slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Tuesday, June 5, 2018

KIGWANGALLA AAGIZA MSAKO MKALI KWA WALIOUA SIMBA TISA SERENGETI

 Baadhi ya simba kati ya tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
....................................................
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameagiza Kikosi Kazi Dhidi ya Ujangili cha Taifa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Serengeti kuwasaka watu waliohusika na mauaji ya simba tisa katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Dkt. Kigwangalla ametoa agizo hilo ofisini kwake Jijini Dodoma jana baada ya kupokea taarifa rasmi ya mauaji hayo ya kikatili yaliyoripotiwa hivi karibuni kwa simba hao kulishwa sumu kali katika kijiji hicho huku mmoja akikatwa miguu, mkia, ngozi ya juu ya mgongo na kuchukuliwa baadhi ya viungo vyake ambapo amesema mauaji hayo hayavumiliki kwa kuwa yana athari kubwa kiikolojia, kiutalii na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

"Bahati mbaya sana ni kuwa anapouawa simba kwa sumu hafi peke yake, inakufa familia nzima ya simba, na mara nyingi wanakufa pia wanyamapori wengine wanaodowea nyama na wanaokula mizoga. Walipouawa simba wa Ruaha hivi karibuni walikufa fisi zaidi ya 70 na ndege mbeshi zaidi ya 100, achilia mbali wadudu," amesema Dkt. Kigwangalla kwa masikitiko makubwa.

Amesema pamoja na faida kubwa za simba kwa Taifa kiuchumi, Kijiji cha Nyichoka pekee walikouwawa simba hao ni katika sehemu iliyofaidika sana na miradi ya ujirani mwema kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Wanyama hawa jamii ya paka wakubwa ni muhimu sana kwa kuweka mizania ya ikolojia sawa, maana wanadhibiti idadi ya wanyama wala nyasi kwa kuwala, bila hivyo hifadhi zote zinaweza kugeuka kuwa jangwa. 

"Hakuna mtalii atakayekuja hifadhini asitamani kumuangalia simba, mfalme wa pori. Wanapouawa maana yake tunashusha hadhi ya hifadhi zetu kiutalii na hivyo kutishia kupoteza mapato yanayotokana na utalii" amesisitiza Dkt. Kigwangalla. 

Amesema tukio hilo la kuuwawa kwa Simba wa Ikolojia ya Serengeti sio la kwanza kutokea hapa nchini ambapo mwishoni mwa mwaka jana simba wengine watano waliuawa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. 

"Mwaka huo huo mwanzoni simba watatu nao walipigwa risasi kikatili wilayani Serengeti huku mwaka 2015 simba 7 wakauwawa tena kwa sumu, huko huko Serengeti".

Akizungumzia sababu za ujangili huo amesema mara nyingi ni kwa ajili ya kulipiza kisasi baada ya ng’ombe wa wananchi kuliwa na simba, changamoto ambayo husababishwa na wananchi wenyewe kusogelea na kuweka makazi karibu kabisa na mipaka ya hifadhi za wanyamapori kwa lengo la kulisha mifugo pembezoni na wakati mwingine ndani ya hifadhi hizo kinyemela.

Simba ambao wanakadiriwa kuwa zaidi kidogo ya 22,000, pamoja na wanyama wengine jamii ya paka wamepungua sana miaka ya hivi karibuni kiasi cha kuwekewa tishio la kutoweka hapa duniani. Duma nao wanakadiriwa kubaki 1,200 pekee.
 Askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakikusanya miili ya simba  tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara  hivi karibuni kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vyao.
 Askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakikusanya miili ya simba  tisa waliouwawa kikatili kwa kulishwa sumu, kukatwa na kuchomolewa baadhi ya viungo vyao na wananchi katika kijiji cha Nyichoka, wilaya ya Serengeti mkoani Mara  hivi karibuni kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi kubaini chanzo cha vifo vyao.

Saturday, June 2, 2018

KIGWANGALLA AFUNGUA MAONESHO YA KIMATAIFA YA UTALII YA KARIBU/KILI FAIR 2018

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Bodi ya Utalii Tanzania, Jaji Mst. Thomas Mihayo (kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla kuhusu Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 kabla ya kuzindua maonesho hayo katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye (wa tatu kulia), Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Kampuni ya Kilifair Promotion, Tom Kunkler (kushoto).

Na Hamza Temba-WMU-Moshi
....................................................................... 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ametoa wito kwa taasisi za Serikali, jamii, sekta binafsi na wadau kwa pamoja kushirikiana kuendeleza utalii katika maeneo yao ili sekta hiyo iweze kunufaisha zaidi taifa kwa kiwango kinachostahiki kuliko ilivyo hivi sasa.


