slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Sunday, July 8, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA AWASIMAMISHA KAZI MAOFISA NA ASKARI WOTE 27 WA TAWA KATIKA PORI LA AKIBA UWANDA

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, akimsikiliza mkazi wa kijiji cha Kilyamatundu, Shija Imeli (kulia) alipokuwa akiwasilisha malalamiko yake kuhusu tuhumu za kuwapa rushwa ya shilingi milioni 5.8 Askari watano wa Wanyamapori wa Pori la Akiaba Uwanda (pichani) ili alishe mifugo yake kwa kipindi cha miezi mitano ndani ya pori hilo.

Na Hamza Temba, Rukwa
.......................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amewasimamisha kazi Maofisa na Askari Wanyamapori wote 27 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA katika Pori la Akiba Uwanda akiwemo Kaimu Meneja, Lackson Mwamezi kwa kushindwa kusimamia vizuri pori hilo na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku tatu tangu amsimamishe kazi meneja wa Pori hilo, Mark Chuwa kwa tuhuma kama hizo pamoja na tuhuma nyingine ikiwemo kushindwa kuondoa ngo'mbe zaidi ya 12,000 ambao wamedaiwa kuwepo ndani ya pori hilo.

Pori la Akiba Uwanda lipo katika bonde la ziwa Rukwa katika wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa na linasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Dk. Kigwangalla amefanya uamuzi huo jana alipotembelea pori hilo sambamba na kufanya mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kilyamatundu ambapo alipokea taarifa ya malalamiko kuhusu askari hao kupokea rushwa kutoka kwa watu wenye uwezo na kuwaruhusu kuchunga hifadhini huku wakiwanyanyasa masikini kwa kukamata mifugo yao.

Alifafanua tuhuma hizo kuwa ni pamoja na kudaiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wavuvi wanaovua samaki Ziwa Rukwa kwa kuwatozwa kila mmoja Sh. 100,000/- kwa mwezi na kuruhusu mifugo kuchungwa hifadhini kwa kipindi cha  miezi mitatu ambapo  kila mfugaji hutozwa  kati ya Shilingi milioni sita hadi saba.

Dk. Kigwangalla pia ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru kuchunguza mali  na tuhuma za rushwa walizopewa askari wote wa pori hilo wakiwemo watano waliotuhumiwa kwenye mkutano wa hadhara kwa kuomba rushwa ya shilingi milioni 6 kwa ndugu Shija Imeli ili wamruhusu kulisha mifugo yake hifadhini kwa muda wa miezi mitano.

Shija alisema mnamo tarehe 05 Januari mwaka huu akiwa nyumbani kwake na Ndugu Shemen Kuzenza, askari watano wa pori hilo walifika nyumbani kwake na kumtishia kuwa endapo atalisha mifugo hifadhini wangemkamata huku wakijua hana sehemu nyingine ya malisho hivyo wakamtaka kutoa rushwa ya shilingi milioni 6 ili aruhusiwe kulisha mifugo yake hifadhini kwa muda wa miezi mitano.

Alisema walifanikiwa kuwapa askari hao jumla ya shilingi mil. 5.8 kwa nyakati tofauti na kwamba walivyoshindwa kumalizia laki 2 zilizobakia askari hao walikamata mifugo yao nje ya eneo la hifadhi.

Kufuatia malalamiko na tuhuma hizo, Dk. Kigwangalla aliitisha gwaride la utambuzi lililohusisha askari wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania (JWTZ), askari  wa usalama barabarani na maofisa na askari wanyamapori wa TAWA waliokuwepo katika mkutano huo wa hadhara.

Shija na mwenzake Kusenza waliweza kuwatambua askari watano wa TAWA waliowatuhumu kuwaomba rushwa na hapo hapo Waziri Kigwangalla akawaamuru kukabidhi silaha zao na kumuagiza  Mkuu wa Polisi wa  Wilaya ya Kipolisi  ya Laela, Aloyce Nyatola kuwakamata mara moja na TAKUKURU ianze uchunguzi wa tuhuma hizo ili sheria ichukue mkondo wake na iwe fundisho kwa wengine. 

Hata hivyo, baada ya mkutano wa hadhara, Dk. Kigwangalla aliamua kukagua baadhi ya maeneo ndani ya pori hilo na kubaini uharibifu mkubwa uliofanywa na mifugo huku dalili zikiwa ni kinyesi cha ng'ombe kilichokuwa kimezagaa kila mahali. 

