slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Monday, April 30, 2018

KUNDI LA WATALII WALIOINGIA NCHINI KWA WAKATI MMOJA WAONDOKA:

Kundi la watalii 310 waliowasili nchini  kwa wakati mmoja wakitokea nchini Australia Aprili 28 mwaka huu, limekamilisha ziara yake katika hifadhi mbalimbali za Taifa nchini ikiwemo  Hifadhi ya Serengeti na Tarangire, huku ujio huu ukitajwa kuendelea kufungua fursa ya utalii wa Tanzania.

Watalii hao waliingia  nchini kupitia Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Kilimanjaro (KIA) kwa kutumia ndege kubwa aina ya Boing 747 inayomilikiwa na Shirika la Ndege la Qantas la nchini Austraria.

DK. KIGWANGALLA ATOA OFA YA MAPUMZIKO YA FUNGATE YA ALI KIBA KATIKA HIFADHI ZA WANYAMAPORI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa ofa maalum kwa Mwanamuziki, Ally Kiba, mke wake na wasaidizi wake ambao ni mdogo wake Abdu Kiba na mkewe kupumzika katika Hifadhi ya Taifa atakayoichagua wakati wa fungate yake ili aweze kufurahi vivutio vya utalii vilivyopo na hivyo kuhamasisha utalii wa ndani. Ametoa ofa hiyo jana wakati wa harusi ya msanii huyo iliyofanyika katika ukumbi wa Serena Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa sherehe hiyo na Waziri wa Afya,  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde na Mbunge wa Viti Maalum, Neema Mgaya.
 Picha ya pamoja katika sherehe hiyo iliyojumuisha Bwana Harusi, Ali Kiba, mke wake na wapambe wake na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali akiwemo Mbunge wa Viti Maalum, Mama Salma Kikwete, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimum, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde na Mwenyekiti wa UVCCM Kheri James.
Picha ya pamoja ya maharusi na viongozi wa chama na Serikali pamoja na Gvana wa Jiji la Mombasa, Rashid Bedzima (wa pili kulia).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde na  Wanamuziki, Ommy Dimpoz na Hamisi Mwanjuma MwanaFA.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akifurahia jambo na Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete wakati wa sherehe hiyo.

Saturday, April 28, 2018

MAKALA: WIZARA YA MALIASILI NA UTALII INAVYOIMARISHA SEKTA YA UHIFADHI NA UTALII NCHINI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwaongoza Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kupiga gwaride la ukakamavu muda mfupi baada ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu mafunzo ya Jeshi Usu hivi karibuni katika kituo cha Mlele mkoani Katavi.

Na Hamza Temba-WMU
........................................................
Wakati huu tunapoadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ni takriban miaka miwili sasa na miezi kadhaa tangu Serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Mhe. Rais, Dk. John Pombe Joseph Magufuli iingie madarakani.

Itakumbukwa kuwa katika hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa mjini Dodoma, Mhe. Rais Magufuli alitoa vipaombele kadhaa vya kutekelezwa na wizara zake huku Wizara ya Maliasili na Utalii akiipa vipaombele vikuu vitatu ambavyo ni kukabiliana na ujangili, kutatua migogoro ya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Wizara ya Maliasili imeendelea kutekeleza vipaombele hivyo pamoja na jukumu lake la msingi la kuhifadhi na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za maliasili na malikale, na kuendeleza Utalii kwa faida ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Ujangili

Wizara imefanikiwa kuanzisha mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori ambayo imeanza kuzaa matunda.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuanzishwa kwa Kikosi Kazi Maalum cha Kudhibiti Uhalifu wa Misitu na Wanyamapori nchini ambacho kilianzishwa mwezi Julai, 2016 sambamba na kuimarishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambayo ilianza majukumu yake rasmi tarehe 1 Julai, 2016.

Mikakati mingine ni mabadiliko ya mfumo wa utendaji kutoka ule wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu, matumizi ya teknolojia ya ndege zisizokuwa na rubani (drones) kwa ajili ya doria, ushirikishwaji wa wananchi kwenye uhifadhi na matumizi ya mbwa maalum wa kunusa ili kutambua nyara katika viwanja vya ndege na bandari.

Kupitia mikakati hiyo, mwaka 2016/2017 Wizara kupitia taasisi zake iliendesha doria mbalimbali ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 7,085 kwa makosa mbalimbali. Aidha, meno ya tembo 129 na vipande 95 vyenye uzito wa jumla ya kilo 810.03 vilikamatwa.

