slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Tuesday, July 3, 2018

DK. KIGWANGALLA ATOA ONYO KALI KWA WANAOCHIMBA MADINI KWENYE MSITU WA HIFADHI JIJINI MBEYA, AAGIZA UONGOZI WA MKOA KUWATAFUTIA MAENEO MBADALA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa Mkoa wa Mbeya akiwemo Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makala wakitembea mwendo wa mchakamchaka alipokuwa akikagua eneo la Hifadhi ya Msitu wa Palamela wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya jana.

Na Hamza Temba, Mbeya
.............................................................

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ametoa onyo kali kwa wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uchimbaji wa mchanga wa madini ya dhahabu (makinikia) ndani Hifadhi ya Msitu wa Palamela katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Amesema sheria za uhifadhi na mazingira hazihusu mtu yeyote kuchimba madini katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria bila ya kuwa na kibali maalum kutoka mamlaka husika.

Ametoa onyo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mwaoga, wilaya ya Chunya mkoani Mbeya baada ya kukagua na kuona uharibifu mkubwa uliofanywa na wachimbaji hao kwenye hifadhi hiyo.

"Yeyote anayehitaji kuchimba madini kwenye maeneo ya hifadhi ni sharti afuate taratibu za kisheria ikiwepo kupewa kibali halali cha kufanya kazi hiyo, la sivyo tutakaowakamata tutawachukulia hatua kali za kisheria" alisema Waziri Kigwangalla.

Ili kudhibiti vitendo hivyo visiendelee, Waziri huyo ameagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuweka kituo cha kudumu cha ulinzi katika eneo hilo ili kuwazuia wananchi watakaojitokeza kufanya shughuli hizo za uharibifu wa hifadhi hiyo.

Amesema, amebaini kuwa maeneo mengi makubwa ya uchimbaji wa madini katika wilaya hiyo yamemilikishwa matajiri wachache hali inayosababisha wananchi wa kawaida kukosa maeneo ya uchimbaji na hivyo kulazamika kuingia kwenye maeneo ya hifadhi.

Kufuatia changamoto hiyo, Dk. Kigwangalla ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Chunya kuona uwezekano wa kuwapa maeneo mbadala wachimbaji wadogowado katika maeneo ya wazi ili nao waweze kufaidika na rasilimali hiyo na hatimaye kuepuka uharibifu wa mazingira kwa kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala alisema kufuatia malalamiko ya wananchi hao juu ya uwepo wa matajiri wachache waliomilikishwa maeneo hayo ya uchimbaji, ndani ya wiki hii atamtuma Kamishna wa Madini wa Kanda na wataalam wengine kuchunguza ukweli wake pamoja na kubaini mahitaji halisi ya wananchi hao ili aweze kumshauri Waziri husika namna kumaliza mgogoro huo.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Zawadi Mbwambo alisema sheria zinarubusu watu kuchimba madini kwenye maeneo ya hifadhi kwa kufuata taratibu maalum.

Alizitaja taratibu hizo kuwa ni pamoja na kutambua eneo husika, mmiliki wake, kuomba leseni Wizara ya Nishati, kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kama itathibitika kutokuwepo kwa athari hizo, muhusika atapewa leseni kutoka kwa Afisa Misitu wa Wilaya husika.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala wakikagua eneo lililoharibiwa kwa kuchimbwa mchanga wa dhahabu (makinikia) kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wikaya ya Chunya mkoani Mbeya jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akikagua mchanga wa dhahabu (makinikia) ambao umetaifishwa na Serikali baada ya kuchimbwa kinyume cha sheria ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wikaya ya Chunya mkoani Mbeya jana. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Amos Makala.
  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi kwenye Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisoma bango lenye ombi la kutoa eneo la uchimbaji wa madini ya dhahabu ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Patamela kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mwaoga, wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani humo jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi kwenye Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya jana.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Mwaoga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutatua changamoto za uhifadhi kwenye Hifadhi ya Msitu wa Patamela katika wilaya ya Chunya mkoani Mbeya jana. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala akiwa anafafanua jambo kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa akizungumza katika mkutano huo.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Zawadi Mbwambo akifafanua kuhusu sheria na taratibu za uchimbaji madini kwenye maeneo ya hifadhi.

No comments:

Post a Comment