Hapo hapo alimuagiza Mkurugenzi Mkuu TAWA, Dk. James Wakaibara ambaye aliwakilishwa na Mkurugenzi wa Biashara na Huduma za Utalii wa mamlaka hiyo, Imani Nkuwi kuwasimamisha kazi wafanyakazi wote wa pori hilo na kuleta wengine wapya wasimamie pori hilo ili kupisha uchunguzi.

"Hawa wote wasimamishwe kazi na uchunguzi ufanyike kitu gani kilikua kinaendelea hapa, kwanza ifanyike parade kuhusu suala la kumuomba rushwa yule mfugaji, wabainike moja kwa moja wafunguliwe mashtaka, na hawa wote nataka wachungunguzwe na mali walizonazo kama ambavyo imeelezwa kuwa hawa wametumia hili pori kama kitega uchumi chao binafsi, huu ni uhujumu uchumi" aliagiza Dk. Kigwangalla.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ametoa siku 30 kwa wananchi wote  wenye mifugo ndani ya pori hilo kuitoa kwa hiari yao wenyewe kabla ya operesheni maalum itakayowaondoa kwa nguvu. Alisema kama walijua pori hilo ni shamba la bibi sasa wasahau na wajipange namna ya kutafuta malisho au kupunguza idadi ya mifugo yao na kuanzisha miradi mingine ya maendeleo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, akiamuru askari watano wa Pori la Akiba Uwanda wanyang'anywe silaha zao na wawekwe chini ya ulinzi kwa ajili ya uchunguzi baada ya kutambuliwa kwenye gwaride kwa tuhuma kupokea rushwa ya shilingi milioni 5.8 kutoka kwa mfugaji, Shija Imeli (Kulia) kwa makubaliano ya kulisha ng'ombe wake ndani ya pori hilo kwa muda wa miezi mitano.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa mkoa wa Rukwa, wakikagua mazingira ya Pori la Akiba Uwanda baada kuwasimamisha kazi maafisa na askari wote 27 wa pori hilo kupisha uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili. Watumishi hao wananalalamikiwa kupewa rushwa ili kuruhusu wananchi wachunge mifug hifadhini na kwa wale ambao hawatoi rushwa huishia kukamtwa mifugo yao. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa mkoa wa Rukwa, wakikagua mazingira ya Pori la Akiba Uwanda baada kuwasimamisha kazi maafisa na askari wote 27 wa pori hilo kupisha uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili. Watumishi hao wananalalamikiwa kupewa rushwa ili kuruhusu wananchi wachunge mifug hifadhini na kwa wale ambao hawatoi rushwa huishia kukamtwa mifugo yao.

Saturday, July 7, 2018

WANANCHI WA KALAMBO WAZUIA KWA MUDA MSAFARA WA WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akijibu kero mbalimbali za wananchi wa kijiji cha Kisumba katika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa baada ya msafara wake kusimamishwa na wananchi hao jana.

Na Hamza Temba, Kalambo, Rukwa
...........................................

Msafara wa Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla umelazimika kusimama kwa muda baada ya kusimamishwa na kundi kubwa la wananchi wa kijiji cha Kisumba kilichopo wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa wakiwa na mabango yanayoeleza kero zao mbalimbali.

Miongoni mwa kero hizo ni pamoja na wanyamapori jamii ya Tembo kuvamia mashamba yao na hivyo kukosa chakula na kukosekana kwa huduma muhimu ya maji iliyotokana na kuchakachuliwa kwa mradi wa maji wa jumla ya shilingi milioni 663 kijijini hapo.

Mkazi wa kijiji hicho, Leonard Kiombe, alisema mara nyingi wamekuwa wakiwasimamisha viongozi kwa sababu ya kero ya maji, "tulipata mradi wa milioni 663 wakasema zaidi ya vijiji 6 vitapata maji lakini kijii cha kisumba mpaka sasa hatuna maji, mradi umechakachuliwa na maji hayatoki" alisema.

Akijibu kero hizo, Waziri Kigwangalla amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha Taasisi za Uhifadhi wa Wanyamapori pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS wanashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kutengeneza vikundi vya wananchi wa vijiji vyote vinavyopakana na Hifadhi ya Msitu wa Kalambo na Pori la Akiba Lwafi ili wawezeshwe fedha za mikopo ama mizinga ya kufugia nyuki ambayo wataipanga pembezoni mwa mashamba yao ili kuzuia tembo wasiingie kwenye mashamba. 

