Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameagiza minada yote ya mifugo
iliyokamatwa Hifadhini baada ya Serikali kushinda kesi mahamakani ifanyike nje
ya Hifadhi ili kuondoa dhana mbaya iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa Wahifadhi hukamata mifugo hiyo ili waweze
kujiuzia wenyewe.
Pia,
Ameagiza minada hiyo itangazwe katika vijiji kabla ya tarehe ya kufanyika kwa
lengo la kuwajulisha Wananchi hata kwa wale walioshindwa kesi hizo ili
waweze kushiriki katika minada hiyo huku
Mkuu wa Wilaya husika ashirikishwe ipasavyo kwenye minada hiyo.
Akizungumza
na viongozi wa vijiji 15 katika kijiji cha Kisondoko ambavyo ni miongoni mwa
vijiji vilivyokutwa ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero lililopo katika wilaya
ya Kondoa Mkoani Dodoma, Mhe.Kanyasu
amesema minada hiyo isifanyike kwa usiri badala yake iwe wazi nje ya Hifadhi
ili kutoa fursa kwa yeyote kushiriki.
Akizungumzia
kuhusu ugumu wa kupata vibali vya
kuingilia hifadhini wakati minada ilipokuwa ikifanyikia ndani, Mhe.Kanyasu amesema kabla ya agizo hilo
wananchi waliokuwa wakishiriki katika minada hiyo walihitajika wawe na vibali vya kuingilia
hifadhini la sivyo walikuwa wakikatwa kwa kosa la kuingia hifadhini bila
kibali.
Amebainisha
kuwa endapo minada hiyo itafanyika kwa uwazi na nje ya Hifadhi kutasaidia
kuepusha shutuma nyingi zikiwemo za rushwa zinazowakabili Wahifadhi kuwa wamekuwa wakishiriki
kuwatafuta wanunuzi wa Ng'ombe kutoka mikoa ya mbali kwa makubaliano ya kulipwa
mara baada ya mnada.
Amesema
kitendo cha minada hiyo kuanza kufanyika nje ya Hifadhi kutasaidia kuondoa malalamiko kutoka kwa
wananchi ambao wamekuwa wakidai kuwa pindi mifugo yao inapotaifishwa wamekuwa
hata hawajulishwi lakini wafanyabiashara wakubwa ndo wamekuwa na taarifa.
Amesema
wananchi ambao mifugo yao imekuwa ikikamatwa na baadaye kutaifishwa wamekuwa na
chuki na Wahifadhi huku wakiwatuhumu kuwa wamekuwa wakishirikiana na
wafanyabiashara hao kwa kuwajulisha ili
wafike Hifadhini kwa ajili ya kuinunua.
Katika hatua
nyingine, Mhe.Kanyasu amewaonya askari wanyamapori wenye tabia ya kuvizia
ng'ombe wakiwa mpakani kati ya kijiji na
Hifadhi na kisha kuwasukumia ng'ombe hao ndani ya Hifadhi ili wazikamate kuwa
vitendo hivyo havikubaliki na sio kazi waliyotumwa na Serikali.
Akizungumza
mbele ya Naibu Waziri huyo, Mwenyekiti wa kijiji cha Ikengwe, Ismail Hamis
amesema licha ya huo utaratibu mpya wa kufanyia minada nje ya Hifadhi, anaiomba
serikali iangalie upya sheria ya kutaifisha mifugo kwani imepelekea wafugaji
wengi kuwa maskini.
Ameshauri
kuwa mifugo ikikamatwa ndani ya Hifadhi, waruhusiwe kulipa fidia kwa sababu
mifugo hiyo ndo imekuwa tegemeo lao kwa kuwasaidia kusomeshea watoto wao.
Kwa upande
wake, Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania,( TAWA)Mabula Misungwi amemuahidi Naibu Waziri hiyo kuwa agizo lake litatekelezwa ipasavyo
ili wananchi wa maeneo ya mifugo ilikokamatwa waweze kujulishwa.
Aidha,
Misungwi amewataka watumishi hao kujiepusha na vitendo vya rushwa pindi
wanapokamata mifugo kutoka kwa wafugaji kuwa yeyote atakayebainika
atawajibishwa kikamilifu ili iwe funzo kwa wengine.