Ametoa wito huo juzi katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi wakati akifungua maonesho ya kimataifa ya utalii ya Karibu/Kili Fair 2018 ambayo yameshirikisha makampuni na wadau wa utalii zaidi ya 350 kutoka nchi zaidi ya 12 duniani huku na kuvutia watu zaidi ya 4,000 kuyatembelea.



Amesema ushirikiano huo utaiwezesha sekta hiyo kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa ambao kwa sasa ni takriban asilimia 17.2 ya pato la Taifa, zaidi ya asilimia 24 ya mapato yote ya fedha za kigeni sambamba na zaidi ya asilimia 10 ya ajira zote nchini.


Amesema mchango huo bado ni mdogo ukilinganisha na aina na idadi ya vivutio vilivyopo hapa nchini.

Dkt. Kigwangalla amesema Serikali ya awamu ya tano imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali zitakazosaidia kuboresha sekta hiyo ikiwemo ujenzi unaoendelea wa reli ya kisasa ya Standard Gauge, ujenzi wa Terminal 3 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Saalam na uboreshaji wa Shirika la Ndege la ATCL.

Pamoja na hayo amesema Serikali kupitia wizara yake inaendelea na mpango wa kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ambapo Mapori matano ya Akiba mkoani Kagera na Geita yatapandishwa hadhi kuwa Hifadhi za Taifa (Burigi, Biharamulo, Kimisi, Ibanda na Rumanyika).

"Napenda kumshukuru sana Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuridhia mapendekezo yetu ya kupandisha hadhi Mapori matano ya Akiba kuwa Hifadhi ya Taifa ambayo itaitwa Chato National Park, 'Tunatake pia advantage' ya uwepo wa uwanja wa ndege wa Chato ambao unajengwa katika kiwango cha kutua ndege kubwa zitakazowawezesha watalii kufika katika hifadhi hiyo" amesema Dkt. Kigwangalla. 

Amesema hatua hiyo itafungua utalii wa kanda ya Kaskazini Magharibi tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo ni kanda ya kaskazini pekee inayofanya vizuri zaidi kwenye sekta hiyo. Amesema mpango huo unakwenda sambamba na kufungua utalii wa kanda ya kusini ambapo mradi wa Kusimamia Maliasili na Kuendeleza Utalii Kanda ya Kusini (REGROW) upo katika hatua ya utekelezaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania, Devotha Mdachi amesema Serikali kupitia bodi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau kutangaza utalii wa Tanzania katika maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi sambamba na kuwashirikisha kunadi kauli mbiu mpya ya utalii wa Tanzania, "Unforgettable, Tanzania".

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye amesema kamati hiyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali na wadau hususan katika eneo la mabadiliko na maboresho ya sheria za kusimamia sekta hiyo iweze kuondokana na changamoto zilizopo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akijaribu kuendesha baiskeli maalum ambayo hutumika kwenye utalii wa baiskeli kwenye maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini baada ya kuzindua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi. 
Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Bodi ya Utalii Tanzania, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo na Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Devotha Mdachi wakiwa katika meza kwenye hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye kabla ya kuzindua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Ltd,Tom Kunkler, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Mkurugenzi wa Karibu Fair, Dominick Shoo na viongozi wengine wa Serikali na sekta binafsi wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kuzindua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi. 
Mkurugenzi wa Karibu Fair, Dominick Shoo akiratibu ratiba nzima ya ufunguzi wa maonesho hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye kwenye eneo la mfano wa kilele cha Uhuru cha mlima Kilimanjaro baada ya kuzindua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye na viongozi wengine wa Serikali na sekta binafsi wakiwa kwenye eneo la mfano wa kilele cha Uhuru cha mlima Kilimanjaro baada ya kuzindua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi. 
Waziri Kigwangalla akisalimia baadhi waoneshaji katika banda la utalii wa kiutamaduni kwenye maonesho hayo.
Waziri Kigwangalla akiangalia moja ya gari la kitalii la wazi katika maonesho hayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akikagua moja ya gari maalum la kusafirisha watalii ambalo limebuniwa hapa nchini na kampuni ya Hanspaul Automechs Ltd ya Jijini Arusha baada ya kufungua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkurugenzi mkuu wa Kampuni hiyo, Satbir Singh Hanspaul.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye (kulia) kwenye moja gari maalum la kifahari la kusafirisha watalii ambalo limebuniwa hapa nchini na kampuni ya Hanspaul Automechs Ltd ya Jijini Arusha baada ya kufungua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.
Waziri Kigwangalla akipanda gari maalum la kusafirisha watalii katika maonyesho hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Bodi ya Utalii Tanzania, Jaji Mstaafu Thomas, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii wa wizara hiyo, Deogratious Mdamu wakiwa ndani ya gari hilo maalum la kusafirisha watalii kwenye maonyesho hayo.
Waziri Kigwangalla akiwa amejilaza kwenye moja ya kitanda maalum katika hema la kitalii katika maonesho hayo. 
Waziri Kigwangalla akiteta jambo na Naibu Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Jorg Herera katika moja ya chumba maalum cha wazi cha kitalii katika maonesho hayo.
Waziri Kigwangalla, Naibu Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Jorg Herera na viongozi wengine wakishuka kutoka kwenye chumba hicho cha wazi cha kitalii katika maonesho hayo.
Waziri Kigwangalla akiwa kwenye banda la Bodi ya Utalii na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa bodi hiyo, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo (kushoto), Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Devotha Mdachi (wa pili kushoto), wafanyakazi wa bodi hiyo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Promotion Tom Kunkler.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akishiriki kupekecha mti maalum uliokuwa ukitumika enzi za mababu kwa ajili ya kufua moto katika Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 yanayoendelea katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye (kulia) na Mbunge wa Jimbo la Longido, Dkt. Steven Kiruswa (wa pili kulia) wakishiriki kucheza ngoma za kimasai na kikundi cha ngoma cha kabila hilo baada ya kuzindua Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Karibu/Kili Fair 2018 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi.