Alisema teknolojia hiyo imethibitika kusaidia kudhibiti tembo wasilete madhara kwenye makazi ya watu kwa kuwa nyuki hufukuza tembo na endapo tembo nao wakinusa harufu ya nyuki huwa sio rahisi kusogelea maeneo hayo, hivyo ameagiza mradi huo utekelezwe ndani ya kipindi cha miezi miwili kabla mvua za masika kuanza.

Waziri Kigwangalla pia ametoa wito kwa wananchi hao kuacha kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo maeneo ya mapito ya wanyamapori kwakuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha na ustawi wao.

Akizungumzia kero ya maji, Dk Kigwangalla aliwaahidi wananchi hao kuiwasilisha kwa waziri husika ili iweze kuapatiwa ufumbuzi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akiondoka kuendelea na ziara yake baada kujibu kero mbalimbali za wananchiwaliosimamisha msafara wake katika kijiji cha Kisumba katika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa jana. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura na Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Rukwa, Albinus Mugonya ambaye amebeba mabango yenye kero za wananchi hao. 
 Sehemu ya wananchi hao wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akijibu kero mbalimbali za wananchi wa kijiji cha Kisumba katika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa baada ya msafara wake kusimamishwa na wananchi hao jana.

Thursday, July 5, 2018

MIFUGO ITAKAYOKAMATWA KWENYE MAENEO YA HIFADHI ITATAIFISHWA BILA YA HURUMA - DK. KIGWANGALLA


 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Said Mtanda (kushoto) alipowasili wilayani hapo jana kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja  ya kukagua shughuli za uhifadhi mkoani Rukwa. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa, Albinus Mugonya.

Na Hamza Temba, Nkasi Rukwa
...............................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametangaza zoezi rasmi la kuanza kutaifishwa mifugo itakayokutwa kwenye maeneo ya hifadhi nchini kinyume cha sheria ili kukomesha vitendo hivyo.

Dk. Kigwangalla ametoa tamko hilo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kizi kinachopakana na Pori la Akiba Lwafi lililopo wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani humo .

Amesema Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009, Kifungu cha 111 kinaruhusu kutaifisha mifugo na mali itakayokamatwa hifadhini. 

Amesema kwa kipindi cha miezi tisa tangu ateuliwe kuiongoza wizara hiyo amekuwa akitoa msamaha kwa wnanchi wanaakamatwa na mifugo hifadhini jambo ambalo kwa sasa hatofanya tena kwakuwa elimu imeshatolewa vya kutosha.

"Maeneo ya hifadhi sio shamba la bibi lisilokuwa na mwenyewe, ni lazima watu waheshimu sheria za uhifadhi, nawahakikishia tukiwakuta kwenye maeneo ya hifadhi, tutawakamata na kutaifisha mifugo yenu, hakutakuwa na huruma wala msalia mtume" alisisitiza Dk. Kigwangalla.

Wakati huo huo Dk. Kigwangalla ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuwasilisha ahadi iliyotolewa na Waziri aliyemtangulia ya shilingi milioni 3 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Kizi. Pia ameiagiza mamlaka hiyo kuchangia mabati kwa ajili ya darasa moja katika kijiji hicho ili wananchi wanufaike na faida inayopatikana kwenye uhifadhi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Said Mtanda (kushoto) alipowasili wilayani hapo jana kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja  ya kukagua shughuli za uhifadhi mkoani Rukwa.

Dk. Kigwangalla akizungumza katika mkutano huo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla na Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda (wa tatu kulia) wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Imani Nkui alipotembelea msitu wa Mfiri ambao ni chanzo cha maji yanayonyesha mji wa Namanyere wilayani Nkasi wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja  kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi mkoani Rukwa.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kizi wilayani Nkasi wakati wa ziara yake ya siku moja kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi mkoani Rukwa.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (wa tatu kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa TAWA, Imani Nkuwi (wa pili kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Pori la Akiba Lwafi alipotembelea maporomoko ya Ntembwa (pichani nyuma) ambayo ni kivutio cha utalii katika pori hilo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi katika wilaya Nkasi mkoani Rukwa jana. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla (wa tatu kushoto waliosomama) na Kaimu Mkurugenzi wa TAWA, Imani Nkuwi (wa pili kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Pori la Akiba Lwafi alipotembelea maporomoko ya Ntembwa (pichani nyuma) ambayo ni kivutio cha utalii katika pori hilo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi katika wilaya Nkasi mkoani Rukwa jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia mandhari ya Pori la Akiba Lwafi alipotembelea maporomoko ya Ntembwa (pichani nyuma) ambayo ni kivutio cha utalii katika pori hilo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani Nkasi mkoani Rukwa jana.

