Alieleza kuwa joto la Makaa wa mawe ya Ngaka  lipo juu sana kati ya Calorific Value (CV) 5800 hadi 6200 wakati joto linalotakiwa kwa ajili ya kupikia ni kati ya CV - 4200 mpaka 4500 hivyo wataalamu wa maabara huuingiza kwenye mitambo maalum na kuuongezea thamani kwa ya kurekebisha joto linalotakiwa kabla ya matumizi ya majumbani.

Alieleza kuwa wanatengeneza aina mbili za mkaa, wenye umbo dogo kwa ajili ya matumizi ya majumbani na wenye umbo kubwa kwa ajili ya matumizi ya taasisi kubwa kama Shule, Hoteli, Vyuo na Magereza.

Akielezea faida za mkaa huo Kapinga alisema “Miongoni mwa faida za makaa haya ya mawe ni pamoja na unafuu wa bei katika manunuzi, kwa mfano tani moja ya mkaa wa miti ni shilingi 2,225,000 lakini mkaa huu unaotokana na makaa ya mawe tani moja ni shilingi 200,000 ukiyanunua kiwandani kwetu”

Alifafanua kuwa makaa ya mawe yenye umbo dogo kwa bei ya rejareja huuzwa shilingi 200 kwa kilo na kwa ule wenye umbo kubwa ambao unafaa kwa matumizi makubwa huuzwa kwa shilingi 350, na kwa kipande kimoja cha mkaa unaweza ukapikia vitu vingi kwakuwa toka kuwaka kwake mpaka kuwa jivu huchukua zaidi ya masaa manane.

Alitaja faida nyingine kuwa ni uhifadhi na utunzaji wa misitu kwakuwa matumizi ya makaa ya mawe yataepusha utegemezi wa rasilmali za misitu kama nishati pekee ya kupikia, aliongeza kuwa utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa uchimbaji wa makaa ya mawe unaweza kuchukua zaidi ya miaka 100, hivyo ukitumika ipasavyo unaweza kuokoa uharibifu wa misitu.

Akizungumzia hali ya soko alisema kuwa ulifanyika utafiti wa mwaka mmoja na baada ya hapo wakaanza uzalishaji kisha elimu kwa wananchi ikatolewa katika vitongoji 8 ambavyo vina zunguka mgodi huo kuhusu matumizi bora ya makaa ya mawe, pia elimu hiyo ilitolewa kwenye vikundi mbalimbali ambavyo vinauza mkaa wa kuni, kwenye maonesho mbalimbali kama Saba Saba na makongamano.

“Watumiaji wengi wamehamasika sana kutumia mkaa huu na mawakala pia wamepatikana kwa ajili ya kusambaza mkaa huu nchi nzima na sasa tunajipanga kwa uzalishaji mkubwa zaidi kwani majaribio ya utengenezaji yameshafanyika na kukamilika” alisema Kapinga.

Alisema kuwa matokeo ya majaribio hayo yameonyesha mafanikio makubwa kutokana na mwitikio wa wananchi kwani vitofali vina ubora vimetengenezwa kwa kutumia mavumbi ya makaa ya mawe na malighafi zingine na wananchi wanaendelea kuvitumia katika shughuli zao za kila siku kuzunguka mgodi.

Akizungumzia ushirikiano baina yao na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) alisema, ushirikiano wao ni mzuri sana kwa kuwa wamepatiwa fedha za kujengea jengo na tanuri la kuchakatia makaa ya mawe, ingawa bado kuna changamoto ya mitambo ya kuzalishia pamoja na umeme wa uhakika.

“Mradi huu ni muhimu sana hivyo tunaziomba Taasisi na Serikali ziweze kutusaidia kukabiliana na changamoto zinazotukabili katika uzalishaji ili tuweze kufanikiwa kusambaza mkaa huu nchi nzima na kufanikisha kampeni ya utunzaji wa misitu kwa kutumia nishati mbadala kwani bila nishati mbadala kamwe vita ya utunzaji wa misitu haiwezi kushinda” alisema Kapinga.