DKT. KIGWANGALLA ASHIRIKI MAZISHI YA MAMA YAKE MZAZI HUSSEIN BASHE WILAYANI NZEGA LEO

Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini, Dkt. Hamisi Kigwangalla akimfariji mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kufuatia kifo cha mama yake mzazi aliyezikwa leo wilayani Nzega. Kulia ni mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye. Wabunge mbalimbali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na Abdallah Bulembo wameshiriki msiba huo pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali.
 Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini, Dkt. Hamisi Kigwangalla (kulia) akimfariji mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kufuatia kifo cha mama yake aliyezikwa leo wilayani Nzega. Kulia ni mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye na mbunge wa Kigoma Vijijini, Peter Selukamba. Wabunge mbalimbali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na Abdallah Bulembo wameshiriki msiba huo pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali.
 Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini, Dkt. Hamisi Kigwangalla akitoa salamu za rambirambi katika msiba wa mama yake mzazi mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe aliyezikwa leo wilayani Nzega.
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (wa tatu kulia), Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini, Hamisi Kigwangalla (wa sita nyuma kutoka kulia), Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (wa nne kulia), viongozi wengine wa chama na Serikali na wananchi mbalimbali wakiwemo wa wilaya ya Nzega wakishiriki kusalia jeneza lenye mwili wa mama yake mzazi Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (haonekani pichani) muda mfupi kabla ya kupelekwa makaburini kwa ajili ya maziko wilayani Nzega leo.
 Jeneza lenye mwili wa mama yake mzazi Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (haonekani pichani) likiondolewa kwenye eneo la makaburi kupisha mwili huo kuhifadhiwa kwenye nyumba yake ya milelel (kaburini) wilayani Nzega leo.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (kulia), Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini, Dkt. Hamisi Kigwangalla (mbele yake kulia) na viongozi wengine wa vyama na Serikali na wananchi mbalimbali wakiwemo wa Jimbo la Nzega wakishiriki kumzika mama yake mzazi, Hussein Bashe katika makaburi wilayani humo leo.

Wednesday, May 23, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA ITALIA NCHINI, ROBERTO MENGONI

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni ofisini kwake Jijini Dodoma leo ambapo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye tafiti za binadamu wa kale katika eneo la Olduvai, kuboresha utoaji wa elimu hususan ya mapishi ya vyakula vya Kiitaliano katika Chuo cha Taifa cha Utalii na Utangazaji wa vivutio vya utalii nchini. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni baada ya mazungumzo ofisini kwake Jijini Dodoma leo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiagana na Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni baada ya mazungumzo ofisini kwake Jijini Dodoma leo.

MAPORI MATANO YA AKIBA MKOANI KAGERA NA GEITA KUPANDISHWA HADHI YA KUWA HIFADHI ZA TAIFA (NATIONAL PARKS)

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamisi Kigwangalla akizungumza bungeni alipokuwa akijibu hoja wa wabunge waliochangia mjadala wa bajeti wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma juzi.