Wednesday, July 4, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA AAGIZA TFS KUCHANGIA MILIONI 20 KWA AJILI YA UJENZI WA ZAHANATI SUMBAWANGA, AMSIMAMISHA KAZI MENEJA WA PORI


 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa mkoa wa Rukwa wakikagua eneo shamba la miti kwenye Msitu wa Mbizi wilayani Sumbawanga jana. Aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda.

Na Hamza Temba, Rukwa
........................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS kuchangia shilingi milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Ametoa agizo hilo kufuatia taarifa iliyowasilishwa kwake na Mtendaji wa Kata ya Majengo, Matage Bikaniko Mjarifu alipotembelea kijiji hicho kinachopakana na Msitu wa Mbizi ambapo amesema wananchi wa kijiji hicho husafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 11 kwa ajili ya kufuata huduma za afya mjini Sumbawanga.

Amesema mpaka sasa wananchi wa kijiji hicho wameshachangia shilingi laki 9 na Mbunge wa Sumbawanga mjini shlingi milioni 5. Hata hivyo amesema jumla ya shilingi milioni 134 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.

Kufuatia taarifa hiyo, Waziri Kigwangalla alisema Wizara yake kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS itachangia shilingi Milioni ishirini hivyo wananchi wapambane kwa kushirikiana na halmashauri yao ili jengo hilo lisimame na hatimaye fedha hizo ziwasilishwe kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake.  

Alisema Falsafa ya Uhifadhi Endelevu ni Uhifadhi Shirikishi Jamii, hivyo wizara yake itaendelea kusimamia sera ya kuhakikisha wananchi hususan wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi wananufaika moja kwa moja na hifadhi hizo kupitia miradi ya maendeleo.

Dk. Kigwangalla ameziagiza taasisi zote za uhifadhi nchini kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii ili wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hizo waone umuhimu wa hifadhi hizo moja kwa moja na hivyo kutoa ushirikiano kwenye uhifadhi.

Katika hatua nyingine, Waziri Kigwangalla amemsimamisha kazi Meneja wa Pori la Akiba Uwanda, katika wailaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Mark Chuwa kwa tuhuma za kushindwa kuondoa mifugo zaidi ya 12,000 iliyopo ndani ya hifadhi hiyo.

Kabla ya uamuzi huo, akisoma taarifa ya mkoa kwa Waziri huyo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Khalfan Haule alisema uvamizi katika pori hilo umekuwa wa kiasi kikubwa  ambapo wafugaji huingia na makundi makubwa ya mifugo na kugeuza eneo hilo sehemu ya malisho.

Alisema licha ya na kufanyika kwa opresheni za mara kwa mara za kuondoa mifugo hiyo, baada ya muda mfupi wafugaji hao hurejea na makundi makubwa ya mifugo kwa ajili ya malisho.

Hata hivyo Dk. Kigwangalla alishangazwa na uongozi wa mkoa na wilaya kwa kushindwa kuchukua hatua za kuondoa mifugo hiyo hifadhini wakati sheria za uhifadhi haziruhusu mifugo hifadhini.
 Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia eneo linalojengwa zahanati ya kijiji cha Mponda ambayo ameahidi wizara yake kuchangia ujenzi wake wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani Sumbawanga jana. Ambapo aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda. Wapili kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Khalfan Haule. 
 Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwapungia mkono wananchi wa kijiji cha Mponda katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani humo jana. Aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda. Kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Khalfan Haule.
 Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akicheza ngoma na wananchi wa kijiji cha Mponda katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani humo jana. Aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda. Kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Khalfan Haule.
 Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Mponda katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani humo jana ambapo aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda. Kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Khalfan Haule.
 Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na baadhi ya wanafunzi katika kijiji cha Mponda Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wilayani humo jana. Aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda. Kulia kwake ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Khalfan Haule.
Waziri wa Maliasili na Ualii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata ufafanuzi kuhusu upandaji wa miti kutoka kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Zawadi Mbwambo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi katika msitu wa Mbizi wilayani Sumbawanga jana. Aliiagiza TFS kuchangia milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda.