Vielelezo kadhaa pia vilikamatwa ikiwemo silaha za kivita 48, silaha za kiraia 150, risasi 1,058, magobore 406, silaha za jadi 22,307 na roda 120,538.

Jumla ya kesi 2,097 zilifunguliwa katika mahakama mbalimbali na kesi 802 zilimalizika. Watuhumiwa 472 katika kesi 262 walifungwa jela jumla ya miezi 42,153 na watuhumiwa 79 katika kesi 43 waliachiwa huru huku watuhumiwa wengine 469 katika kesi 276 wakilipa faini ya jumla ya shilingi  milioni 452.1.

Katika kuelekea kwenye Mfumo wa Jeshi Usu, Wizara imeendesha mafunzo kwa watumishi 661 kuhusu ukakamavu, uongozi na ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia kuhusu Ujangili. Watumishi walioshiriki mafunzo hayo ni 139 kutoka TAWA, 388 kutoka TANAPA, 117 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na 17 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. 

Kutokana na jitihada hizi hali ya ujangili imepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, katika Pori la Akiba Selous idadi ya Tembo waliouwawa imepungua kutoka tembo 17 mwaka 2015/16 hadi tembo 7 mwaka 2016/17.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, wanyamapori hasa tembo wameanza kuonekana katika maeneo mbalimbali ambayo kwa kipindi kirefu hawakuwa wakionekana, mfano hivi karibuni tembo kadhaa walionekana katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Aprili 18 mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini Dodoma, alinukuliwa akisema kuwa ujangili hapa nchini umepungua kwa zaidi ya asilimia 50.

Alisema katika kipindi cha miezi sita iliyopita hadi kufikia mwezi huu wa Aprili hakuna mauaji mapya ya wanyamapori yaliyoripotiwa kuhusiana na ujangili na kwamba nyara zinazokamatwa hivi sasa ni masalia ya zamani ambayo yanatafutiwa masoko. 

Alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama sambamba na kuwashirikisha wananchi kwa kuimarisha ulinzi na doria za mara kwa mara za kiitelijensia katika maeneo ya hifadhi.

Utalii

Katika kuongeza idadi ya watalii nchini, Wizara imeendelea kutekeleza shughuli mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya hifadhi, kuboresha miundo mbinu kwenye maeneo ya vivutio, kuanzisha huduma mpya za utalii pamoja na utangazaji.

Juhudi hizo zimewezesha ongezeko la watalii wa kimataifa kutoka 1,284,279 mwaka 2016 hadi kufikia 1,327,143 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 3.2.

Aidha, mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka 2016 hadi Dola za Marekani bilioni 2.2 mwaka 2017.

Sekta hii ya utalii imetoa ajira takriban 500,000 za moja kwa moja na ajira nyingine milioni moja zisizo za moja kwa moja kwa mwaka.

Sekta hii pia inachangia takriban asilimia 17.5 ya Pato la Taifa na wastani wa asilimia 25 ya fedha zote za kigeni.

Aidha, Wizara imedhamiria kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini kwa kufungua utalii wa Kanda ya Kusini ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ya Serikali. 

Kupitia dhamira hiyo Serikali imesaini mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia wa Dola za Marekani milioni 150, sawa na takriban shilingi bilioni 340 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Kusimamia Maliasili na Kuendeleza Utalii wa Ukanda wa Kusini –REGROW.

Mradi huu ambao maandalizi yake yalianza mwezi Novemba 2014 ulizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 12 Februari, 2018 katika viwanja vya Kihesa Kilolo Mjini Iringa huku Kauli Mbiu yake ikiwa “Utalii kwa Maendeleo Endelevu- Karibu Kusini”.

Mama Samia alisema lengo la mradi huo ni kuongeza mchango wa sekta ya maliasili na utalii katika uchumi wa taifa kwa kuboresha vivutio vya utalii, miundombinu, usimamizi wa vivutio na kuongeza faida za kiuchumi kwa jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi katika ukanda huo wa kusini.

Katika kuongeza jitihada za kutangaza utalii ndani na nje ya nchi, Wizara imeendelea kuongeza bajeti ya utangazaji ambapo Bodi ya Utalii Tanzania kwa mwaka wa fedha 2017/18 imeongezewa bajeti kufikia shilingi bilioni 6.6 ikilinganishwa na shilingi bilioni 4.1 mwaka 2016/2017 na bilioni 4.3 mwaka 2015/16.