Awali Meneja huyo wa Uzalishaji alisema kuwa Mbalawala Women Organization ni matokeo ya juhudi za Tancoal Energy Limited katika kuisaidia jamii inayozunguka mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka na kwamba Shirika la Mbalawala Women Organization limeundwa na vijiji vya Ruanda na Ntunduwaro, Tancoal Energy Limited na kikundi cha Umoja wa Wanawake Mbalawala (Mbalawala Women Association).

Alisema kuwa Ruanda na Ntunduwaro ni vijiji jirani vinavyozunguka mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka ambapo Umoja wa Wanawake Mbalawala ni kikundi cha wanawake walioungana kutoka vijiji vya Ruanda na Ntunduwaro.

Tancoal ni mwekezaji wa mgodi wa makaa ya mawe ya Ngaka na maana ya neno Mbalawala limetokana na jina la mto uliopo karibu na eneo la mgodi mmojawapo wa machimbo ya Ngaka wilayani Mbinga.

Wakati huo huo baadhi ya wananchi wa Dar es Salaam wametoa maoni yao tofauti juu ya dhana ya rasilimali za misitu kuwa ndiyo nishati rahisi zaidi nchini na kueleza kuwa matumizi ya nishati mbadala hususani gesi asilia katika matumizi ya kupikia ni rahisi zaidi na ina faida nyingi kuliko matumizi ya mkaa wa miti.

Anthony Ntiina ni Mkazi wa Kata Mwinjuma Wilaya ya Kinondoni, amesema yeye na familia yake ya watu watano hutumia nishati ya gesi kupikia na wamegundua faida nyingi za kiuchumi kwakuwa hutumia kiasi kidogo cha fedha katika nishati hiyo kuliko walivyokuwa wakitumia nishati ya mkaa hapo awali.

“Nilikuwa natumia karibu 4,000 kila siku kununua mkaa wa reja reja, kwa wiki mbili ilinigharimu shilingi 60,000. Kwa sasa natumia nishati ya gesi kupikia ambapo kwa wiki mbili hutumia mtungi wa gesi wa kilo sita ambao kuujaza hunigharimu shilingi 18,000 tu, hiyo ni faida kubwa” alisema Ntiina.

Alisema kwa sasa ameacha kabisa matumizi ya mkaa kwa kuwa hayana faida kiuchumi na athari zake kimazingira ni kubwa ukilinganisha na gesi ambayo matumizi yake ni rahisi na hupika kwa haraka zaidi.

Kwa upande wake mfanyabiashara, Hassan Rashid Ally ambaye ni wakala wa mitungi ya Oryx maeneo ya Mkwajuni Wilaya ya Kinondoni, amesema tatizo lililopo kwa baadhi ya wananchi ni uoga wa kuingia kwenye matumizi ya gesi wakiamini kuwa nishati hiyo ni ghali zaidi kuliko matumizi ya mkaa ambayo wameyazoea jambo ambalo sio la kweli.

Hassan alisema kuwa kwa sasa bei ya kununua mtungi na gesi ya kilo 15 ni shiingi 85,000 na bei ya kujaza mtungi mtupu ni shilingi 45,000. Kwa upande wa mtungi wa kilo 6 alisema unauzwa shilingi 70,000 pamoja na jiko lake na hujazwa kwa shilingi 18,000.

Alisema ukipiga mahesabu ya matumizi ya kawaida, mtungi wa kilo 15 huweza kutosha familia ya watu watano kwa zaidi ya mwezi mmoja. Akifananisha matumizi hayo na yale ya mkaa alisema kiwango cha mkaa kwa mwezi kwa ukubwa wa familia kama hiyo hata kama wanatumia kiwango cha chini kabisa cha 2,000 kwa siku, kwa mwezi itakua shilingi 60,000 matumizi ambayo ni ghali zaidi ukilinganisha na bei ya kujaza mtungi wa kilo 15 ambao ni shilingi 45,000 na bado matumizi yake huweza kuzidi mwezi mmoja.


Aliongeza kuwa kinachotakiwa ni wananchi kuacha uoga na kuwa na mtaji kidogo wa kuweza kumiliki mtungi wa gesi na jiko lake kwa wale watakaotumia mitungi mikubwa kuanzia kilo 15 kwenda juu na kuanza mara moja matumizi ya nishati ya gesi ambapo wataona faida zake kiuchumi na kimazingira.