WAZIRI KIGWANGALLA AHITIMISHA ZIARA YAKE MKOANI MBEYA, ATEMBELEA MAPOROMOKO YA KIMANI

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipiga picha ya pamoja (Selfie) kwa kutumia simu yake ya mkononi na baadhi ya wafanyakazi wa Pori la Akiba Mpanga Kipengere alipotembelea pori hilo jana kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi. Nyuma yao ni Maporomoko ya Mto Kimani ambayo yana urefu wa mita 70, na ni chanzo kikuu cha maji yanayounda mto Ruaha hadi mto Rufiji. 

Mbali na maporomoko hayo pori hilo pia lina wanyamapori mbalimbali ikiwemo Tumbili, Nyani, Tandala, jamii ya ndege mbalimbali ikiwemo wahamao kutoka ulaya wakati wa baridi kali na aina mbalimbali za maua ya asili ya kuvutia. 

 Dk. Kigwangalla amesema maporomoko hayo hayakuwahi kutumika ipasavyo kiutalii kutokana na kukosekana kwa miundombinu muhimu ikiwemo barabara ya kufika eneo hilo. Amesema katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha barabara hizo pamoja na kujenga ngazi kushuka kwenye kina cha maporomoko hayo hadi upande wa pili. Pori hilo pia lina kivutio cha pango alilojificha chief Mkwawa wakati wa vita ya pili ya dunia. 

Kuna aina mbalimbali za utalii katika pori hilo ikiwemo utalii wa kupanda mlima, utalii wa kuogelea, utalii wa kutembea kwa miguu na utalii wa picha.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Mpanga Kipengere ambalo lipo katika wilaya za Mbarali (Mbeya), Makete na Wanging'ombe (Njombe) jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Mpanga Kipengere ambalo lipo katika wilaya za Mbarali (Mbeya), Makete na Wanging'ombe (Njombe) jana.
 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipiga jaramba wakati akikagua shughuli za uhifadhi katika Pori la Akiba Mpanga Kipengere ambalo lipo katika wilaya za Mbarali (Mbeya), Makete na Wanging'ombe (Njombe) jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akioneshwa Maporomoko ya Mto Kimani (hayako pichani) na Meneja wa Pori la Akiba Mpanga Kipengere, Stanslaus Odhiambo alipotembelea pori hilo kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi katika wilaya ya Makete mkoani Njombe jana. Maporomoko hayo yenye urefu wa mita 70 ni chanzo kikuu cha mto Ruaha Mkuu na Mdogo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akioneshwa ramani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Dk. Chris Timbuka (wa pili kulia) alipotembelea bonde la Ihefu kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi  mkoani Mbeya jana. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Imani Nkuwi na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfaume.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akioneshwa Maporomoko ya Mto Kimani na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Imani Nkuwi alipotembelea Pori la Akiba Mpanga Kipengere ambalo lipo katika wilaya za Mbarali (Mbeya), Makete na Wanging'ombe (Njombe). Maporomoko hayo yenye urefu wa mita 70 ni chanzo kikuu cha mto Ruaha Mkuu na Mdogo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Wawindi iliyopo wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo iliyofadhiliwa na Shirika la  Hifadhi za Taifa (TANAPA) shuleni hapo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya Sekondari Igaza iliyopo wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo iliyofadhiliwa na Shirika la  Hifadhi za Taifa (TANAPA) shuleni hapo. 

Tuesday, July 3, 2018

DK. KIGWANGALLA ATOA ONYO KALI KWA WANAOCHIMBA MADINI KWENYE MSITU WA HIFADHI JIJINI MBEYA, AAGIZA UONGOZI WA MKOA KUWATAFUTIA MAENEO MBADALA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa Mkoa wa Mbeya akiwemo Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makala wakitembea mwendo wa mchakamchaka alipokuwa akikagua eneo la Hifadhi ya Msitu wa Palamela wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya jana.

Na Hamza Temba, Mbeya
.............................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa onyo kali kwa wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uchimbaji wa mchanga wa madini ya dhahabu (makinikia) ndani Hifadhi ya Msitu wa Palamela katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Amesema sheria za uhifadhi na mazingira hazihusu mtu yeyote kuchimba madini katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria bila ya kuwa na kibali maalum kutoka mamlaka husika.