Aidha, katika kufungua masoko mapya ya utalii nje ya nchi, Wizara inaangazia masoko mapya katika nchi za China, Israel, Urusi, Australia na nchi nyingine za Skandinavia.

Wananchi wanavyonufaika na uhifadhi 

Wizara ya Maliasili inaendelea na juhudi za kuhakikisha wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi wananufaika na rasilimali zilizopo. Kupitia Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori, jamii zinanufaika kwa kupata ajira, kitoweo, elimu, miradi ya kijamii na kuongeza kipato.

Hadi hivi sasa jumla ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori 38 zimeanzishwa. Aidha, wananchi wanaoishi jirani na misitu wananufaika kupitia miradi ya ufugaji nyuki ambapo kupitia uwezeshaji wa Mfuko wa Misitu Tanzania miradi 254 ya kuboresha kipato cha jamii zinazoishi pembezoni mwa misitu imetekelezwa.

Miradi hiyo ni ya ufugaji nyuki ambapo vikundi vya ufugaji nyuki 399 na watu binafsi 27 wamewezeshwa kupata mizinga ipatayo 11,730.

Udhibiti wa migogoro baina ya wananchi na hifadhi

Katika kudhibiti migogoro ya mipaka kati ya wananchi na maeneo jirani na hifadhi, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali na Wadau imeendelea kuhakiki mipaka yote ya maeneo ya hifadhi na kuweka alama za kudumu na mabango ya tahadhari.

Hadi kufikia mwezi Mei, 2017 vigingi 14,755 vimesimikwa sawa na asilimia 62.4 ya vigingi 23,638 vinavyohitajika katika Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro.

Aidha, kupitia program ya Panda Miti Kibiashara, Wizara imewezesha vijiji 48 kuandaa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika Wilaya za Ludewa, Madaba, Makete, Mufindi, Njombe Mjini, Njombe Vijijini, Kilolo na Nyasa.

Mikakati mipya chini ya Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla

Aidha chini ya Uongozi Mpya wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ipo baadhi ya mikakati yake mipya inayolenga kutoa uelekeo mpya wa kuimarisha sekta Maliasili na Utalii nchini.

Dk. Kigwangalla anaeleza mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuanzisha kwa mwezi maalum wa Urithi wa Mtanzania (Tanzania Heritage Month) ambao utaadhimishwa mwezi Septemba kila mwaka, kuanzishwa kwa Makumbusho ya Marais Wastaafu waliotawala Tanzania mjini Dodoma na Kuboresha na kuendeleza utalii wa fukwe kwa kuanzisha Mamlaka ya Fukwe.

Mikakati mingine ni pamoja na kujenga makumbusho ya meno ya tembo katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Iringa pamoja na kutambua barabara iliyokuwa ikitumika katika biashara ya utumwa wakati wa ukoloni ili iweze kutumika kiutalii.

Akizungumzia migogoro ya mipaka iliyopo baina ya wananchi na maeneo ya hifadhi, Dk. Kigwangalla amesema Serikali itatatua migogoro hiyo kwa kushirikisha wananchi sambamba na kuwasaidia kutatua changamoto za msingi ambazo ni kuimarisha maeneo ya malisho ya mifugo, upatikanaji wa maji kwa ajili ya wananchi na mifugo, mpango bora wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa kilimo na ufugaji.

Kwa upande wa vitalu vya uwindaji wa kitalii, Dk. Kigwangalla amesema Serikali itafanya mabadiliko katika mfumo wa ugawaji vitalu vya uwindaji wa kitalii kutoka mfumo unaotumika hivi sasa wa Kamati “Administrative Allocation” na kutumia mfumo wa mnada “Auction”.

Lengo ikiwa ni kuongeza uwazi na kuruhusu nguvu ya soko kuamua bei ambapo mapato ya Serikali nayo yatatarajiwa kuongezeka maradufu. Ili kutekeleza hilo, sheria na kanuni zinafanyiwa marekebisho.