............................................................

Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza kuanza mchakato wa kuyapandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Burigi, Kimisi, Biharamulo, Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa.

Mchakato huo tayari umeungwa mkono na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Hayo yameelezwa juzi bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati akihitimisha mjadala wa bajeti wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

“Mheshimiwa Spika, ninaomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa  Mhe. Rais ameridhia ombi letu la kupandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Burigi, Kimisi, Biharamulo, Ibanda na Chief Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa, kipekee namshukuru sana Mhe. Rais kwa kuridhia ombi letu hilo” amesema Dkt. Kigwangalla.

Amesema kufuatia hatua hiyo, wizara yake inaanzisha mchakato rasmi wa kukamilisha taratibu  za kupandisha hadhi mapori hayo ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii katika kanda ya Kaskazini Magharibi na hivyo kufikia azma ya Serikali kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 8 na mapato ya dola za kimarekani bilioni 16 katika kipindi cha miaka 7 ijayo.

Inaelezwa kuwa mchakato huo utapitia hatua mbalimbali ikiwemo kuwashirikisha wadau husika kupata maoni yao, mapendekezo kuwasilishwa baraza la mawaziri kabla ya kujadiliwa bungeni na hatimaye kuwasilishwa kwa Mhe. Rais kwa ajili ya kuidhinishwa kuwa Sheria kamili ya kupandisha hadhi mapori hayo.

Akizungumzia mikakati mingine mipya ya kuboresha sekta ya maliasili na utalii itakayotekelezwa, Dkt. Kigwangalla amesema ni pamoja na kuanzisha mamlaka ya usimamizi na uendelezaji wa utalii wa fukwe nchini, kuhuisha maeneo ya vivutio vya Mambo ya Kale na kuviunganisha katika 'package' moja ya utalii na vivutio vya wanyamapori.

Mikakati mingine ni kuunda mfumo mmoja funganishi wa TEHAMA uitwao "MNRT Portal" kwa ajili ya kutoa leseni na vibali, ukusanyaji wa takwimu na mapato kutoka vyanzo mbalimbali vya sekta ya maliasili na utalii, ambapo utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali iliwemo GePG, NIDA, TIRA, BRELA, TRA na NBS.

Amesema mikakati mingine ni kuanzisha Jeshi Usu, Utambulisho wa Utalii wa Tanzania Kimataifa ujulikanao kama "Tanzania, Unforgettable", kufungua utalii wa kanda ya kusini, kuanzisha mwezi wa maadhimisho ya Urithi wa Mtanzania "Urithi Festival"  (Septemba), kuhuisha sheria za TANAPA, TAWA na TFS, pamoja na kuunda kanuni mpya za kusimamia vizuri sekta hizo.

Pori la Akiba Burigi lina ukubwa wa kilomita za mraba 2,941 katika wilaya za Karagwe, Muleba na Ngara mkoani Kagera, wakati Pori la Kimisi likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1,030 katika wilaya za Ngara na Karagwe mkoani humo.

Pori la Akiba Biharamulo lina ukubwa wa kilomita za mraba 731 katika wilaya ya Muleba mkoani Kagera na wilaya ya Chato mkoani Geita, huku Pori la Akiba Ibanda likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 200 na Pori la Akiba Rumanyika kilomita za mraba 800 katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.

Mapori haya yapo katika ukanda muhimu wa kuunganisha watalii kutoka ikolojia za Magharibi na Mashariki ambapo uwanja wa ndege wa Chato utakuwa muhimu katika kutoa mawasiliano.

Mapori hayo ambayo yanasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA sasa yatakuwa chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania - TANAPA punde baada ya mchakato wa kuyapandisha hadhi kukamilika. 

Bunge limeidhinisha Sh. bilioni 115.794 kwa ajili ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Sh. bilioni 85.816 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh. bilioni 29,978 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza bungeni alipokuwa akijibu hoja wa wabunge waliochangia mjadala wa bajeti wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma juzi.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamisi Kigwangalla na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga wakipongezwa na wabunge mbalimbali baada ya bajeti ya wizara yao kupitishwa na Bunge juzi jioni.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa - TANAPA na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali George Waitara (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania - TAWA, Meja  Jenerali (Mstaafu) Hamis Rajabu SEMFUKO wakiwa kwenye picha ya pamoja nje ya ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitishwa na Bunge.
 Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, Katibu Mkuu, Maj. Gen. Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki, Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi pamoja na wafanyakazi wa wizara hiyo baada ya bajeti ya wizara yao kupitishwa na Bunge juzi jioni.