Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akijibu kero mbalimbali za
wananchi katika kijiji cha Mariwanda kata ya Hunyari wilaya ya Bunda mkoani Mara wakati
wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo,
Lydia Bupilipili na Mbunge wa Bunda Vijijini, Bonafasi Mwita Getere (kulia).
Na Hamza Temba, Bunda, Mara
.........................................................................
Kilio cha muda mrefu cha wananchi wa wilaya ya Bunda hususan katika ukanda unaopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuhusu wanyamapori waharibifu jamii ya Tembo kuvamia makazi yao na mashamba kinaelekea kupata ufumbuzi wa kudumu.
Hatua hiyo inakuja kufuatia agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki kwa vijiji kumi vinavyopakana na hifadhi hiyo ili watumike kama uzio wa kudhibiti wanyamapori hao.
Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mariwanda, kata ya Hunyari wilaya ya Bunda mkoani Mara wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani humo.
"TANAPA wakishirikiana na TFS waje waanzishe mradi wa ufugaji nyuki wa kisasa katika vijiji vyote 10 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti, waje wahamasishe uundwaji wa vikundi, wafundishe namna ya kuweka mizinga ya kisasa na namna ya kufuga nyuki na kuvuna, na mwisho wa siku wananchi wapate faida ya kuzuia wanyamapori kuvamia mashamba na makazi yao pamoja na kuvuna asali itakayowatengenezea kipato mbadala" ameagiza Dk. Kigwangalla.
Akielezea mbinu hiyo mpya inavyofanya kazi Dk. Kigwangalla amesema, wataalamu ndani ya wizara yake wameeleza kuwa mbinu hiyo ya kuweka mizinga ya nyuki kuzunguka maeneo ya mashamba na makazi ya wananchi itasaidia kudhibiti Tembo kwakuwa huogopa sana nyuki na endapo wakisikia tu harufu yake huwa vigumu kusogelea maeneo hayo.
Awali akiwasilisha malalamiko kwa niaba ya wananchi wa vijiji hivyo, Mbunge wa Bunda Vijijini, Bonifasi Mwita Getere alisema kwa muda mrefu sasa wananchi hao wamekuwa wakipata madhara ya kuvamiwa na Tembo ambao hula mazao yao mashambani na hata majumbani, kuwajeruhi wananchi na wengine kupoteza kabisa maisha.
Baraka Abdul ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mariwanda wilayni humo alisema, mbinu zinazotumika kufukuza Tembo hivi sasa ikiwemo kupiga makelele na madebe na kutumia tochi za mwanga mkali zimekua hazisaidii, hivyo ameiomba Serikali kuongeza idadi ya askari na vituo katika maeneo yanayoathirika zaidi na matukio hayo.
Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla ametoa onyo kali kwa wananchi wanaofanya vitendo vya ujangili na uingizaji mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuwataka kuacha mara moja kwakuwa wakikamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kutaifishwa mifugo yao kwa mijibu wa kifungu cha 111 Na. 5 cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009.
Katika hatua nyingine, ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kupitia eneo la mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Bufer Zone) kuanzia Ghuba ya Speke hadi kwenye mpaka na nchi ya Kenya, wabaini mipaka halisi na ramani na kuainisha mahitaji ya wananchi na changamoto zilizopo na hatimaye kuwasilisha kwake mapendekezo ya kuondoa changamoto zilizopo.Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana na uongozi wa wilaya ya Bunda alipowasili wilayani hapo jana kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja.Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza uongozi wa wilaya ya
Bunda ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Lydia Bupilipili (kulia kwake) wakati
wa ziara yake ya siku moja kwa ajili ya kutatua changamoto za uhifadhi wilayani
humo jana.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa kata
Nyatwali wakati wa ziara yake ya siku moja kwa ajili ya kutatua changamoto
mbalimbali za uhifadhi katika wilaya ya Bunda mkoani Mara jana. Wengine pichani
kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TANAPA, Martin Loibooki na Mkuu
wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili (wa pili kulia).
Mwananchi wa kata Nyantwali akitoa maoni yake kwa Waziri Kigwangalla.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wananchi wa
kijiji cha Bukore wakati wa ziara yake ya siku moja kwa ajili ya kutatua
changamoto mbalimbali za uhifadhi katika wilaya ya Bunda mkoani Mara jana.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na Mbunge wa Jimbo
la Bunda Vijijini, Bonifasi Mwita Getere muda mfupi baada ya kuzungumza na
wananchi wa kijiji cha Bukore wakati wa ziara yake ya siku moja kwa ajili ya
kutatua changamoto mbalimbali za uhifadhi katika wilaya ya Bunda mkoani Mara
jana.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mariwanda wakati ziara ya Waziri Kigwangalla wilayani humo.
Baraka Abdul, mkazi wa kijiji cha Mariwanda akiwasilisha maoni yake kwa waziri Kigwangalla katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Dk. Kigwangalla akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mariwanda.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akijibu akifafanua jambo katika mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Mariwanda kata ya Hunyari wilaya ya Bunda mkoani Mara wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Dk. James Wakibara akifafanua jambo kwenye mkutano huo.
No comments:
Post a Comment