#MWISHO#

Friday, April 27, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA SAUDI ARABIA, KUWAIT NA MSIMAMIZI WA JUMUIYA YA MAKAMPUNI YA ALBAWARDI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Msimamizi wa Makampuni ya Albawardi, Fouad Mustafa ya Umoja wa Falme za Kirabu ofisini kwake Jijini Dodoma jana ambapo walijadili uwekezaji wa kuimarisha sekta ya utalii na uhifadhi nchini. Umoja huo umeahidi kutoa ushirikiano wa ujenzi wa barabara inayounganisha Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
.........................................................................
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameonana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia na Kuwait pamoja na Msimamizi wa Jumuiya ya Makampuni ya Albawardi inayoendesha hoteli mbalimbali za kitalii nchini ikiwemo Hyatt Regency  na Four Season Serengeti ofisini kwake Jijini Dodoma jana.
Mazungumzo hayo yaliyolenga kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha sekta ya uhifadhi na utalii kwa maslahi ya nchi hizo tatu. Mabalozi hao ni Bandar Abdulla wa Saudi Arabia, Mohammad Rashed Alamiri wa Kuwait na Fouad Mustafa Msimamizi wa Makampuni ya Albawardi ya Umoja wa Falme za Kirabu kwa upande wa Tanzania na Afrika ya Mashariki.
Dk. Kigwangalla aliwaomba mabalozi hao kupitia jumuiya zao za uwekezaji kuwekeza katika miundombinu ya hoteli za kitalii Jijini Dodoma na kwenye Mapori ya Akiba katika Sakiti ya Kaskazini, Kusini na Magharibi hususan Pori la Akiba la Burigi.
Naye Msimamizi wa Jumuiya ya Makampuni ya Albawardi, kwa upande wa Tanzania na Afrika ya Mashariki, Fouad Mustafa alisema jumuiya hiyo ipo tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika ujenzi wa miundombinu ya barabara inayounganisha Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Alisema mbali na uwekezaji uliopo hivi sasa jumuiya hiyo inajenga hoteli nyingine za kitalii tatu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hifadhi ya Ngorongoro na katikati ya Jijini la Arusha ambapo ameiomba Serikali kuzifungua kupitia viongozi wake wa juu pale ujenzi wake utakapokamilika hususan Mhe. Rais.Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Msimamizi wa Makampuni ya Albawardi, Fouad Mustafa ya Umoja wa Falme za Kirabu ofisini kwake Jijini Dodoma jana ambapo walijadili uwekezaji wa kuimarisha sekta ya utalii na uhifadhi nchini. Umoja huo umeahidi kutoa ushirikiano wa ujenzi wa barabara inayounganisha Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Balozi wa Kuwait hapa nchini, Mohammad Rashed Alamiri (kushoto) ofisini kwake Jijini Dodoma jana ambapo walijadili namna ya kuimarisha sekta ya utalii na uhifadhi nchini. Wa pili kulia ni Msimamizi wa Makampuni ya Albawardi, Fouad Mustafa ya Umoja wa Falme za Kirabu ambao wameahidi kutoa ushirikiano wa ujenzi wa barabara inayounganisha Hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.Mazungumzo yakiwa yanaendelea.Waziri Kigwangalla akizungumza katika kikao hicho.Waziri Kigwangalla akiagana na msafara huo.

Tuesday, April 24, 2018

MILANZI AFAGILIA JESHI LA WANANCHI KWA MCHANGO WAKE KATIKA UHIFADHI NA ULINZI WA MALIASILI NCHINI

Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza na wanajeshi wa nchi mbalimbali za Afrika ambao wapo nchini kujifunza mambo mbalimbali ya sekta ya utalii nchini na mchango wake kwenye uchumi na namna ambavyo jeshi linashiriki kwenye ukuaji wake.

Na Mwandishi Maalum-Dar es Salaam
...................................................................................
JESHI la Wananchi licha ya kuwa na majukumu yake ya msingi ya ulinzi, limetajwa kuwa na mchango mkubwa kwenye utunzaji wa maliasili za nchi na uhifadhi kwa ujumla.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, alipokuwa akizungumza na wanajeshi wa nchi mbalimbali Afrika, ambao wanasoma kwenye chuo cha ukamanda na unadhimu cha nchini Ghana.

Wanajeshi hao, ambao wapo nchini kwa siku saba kwa ziara ya mafunzo, walikutana na Meja Jenerali Milanzi, ili kufahamu juu ya masuala mbalimbali ya sekta ya utalii nchini na mchango wake kwenye uchumi na namna ambavyo jeshi linashiriki kwenye ukuaji wake.