Ametoa onyo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mwaoga, wilaya ya Chunya mkoani Mbeya baada ya kukagua na kuona uharibifu mkubwa uliofanywa na wachimbaji hao kwenye hifadhi hiyo.

"Yeyote anayehitaji kuchimba madini kwenye maeneo ya hifadhi ni sharti afuate taratibu za kisheria ikiwepo kupewa kibali halali cha kufanya kazi hiyo, la sivyo tutakaowakamata tutawachukulia hatua kali za kisheria" alisema Waziri Kigwangalla.

Ili kudhibiti vitendo hivyo visiendelee, Waziri huyo ameagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuweka kituo cha kudumu cha ulinzi katika eneo hilo ili kuwazuia wananchi watakaojitokeza kufanya shughuli hizo za uharibifu wa hifadhi hiyo.

Amesema, amebaini kuwa maeneo mengi makubwa ya uchimbaji wa madini katika wilaya hiyo yamemilikishwa matajiri wachache hali inayosababisha wananchi wa kawaida kukosa maeneo ya uchimbaji na hivyo kulazamika kuingia kwenye maeneo ya hifadhi.

Kufuatia changamoto hiyo, Dk. Kigwangalla ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Chunya kuona uwezekano wa kuwapa maeneo mbadala wachimbaji wadogowado katika maeneo ya wazi ili nao waweze kufaidika na rasilimali hiyo na hatimaye kuepuka uharibifu wa mazingira kwa kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala alisema kufuatia malalamiko ya wananchi hao juu ya uwepo wa matajiri wachache waliomilikishwa maeneo hayo ya uchimbaji, ndani ya wiki hii atamtuma Kamishna wa Madini wa Kanda na wataalam wengine kuchunguza ukweli wake pamoja na kubaini mahitaji halisi ya wananchi hao ili aweze kumshauri Waziri husika namna kumaliza mgogoro huo.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Zawadi Mbwambo alisema sheria zinarubusu watu kuchimba madini kwenye maeneo ya hifadhi kwa kufuata taratibu maalum.

Alizitaja taratibu hizo kuwa ni pamoja na kutambua eneo husika, mmiliki wake, kuomba leseni Wizara ya Nishati, kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kama itathibitika kutokuwepo kwa athari hizo, muhusika atapewa leseni kutoka kwa Afisa Misitu wa Wilaya husika.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala wakikagua eneo lililoharibiwa kwa kuchimbwa mchanga wa dhahabu (makinikia) kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wikaya ya Chunya mkoani Mbeya jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua mchanga wa dhahabu (makinikia) ambao umetaifishwa na Serikali baada ya kuchimbwa kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wikaya ya Chunya mkoani Mbeya jana. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Amos Makala.
  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi kwenye Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisoma bango lenye ombi la kutoa eneo la uchimbaji wa madini ya dhahabu ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mwaoga, wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani humo jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi kwenye Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Mwaoga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi kwenye Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya jana. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala akiwa anafafanua jambo kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa akizungumza katika mkutano huo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Zawadi Mbwambo akifafanua kuhusu sheria na taratibu za uchimbaji madini kwenye maeneo ya hifadhi.

Sunday, July 1, 2018

DK.KIGWANGALLA ATOA SIKU 90 KWA TAWIRI KUFANYA SENSA YA MAMBA ZIWA RUKWA NA TFS KUANDAA MPANGO WA KITAIFA WA UVUNAJI MISITU


Na Hamza Temba, Songwe
....................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kufanya utafiti na sensa ya mamba katika ziwa Rukwa ili kubaini idadi yake na hatimaye kuishauri Serikali namna ya kudhibiti madhara yanayosababishwa na mamba hao kwa wananchi hususan wa jimbo la Songwe ikiwemo kuwavuna kama idadi yao itabainika kuwa kubwa kupita kiasi.

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo jana katika kijiji cha Maleza, kata ya Mbangala, wilaya ya Songwe mkoani Songwe alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua mgogoro uliopo baina ya wananchi na Mamba wa ziwa Rukwa.

"Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori ambayo ipo chini ya wizara yangu, nawaagiza wafike hapa mara moja, ndani ya miezi mitatu wanipe majibu nini kifanyike kupunguza madhara yanayotokana na mamba kwenye ziwa Rukwa, wafanye sensa watuambie kuna Mamba wangapi lakini pia watushauri nini tufanye ili kudhibiti mamba hao wasiendelee kusababiaha athari kubwa kwenye maisha ya watu wanaoishi jirani, lakini pia wanaoutumia ziwa.

"Kwa sababu madhara yanaweza yakawa mengi, inawezekana mamba wameshakuwa wengi na samaki wamebaki wachache, kwahivyo hata mamba nao mwishowe wataanza kufa ama wataanza kutafuta chanzo kingine cha chakula pengine ndio maana wameanza kutafuta binadamu wanakwenda ziwani kwasababu wanakuwa na njaa, inabidi wasogee ufukweni wawinde chochote kinachosogea karibu na maji" alifafanua Dk. Kigwangalla. 

Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo kufuatia malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa kwake na mbunge wa Jimbo la Songwe, Phillipo Mulugo ambaye amesema kumekuwepo na matukio mengi ya mamba kushambulia na kuuwa wananchi wa vijiji jirani wanaofata huduma mwambao wa ziwa Rukwa. 

Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa Wakala wa Huduma za misitu Tanzania kuandaa mpango wa kitaifa kwa kila wilaya na vijiji nchini utakaoweka utaratibu maalum wa namna na sehemu wananchi watakayopata huduma ya kuni mkaa.

"Utaratibu uwekwe na muuweke nchi nzima, kila wilaya, kila kata, kila kijiji uwekwe utaratibu wananchi watapata wapi mkaa, watapata wapi kuni, kibali cha kuvuna kitapatikana wapi, utaratibu uwe wazi, sio kusubiri kwenye mageti unakamata, hapana weka utaratibu kwanza, ukishaweka utaratibu atakayevunja sheria hata ukimkamata ukimpeleka polisi utakuwa umemrahisishia OCD kazi. 

"Kwa sababu hata OCD atakuwa anajua kwamba katika hii wilaya ninayoiongoza hapa ndio mipaka ya mkaa, hapa ni mipaka ya kuni, wewe umetoa wapi, kibali chako kiko wapi, umevunja sheria, mahakamani" ameeleza Dk. Kigwangalla. 

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ametangaza kutaifishwa kwa greda ambalo limekutwa likiwa limetelekezwa na watu wasiojulikana ambao walikuwa wakichimba mchanga wa dhahabu (makinikia) kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi ya msitu wa Patamela wakati wa ziara yake wilayani Songwe.

Kufuatia tukio hilo, amemuagiza Kamanda wa Polisi wa wilaya hiyo kulinda eneo hilo na kutafuta dereva atakayeendesha greda hilo hadi kituo cha polisi kwa ajili ya kufuata taratibu za sheria za kulitaifisha na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa kijiji cha Maleza kata ya Mbangala wilaya ya Songwe mkoani Songwe alipofanya ziara ya kikazi katika kijiji hicho jana kwa ajili ya kutatua mgogoro wa mamba wa ziwa Rukwa ambao wamekuwa wakidhiru wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akitoa agizo la kutaifishwa kwa greda (pichani nyuma) lililokutwa ndani Hifadhi ya Msitu wa Patamela baada ya kutelekezwa na watu watu wasiojulikana waliokuwa wakichimba mchanga wa dhahabu (makinikia) kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi hiyo katika wilaya ya Songwe mkoani Songwe jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akitoa maelekezo kwa uongozi wa wilaya ya Songwe kufuatia greda lililokutwa ndani Hifadhi ya Msitu wa Patamela ambalo limetelekezwa na watu wasiojulikana waliokuwa wakichimba mchanga wa dhahabu (makinikia) kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi hiyo katika wilaya ya Songwe mkoani Songwe jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akishirikiana na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Songwe kuzima moto uliokutwa ukiwaka ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo jana.
Dk Hamisi Kigwangalla akishirikiana na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Songwe kuzima moto uliokutwa ukiwaka ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo jana.
Juhudi za kuzima moto zikiwa zinaendela.
Dk Kigwangalla akiwa anazungumza na wananchi wa kijiji Maleza.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Songwe, Philipo Mulugo alipokuwa akiwasilisha malalamiko ya wananchi wa jimbo lake ambao wamekuwa wakipata madhara makubwa ya mamba wa ziwa Rukwa.