Akizungumza kwenye hotuba yake, Milanzi alisema sekta ya utalii pamoja na faida zake lukuki kwenye taifa lolote ikiwemo Tanzania, ina changamoto nyingi ambazo kwa namna moja au nyingine utatuzi wake unaweza kufikiwa haraka kama jeshi litashirikishwa.

"Sekta ya utalii ina changamoto kadhaa ikiwemo suala la ujangili, ambayo kwa Tanzania tumejitahidi kupambana nayo kwa msaada wa majeshi yetu ambapo kwa kufanya hivyo tumefanikiwa pakubwa," alisema.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka wanajeshi hao kutumia ziara hiyo ya kimafunzo, kujifunza namna ya kusaidia ukuaji wa sekta ya utalii nchini mwao na Afrika kwa ujumla huku pia akiwashauri wajifunze kuhusu utangamano wa bara la Afrika.  

"Nchi za Afrika ni ndugu, nimewaambia waendelee kujifunza vitu vingi kuhusu utalii wa nchi mbalimbali hasa ikizingatiwa wanyamapori hawana mipaka, kwa hivyo kama udhibiti wa ujangili utafanyika sehemu moja na nyingine pakawa hapana chochote, tatizo litaendelea kuwepo," alifafanua.

Wakitoa shukrani kwa Wizara ya maliasili na utalii, askari hao kwa nyakati tofauti walisema wamejifunza mengi kutokana na uwasilishaji wa Katibu Mkuu Milanzi na kwamba itawasaidia kwenye kukamilisha mafunzo yao mara watakaporudi chuoni.

Kwa mujibu wa Kanali Hamza Mzee, ambaye ni mwenyeji wa ugeni huo, msafara wa askari hao unahusisha watu 16 na kwamba ni ziara ya kawaida ya mafunzo kwa askari kama wanavyofanya askari wa JWTZ, wanaosoma chuo cha ukamanda na unadhimu Duluti, Arusha. 

Saturday, April 21, 2018

MASHINDANO YA OLIMPIKI 2020 NCHINI JAPAN KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII VYA TANZANIA - DK. KIGWANGALLA



Na Hamza Temba-Ngorongoro, Arusha
.....................................................................................
Mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika nchini Japan mwaka 2020 yatatumika kunadi vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia timu ya Taifa ya riadha na banda la maonesho ya utalii.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati akizungumza na wananchi muda mfupi baada ya kukamilika kwa mashindano ya riadha ya Ngorongoro Marathon 2018 katika mji wa Karatu, wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha jana.

Dkt. Kigwangalla alitoa kauli hiyo wakati akijibu ombi la Rais wa Chama cha Riadha Tanzania, Anthony Mtaka ambaye aliiomba wizara yake kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kusaidia maandalizi ya timu ya Taifa ya riadha itakayoshiriki mashindano hayo.

Mtaka pia aliomba Mamlaka hiyo itumie timu ya Taifa ya riadha Tanzania kama mabalozi wao wa kutangaza vivutio vya utalii vya hifadhi hiyo ya Ngorongoro ndani na nje ya nchi.

Akijibu maombi hayo, Dk. Kigwangalla alisema kitaundwa kikosi kazi cha pamoja kati ya wizara yake kupitia taasisi zake hususan Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Chama cha Riadha Tanzania ili kuainisha mahitaji ya mashindano hayo na kuweka makubaliano yatakayonufaisha pande zote.

"Kama tunaweza kupata jukwaa la nchi zaidi ya 50 au 100 kwa kufadhili wanariadha 200 kwenda kushiriki, manake hilo jukwaa linatulipa, kwa sababu tunawekeza kidogo tunaonekana kwa kiasi kikubwa.

"Mwaka 2020 kwenye Olimpiki lazima tuwekeze, na sisi Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zetu tutapenda tuunde kikosi kazi cha pamoja ili tuangalie gharama zinazohusika, maandalizi yanayohitajika ili na sisi kama Wizara kupitia taasisi zetu kama Ngorongoro tuweze kuona nini mchango wetu, lakini sisi tutataka tujue faida yetu hasa itakuwa ni nini" alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema mashindano hayo yatatoa fursa pana kwa Taifa kutangaza vivutio vyake mbali na juhudi zinazofanywa hivi sasa kupitia maonesho ya kimataifa. "Kupitia mashindano hayo tutapeleka pia maombi kwenye ofisi ya balozi wetu nchini Japan ili tupewe banda la kunadi vivutio vyetu vya utalii" alisema.

Dk. Kigwangalla pia aliitaka Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kukubali ombi la Chama cha Riadha Tanzania la kuanzisha kituo cha mafunzo ya riadha mjini Karatu ili kuimarisha mchezo huo na timu ya riadha Tanzania sambamba na kutumia kituo hicho kama fursa ya kutangaza utalii wa hifadhi hiyo.

Alisema kituo hicho pia kijengwe sanamu za wanariadha mashuhuri waliowahi kuiletea sifa Tanzania na kuweka rekodi mbalimbali ili kutoa motisha kwa wanariadha wengine wanaochipukia.

Alisema mbali na kuanzisha kituo hicho, timu hiyo ya Riadha Tanzania inaweza pia kupewa jina la Ngorongoro ili kuitangaza hifadhi hiyo yenye vivutio vya kipekee duniani ambavyo vimeifanya itambulike kama sehemu ya urithi wa dunia.

Mashindano ya Ngorongoro Marathon kwa mwaka huu 2018 yamehusisha washikiri kutoka Tanzania na Kenya ambapo washindi wa kwanza wa mbio hizo za kilomita 21 upande wanaume na wanawake wametoka nchini Kenya. Kaulimbiu ya mashindano hayo imelenga kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akimsalimia Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Dkt. Fredy Manongi muda mfupi kabla ya kuanza kwa mashindano hayo. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani.
Waziri Kigwangalla akiwa tayari kuzindua mashindano hayo katika umbali wa kilomita 21.
Washiriki wa mbio hizo kutoka Tanzania na Kenya wakitimua mbio kuanza mashindano hayo ya Ngorongoro Marathon 2018 umbali wa Kilomita 21 mjini Karatu mkoani Arusha. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akishiriki mashindano ya mbio za Ngorongoro Marathon 2018 na wanariadha wengine mjini Karatu mkoani Arusha jana ambapo alimaliza mbio hizo kwa kukimbia kilomita 21. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani.
Baadhi ya watalii nao walitumia fursa hiyo kusaka medali.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akishiriki mashindano ya mbio za Ngorongoro Marathon 2018 na wanariadha wengine mjini Karatu mkoani Arusha jana ambapo alimaliza mbio hizo kwa kukimbia kilomita 21. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani.
Baadhi ya washiriki wa mashindano hayo wakiwa katika harakati za kusaka medali.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akishiriki mashindano ya mbio za Ngorongoro Marathon 2018 na wanariadha wengine mjini Karatu mkoani Arusha jana ambapo alimaliza mbio hizo kwa kukimbia kilomita 21. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akihitimisha mbio za kilomita 21 za mashindano ya Ngorongoro Marathon 2018 yaliyofanyika katika mji wa Karatu mkoani Arusha jana. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani.
Haikuwa kazi rahisi, washiriki wengine walilazimika kuvua viatu na kuvaa kandambili ili kurahisiha kazi yao ya kutafuta medali.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akionesha medali aliyopewa pamoja na washiriki wengine wa mashindano ya mbio za Ngorongoro Marathon 2018 yaliyofanyika mjini Karatu mkoani Arusha jana ambapo alimaliza mbio hizo kwa kukimbia kilomita 21. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani. 
 Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki nchini Tanzania, Filbert Bayi akizungumza wakati wa hafla hiyo.
 Rais wa Chama cha Riadha Tanzania, Anthony Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akitoa salamu zake katika hagla hiyo ambapo ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kufadhili mashindano hayo.
 Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mfaume Taka akizungumza na wananchi muda mfupi baada ya kumalizika kwa mbio hizo mjini Karatu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kuhitimisha mashindano hayo mjini Karatu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi cheti cha shukurani Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Dkt. Fredy Manongi kwa kufanikisha mashindano ya mbio za Ngorongoro Marathon 2018 zilizofanyika katika mji wa Karatu mkoani Arusha jana. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi milioni moja mshindi wa kwanza wa kilomita 21  kwa wanawake, Monica Chemko kutoka Kenya katika mashindano ya mbio za Ngorongoro Marathon 2018 zilizofanyika katika mji wa Karatu, wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha jana. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akimkabidhi milioni moja mshindi wa kwanza wa kilomita 21  kwa wananume, Joseph Patha kutoka Kenya katika mashindano ya mbio za Ngorongoro Marathon 2018 zilizofanyika katika mji wa Karatu, wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha jana. Kaulimbiu ya mashindano hayo na kupiga vita ujangili na kuhamasisha utalii wa ndani.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wengine wa mashindano ya mbio za Ngorongoro Marathon 2018 yaliyifanyika mjini Karatu mkoani Arusha jana ambapo alimaliza mbio hizo kwa kukimbia kilomita 21. 

Thursday, April 19, 2018

TANZANIA KUNADI VIVUTIO VYA UTALII DUNIANI KUPITIA TAMASHA LA URITHI WA UTAMADUNI WA MABARA NCHINI UFARANSA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na tamasha la ‘Urithi wa Utamaduni wa Mabara’ Jijini Dar es Saalam jana.

...........................................

Tanzania ni miongoni mwa nchi 54 za bara la Afrika zitakazoshiriki katika tamasha la ‘Urithi wa Utamaduni wa Mabara’ linalotarajiwa kufanyika nchini Ufaransa katika mji wa ‘Cherbourg’ mwezi Julai mwaka huu.

Tanzania inashiriki tamasha hilo la kihistoria kwa mara ya kwanza ambapo itapata fursa ya kutangaza utamaduni wake na vivutio vya utalii vya mambo ya kale hivyo kuongeza idadi ya watalii na mapato.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na tamasha hilo Jijini Dar es Saalam jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, alisema tamasha hilo litatoa fursa pana kwa nchi kutangaza vivutio vyake ikiwemo vile vya Zamadamu.

“Kimsingi tamasha hilo linatarajiwa kutoa fursa kwa Tanzania kutangaza vivutio vyake na hivyo kuvutia watalii wengi kuja nchini, kila nchi itapewa banda lake la kuonyesha vivutio vyake , Tanzania naamini inakuwa na vivutio vingi vyenye kupendeza watalii kama vile Zinjathropus, Ngoma za makabila mbalimbali pamoja na nyimbo.

“Baada ya tamasha hilo, kutakuwa na ongezeko kubwa la watalii nchini na ninaamini hata zile nchi ambazo hazina rekodi nzuri ya kuja Tanzania kwa wingi  zilizopo Bara la Asia zitaanza kuja,’’. alisema Kigwangla.

Alisema tamasha hilo linalotarajiwa kuhusisha takriban nchi zote za bara la Afrika, zaidi limelenga kutangaza tamaduni na vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika mataifa yote yatakayoshiriki  huku likitajwa kuwa tamasha bora na kubwa  la utalii pengine kuliko matamasha mengine yote kutokana na kila nchi kujitokeza kuonyesha vivutio vinavyopatikana katika mataifa yao.

“Tanzania tunavyo vivutio mbalimbali tunavyotarajia kwenda kuvionyesha katika tamasha hilo, ukiacha vivutio vya mambo kale, tuna bonde la Olduvai Gorge na mengineyo, tunayoamini kuwa  kupitia tamasha hilo tutaweza kuyatangaza na hivyo kuvutia watalii wengi kuja nchini” alisema Dkt. Kigwangalla. 

Hata hivyo alisema baada ya kukamilika kwa tamasha hilo, Septemba mwaka huu hapa nchini kutakuwa na tamasha la ‘Urithi wa Mtanzania’ linalotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza na litakuwa likifanyika kila mwaka kuadhimisha urithi wa Mtanzania.

Alisema tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika kwa kipindi cha mwezi
mzima, pia litatoa fursa kwa kila wilaya kutangaza vivutio vyake, huku akizitaka kila wilaya kujiandaa na tamasha hilo, litakalotoa fursa pia kwa mikoa na wilaya hizo kukuza utalii wa maeneo yao.
 Waziri Kigwangalla akisalimiana na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo.
 Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Asngya Bangu akiongoza zoezi la utambulisho.
  Baadhi ya washiriki wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha pili cha wadau wa utalii kutoka nchi mbalimbali zinazohusika na tamasha la ‘Urithi wa Utamaduni wa Mabara’ Jijini Dar es Saalam jana.
 Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Prof. Audax mabula akizungumza katika mkutano huo.
 Picha ya pamoja ya Waziri Kigwangalla na washiriki wa mkutano huo.
 Waziri Kigwangalla akifurahia jambo na baadhi ya washiriki wa mkutano huo.